Tuujue Mtaguso Mkuu |
![]() |
TUUJUE
MTAGUSO MKUU
UTANGULIZI
Yesu Kristo aliwakabidhi mitume kumi na wawili
uongozi wa Kanisa wakiwa kundi moja lenye mkuu wake, yaani Petro. Vilevile
waandamizi wao, yaani maaskofu wote, ni kundi moja na papa wa Roma ndiye mkuu
wao. Huyo peke yake, na kundi la maaskofu likiwa pamoja naye na chini yake, ndio
wenye mamlaka ya juu katika Kanisa lote. Mamlaka hiyo inatumika kwa namna ya
pekee unapofanyika mtaguso mkuu, yaani mkutano maalumu wa maaskofu uliokubaliwa
na papa kuwa unawakilisha kundi hilo lote.
ORODHA
YA MITAGUSO MIKUU
KATIKA MILENIA YA
KWANZA ILIFANYIKA MASHARIKI (UTURUKI):
1.
Nisea I (mwaka
325)
2.
Kostantinopoli
I (381)
3.
Efeso
(431)
4.
Kalsedonia
(451)
5.
Kostantinopoli
II (553)
6.
Kostantinopoli
III (680-681)
7.
Nisea II
(787)
8.
Kostantinopoli
IV (869-870)
KATIKA
MILENIA YA PILI ILIFANYIKA MAGHARIBI (ITALIA, UFARANSA, UJERUMANI):
9.
Laterano
I (1123)
10.
Laterano
II (1139)
11.
Laterano
III (1179)
12.
Laterano
IV (1215)
13.
Lyon I
(1245)
14.
Lyon II
(1274)
15.
Vienne
(1311-1312)
16.
Kostansa
(1414-1418)
17.
Firenze
(1439-1445)
18.
Laterano
V (1512-1517)
19.
Trento
(1545-1563)
20.
Vatikano
I (1869-1870)
21.
Vatikano
II (1962-1965)
Mitaguso
mikuu ya kwanza ilifanyika hasa ili kubainisha katika mafundisho yaliyogongana
yapi yanalingana na imani sahihi. Mwisho wake ulikuwa kutangaza dogma fulani na
kutenga na Kanisa watakaokataa kuiamini na watakaofundisha tofauti.
Mitaguso
iliyofanyika baada ya farakano la mwaka 1054 kati ya Kanisa la Mashariki na la
Magharibi, pamoja na kulenga umoja uliovunjika na kufundisha dogma mpya,
ilishughulikia zaidi urekebisho wa Kanisa katika ngazi na nyanja zote. Kwa namna
ya pekee mtaguso wa pili wa Vatikano tangu uitishwe ulijulikana kuwa wa
kichungaji, yaani usio na lengo la kufundisha dogma mpya wala kulaani mafundisho
mengine.
Mzee wetu Fransisko anasifika kwa ukatoliki wake:
alishikamana kabisa na Kanisa akiwatii viongozi wake na kuwa rafiki yao. Tangu
mwanzo alitaka kuweka utawa wake chini ya Mama Kanisa Takatifu la Roma
akakubaliwa kwa moyo. Kinyume cha uzushi mwingi wa wakati wake, karama ya
Fransisko ilionyesha wazi kuwa Injili imekabidhiwa kwa Kanisa, hivyo ishikwe
kikamilifu ndani ya Kanisa na kwa msaada wake.
Tukiangalia zaidi uhusiano huo tunaona kuwa Fransisko
aliingia kabisa katika juhudi za urekebisho wa liturujia na maadili ambazo
kilele chake ni mtaguso wa nne wa Laterano (1215). Wengi wanadhani kuwa mwenyewe
aliuhudhuria akiwa ni mkuu wa utawa; kwa vyovyote ni hakika kuwa baadaye
alionekana kujua sana malengo na maamuzi ya mtaguso huo, na kutaka kuyatekeleza
pamoja na wafuasi wake na waamini wote.
Kwa mfano, barua zake zinahimiza heshima kwa ekaristi
na kwa yale yote yanayohusu liturujia: katika kuziandika alitumia hata maneno
yenyewe ya hati za mtaguso na za papa. Zaidi tena, Fransisko alipokea kwa moyo
mpango wa Inosenti III wa kufanya Kanisa lote (hasa makleri) liongoke kwa
kusulubisha mwili na tamaa zake, likitumia ile tau inayoongelewa na Ezekieli 9
kuwa ni muhuri waliotiwa wateule wa Mungu waliokubali msalaba katika maisha yao.
Hivyo tau ikawa kwa Fransisko pia ishara ya toba aliyojitahidi kuieneza kati ya
waamini. Kwa kuungana kabisa na Msulubiwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu katika
yote, akawa chombo cha kurekebishia Kanisa si kwa kulilaumu wala kwa kulipinga,
bali kwa njia ya utakatifu.
Kwa namna fulani Kanisa linajikuta leo katika nafasi
inayofanana na ile ya zamani za Fransisko na linahitaji watu ambao wamefanywa
wapya kwa kushiriki mateso ya Kristo, na ambao Roho aweze kuwatumia bila ya
pingamizi kwa ujenzi wa ufalme wa Mungu. Mtaguso wa pili wa Vatikano umepanga
kwa upana wote kazi ya kutengeneza upya maisha ya Kikristo, lakini kazi hiyo
haiwezi kufanyika bila ya mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu, naye anafanya kazi
hasa katika watu waliokubali kujazwa naye hata kuwashirikisha ndugu zao.
Basi, mfano wa Fransisko unawahimiza Wakristo
washikamane na Kanisa kwa nguvu zao zote; ndani yake mfumo au muundo wowote
usikubali kuwa na mpango wake wenyewe, bali utumie kwa unyenyekevu karama yake
katika kutimiza mpango uliofanyika katika mtaguso kwa ushirikiano wa Roho na
maaskofu wote. La sivyo miongozo na maagizo yake bora yatabaki maandishi matupu
ambayo hayazai matunda yale yote yaliyotarajiwa. Hasa Kanisa linatazamia kuwa
wafuasi wote wa Fransisko watatoa mchango wa utakatifu wao ambao kwa namna
fulani umfufue kwa ulimwengu wa leo.
MALENGO
YA MTAGUSO WA PILI WA VATIKANO
Muda mfupi baada ya kuchaguliwa papa mwenye heri
Yohane XXIII alitangaza uamuzi wake wa kuitisha mtaguso mkuu akiamini kwamba
utaweza kuandaa na kusababisha ustawi mpya wa maisha ya Kanisa. Lengo kuu la
mtaguso lilikuwa kuliamsha Kanisa likumbuke wito wake na kwa kujifanya upya kwa
ndani lipate msukumo mpya wa kimisionari ili kuwatangazia watu wote ujumbe wa
milele wa wokovu, amani na umoja.
Tangazo hilo lilitolewa tarehe 25-1-1959. Baada ya
maandalizi mtaguso wa pili wa Vatikano ulifunguliwa tarehe 11-10-1962. Vikao
vinne vikafanyika mpaka ulipofungwa tarehe 8-12-1965. Kila kikao kilianza Oktoba
na kumalizika Desemba ya miaka hiyo.
Kwa kuwa Yohane XXIII alifariki tarehe 2-6-1963,
vikao vitatu vya mwisho viliongozwa na mwandamizi wake, Paulo VI, na hati zote
kumi na sita zikatolewa chini yake pia kwa kupigiwa kura ya ndiyo karibu kwa
kauli moja. Maaskofu na wakuu wa mashirika kadhaa wenye haki ya kupiga kura
walikuwa kama elfu tatu, wakiwakilisha karibu Kanisa lote duniani, isipokuwa
nchi zile zenye kuwadhulumu Wakristo.
ORODHA
YA HATI 16 ZA MTAGUSO
|
HADHI |
JINA LA
KILATINI |
KIFUPISHO |
YAHUSUYO |
TAREHE |
|
KATIBA |
1. Sacrosanctum Concilium |
SC |
Liturujia takatifu |
4-12-1963 |
|
2. Lumen Gentium |
LG |
Kanisa |
21-11-1964 |
|
|
3. Dei Verbum |
DV |
Ufunuo wa Kimungu |
18-11-1965 |
|
|
4. Gaudium et Spes |
GS |
Kanisa katika ulimwengu wa kisasa |
7-12-1965 |
|
|
MAAGIZO |
1. Inter Mirifica |
IM |
Vyombo vya upashanaji habari |
4-12-1963 |
|
2. Orientalium Ecclesiarum |
OE |
Makanisa katoliki ya Mashariki |
21-11-1964 |
|
|
3. Unitatis Redintegratio |
UR |
Ekumeni |
21-11-1964 |
|
|
4. Christus Dominus |
CD |
Huduma ya kichungaji ya maaskofu |
28-10-1965 |
|
|
5. Perfectae Caritatis |
PC |
Kurekebisha upya maisha ya kitawa |
28-10-1965 |
|
|
6. Optatam Totius |
OT |
Malezi ya kipadri |
28-10-1965 |
|
|
7. Apostolicam Actuositatem |
AA |
Utume wa walei |
18-11-1965 |
|
|
8. Ad Gentes |
AG |
Utendaji wa kimisheni wa Kanisa |
7-12-1965 |
|
|
9. Presbyterorum Ordinis |
PO |
Huduma na maisha ya kipadri |
7-12-1965 |
|
|
MATAMKO |
1. Gravissimum Educationis |
GE |
Malezi ya Kikristo |
28-10-1965 |
|
2. Nostra Aetate |
NA |
Uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo |
28-10-1965 |
|
|
3. Dignitatis Humanae |
DH |
Uhuru wa dini |
7-12-1965 |
MAPOKEZI
YA MTAGUSO
Kwa kuwa Roho Mtakatifu alitaka hivyo, Wakristo walio
wengi walipokea kazi ya mtaguso kwa mikono miwili, na wengi nje ya Kanisa pia
waliridhika sana. Kutokana nao yamepatikana matunda mengi, lakini zimejitokeza
hata kasoro na shida kwa sababu mbalimbali, hasa kwa kutoelewa wala kutotekeleza
sawasawa maagizo yake. Kwa vyovyote hatuwezi kusema yote yaliyotokea baada ya
mtaguso yamesababishwa nao, k.mf. maovu yaliyofanywa na baadhi ya mapadri hayamo
kabisa.
