Morogoro: cappella maschile - Morogoro: kikanisa chajumuia ya kiume - Morogoro: the chapel of the brothers

Home Karama Historia Maisha na utendaji Katiba Safari ya Malezi Maktaba Pepe

SAFARI YA MALEZI

ya Utawa wa Ndugu Wadogo wa Afrika

 

 

 

YALIYOMO

 

 

0. UTANGULIZI

 

1. KUSHIKA INJILI

 

2. KUENEZA INJILI

 

3. WATENDAJI

 

4. UTU NA UKRISTO

 

5. HATUA ZA KUINGIZWA

 

6. MALEZI YA KUDUMU

 

7. HATIMA: MAMA MARIA

 

 

 

 

 

0.    UTANGULIZI

 

0.1.           AINA ZA UFUASI

 

Yesu, Mwana wa Baba, ndiye ukombozi na ukamilifu wetu.

Kadiri ya matakwa ya Baba na kwa msukumo ya Roho Mtakatifu, kila wakati wanapatikana waamini ambao wanamfuata Yesu na kushuhudia fumbo lake kwa namna mbalimbali, hasa: walei kwa kuratibu malimwengu, wenye daraja kwa kutoa huduma walizokabidhiwa mitume, na wanaoshika mashauri ya Kiinjili kwa kufanana zaidi na Yesu safi, fukara na mtiifu ili wote watambue kuwa kweli yu pamoja nasi hata mwisho wa dunia.

 

 

0.2.           KARAMA YETU

 

Mungu Baba ametujalia tuanzishe chama cha kimisionari chenye jamaa mbalimbali ndani yake, ambamo tufuate nyayo za Mwanae katika kujishusha mfululizo ili kutumikia kwa upendo hata kufa msalabani.

Sisi sote wanachama tuishi kati ya watu wa nyakati zetu tukiwa na msimamo huohuo aliokuwanao yeye, ingawa kila mmojawetu kadiri ya hali maalumu aliyonayo ndani ya Kanisa, kama mlei, kleri au mshikamashauri ya Kiinjili.

Tarajio la chama ni kujaliwa kwa wingi mashahidi wa imani ambao wamelishwa sana Injili hata waweze kuishi kama ndugu wadogo wa wote, tena kwa namna bora zaidi na zaidi, katika mazingira mbalimbali watakayopangiwa.

 

 

0.3.           SAFARI HII

 

Kwa ajili hiyo yanahitajika malezi ambayo yafuate maelekezo ya Kanisa na kulingana na karama yetu maalumu, tusiisawazishe na miito mingine tusije tukamzimisha Roho Mtakatifu na kulidhoofisha taifa la Mungu.

Malezi hayana mwisho kamwe: ingawa kuna hatua za kupigwa, ni mtiririko mmoja tu wa ustawishaji wa maadili n.k.

Ulinganifu wa malezi ya Kiroho, ya kitume, ya kielimu na ya kiufundi utusaidie tangu tunuie kukomaa ndani ya Kristo mpaka tukutane naye moja kwa moja kwa kupokea ndugu kifo.

 

 

0.4.           MIONGOZO MAALUMU

 

Mpango huu unakusudiwa kuonyesha wazi namna ya kuchochea karama yetu.

Upande mmoja utuonyeshe namna ya kuitekeleza katika hatua mbalimbali za maisha hadi kufikia utakatifu.

Upande mwingine utuonyeshe namna ya kuishirikisha kikamilifu kwa vizazi vijavyo viweze kuitimiza katika utamaduni wowote, kwa kuwa Ufransisko unafaa kuutakasa na kuuboresha kila utamaduni kwa chumvi na chachu ya Injili, bila ya kukwama katika wowote ule.

Lakini malezi hayawezi kupangwa jumla tu, pasipo kuzingatia wahusika ni wepi na wanaishi wapi: kwa hiyo mpango huu utimilizwe na halmashauri kuu kwa kila jamaa, hatua na nyumba.

Miongozo yake hiyo iwe sahili, mifupi na wazi, ilingane na mpango huu halafu ipitiwe kwa marekebisho kila baada ya miaka mitatu.

 

 

 

 

1. KUSHIKA INJILI

 

1.1.           UTATU NA UTAWA

 

Karama yoyote ya kitawa inaongoza kwa Baba, ikitia hamu ya kutimiza matakwa yake yote: humo utiifu unazaa uhuru wa kweli, useja mtakatifu unatokeza jinsi moyo usivyoweza kutosheka na upendo wa viumbe, na ufukara unachochea njaa ya haki aliyoahidi kuishibisha.

Halafu inaongoza kwa Mwana, ikirahisisha ushirika wa ndani naye, katika kuwatumikia kwa bidii Mungu na watu, na katika kusali na kuteseka ili kueneza ufalme.

Hatimaye inaongoza kwa Roho Mtakatifu, ikiandaa kujiachia kwake na kutegemezwa naye katika maisha ya Kiroho, ushirika wa kidugu na utume.

 

 

1.2.           KARAMA ZA KITAWA

 

Namna mbalimbali za kuishi kitawa zinatokana na karama maalumu ambazo waanzilishi walijaliwa na ambazo wafuasi wao wakashirikishwa ili wazitekeleze, wazitunze, wazichimbe na kuziendeleza mfululizo kulingana na ustawi wa Mwili wote wa Kristo.

Kanisa linataka kila utawa ustawi kadiri ya karama hai na bunifu ya mwanzilishi, kufuatana na mapokeo yake maalumu ya Kiroho, ya kijumuia na ya kitume.

Hivyo sio tu kwamba tuna historia tukufu ya kuikumbuka na kuisimulia, bali pia tunayo nyingine ya kuitimiza bado ili katika milenia mpya ulimwengu uliokabidhiwa mikononi mwetu binadamu uwe na imani na upendo, haki na amani zaidi, uwe kama utangulizi wa ulimwengu ujao.

Roho anatusukuma tukafanye makuu, hivyo tuitazame kesho kwa tumaini.

 

 

1.3.           UTAWA NA NYAKATI ZETU

 

Tumeitwa tutambue na kuhudumia mpango wa Mungu kwa ajili ya watu, ambao unatangazwa na Maandiko Matakatifu na kujitokeza katika maisha yao.

Kwa hiyo tuwe tayari kuchochewa na Neno la Mungu na ishara za nyakati, tukiunganisha daima upya wa Kiroho na ari ya kitume, ambavyo cha kwanza kinawezesha cha pili.

Tumshiriki Mungu ili kukabili changamoto za nyakati zetu, tukiamini ya kuwa Roho anaweza kutoa majibu ya kufaa hata kwa zile ngumu zaidi.

Mbele ya changamoto kuu tatu za ulimwengu tuonyeshe jinsi mashauri ya Kiinjili yanavyotustawisha kwa kutuelekeza moja kwa moja kwa Mungu aliye Wema mkuu, badala ya kufuata mielekeo ya kibinadamu iliyoathiriwa na dhambi.

Hasa siku hizi wanahitajika watakatifu ambao watumainishe wale waliokata tamaa kuhusu maisha na maana yake: ubora wa utawa unaweza kuwatuliza wale wanaoona kiu ya tunu halisi.

 

 

1.4.           USEJA MTAKATIFU NA UTAMADUNI WA ANASA

 

Changamoto ya kwanza ni utamaduni wa anasa unaoona jinsia ni mchezo tu usio na masharti: matokeo ni maovu ya kila aina yanayoathiri kinafsi na kiuchumi jamii, familia na watu mmojammoja, kuanzia watoto.

Itikio la maisha ya wakfu ni kuishi useja mtakatifu kwa furaha, na hivyo kushuhudia uwezo wa Mungu unaofanya kazi katika udhaifu wa binadamu hata akampenda yeye kuliko yote na kumpenda yeyote kwa uhuru wa wanae.

Ushuhuda huo unahitajiwa na wote kadiri wanavyoshindwa kuuelewa, ili wajifunze kuwa wa kweli katika mafungamano.

Mapendo yao ya kibinadamu yanapewa kielelezo cha yale safi ya mtawa ambaye anachota katika Mungu-Upendo: kwa kuzama katika fumbo la Utatu anajisikia apende wote pasipo mipaka na kwa kujitawala.

Hakika, usafi unaukomboa moyo kwa namna ya pekee na kuzidi kuuwasha upendo kwa Mungu na kwa watu wote.