Pamoja na upinzani wa wazi wa mifumo kadhaa ya
kisiasa (ukomunisti na ubepari) na matapo mengine (Wamasoni n.k.) dhidi ya
Kanisa, hali ya jumla ya ulimwengu inazidi kuelekea anasa na kuabudu utajiri
hata kuzima maisha ya Kiroho. Hivyo ni vigumu kufanikisha mtaguso.
Hata ndani ya Kanisa wengi wamesoma hati zake
kijuujuu, wakishikilia upande mmoja na kutojali wa pili. Wengine wamevunjika
moyo kuona utekelezaji wa mtaguso unavyokwenda polepole. Wengine wameshughulikia
miundo tu ya Kanisa, bila ya kujali fumbo la Kimungu lililomo ndani yake.
Pengine umekosekana upambanuzi, k.mf. wengi walipofuata mitazamo ya ulimwengu
uliomuasi Mungu badala ya kujadiliana nao ili kuuokoa.
Matatizo yaliyojitokeza baada ya mtaguso yanaonyesha
haja ya kuupokea vizuri zaidi, kwa kupiga hatua nne zifuatazo:
1.
Hati za mtaguso zijulikane na watu wengi zaidi na kwa dhati zaidi.
2.
Zipokewe kwa moyo.
3.
Zizingatiwe kwa upendo.
4.
Zitekelezwe maishani.
NAMNA
YA KUELEWA MTAGUSO
Tukitaka kuelewa vizuri hati za mtaguso, ni lazima
tuzizingatie zote 16 zilivyo na zinavyofungamana. Ni lazima pia tutie maanani
hasa katiba zake 4, kwa kuwa ndizo hati kuu zinazotuwezesha kuelewa maagizo 9 na
matamko 3. Tena hatutakiwi kutenganisha mtazamo wa kichungaji na msingi wa imani
wa hati hizo, wala kutenganisha roho ya mtaguso na hati zenyewe. Mwishowe
mtaguso ueleweke katika mapokeo ya Kanisa kwa kuwa katika mitaguso yote Kanisa
ni lilelile. Hivyo tu tutapata mwanga tunaouhitaji kwa wakati huu.
Tahadhari hizo zote zinahitajika kwa sababu katika
kutekeleza mtaguso yamejitokeza maelekeo mawili ambayo yanapingana na kuvuruga
hali ya Kanisa. La kwanza linadai mabadiliko yasiyolingana na mtaguso, ingawa
wenyewe wanasema ni maendeleo yanayotakiwa na roho ya mtaguso. Maendeleo ya
namna hiyo hayakubaliki kwa sababu hayajali mapokeo ya mitume yanayodai imani
idumu kuwa ileile. La pili linaambatana na mambo ya zamani, bila ya kujali
ishara za nyakati zetu zinazodai mambo mapya pia kwa wokovu wa watu wa leo na wa
kesho.
Ni wajibu wa maaskofu chini ya papa kutambua yapi
yanajenga na yapi yanazuia ujenzi au pengine yanabomoa Kanisa. Ndiyo kazi
inayofanyika hasa katika sinodi (= pamoja-njia, yaani kusafiri pamoja). Kati ya
sinodi za ngazi mbalimbali kuanzia ile ya jimbo, muhimu zaidi ni zile za
kimataifa zinazofanyika mara kwa mara huko Roma (mtaa wa Vatikano), zikikusanya
maaskofu wawakilishi wa nchi zote na baadhi ya wakuu wa mashirika ya kitawa.
JUHUDI
ZA KUTEKELEZA MTAGUSO
Kama vile mitaguso mikuu iliyotangulia kupanga
urekebisho wa hali ya Kanisa, mtaguso wa pili wa Vatikano pia ujumbe wake
hautaweza kuzaa matunda isipokuwa kwa juhudi za muda mrefu. Miaka ishirini baada
ya mtaguso kumalizika, sinodi maalumu iliyoitishwa ili kutathmini matokeo yake
ilisema wazi kuwa kazi bado sana, kwa namna ya pekee kuhusu kulenga utakatifu
kwa waamini wote. Ndiyo maana ilihamasisha tufanye juu chini ili ujumbe wa
mtaguso usikilizwe upya katika kila jimbo. Ni lazima tushike jembe kwa kazi hiyo
bila ya kuangalia nyuma tukipatwa na matatizo yasiyoepukika.
SACROSANCTUM
CONCILIUM
Kikao cha pili cha mtaguso kilipitisha hati mbili za
kwanza. Ya kwanza kabisa inahusu liturujia ambayo ni moyo wa Kanisa kwa kuwa
ndipo linapoungana na Mungu wake na kuonekana katika sura yake takatifu. Lengo
la hati hiyo ni kufanya kwanza mapadri, halafu Wakristo wengine pia waelewe na
kutimiza liturujia ili kwa njia yake wamtukuze kweli Mungu na kufaidika Kiroho.
Karne ya XX iliiandaa kwa kuwa wataalamu walijitahidi
kwa muda mrefu kuchambua maana ya liturujia kwa jumla na ya ibada zake
mbalimbali. Mapapa wote walipokea na kuagiza marekebisho kadhaa yalitopendekezwa
na wataalamu hao. Lakini kazi kubwa zaidi ilikuwa bado.
Kikwazo kikuu kilikuwa ni lugha ya Kilatini
iliyokwishakufa tangu miaka elfu hivi. Muda huo wote wasomi tu waliweza kuelewa
masomo na mengineyo ya liturujia. Hivyo watu wa kawaida wakawa watazamaji tu wa
matendo ya ibada. Bila ya kupata mafundisho wala sakramenti ya ekaristi,
Wakristo wa Magharibi walijitungia ibada zao badala ya kutegemea liturujia ya
Kanisa.
Huko Mashariki hali ilikuwa tofauti kabisa: ndiyo
sababu hati hiyo inahusu liturujia ya Roma tu, isipokuwa misingi ya liturujia
yoyote na mengineyo yanayofaa hata Mashariki.
Sura ya kwanza inahusu
kanuni za jumla kwa urekebisho na ustawishaji wa liturujia. Kwanza inaeleza
undani na umuhimu wake, halafu inasisitiza haja ya malezi ya kiliturujia kuanzia
seminari na nyumba za kitawa ambapo maisha yote yafuate roho ya liturujia na
masomo yote yafundishwe kwa kuonyesha uhusiano wake na liturujia ambayo
ihesabiwe kati ya masomo muhimu zaidi na kufundishwa na wataalamu. Hivyo waamini
wote watasaidiwa kuchota roho halisi ya Kikristo katika chemchemi hiyo ya kwanza
na ya lazima; pia wataweza kushiriki ibada kwa jinsi iliyo haki na wajibu wao.
Baadaye tu yanaagizwa marekebisho ya jumla ya
liturujia na vitabu vyake vyote; msingi wake ni kwamba liturujia, mbali ya mambo
yaliyoagizwa na Bwana, ina mengi yaliyopangwa na Kanisa lenyewe katika historia
yake kulingana na mahali na nyakati mbalimbali. Kwa hiyo mara kwa mara linaweza
na kupaswa kuyapanga upya kwa manufaa ya waamini.
Kwa kuwa liturujia ni kazi ya Kanisa lote,
inaratibiwa na uongozi wake tu: wengine wasithubutu kubadilisha lolote
wanapofanya ibada zake. Hata uongozi wa Kanisa usirekebishe vitabu harakaharaka
na pasipo lazima, bali uhakikishe kwamba mapya yanalingana na ya zamani.
Kwa namna ya pekee ni lazima neno la Mungu katika
liturujia liheshimiwe linavyostahili, tena lionjwe kama ilivyokuwa mwanzoni mwa
Kanisa.
Maagizo mengine yanatokana na hali ya kijumuia ya
liturujia, yaani kwamba ibada zake si za binafsi, bali ni za Kanisa lote, na
kila mmoja anahusika namna yake kama mwamini wa kawaida au kama mwenye daraja au
huduma fulani. Hivyo ipendelewe ibada ya pamoja ambapo kila mmoja ashike nafasi
yake na kulingana vizuri na wengine wanaoshika nafasi zao.
Maagizo mengine yanazingatia faida ya waamini upande
wa imani ikiwa ni pamoja na kujifunza undani wa imani yenyewe. Kwa ajili hiyo
mtaguso umeamua ibada zieleweke kwa urahisi, mapadri watoe hotuba na mawaidha
mbalimbali wakati wa ibada, pia ziruhusiwe lugha hai za watu ingawa Kilatini
kinabaki lugha rasmi ya madhehebu ya Kanisa la Magharibi na waamini wake wote
wanatarajiwa kujua kuitikia na kuimba kwa Kilatini wakati wa Misa.
Mbali ya lugha, mtaguso umekubali yafanyike
marekebisho mengine ili kupokea katika liturujia ya Roma utamaduni wa makabila
yoyote mradi usipingane na imani. Utamadunisho huo ufanyike chini ya Baraza la
Maaskofu na kukubaliwa na Roma.
Mwisho wa sura hiyo unasisitiza umuhimu wa watu
kushiriki liturujia ya askofu katika Kanisa kuu na ile ya parokia ili waamini
wajisikie kweli Kanisa moja.
Ili kustawisha liturujia mtaguso umeagiza ziwepo
kamati maalumu kitaifa na kijimbo.
Ili kutekeleza yaliyosemwa hapo juu,
sura ya pili inaagiza namna ya kurekebisha madhehebu ya Misa, sura
ya tatu inafanya vilevile kuhusu sakramenti nyingine na visakramenti, na sura
ya nne kuhusu Sala ya Kanisa. Vitabu vyote vinavyohusika tunavyo tayari
vimerekebishwa: katika kuvitumia ni muhimu kujisomea utangulizi wake.
Sura ya tano
inarekebisha mwaka wa Kanisa kusudi mpango wake ueleweke zaidi bila ya kujaa mno
sikukuu za watakatifu: hasa siku ya Bwana na vipindi maalumu vya mwaka vipate
nafasi vinavyostahili.