Mchango mmojawapo mkubwa wa mtawa ni kuonyesha kwa maisha yake uwezekano wa kujitoa kwa wengine na kushiriki furaha na huzuni zao kwa uaminifu na udumifu, pasipo vitendo vya jinsia wala misimamo ya utawala na ubaguzi.

Pia utawa unamaanisha na kuelekea moja kwa moja uzima wa milele, hasa kwa njia ya useja unaotugeuza tayari kwa ajili ya ulimwengu ule ambapo watu hawaoi wala hawaolewi.

 

 

1.5.           KUZINGATIA TUNU NA GHARAMA YAKE

 

Kwa kuwa useja huo unadai usafi kamili na kuyahusu sana maelekeo yetu ya dhati, wanazoezi wasiuahidi wala wasikubalike kabla ya kujaribu vya kutosha na kufikia ukomavu wa kufaa upande wa nafsi na wa hisi za moyo.

Watambue kwamba elekeo la umimi tulilonalo linataka tutie maanani mno mapendo ya kibinadamu, na kumtumia mwenzetu kama njia ya kujipata heri fulani.

Lakini wasiangalishwe tu kuhusu hatari zinazowakabili, bali walelewe kukumbatia useja kwa ajili ya ufalme wa Mungu, kama tunu kwa ustawi wao na wa Kanisa.

 

 

1.6.           MALEZI YA USEJA

 

Malezi ya useja mtakatifu yajitahidi:

- kuchochea furaha na shukrani kwa upendo ule ambao kila mmoja ametazamwa na kuteuliwa na Yesu;

- kuangazia matunda ya moyo usiogawanyika, yaani uzazi mwingi wa Kiroho hasa katika utume;

- kuhimiza adhimisho la upatanisho, uongozi wa Kiroho na upendo halisi katika jumuia;

- kujenga hali ya kuaminiana kati ya walelewa na mlezi, ambaye awe tayari kusikiliza yoyote kwa upendo ili aangaze na kutegemeza;

- kumsaidia kila mmoja akubali mang'amuzi yake mabaya ya zamani kwa kutambua udhaifu, kujinyenyekeza na kukesha;

- kumshukuru Mungu tu na kuzuia kiburi cha kujipongeza kwa usafi, usije ukazua ugumu wa moyo;

- kufundisha juu ya jinsia mbili upande wa mwili, nafsi na roho;

- kueleza maana ya mwili na namna ya kutunza afya yake;

- kuelekeza kujitawala upande wa ashiki na wa moyo, na vilevile upande wa ulafi na ulevi;

- kuwa waangalifu katika kutumia vyombo vya upashanaji habari na katika mafungamano na watu (busara inawadai watumishi, walinzi na walezi pia wachukue hatua za kufaa).

 

 

1.7.           UFUKARA NA UTAMADUNI WA FEDHA

 

Changamoto ya pili inatokana na ulimwengu kuabudu pesa na mali, kwa kutoelewa maana yake kwa maisha, wala kufuata kiasi kinachofaa, wala kujali mahitaji na mateso ya wanyonge, wala kuhifadhi mazingira kwa ajili ya wajukuu wetu.

Hivyo leo ufukara unatawala maisha ya watu wengi na ya nchi nyingi kwa sababu ulimwengu unaendeshwa namna inayozidisha hali ya njaa, ujinga, maradhi, kukosa kazi, kunyimwa haki za msingi, ukoloni mamboleo, rushwa n.k.

Itikio la maisha ya wakfu ni ufukara wa Kiinjili ambao upendo unahimiza kupokea mlio wa wenye mashaka katika matatizo, mateso na matarajio yao ili kuwasaidia wakabili maisha kwa mshikamano wa wote.

 

 

1.8.           YESU NA UFUKARA

 

Asili ya ufukara huo wa Kiinjili ni kutafakari alivyoishi Yesu fukara msulubiwa; udhihirisho wake ni kushika maisha ya kawaida ya watu wadogo kuhusu chakula, mavazi na nyumba, na kukwepa uwezo wowote wa kutawala wengine kisiasa, kijamii, kiuchumi, kielimu na kidini.

Moyo wa maskini tu ulioamua kumfuata Yesu hivyo unaweza kushikamana na watu usiambatane na vitu.

Jumuia ndogo za kitawa katika mazingira duni zinatokeza ule upendeleo wa Kiinjili kwa fukara, unaotufanya sio tu tuwashughulikie, bali tuishi pamoja nao, tena sawa nao kadiri inavyofaa kulingana na hali halisi na mahitaji ya kila mmojawetu, hasa akiwa bado katika hatua za kuingizwa.

Upendeleo huo unatokana na upendo ambao Yesu aliuishi, hivi kwamba kila mfuasi wake anapaswa kuwa nao, hasa sisi tunaomfuata kwa karibu zaidi katika maisha ya wakfu, ambayo ni ya kifukara na ya kuwatetea fukara.

Mshikamano nao ndio msimamo unaotufanya ndugu wadogo, ni mhuri wa Ukristo halisi, kichocheo cha wongofu, tendo la kitume na thibitisho la ujio wa ufalme wa Mungu, ambapo fukara wanahubiriwa na kuhubiri Injili.

Zaidi ya hayo ufukara wenyewe ni tunu iliyotangazwa na maisha yote ya Yesu kama heri ya kwanza na ushuhuda wa kuwa Mungu ndio utajiri pekee wa moyo.

 

 

1.9.            MALEZI YA UFUKARA

 

Malezi ya ufukara yakazie maisha ya Yesu aliyejifanya maskini kwa ajili yetu.

Halafu yahimize:

- kuwa na unyenyekevu;

- kuishi kwa imani kama wana wa Baba wa mbinguni anayejua mahitaji yetu na kututunza siku kwa siku;

- kuwajibika katika kazi;

- kujali vitu vinavyopatikana jumuiani;

- kutaka vyote viwe kweli vya wote ili kila mmoja apate anavyohitaji;

- kutumia fedha na vitu kwa usimamizi wa viongozi;

- kubana matumizi iwezekanavyo, bila ya kufuata uwezo uliopo wala ruhusa tu;

- kuwa tayari kukosa vitu mbalimbali;

- kujiepusha na vitu ambavyo watu wadogo hawawezi kujipatia, ili kuishi ufukara kwa ukweli zaidi;

- kujinyima kwa hiari hata vitu halali.

Pia yazingatie:

- historia ya kila ndugu kabla ya kupata wito (wengine walijitegemea na kupata vingi, kumbe wengine walikuwa na hali ngumu kuliko ile ya jumuia);

- hali ya sasa ya familia yake na matarajio iliyonayo juu ya mwanae;

- mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii, kwa kuwa ufukara wetu haulengi maendeleo ya roho tu.

 

 

1.10.       UTIIFU NA UTAMADUNI WA UHURU USIO NA MASHARTI

 

Changamoto ya tatu inatokana na mtazamo ambao unadai hiari ya mtu isibanwe sana na maadili, na hivyo unasababisha kwa wingi ubinafsi, dhuluma, ukatili n.k.

Itikio la kufaa ni utiifu wa kitawa unaoonyesha kwamba kutimiza matakwa ya Mungu kunatukamilisha kwa kukuza ukweli wetu kama viumbe tunaomtegemea kabisa Muumba, na kama watoto wapenzi tunaotafuta na kutekeleza kwa pamoja yale yote yanayompendeza Baba.

Umoja huo wa jumuia ni ishara kubwa ya jinsi ya kushinda ugomvi na utengano, na ni hakika ya kufuata njia tuliyopangiwa.

Katika malezi na maisha ya kila siku, chama kinatusaidia tupate msimamo wa kudumu, kwa mafundisho ya hakika kuhusu kufikia ukamilifu, kwa ushirika wa kidugu katika kumfuata Yesu na kwa utiifu unaoimarisha hiari yetu katika kuitikia wito.

 

 

1.11.       KUSHIRIKI UTIIFU WA YESU

 

Shauri hilo, tunalolipokea kwa upendo ili kumfuata Yesu aliyetii hata kufa msalabani, linatuelekeza tuweke matakwa yetu chini ya yale ya wakili wa Mungu, yaani mlinzi, mtumishi, askofu na hasa Baba Mtakatifu.

Utiifu huo hautudhalilishi bali unastawisha uhuru wetu kama wana wa Mungu wanaoendeleza ule wa Yesu kwa wokovu wa ulimwengu.

Nidhamu utawani isishikwe tu ili kulinda maisha ya kijumuia na upendo, bali kama sharti la kujijengea tabia ya kujitawala, kukomaa n.k.