Sura mbili za
mwisho zinahusu
muziki na sanaa takatifu ili liturujia ipendeze kwa uzuri wake, iinue roho kwa
Mungu na kuwa kielelezo cha ile ya mbinguni. Hivyo vipawa mbalimbali vya
binadamu vitumike kumtukuza Mungu. Hayo yameelezwa baada ya vitabu kwa sababu
hivyo vina neno la Mungu na maitikio yetu kwa neno hilo lenye kututakasa.
Vilevile muziki unaelezwa kabla ya sanaa nyingine kwa sababu unaambatana na
maneno matakatifu. Mtaguso umesisitiza umuhimu wa kuimba katika liturujia,
ukiagiza malezi kwa ajili hiyo, uundaji wa kwaya, utungaji wa nyimbo ambazo
zichote hasa katika vitabu vya Biblia na liturujia. Kuhusu aina za muziki
mtaguso umekubali aina yoyote inayoweza kulingana na utakatifu wa ibada;
vilevile umeruhusu ala mbalimbali za kufaa. Hata hivyo liturujia ya Roma
inapendelea muziki wa Kigregori na kinanda cha mabomba. Sanaa nyingine pia
zinaheshimiwa na kutumiwa na Kanisa kwa ujenzi, mapambo, vifaa na picha takatifu.
Kadiri ya mahali na nyakati limekubali mitindo mbalimbali mradi ilingane na
imani, maadili na ibada ya Kikristo. Mtaguso umeagiza maaskofu hasa wajitahidi
kudumisha msimamo huo na uzuri wa yote yanayohusu liturujia, kwa kuelimisha
wanasanaa na makleri.
LUMEN
GENTIUM
Hati hiyo juu ya Kanisa ndiyo muhimu kuliko nyingine
zote za mtaguso. Inajibu swali la PauloVI, “Kanisa, unasemaje juu yako?”.
Sura ya kwanza inafafanua
fumbo la Kanisa ambalo, kama sakramenti, lina mawili yasiyotenganika: kwa nje
linaonekana kwa namna fulani, na kwa ndani mwa neema isiyoonekana inayoletwa na
yale yanayoonekana. Ndani ya Kanisa la watu Mungu anaishi na kufanya kazi.
Kwa hiyo hati inaanza kwa kueleza jinsi Baba, Mwana
na Roho Mtakatifu wanavyohusika na Kanisa. Halafu unaonyesha kuwa Kanisa ni
mwanzo wa ufalme wa Mungu, nalo linafananishwa na kundi la kondoo, shamba, jengo
na hekalu la Mungu au bibiarusi anayeungana na Bwanaarusi wake kuwa mwili mmoja,
yaani mwili wa Kristo: ndio ukweli wenyewe wa Kanisa.
Baada ya kuona ukweli huo wa ndani, sura
ya pili inaelekea kutazama watu wanavyohusika na fumbo la Kanisa. Kuanzia
Agano la Kale Mungu hakupenda kuokoa watu mmojammoja bali aliwaunganisha wawe
taifa lake lenye kujua ukweli na kumtumikia kitakatifu. Katika taifa hilo wote
wamejaliwa ukuhani ambao unatumika katika adhimisho la sakramenti, na unabii
wenye karama mbalimbali.
Katika taifa hilo watu wote wanapaswa kuingia bila ya
ubaguzi ili wawe kitu kimoja. Ndiyo maana ya jina “Katoliki”: la mahali pote
na nyakati zote. Wote wanahusiana na Kanisa ila kwa namna mbalimbali. Kwanza
wapo Wakatoliki, yaani waliojiunga nalo kikamilifu kwa kumkubali Roho Mtakatifu
na miundo yake yote. Halafu wapo Wakristo wengine waliokwishabatizwa na hivyo
wameungana nalo ingawa si kikamilifu, kwa sababu hawakubali baadhi ya mafundisho
na miundo yake. Hatimaye wapo watu wengine pia, wenye dini mbalimbali au wasio
na dini, ambao wote wanaitwa na Mungu wajiunge na Kanisa kwa kuwa linahitajika
kwa wokovu, ingawa Mungu anaweza kuwaokoa wenye nia njema wasiopata habari njema.
Bila ya shaka hali ya Wakatoliki ni bora zaidi, nao
wanapaswa kuwashirikisha wengine wote ili kuwaokoa kutoka udanganyifu wa shetani
na ulimwengu. Ndiyo maana ya kazi ya kimisionari ambayo imeagizwa na Yesu na ni
wajibu wa kila Mkristo.
Sura ya tatu inatoa
mafundisho muhimu tena mapya kuhusu muundo wa uongozi wa Kanisa, hasa uaskofu.
Ni kwamba mtaguso wa I wa Vatikano ulifundisha sana kuhusu papa lakini haukupata
nafasi ya kutoa hati iliyopangwa juu ya maaskofu, kwa sababu ulisambaratika
jeshi la Italia lilipoteka Roma. Hivyo mtaguso wa PILI wa Vatikano ulikusudia
kukamilisha kazi hiyo.
Hasa umefundisha kwamba kama vile mitume walivyokuwa
kundi moja na Petro na chini yake, maaskofu wote ni kundi moja na papa wa Roma
na chini yake. Kwa mpango wa Mungu kundi hilo ni la kudumu, maaskofu wakiwa
waandamizi halisi wa mitume, na papa mwandamizi halisi wa Petro, mkuu wao.
Kwa namna ya pekee mtaguso umefundisha kuwa ibada ya
kumweka wakfu askofu ni ngazi ya juu kabisa ya sakramenti ya daraja, si baraka
fulani kwa padri anayepewa kazi ya juu kama wengine walivyodhani awali. Hivyo
uaskofu unatia alama isiyofutika milele. Kutokana na fundisho hilo, mtaguso
umesisitiza kila mara umuhimu wa maaskofu katika maisha yote ya Kanisa.
Lakini mtaguso umesisitiza pia umoja wa maaskofu,
ukidai kila mmoja wao afanye kazi yake akishirikiana na kundi lote na achangie
ustawi wa Kanisa zima, si jimbo lake tu. Katika hilo askofu ndiye nguzo ya umoja
wa waamini wake wao kwa wao tena kati yao na waamini wote duniani: hivyo
linafanya listahili kuitwa Kanisa, kwa kuwa ndani yake Kanisa lote limo kweli.
Kwa msingi huo askofu anawakilisha Kanisa lake maalumu katika Kanisa Katoliki,
na kulifundisha, kulitakasa na kuliongoza kwa msaada wa mapadri wake na wa
mashemasi, ambao wote wanashiriki ukuhani wake mkuu.
Mwishoni mwa sura hiyo Kanisa la Magharibi linaruhusu
ushemasi wa kudumu urudishwe na kutolewa kwa wanaume wenye ndoa pia.
Mara baada ya sura inayohusu wale wachache waliopata
daraja takatifu (wanaoitwa makleri), inafuata sura ya nne juu ya Wakristo wa kawaida (wanaoitwa walei). Kwa karne
nyingi hao walibaki kama wasikilizaji na watazamaji tu katika ibada na katika
maisha yote ya Kanisa, lakini kuanzia karne ya XIX utume wao ulianza kuamka upya.
Mtaguso umesisitiza kwa nguvu wajibu na haki yao ya kutumia neema na vipaji
walivyojaliwa na Mungu kwa ujenzi wa taifa lake na kwa wokovu wa ulimwengu.
Msingi wake ni ubatizo uliowafanya manabii, makuhani na wafalme; hivyo
wamejaliwa huduma na karama mbalimbali ambazo wachungaji wanapaswa kuziheshimu
wakiwaachia uhuru na nafasi katika utendaji. Kwa namna ya pekee ni juu yao
kulenga utawala wa Mungu kwa kushughulikia malimwengu.
Baada ya kuona hayo makundi mawili ya waamini,
wanaotofautiana kwa alama walizotiwa rohoni na ubatizo na kipaimara tu, au na
daraja takatifu pia, sura ya tano
inahusu wito unaowaunganisha wote, yaani kupata utakatifu. Karne za nyuma wengi
walidhani hiyo ni kazi ya watawa tu, waliojichagulia “hali ya ukamilifu”, au
sanasana mapadri. Kumbe sivyo: Wakristo wote wanapaswa kulenga utakatifu, kila
mmoja kadiri ya wito wake maalumu na hali yake maishani. Hati inaorodhesha aina
mbalimbali za waamini na jinsi kila moja ilivyo na njia yake; halafu inakumbusha
njia mbili bora, yaani kifodini na mashauri ya Kiinjili: kwa maisha na kifo chao
mashahidi na watawa wanahimiza Wakristo wote kutafuta ukamilifu wa upendo.
Hivyo ni rahisi kuelewa kwa nini sura
ya sita inazungumzia watawa. Hao hawahusiki na uongozi wa Kanisa (isipokuwa
kama wamepata pia daraja takatifu), ili wanahusika moja kwa moja na utakatifu na
uhai wake. Si kundi la tatu kati ya makleri na walei, bali ni walei au makleri
waliojifunga kulenga utakatifu kwa kushika mashauri ya Kiinjili, yaani useja
mtakatifu, ufukara na utiifu. Mtaguso umesisitiza umuhimu wa mtindo huo wa
maisha na asili yake katika maneno na mifano ya Yesu: utawa hautokani na
historia ya Kanisa tu, bali upo na lazima uwepo kwa mpango wa Mungu. Hivyo
uongozi wa Kanisa unapaswa kuuratibu na kuudumisha katika mitindo yake mingi.
Mtawa amewekwa wakfu kwa ubatizo, halafu anaimarisha hali hiyo kwa nadhiri ili
achume kwa wingi zaidi matunda ya neema kwa kuondoa mapingamizi yoyote
yanayoweza kumzuia maishani.
Baada ya kuwaongelea watawa, wanaoshuhudia kwa namna
ya pekee ulimwengu mpya ambapo hapana ndoa, sura
ya saba inakuja kufundisha kuwa Kanisa lote hapa duniani liko safarini
kuelekea mbinguni, huku likiwa na umoja na watakatifu. Sura hiyo inasisitiza
tena imani yetu kuhusu mambo ya mwisho ikituhimiza tutazame juu na pia
tuzingatie mifano bora ya wale waliokwishafikia heri ya milele. Hao wanastahili
tuwaheshimu na kuwaomba watuombee, mradi tuepuke makosa mbalimbali
yaliyojitokeza huku na huku. Daima ionekane wazi kuwa tunamuabudu Mungu tu na
kwamba tukiwaheshimu watakatifu ni kwa sababu ni marafiki wa Mungu na wafuasi
hodari wa Mwanae. Tunawaheshimu sio tu ili kupata msaada fulani, bali hasa kwa
kufuata mifano yao ili tuwafikie katika liturujia ya mbinguni kuwaabudu Mungu na
Mwanakondoo.
Mwishoni mwa hati hii yanapatikana mafundisho kuhusu
Bikira Maria, akiwa ni mkuu wa watakatifu na mfano wa Kanisa lote. Baada ya
mabishano makali kati ya washiriki wa mtaguso, wingi wa kura ulikataa kutoa hati
maalumu juu ya Maria peke yake, kwa kuwa hawezi kueleweka nje ya fumbo la Kristo
na la Kanisa. Hivyo mafundisho hayo yamepangwa katika sura
ya nane ya hati hii, si kwa nia ya kuamua mabishano kati ya wanateolojia,
wala kufundisha mapya, bali kupanga upya mafundisho ya Maandiko na ya Mapokeo.
Baada ya kumsifu sana Bikira, mtaguso umesisitiza juu yake pia kuwa Kristo ndiye
mshenga pekee kati ya Mungu na watu, hivyo hatuwezi kumlinganisha Maria na yeye
kama walivyowahi kufanya baadhi ya waamini. Mchango wake kwa ukombozi wetu
ulitokana na ukombozi ulioletwa na Yesu, ni kushiriki kazi yake tu. Hivyo Maria
azidi kuigwa na kuheshimiwa kwa namna ya pekee, hasa kwa njia ya liturujia,
lakini kwa kukwepa neno lolote ambalo linapita kiasi au kumweka pembeni Kristo.
Wazo kuu la
hati hii kuhusu Kanisa ni kwamba lenyewe hasa ni ushirika wa Mungu nafsi tatu na
watu, ni ushirika wa watakatifu wa duniani, toharani na mbinguni, ni ushirika wa
waamini wa aina mbalimbali, kama vile wenye daraja na walei, au watawa na wenzao
wote. Ushirika huo unatakiwa kuonekana wazi katika maisha ya Kanisa katika ngazi
zote; hivyo litaonekana lilivyo, yaani ishara na chombo cha kuwaunganisha watu
wote katika umoja wa Utatu mtakatifu.
DEI
VERBUM
Katika Kanisa Katoliki tangu zamani sana
zilisisitizwa liturujia na sakramenti, ingawa lugha ya kawaida ilikuwa haitumiki
katika ibada hizo. Hivyo waamini walikuwa hawaelewi masomo ya Biblia wala matini
mengine. Kwa jumla walikuwa hawaelewi Neno la Mungu kwa kukosa tafsiri za vitabu
vyake hata nyumbani. Kuanzia karne ya kumi na mbili tafsiri hizo zilianza
kupatikana kwa juhudi za wazushi waliozitumia kupinga ualimu wa Kanisa. Baadaye
watu walipobuni uchapishaji, kitabu cha kwanza kutolewa kikawa ni Biblia huko
Ujerumani. Mara ukaanza Uprotestanti pia ambao katika madhehebu yake yote
ulisisitiza Maandiko kwa kukataa Mapokeo na Ualimu wa Kanisa. Ndiyo sababu
yenyewe yalifanya kazi kubwa ya kutafsiri na kueneza Biblia ulimwenguni kote.
Upande wake Kanisa Katoliki likaogopa kwa kuona nchi ngapi zimeliasi, hivyo
likachukua msimamo wa kinyume kwa kusisitiza tena Mapokeo na Ualimu wake. Basi,
Biblia ikazidi kubaki pembeni mwa maisha ya Wakatoliki wengi. Hata mwanzoni mwa
karne ya XX walipojitokeza wataalamu wa Biblia walikatazwa wasifundishe baadhi
ya mambo mapya kuhusu utungaji na maana ya Maandiko. Hivyo kabla ya mtaguso
Wakatoliki kwa jumla walikuwa wakiogopa Biblia badala ya kuipenda.
Kumbe hati hiyo kuhusu ufunuo wa Kimungu ilipotolewa
baada ya majadiliano na marekebisho mengi imelirudishia Kanisa lote Maandiko
Matakatifu. Hapo Wakatoliki wataalamu wa Biblia wamefanya kazi kubwa sawa na
wenzao Waprotestanti. Waseminari na watawa wengi wamefundishwa sana Neno la
Mungu, na hata walei wameanza kulifurahia. Matunda yake yamepatikana tayari
katika uzima mpya unaoonekana katika mifumo ya Kiroho, vyama na jumuia
mbalimbali.
Baada ya dibaji,
inayotamka nia ya kufuata nyayo za mitaguso iliyotangulia, sura
ya kwanza inahusu ufunuo wa Mungu. Ni kwamba hatuwezi kuelewa Biblia mbali
na historia ya wokovu, kwa sababu si kitabu kilichoandikwa leo kwa ajili yangu
mimi, bali kilipatikana zamani Mungu alipojifunua hatua kwa hatua.
Sura ya pili
inafundisha jinsi ufunuo huo uliokamilika zamani za Yesu unavyotufikia sisi watu
wa leo, yaani kwa njia ya Mapokeo ya Mitume yakiwa na Maandiko Matakatifu ambayo
kwa pamoja ni hazina takatifu ya Neno la Mungu, si chemchemi mbili tofauti.
Hazina hiyo imekabidhiwa kwa Kanisa ambalo linaweza kuifafanua rasmi kwa njia ya
Ualimu wake. Basi, Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Ualimu wa Kanisa
yameshikamana na kuunganika kiasi kwamba moja haliwezi kusimama bila ya mengine.
Baada tu ya kuelewa hayo tunaweza kukabili Biblia
yenyewe (sura ya tatu) kwa kuzingatia
jinsi Roho Mtakatifu alivyovuviwa juu ya waandishi wake. Hao walifanya kazi kama
waandishi wowote, lakini vitabu vilivyopatikana vinafundisha tu kwa hakika na
bila ya kosa ule ukweli ambao Mungu alitaka uandikwe kwa wokovu wetu. Si ukweli
wowote (k.mf. wa sayansi) bali ule unaohusu wokovu. Hivyo Biblia mwandishi wake
hasa ni Mungu, lakini yeye alijieleza kwa njia ya watu tena kwa namna ya
kibinadamu. Basi, tukitaka kumuelewa tunapaswa kuelewa kwanza waandishi walitaka
kusema nini tukizingatia pia mitindo waliyoitumia. Utaalamu huo ni muhimu ingawa
hautoshi, kwa sababu tunapaswa bado kuzingatia umoja wa Biblia nzima, Mapokeo ya
Kanisa na kweli za imani.
Baada ya kuona habari za Biblia kwa jumla, sura
ya nne inaeleza umuhimu wa Agano la Kale kwa Wakristo pia, kwa kuwa
linashikamana na Agano Jipya kama kitabu kimoja ambacho pande zake mbili
zinahitajiana.
Sura ya tano inaeleza
juu ya Agano Jipya: kwanza ubora wake unaozidi vitabu vya kale; halafu asili ya
Kitume ya Injili nne ambazo tena zinapita hata Maandiko mengine ya Agano Jipya;
mwishowe hakika ya kihistoria ya Injili hizo. Hati hii imepokea pia mtazamo mpya
uliosema Wainjili waliandika historia ya Yesu kwa kuchagua baadhi ya habari,
kufupisha nyingine na kueleza upya nyingine kadiri ya mazingira, wakidumisha
namna ya kuhubiri kwa lengo la kufanya watu waamini. Habari zenyewe ziliwaelea
kwa mwanga wa Roho Mtakatifu aliyelifikia Kanisa baada ya Kristo kufufuka ili
kuliongoza kwenye ukweli wote.
Hatimaye sura
ya sita inatoa maagizo kuhusu Maandiko Matakatifu katika maisha ya Kanisa.
Kwanza ziwepo juhudi mpya ili wote wapate lishe katika meza ya Neno la Mungu
ambalo ni hai na lina nguvu. Pia juhudi zifanyike ili waamini wapate Maandiko
hayo katika lugha zao. Wataalamu pamoja na kuyatafsiri wayafafanue na kuelimisha
wengine. Wale wote wanaotoa mafundisho ya imani katika ngazi zozote washikamane
na Maandiko kwa kuyasoma pamoja na kusali ili Biblia iwe kiini cha mafundisho
yao. Waamini wote, hasa watawa, wanahimizwa kuisoma sana kwa sababu kutoijua ni
sawa na kutomfahamu Kristo.
GAUDIUM
ET SPES
Hati hiyo, ndefu kuliko zote za mtaguso, inaitwa ya
kichungaji kwa sababu inataka kutazama mambo kwa lengo la kuongoza maisha ya
watu. Sehemu yake ya kwanza inaweka misingi juu ya imani, na sehemu ya pili
inaonyesha msimamo wa Kanisa kuhusu ulimwengu wa leo. Kichwa kinasema wazi kuwa
hati inahusu Kanisa katika ulimwengu “wa kisasa”, kwa kuwa tunapaswa daima
kuishi na kutenda “leo”, huku tukijua vizuri mambo yalivyo, tukitambua
ishara za nyakati zijazo ili tuone njia za kufaa kwa wokovu wa ulimwengu.
Bila ya shaka imepita miaka mingi tangu hati iandikwe,
hivyo yameshatokea mabadiliko mengi, yaliyochunguzwa na mapapa na sinodi
mbalimbali. Ingawa baadhi ya mambo leo yanaonekana tofauti kidogo, hati hiyo
inabaki muhimu: kwanza kwa mtazamo wake wa jumla, pili kwa mtindo wa kuwaelekeza
watu katika mambo ya kawaida yanayowahusu maishani, tatu kwa mafundisho ya
msingi yasiyoweza kubadilika, nne kwa kuwa misimamo mbalimbali inafaa mpaka leo.
Kanisa halijioni tena mbali na ulimwengu, wala dhidi
ya ulimwengu, bali ndani ya ulimwengu. Wakristo wanasafiri duniani pamoja na
binadamu wenzao, wakishirikiana nao katika yale yote yasiyopingana na imani na
maadili ya Kikristo. Hasa walei, ambao idadi yao ni karibu sawa na idadi ya
wanakanisa wote, wanapaswa kuishi ulimwenguni kama chachu mpaka donge lote
liumuke. Basi, Kanisa linajisikia kuhusika kabisa na maisha ya watu wote, hasa
fukara. Ndiyo maana maneno ya kwanza ya hati hiyo yanasema kuwa “furaha na
matumaini, huzuni na mafadhaiko ya watu ni pia ya wanafunzi ya Kristo”.
Hati hiyo ni ujumbe wa Kanisa kwa watu wote unaotaka
kuwasaidia waelewe mambo yanayotukia siku hizi, kwa kuwa katika hayo binadamu
anaweza kujipatia maisha bora kweli na halafu uzima wa milele, au kinyume chake
anaweza kudanganyika na kupotoka. Siku hizi ugumu wa pekee kwa binadamu ni
kwamba mabadiliko ya kila aina yanatokea haraka ajabu, tofauti na zamani. Mtu wa
kawaida hapati nafasi ya kuyafikiria kwa dhati na kuyachambua. Hivyo hatari yake
ni kufuata mkondo au kuongozwa na matukio badala ya kujifanyia mpango wa kumfaa,
hata anaweza akafikia hatua ya kushindwa kujielewa ni nani, pamoja na kukosa
msimamo maishani na raha moyoni mwake. Basi, anahitaji kuchungwa na kuelekezwa
kwa imani na upendo: ndiyo kazi ya Kanisa ambalo lina nafasi nzuri ya
kuwatangazia watu majibu ya Injili kwa maswali yanayowakera.
Kwa ajili hiyo hati inamuongoza msomaji hatua kwa
hatua kufikiria utatanishi wa kisasa katika nadharia, jamii, uchumi na siasa
unaomfanya afadhaike, hasa akiona maendeleo hayafaidishi wote na pengine
yanatumika dhidi ya binadamu. Hivyo anaweza kutambua kuwa shida zinaanza moyoni
mwake, ambamo mna mashindano makali na maswali ya msingi kama vile, “Mtu ni
nani? Mateso na kifo vinavyodumu hata wakati huu wa maendeleo makubwa maana yake
nini? Mtu ailetee nini jamii na atarajie kupata nini toka kwake? Baada ya maisha
haya kutakuwa na nini?”. Jibu ni Kristo, mwokozi pekee, kiini na lengo la
historia yote, msingi hasa usiobadilika. Katika mwanga wake mtaguso umechunguza
fumbo la binadamu na wito wake.
Katika sehemu
ya kwanza, sura ya kwanza inaeleza hadhi ya binadamu yeyote. Ingawa karibu wote wanakubali kuwa
mtu ni kiumbe bora duniani, Kanisa linasisitiza ukweli huo kwa kumuona na
kumuita “sura ya Mungu” hata baada ya kuathiriwa na dhambi. Ndio msingi wa
heshima anayostahili katika mwili na zaidi katika roho ambayo kwa akili inaweza
kujipatia ukweli na hekima, kwa dhamiri inasikia wito wa Mungu, na kwa hiari
inaweza kuuitikia. Lakini Kanisa, pamoja na kusisitiza hiari kama wanavyofanya
wengi siku hizi, linahimiza pia kuitumia vizuri, kwa kuwa mwishoni kila mtu
atahukumiwa juu ya matumizi ya vipawa vyake.
Baada ya kukabili swala la kifo kwa kutangaza habari
njema ya ufufuko, hati inakabili janga mojawapo la siku hizi, yaani kwamba wengi
wanakanusha uwepo wa Mungu au wanaishi bila ya kumjali. Mtaguso ulifikiria hasa
ukomunisti na misimamo mingine ya kupinga na kuzuia dini zote, lakini badala ya
kuilaani tu, umetuhimiza kujadiliana na kushirikiana nayo, pamoja na kutoa
ushuhuda wa maisha bora ya Kikristo, ukikiri kuwa pengine mifano yetu mibaya
ndiyo iliyosababisha wengi wakose imani. Mwisho inachorwa taswira ya Kristo, mtu
mpya, ambaye pekee yake anaangaza fumbo la binadamu pamoja na uchungu na kifo.
Sura ya pili inatupatia
mafundisho kuhusu jamii yanayozingatia mpango wa Mungu wa kuwa watu waishi kwa
ushirikiano. Kuukamilisha ushirikiano huo kwa msingi wa haki ni muhimu kuliko
maendeleo ya ufundi tu. Kwa ajili hiyo kila mtu awajibike kuhusu wenzake wote
bila ya kumsahau hata mmoja, akijifanya jirani wa wenye shida na kujitahidi
kustawisha usawa kwa kutumia nafasi yoyote aliyonayo katika jamii. Maadili ya
kibinafsi hayakubaliki, bali wajibu mkuu mmojawapo ni kujihusisha na ustawi wa
jamii na mshikamano ili wote kwa neema ya Kristo waishi kijamaa.
Sura ya tatu inatoa
msimamo kuhusu utendaji wa binadamu ulimwenguni. Hasa leo ambapo maendeleo ni ya
haraka tunajiuliza kuhusu maana ya juhudi zetu na namna ya kuziendeleza. Ni
hakika kuwa Mungu ametuagiza tufanye kazi na kutawala ulimwengu ili wote wapate
hali ya maisha wanayostahili walio sura yake. Wakristo wanapaswa kuwa mstari wa
mbele bila ya kudhani eti, Mungu anauonea kijicho ushindi wowote wa binadamu juu
ya maadui wake (ujinga, maradhi na ufukara). Kinyume chake ushindi huo
unatangaza ukuu wa Mungu aliyemuumba mtu akiwa na akili nyingi.
Lakini binadamu asisahau kuwa ubora wake hautokani na
wingi wa vitu anavyojipatia, bali unategemea tuni za kiadili anazostawisha kwa
kazi yake, hasa haki na udugu. Shida ni kwamba mara nyingi akishindwa na dhambi
anafuata ubinafsi au utaifa na kuanzisha miundo ya dhuluma na vita hata
kutengeneza silaha za kutosha kuangamizia uhai wowote duniani. Mbele ya hali
hiyo Wakristo wanapaswa kutofuata mitindo ya ulimwengu bali njia ya upendo nyuma
ya Kristo, wakiwa tayari kubeba msalaba wanaotwishwa wale wanaotafuta haki na
amani. Tumaini la uzima wa milele lisipunguze bidii yetu kwa maisha ya binadamu
wa leo, kwa kuwa huyo anaandaliwa hapa duniani kuingia katika ufalme wa mbinguni.
Katika utendaji wake mtu ana haki ya kufuata taratibu
za elimudunia , siasa n.k. Imani haiogopi kumuachia nafasi hiyo, kwa kuwa Mungu
yuleyule aliyejifunua kwetu kwa imani ameumba pia vitu vyote na kutujalia akili
na uvumbuzi. Mtaguso umelaumu mawazo finyu yanayogonganisha imani na sayansi.
Sura ya nne inaeleza
yatokanayo na zile zilizotangulia, yaani uhusiano wa Kanisa na ulimwengu. Kanisa
likiwa na lengo la milele, linaishi duniani na wanae ni pia raia wa nchi hii.
Hivyo linachangia ustawi wa binadamu pamoja na kupokea kwa shukrani misaada
mbalimbali ya walimwengu. Lina ujumbe kwa watu wote kuhusu wokovu, lakini pia
kuhusu maisha haya, hasa hadhi na haki za kila mtu. Kwa hiyo, ingawa utume wa
Kanisa ni wa kidini hasa, linashughulikia pia ustawi wa jamii na umoja wa
mataifa. Wakristo wasisahau tena majukumu yao ya kidunia, wala wasiyaone
hayahusiki na imani. Mojawapo kati ya makwazo makubwa zaidi ya nyakati zetu ni
utengano huo kati ya imani na maisha ya Wakristo wengi. Kwa namna ya pekee,
walei wanapaswa kushughulikia malimwengu yote kwa mfano wa Yesu huko Nazareti.
Wasisubiri kuagizwa na wachungaji wao, kwa kuwa kuratibu hayo ni kazi yao hasa.
Mtaguso umekiri tena ukosefu wa wanakanisa na kuwahimiza kujirekebisha wasije
wakazuie uenezaji wa Injili. Vilevile umeshukuru kwa juhudi za watu wowote kwa
ajili ya ustawi wa familia, utamaduni, uchumi, jamii, amani na mshikamano wa
kimataifa, hata ukakiri Kanisa limefaidika sana na upinzani na dhuluma za maadui
wake.
Baada ya kumaliza kueleza kwa jumla jinsi Kanisa
linavyohusika na wito wa binadamu, hati hii katika sehemu ya pili inakabili maswala kadhaa yaliyo muhimu zaidi kwa watu
wa leo.
Kati ya hayo sura
ya kwanza inafafanua kwanza hadhi ya ndoa na familia na namna ya kuzipa
nafasi za kufaa, kwa sababu mengine mengi yanategemea hali ya familia. Baada ya
kueleza utakatifu wa ndoa, kwa kuifananisha na hali ya kuwekwa wakfu kwa njia ya
sakramenti za kudumu, mtaguso umeonyesha ubora wa upendo kati ya mume na mke na
namna ya kuutekeleza, ukisisitiza unavyoelekea uzazi. Hivyo watu wa ndoa
wanapaswa kupanga kwa pamoja mbele ya Mungu na kwa kuzingatia mafundisho ya
Kanisa ili wazae kwa busara na ukarimu. Kwa namna ya pekee inasisitizwa kuwa ni
lazima uhai wa binadamu kisha kuanza ulindwe kwa bidii zote: kuua mimba au mtoto
ni maovu ya kutisha. Katika magumu yanayohusu uzazi wa mpango, wanandoa
wajitahidi kufuata usafi wa moyo unaowafaa. Hata jamii nzima inatakiwa kuchangia
ustawi wa familia: viongozi watunge sheria na kufanya mipango kwa ajili hiyo;
wanasayansi waendelee kutafuta njia halali za kupanga uzazi; mapadri wafanye juu
chini familia ziishe kwa utulivu.
Sura ya pili inafikiria
namna za kustawisha utamaduni, yaani zile namna maalumu ambazo binadamu
anakabili maisha katika mazingira na nyakati mbalimbali kulingana na orodha ya
tunu anazothamini. Tofauti na wanyama, yeye hawezi kufikia hali ya maisha ya
kumfaa kweli asipoyafanyia kazi mema yaliyoumbwa na Mungu ndani mwake na
kandokando yake. Kila kabila na kundi la watu lina utajiri wake ambamo binadamu
achote ili kujiendeleza na kuwaendeleza wenzake.
Lakini huu wa leo ni wakati mpya wa historia kwa
sababu ya mabadiliko ya haraka mno. Upande mmoja zimefunguliwa njia mpya za
kukuza na kueneza elimu na za kuunganisha aina tofauti za utamaduni. Upande
mwingine kuna hatari za kufuta hekima na sura maalumu za kila jamii, kuvuruga
mafungamano kati ya vizazi, kuacha elimu ya juu mikononi mwa wataalamu tu n.k.
Kufuatana na amri ya upendo Wakristo wanatakiwa
kuchangia na wenzao ujenzi wa ulimwengu ili wote waone vizuri kazi ya Mungu na
namna ya kuiendeleza. Kama vile yeye alivyotumia utamaduni wa watu ajifunue kwao,
ndivyo Kanisa pia lilivyofanya na linavyopaswa kufanya katika kueneza habari
njema. Lenyewe limetumwa kwa mataifa yote, hivyo halibanwi na utamaduni wowote,
bali linautumia na kuuchangia, linausafisha na kuuinua lisiishie ndani yake. Ni
wajibu wa wote kujitahidi kufuta ujinga kwa kueneza elimu hasa ya msingi ili
kila mtu aweze kuchangia zaidi ustawi wa jamii. Vilevile kila mtu aelewe wajibu
wa kujiendeleza kiutu na Kiroho bila ya kutawaliwa na kazi za mikono tu,
akitumia vitabu na vyombo vingine vya upashanaji habari, muda huru ulio nje ya
kazi n.k.
Sura ya tatu inafundisha
kuhusu maisha ya kiuchumi na ya kijamii ya mtu wa nyakati zetu. Ni lazima huyo
awekwe juu kabisa kuliko maendeleo ya vitu, kwa kuwa ndiye mtendaji, kiini na
lengo la uchumi na la jamii. Kumbe wengi wanazingatia sheria za uchumi tu ili
kutajirika iwezekanavyo. Matokeo ni kwamba mtengo kati ya mataifa, na kati ya
matabaka ndani ya nchi, unazidi kuwa mkubwa. Anasa za wachache zinaleta ufukara
wa kutisha wa umati hata kuhatarisha amani duniani.
Binadamu wa leo anaweza kurekebisha hali hiyo, lakini
yanahitajika mageuzi mengi katika mitazamo, mazoea na miundo pia. Hapo tu
ongezeko la uzalishaji litasaidia kweli, yaani litamsaidia mtu yeyote katika
mahitaji yake yote (ya mwili, ya nafsi na ya roho). Kwa ajili hiyo ni lazima
uchumi usiachwe uende zake wala usitawaliwe na wachache, bali wote waweze
kuuchangia ustawi na uongozi wake bila ya ubaguzi, wakisaidiwa kushika nafasi
yao hasa kwa njia ya ustadi. Kazi ya binadamu iheshimiwe kuliko mengine
yanayohusu uchumi (k.mf. mtaji au malighafi). Wote wana wajibu na haki ya
kufanya kazi na kujipatia hivyo riziki za kutosha. Vilevile wana haki ya kupata
muda kwa maisha ya kifamilia, hasa akina mama. Wafanyakazi ni haki yao kuchangia
uongozi wa kampuni, na vilevile kuunda vyama vya kutetea haki zao hata kwa
migomo.
Mojawapo kati ya mambo yaliyozingatiwa zaidi na
mtaguso ni njaa ya umati; kwa ajili hiyo umekumbusha kuwa Mungu ameumba vyote
kwa ajili ya wote, basi ni lazima mali zigawiwe kwa haki na upendo. Ingawa mtu
yeyote ana haki ya kumiliki vitu kadhaa, ni lazima kila mmoja awe na mali za
kutosha, wasiwepo wenye kujipatia mali nyingi kiasi cha kuacha wengine wakose
hata mahitaji. Matajiri wawajibike haraka kuwashirikisha wengine, la sivyo
watakuwa wauaji wa wenye njaa. Hao wa mwisho ni haki yao kujipatia riziki kutoka
utajiri wa wenzao. Kadiri ya mazingira tunaweza kuwa na njia mbalimbali za
kuhakikisha wote wapate riziki zao (desturi za ukarimu, pensheni n.k.). Mashamba
yagawiwe kwa wakulima wasiyonayo.Pesa zitumike ili kuandaa nafasi za kazi kwa
watu wa leo na wa kesho wa nchi zote (vitegauchumi). Wakristo watafute ufalme wa
Mungu hata katika uchumi na shughuli nyingine za kijamii.
Sura ya nne inafikiria
siasa ambayo pia siku hizi inapitia mageuzi makubwa. Mchango wa Kanisa ni
kutetea heshima ya kila mtu kwa kusisitiza kwamba lengo la siasa ni ustawi wa
jamii nzima kuanzia watu na familia. Uongozi unahitajika ili kulinganisha kwa
haki madai ya watu mbalimbali. Wananchi wote waelimishwe kuhusu siasa ili watoe
mchango wao kwa kutumia nafasi wanazopewa (kura n.k.) na kwa kutetea haki zao
bila ya kuwadai mno viongozi. Jamii na Kanisa vinawahudumia watu walewale lakini
kwa namna tofauti, hivyo havichanganyikani bali ni vema vishirikiane. Hata hivyo
Kanisa halifungamani na siasa yoyote, liweze kutangaza kwa uhuru maadili
yanayotakiwa hata katika siasa, likipima mambo yote na kuhimiza yaliyo mema.
Hatimaye, sura
ya tano inaongelea ujenzi wa amani na umoja kati ya mataifa. Wakati
ilipoandikwa ulikuwa wa mafadhaiko makubwa kuhusu dunia nzima kuja kuangamizwa
na wingi na ukali wa silaha zilizotengenezwa. Kwa msingi huo swala la vita
linatakiwa tulifikirie upya kabisa, tusiridhike na msimamo wa zamani kuhusu
masharti ya uhalali wake. Vilevile Wakristo wa madhehebu yoyote tuungane kati
yetu, tena na wote wenye mapenzi mema, katika kujenga amani na haki. Kwa kuwa
amani ya kweli sio tu kusimama kwa vita, labda kwa hofu tu ya silaha
zilizolundikana; amani ni tunda la haki ambayo itafutwe mfululizo kwa bidii,
tena ni tunda la upendo ule wenye msingi ndani ya Mungu. Kuhusu vita
vinavyoendelea huku na huku, kwanza ukatili wake upunguzwe (kumbe siku hizi
umezidi kwa sababu ya silaha mpya, mashambulizi ya raia, uangamizaji wa kabila
zima n.k.). Utiifu kwa maagizo hauwezi kuwa kisingizio cha kutenda maovu, bali
ni wajibu kuyakataa. Mapatano ya kimataifa kuhusu vita yaheshimiwe na wote. Ni
wajibu wa viongozi wa nchi kuzilinda hata kijeshi, lakini wasitumie jeshi ili
kugandamiza wengine. Pia waheshimu dhamiri ya wasiojisikia kutumia silaha.
Vitendo vinavyowezekana leo vya kuangamiza miji mizima au maeneo mapana pamoja
na wote waliopo ni makosa ya jinai yasiyovumilika. Wanaotengeneza au kununua
silaha ili kujikinga na maadui wasije wakashambuliwa, wafikirie hatari ya silaha
hizo kuja kutumika kweli, tena hasara ya maskini wanaokosa misaada wanayostahili
kwa sababu tu pesa nyingi sana zinatumika kwa silaha. Tutafute mapema njia za
upatanisho na muundo wa kimataifa wenye uwezo wa kudumisha amani na haki kwa
wote. Hapo katikati akiba za silaha zipunguzwe kwa mpango wa pamoja. Viongozi na
watu wao waache utaifa na misimamo yo yote inayotenganisha watu. Hasa malezi ya
vijana na upashanaji habari vieneze mawazo ya amani na mitazamo mipana yenye
faida kwa binadamu wote. La sivyo tutafikia tu ile amani ya kutisha
itakayopatikana kwa kufa wote. Kanisa likisema hivi haliachi kutumaini na
kuhimiza wongofu wa mioyo.
Kuhusu kujenga umoja kati ya mataifa, mara nyingi
misingi ya kutoelewana ni hali tofauti mno za uchumi, nia ya kutawala, dharau ya
wengine na vilema mbalimbali. Basi, ushirikiano mkubwa unaowezekana leo uwe njia
ya kutatua matatizo hayo na kukidhi mahitaji ya watu, hasa maskini. Miundo ya
kimataifa iliyopo iwajibike kuzingatia zaidi nchi zinazoendelea, wakimbizi na
wengine wenye shida maalumu.
Ingawa miaka ileile ya mtaguso nchi nyingi zilipata
uhuru wa kisiasa, hali ya uchumi inazirudisha chini ya ukoloni wa namna mpya.
Basi, mshikamano uendeleze kweli nchi hizo. Lakini maendeleo yanategemea watu
kuliko pesa, kwa hiyo kazi ya kwanza ni kuandaa raia wa nchi maskini kwa elimu
na ufundi. Inahitajika misaada, mikopo na vitegauchumi tena kwa ukarimu, lakini
pia kurekebisha sana sheria za uchumi wa kimataifa. Upande wao viongozi wa nchi
maskini wapokee misaada hiyo kwa uaminifu, na raia wao wajitahidi kutumia vile
vyote walivyo navyo. Maendeleo ya uchumi yasitusahaulishe roho ya binadamu, kwa
kuwa huyo haishi kwa mkate tu.
Wengi leo wanafadhaishwa na kasi ya ongezeko la watu.
Utatuzi wa kwanza ni kuleta usawa mkubwa zaidi kati ya watu na kueneza ujuzi
kuhusu kilimo n.k. Halafu zitungwe sheria zinazosaidia familia, izuiwe kasi ya
watu kuhamia mijini, watu waelimishwe kwa ukweli kuhusu hali ya nchi na uzazi wa
mpango. Wote wajiepushe na njia za mkato zinazokwenda kinyume cha maadili na cha
haki ya msingi ya wananchi kufunga ndoa na kuzaa wanavyoona vema wenyewe. Basi,
wasaidiwe kuunda dhamiri na kujifunza njia halali za kupanga uzazi.
Wakristo wawe mstari wa mbele katika mshikamano wa
kimataifa, wakijua Yesu katika maskini analia na kudai upendo. Mtaguso uliita
kikwazo kuona nchi za Kikristo zikitapanya mali, wakati nyingine zinalemewa na
njaa, maradhi n.k. Wakristo wajitolee kuhamia kwenye shida ili kusaidia kwa hali
na mali wakishirikiana na miundo na watu wowote, kwa kuwa tunaye Baba mmoja na
tunapaswa kuishi wote kidugu. Hapo watatambulikana kama wafuasi halisi wa Kristo.
Tukikumbuka kuwa hatutaingia mbinguni kwa kusema tu, Bwana, Bwana, bali kwa
kutimiza mapenzi ya Baba, tukabili kazi hiyo kubwa ambayo tutahukumiwa siku ya
mwisho kwa jinsi tulivyoifanya.
INTER
MIRIFICA
Hati hiyo ilitolewa na mtaguso mapema ili kukabili
jambo ambalo siku hizi ni zito sana kwa jinsi linavyochangia maisha na utamaduni
wa watu duniani kote, yaani vyombo vya upashanaji habari. Hivyo vimeendelea hasa
katika karne ya XX na kuwafikia karibu watu wote vikieneza habari, mawazo,
maadili n.k. Kanisa linavipokea kwa shukrani kwa Mungu aliyempa binadamu akili
ya kuvumbua na kubuni njia hizo zinazoweza kumuinua hata kidini. Lakini kwa
ubaya wa moyo wake anaweza pia kuzitumia kwa uharibifu wake na wa wengine wengi,
hasa watoto na vijana wasio na kinga. Kwa hiyo Kanisa linapaswa kushughulika ili
vyombo hivyo vyote vitumike vema kwa kueneza habari njema, maadili na taarifa za
kweli ili watu wakabili maisha vizuri na kuokoka. Pia liwaelimishe wote kuhusu
namna ya kuchuja na kutumia vilivyo magazeti, vitabu, filamu, redio, televisheni
n.k., wakielewa urahisi wa kudanganywa na kupotoshwa na vyombo hivyo. Hiyo ni
kazi ya wachungaji, wazazi na walezi, lakini serikali pia isaidie kutunza
mazingira safi. Mtaguso umeagiza shughuli hizo ziratibiwe kijimbo, kitaifa hata
kimataifa. Kwa kuwa shughuli hizo zina gharama kubwa, Wakristo wanahimizwa
kujitolea kwa ukarimu hasa Jumapili maalumu moja kwa mwaka.
ORIENTALIUM
ECCLESIARUM
Mtaguso ulizingatia hali duni ya Makanisa Katoliki ya
Mashariki ukaamua kuirekebisha. Kwanza ulitamka kuwa yanastahili kuheshimiwa
sana pamoja na mambo yote (liturujia, teolojia, sheria, miundo n.k.) kama sehemu
ya hazina ya Kimungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Liturujia zitunzwe kiaminifu na
kurekebishwa kama zimeachana na mapokeo ya Mashariki, hasa sakramenti zirudi
kufuata taratibu asili. Mashirika ya Kilatini yajitahidi kuanzisha jumuia za
Mashariki. Madhehebu yoyote ya Kikatoliki yana haki na wajibu sawa hata kuhusu
uenezaji Injili duniani kote. Wachungaji wa hayo yote wazoee kushirikiana, na
wanaojiandaa kupata upadri waelimishwe juu ya uhusiano kati ya madhehebu hayo.
Waamini wa Mashariki wapatiwe mapadri na maaskofu wao popote wanapohitaji.
Waortodoksi wakijiunga na Kanisa Katoliki waendelee kufuata madhehebu yao, na
wenye daraja kati yao waendelee kuitumia. Kutokana na umuhimu wa patriarki kwao,
hadhi na haki zake zirudishwe kama kabla ya utengano na Waortodoksi, na Makanisa
yasiyo naye yafikiriwe. Hatimaye hati hiyo inahimiza Wakatoliki wa Mashariki
kushughulikia ekumeni hasa upande wa Waortodoksi, ikiruhusu kutoleana nao
sakramenti kadhaa na mengineyo.
UNITATIS
REDINTEGRATIO
Kurudisha umoja kati ya Wakristo wote ni lengo kuu
mojawapo la mtaguso. Matengano yaliyokata vipandevipande mwili wa Kristo ni
kinyume cha matakwa yake na yanakwaza ulimwengu usiweze kuamini. Siku hizi Mungu
ametuhurumia na kututia hamu ya umoja hata ukatokea mfumo wa ekumeni. Kwa hati
hiyo Kanisa Katoliki linawajibika kushirikiana na madhehebu yoyote ya Kikristo
lisije likazuia kazi hiyo ya Roho Mtakatifu.
Sura ya kwanza inaeleza
msimamo wa Kikatoliki kuhusu ekumeni. Imani yetu ni kwamba Kanisa ni moja tu,
nalo limekabidhiwa kwa waandamizi wa mitume chini ya waandamizi wa Petro.
Tunakiri kuwa mafarakano yaliyotokea kati ya Wakristo yalisababishwa na makosa
ya pande zote. Waliolelewa Kikristo nje ya Kanisa Katoliki hawawezi kulaumiwa,
tena ni Wakristo halisi na ndugu zetu, ingawa ushirika wetu si kamili.
Tuwaheshimu pamoja na mema yao mengi ambayo yanatokana na Mungu na kuelekea
ujenzi wa Kanisa. Makanisa yao au jumuia zao vinatumiwa na Mungu kama vyombo vya
wokovu, ila katika Kanisa Katoliki tu unapatikana ukweli mzima na vifaa vyote
vya wokovu. Hata hivyo tunakiri kwamba hatutumii vizuri neema hizo hata
tunawakwaza wenzetu; basi, tunapaswa kulenga ukamilifu wa Kikristo ili Kanisa
ling’ae mbele ya wote. Mbali ya matendo ya kupendana ni muhimu pia majadiliano
ya kiteolojia na mikutano ya sala ya pamoja.
Sura ya pili
inaeleza utekelezaji ikisisitiza kuwa unawapasa waamini wote, kwa njia ya
kurekebisha Kanisa, kuongoka, kusali, kushirikishana sakramenti, kufahamiana,
kueleza imani kwa usahihi na bila ya kudharau madhehebu mengine, kushirikiana
katika kutetea haki na amani na kuleta maendeleo.
Sura ya tatu
inaeleza kifupi historia ya mafarakano kwa kutofautiana sana yale yanayohusu
Waortodoksi na yanayohusu Waprotestanti, hasa kutokana na makundi hayo mawili
kuwa au kutokuwa na daraja halisi na hivyo kuwa au kutokuwa na ekaristi. Kwa
msingi huo yanastahili kuitwa Makanisa au jumuia za Kikanisa tu. Uhusiano wetu
na makundi hayo ni tofauti, na uwezekano wa kushirikiana katika sakramenti ni
mkubwa kwa Waortodoksi bali ni mdogo kwa Waprotestanti.
Mwishoni hati hii inakiri kuwa ekumeni inapita uwezo
wetu, kwa hiyo tegemeo lote ni katika sala ya Yesu kwa Kanisa, katika upendo wa
Baba na katika uwezo wa Roho Mtakatifu.
CHRISTUS
DOMINUS
Mtaguso, baada ya kufundisha wazi juu ya daraja ya
maaskofu, ulitunga hati nyingine kuhusu utendaji wao katika ngazi tatu: Kanisa
zima, Makanisa maalumu na ujirani mwema wa majimbo.
Kwanza
askofu yeyote ni kiungo cha kundi la maaskofu ambalo linaongozwa na askofu wa
Roma na kuwajibika kulichunga Kanisa zima. Wajibu huo unatimizwa kwa kushiriki
mtaguso mkuu, ambako ni haki ya maaskofu wote, kuchangia muundo mpya wa sinodi
ya maaskofu, kushughulikia kwa hali na mali misheni na majimbo yasiyo na mapadri
au mali za kutosha, kuwaombea maaskofu wafungwa na wanaodhulumiwa, kuchangia
katika ofisi za papa.
Pili,
ni wajibu wa baadhi ya maaskofu kuchunga kwa jina la Bwana sehemu fulani ya
taifa la Mungu wakitimiza kazi za kufundisha, kutakasa na kuongoza kama
wachungaji halisi, ingawa wanapaswa kuheshimu mamlaka ya papa, patriarki na
maaskofu wakuu. Chini ya askofu wake jimbo ni Kanisa maalumu ambamo Kanisa pekee
linaishi na kutenda. Hati hiyo inaelekeza namna ya kutimiza wajibu huo (pamoja
na kuagiza utungwe mwongozo maalumu ambao ufafanue zaidi), inaagiza mipaka ya
majimbo irekebishwe yasiwe makubwa mno wala madogo mno, na inaratibu uhusiano na
maaskofu waandamizi na wasaidizi, nafasi ya makamu na halmashauri za askofu,
uhusiano na maparoko na mapadri wengine. Swala lingine gumu ni uhusiano na
watawa hasa walio mapadri, ambao wamehimizwa sana kuishi kweli kama viungo vya
jimbo na kujihusisha na maendeleo yake ya Kiroho na ya kitume kwa kushirikiana
na askofu, mapadri na walei pamoja na watawa wengine. Pia maaskofu wazee au
wenye shida nyingine wanahimizwa kujiuzulu.
Tatu, maaskofu
wanahimizwa kuchangia ustawi wa Kanisa katika maeneo yao kupitia sinodi,
mitaguso ya kanda au ya nchi, mabaraza ya maaskofu, ushirikiano katika kanda,
pia na maaskofu waliopewa kazi tofauti na jimbo (k.mf. uchungaji wa askari wote
wa nchi yao).
Maagizo yote ya hati hiyo yalikusudiwa kuongoza
marekebisho ya sheria za Kanisa.
PERFECTAE
CARITATIS
Siku hiyohiyo iliyotolewa hati kuhusu uchungaji wa
maaskofu ilitolewa nyingine kuhusu kurekebisha upya maisha ya kitawa, nayo pia
msingi wake ni hati Lumen Gentium juu ya Kanisa ambamo watawa wana nafasi yao (sura
ya sita). Mtaguso ulitaja marekebisho makuu tu ya kufanywa, ukimuachia papa
atunge sheria hapo baadaye. Hasa ulisisitiza hali mpya ya utawa inayotakiwa
kutokana na mambo matano: kushika Injili kama kanuni kuu, kufuata kiaminifu
karama ya mwanzilishi na mapokeo bora ya shirika, kujihusisha na maisha na
malengo yote ya Kanisa, kupima hali na mazingira ya watu wa leo, kuweka mbele
maisha ya Kiroho kuliko mipango mingine. Ili kuzingatia hayo yote, sheria za
watawa zirekebishwe kwa kuwahusisha wanashirika wote.
Kabla ya kueleza juu ya aina mbalimbali za utawa,
hati hiyo inasisitiza mambo kadhaa yaliyo sawa kwa zote: kushika mashauri ya
Kiinjili, kujikatalia ulimwengu, kuwekwa wakfu kwa Mungu juu ya msingi wa
ubatizo, kulitumikia Kanisa, kutekeleza maadili, kumfuata Kristo kwa bidii kama
jambo pekee la lazima, kuunganisha sala hasa na moyo wa kitume. Nafasi ya kwanza
inayo maisha ya Kiroho yaliyo chemchemi ya upendo unaohuisha hata utekelezaji wa
mashauri ya Kiinjili. Watawa katika kulisha maisha ya sala wazingatie kila siku
Maandiko matakatifu halafu liturujia.
Katika kutofautisha aina za utawa, kwanza yanatajwa
mashirika yanayoshughulikia sala tu katika upweke na kimya; baadaye yanatajwa
mashirika yale mengi yaliyoanzishwa waitimize huduma maalumu kwa niaba ya Kanisa
na kama sehemu ya maisha yao ya kitawa; mwishoni yanatajwa mashirika
yanayotakiwa kuunganisha kiaminifu ratiba ya sala na taratibu nyingine za
kijumuia pamoja na utume fulani.
Halafu hati inaongelea maisha ya kitawa ya mabradha
na masista, ikisisitiza kuwa ni muhimu yalivyo, bila ya kuhitaji yakamilishwe na
daraja takatifu. Vilevile inasisitiza sura ya mashirika ya kilimwengu
yanayopaswa kutafuta utakatifu kwa kuishi katika mazingira ya watu wa kawaida:
kwa ajili hiyo yanahitajika malezi bora.
Baadaye hati inarudi kufafanua mambo yanayowahusu
watawa wowote, hasa mashauri makuu matatu ya Kiinjili, ikitanguliza useja kwa
kuwa ndio msingi hasa wa kubainisha waliowekwa wakfu kwa Mungu na kwa ufalme
wake kwa namna ya pekee. Hati inaonyesha ubora wa useja na njia za kuushika
sawasawa baada ya jaribio la kutosha. Halafu inasisitiza ufukara kama ushahidi
unaothaminiwa sana siku hizi: basi, usiwe wa kiroho tu au wa binafsi tu, bali
uonekane wazi katika maisha ya jumuia pia. Kuhusu utiifu umesisitizwa ukuu wa
sadaka hiyo ambayo mtawa anaungana kwa hakika na matakwa ya Mungu kwa mfano wa
Yesu. Pamoja na hayo ajitahidi kutoa mchango wake na kuwajibika chini ya
viongozi kama mtu aliyekomaa. Upande wao viongozi wasitawale kwa mabavu bali
waonyeshe upendo wa Mungu kwa mtawa, wakimheshimu na kumsikiliza na kumuachia
nafasi ingawa wana haki na wajibu wa kumuagiza la kufanya. Pia mikutano na
halmashauri vishiriki katika uongozi.
Sifa nyingine ya mashirika ya kitawa ni maisha ya
pamoja ambayo yamesisitizwa upya kwa kutia maanani misingi yake na utekelezaji
wa upendo kamili katika ushirika wa kidugu. Kwa lengo hilo tunakuta himizo la
kufuta matabaka kati ya masista na la kushirikisha zaidi mabradha katika maisha
ya jumuia, pamoja na kibali cha kuleta usawa kati ya wanashirika makleri na
walei.
Katika kulinda utawa toka zamani unatumika ugo, ambao
kwa baadhi ya watawa wa kike unafuata sheria za papa. Hati hii inadai hizo
zirekebishwe, halafu zisibane wale wanaofanya utume fulani. Kinga nyingine ya
watawa ni nguo maalumu. Kwa mara ya kwanza katika historia mtaguso uliongelea
swala hilo na kulitia maanani kama alama ya kuwekwa wakfu, pamoja na kuagiza
baadhi zibadilishwe.
Upande wa malezi hati hii imeyasisitiza sana kama
msingi wa urekebisho, ikikataza watawa wasitumwe kufanya shughuli mara baada ya
unovisi, bali waendelee kuundwa katika nyumba maalumu. Halafu malezi yaendelee
maisha yote kwa ushirikiano wa watawa na viongozi wao, ambao wajitahidi hasa
kuandaa walezi wa kufaa.
Zinafuata taratibu kuhusu kuunda mashirika mapya,
halafu kuhusu kueneza aina mbalimbali za utawa katika Makanisa machanga kwa
kuzingatia utambuzi na utamadunisho. Mashirika yaendelee kutimiza shughuli zake
maalumu kulingana na karama na nyakati pamoja na kustawisha moyo wa kimisionari.
Yale yasiyostawi yakatazwe yasipokee tena wanovisi au yaunganishwe na lingine la
kufanana nayo. Tofauti na muungano, mtaguso umependekeza pia shirikisho la
monasteri au mashirika ya familia moja ya kiroho, vyama vya mashirika yenye kazi
ileile, mabaraza ya wakuu wa mashirika yote ya nchi au jimbo fulani ili
kurahisisha ushirikiano kati ya watawa, tena kati yao na maaskofu.
Swala la mwisho ni namna ya kupata miito ya kitawa:
hiyo ni kazi ya Kanisa lote, kuanzia mapadri, wazazi na walezi. Mashirika
yenyewe yanaweza kujitafutia miito kwa kufuata taratibu za Kanisa, lakini njia
bora ni kutoa mfano mzuri. Hatimaye watawa wote wanahimizwa kuitikia upya wito
wao.
OPTATAM
TOTIUS
Siku hiyohiyo ilitolewa hati nyingine tena inayohusu
malezi ya kipadri: toka mwanzo hayo yanatiwa maanani sana kwa kusema urekebisho
unaotumainiwa wa Kanisa lote unategemea kwa kiasi kikubwa upadri ukitimizwa kwa
roho ya Kristo. Kuhusu jambo hilo mtaguso ulikusudia kulinganisha mang’amuzi
ya karne zilizopita na mahitaji mapya. Kwa kuwa malezi yanapaswa kuwa tofauti
kwa kila mtu na kila aina ya watu, basi maagizo ya hati hiyo yanayolenga kulinda
umoja wa upadri, yatekelezwe kwa namna tofauti kadiri ya mazingira, madhehebu na
aina ya upadri (watawa, wanajimbo waseja na wenye ndoa).
Kwanza jumuia nzima inapaswa kuwajibika kwa malezi ya
vijana na ustawi wa miito hasa kwa njia ya sala. Wakurugenzi wa miito
wasishindanie vijana, bali tujifunze wote kuwa na mtazamo wa Kikanisa na wa
kimataifa. Njia ya kawaida ya kuotesha mbegu za miito ni seminari ndogo. Hizo si
za lazima, kinyume na seminari kuu ambapo malezi yote yanalenga upadri moja kwa
moja. Walezi wachaguliwe kati ya mapadri bora, kwa kuwa malezi yanawategemea
hasa wao. Waseminari waendelee kuchambuliwa kwa imani ya kwamba Mungu hatakubali
Kanisa likose wahudumu ikiwa wasiofaa wanaelekezwa kwingine. Namba nyingine
zinahusu malezi ya kiroho, upendo kwa Kanisa, malezi ya kijinsia, ukomavu wa
kibinadamu na uwezekano wa marekebisho ya sheria. Yanafuata maagizo kuhusu
masomo yenyewe ambayo moyo wake uwe ni Biblia, na masomo ya juu. Pia
inasisitizwa kuwa masomo na malezi hayo yote yanalenga uchungaji katika nyanja
zote.
APOSTOLICAM
ACTUOSITATEM
Mtaguso uliwaongelea walei katika hati mbalimbali
ukionyesha nafasi yao katika maisha ya Kanisa (liturujia, upashanaji habari,
ekumeni n.k.). hata hivyo uliona umuhimu wa kuwaandikia hati maalumu iwaongoze
hasa katika utume ili watimize wajibu wao kwa wokovu wa ulimwengu. Karibu
waamini wote ni walei, tena ndio wanaoshirikiana zaidi na watu wowote katika
yote: hivyo wasipotoa mchango wao, utume wa Kanisa utakuwa mlemavu, hasa siku
hizi. Si kwamba wanapaswa kufanya utume kutokana na upungufu wa mapadri na
watawa, bali kutokana na wito walioupata katika ubatizo na kipaimara.
Sura ya kwanza inaeleza wito