Hivyo itekelezwe namna inayostawisha utayari wa kutii si kwa hofu, bali kwa kufuata dhamiri na maadili.

Polepole ndugu wazoee kutumia vema hiari yao katika kujifanyia mipango na kutenda kwa uelewano na watu wa ndani na wa nje ya jumuia, hasa viongozi.

Mtumishi au mlinzi anayejadiliana na ndugu zake anawasaidia kutii kwa uwajibikaji, mradi hatimaye awe tayari kutoa uamuzi na kuagiza la kufanya kwa niaba ya Mungu.

Katika majadiliano hayo tuzuie mawazo ya kibinadamu mno yasijiingize upande wa kiongozi wala wa ndugu wala kati yao, bali wote tulenge tu matakwa ya Mungu yafanyike.

 

 

1.12.       MALEZI YA UTIIFU

 

Katika malezi ya utiifu tukumbuke kwamba:

- ni lazima kwanza tutambue na kutambuliwa hadhi yetu kama watu na watoto wa Mungu ili tutii kibinadamu, si kwa unyonge;

- tunapaswa kuvuka toka yale yanayotupendeza sisi hadi yale yanayompendeza Mungu, ambayo yanajitokeza kwa namna ya pekee kwa njia ya wachungaji wa Kanisa na ya kanuni na katiba walizotuthibitishia;

- ushuhuda wetu kama watawa watiifu una uzito kuliko nadharia tunayowafundisha walelewa, ingawa hao wanatakiwa kufuata njia nyofu bila ya kukwazwa na mifano yetu mibaya.

 

 

1.13.       USHUHUDA WA JUMUIA

 

Kwa kuwa tendo la kuweka ahadi linatuingiza katika chama kwa haki na wajibu vinavyoelezwa na katiba, tunapaswa kuishi kidugu katika jumuia yake mojawapo kama mahali ambapo upendo, ukichota nguvu katika sala, uongoze maisha yote na kuzaa heri.

Hivyo uanachama unatuwezesha kumpatia Yesu ushuhuda wa hadhara na wa pamoja, mradi maisha yetu yawe ishara ya ufalme wa Mungu na tangazo hai la Injili.

Kwa ushuhuda huo wa jumuia zilizojaa furaha na Roho Mtakatifu, ambapo ubinafsi unashindwa na uwajibikaji kwa ajili ya wengine, ambapo madonda yanaponywa na msamaha, na ambapo karama inaongoza uaminifu wa wote katika wito na utume, ndivyo Kanisa linavyojitambulisha kama sakramenti ya umoja na Mungu na kati ya watu, na kuonyesha matunda ya amri mpya aliyotuachia Bwana.

Pamoja na hayo, Kanisa linataka kuonekana wazi ulimwenguni hata kwa njia ya kanzu zetu.

 

 

1.14.       KATIKA USHIRIKA WA KANISA

 

Maisha ya Wakristo wa kwanza huko Yerusalemu ndiyo kielelezo ambacho Kanisa lilikizingatia kila lilipojaribu kuchochea ari ya mwanzoni na kuendelea Kiinjili safari yake.

Kwa mfano wao tuzidi kuchanga na waamini wote neema na juhudi ili sura ya Kanisa ipendeze, nalo likabili kwa nguvu ya umoja changamoto za nyakati zetu.

Basi, tusimbane Roho katika chama chetu, lakini tusaidie wengine kufaidika na karama yetu.

Sisi watawa tunaitwa kuwa wataalamu wa ushirika, mashahidi na wajenzi wa ule umoja ulio lengo la mpango wa Mungu: tuwe hivyo kutokana na tamko letu la kushika mashauri ya Kiinjili ambayo yanakomboa ari ya upendo isiwe na kizuio chochote; tena kutokana na mang'amuzi yetu ya kila siku katika kuishi, kusali na kufanya kazi kama jumuia ya Kikanisa.

Kwa namna ya pekee ushirika wa Kanisa unatudai utiifu wa akili na moyo kwa maaskofu, ambao utekelezwe mbele ya watu wote, hasa tukishughulikia katekesi, ufundishaji, uandishi na upashanaji habari.

Msimamo wetu watawa kuhusu jambo hilo ni muhimu kwa sababu tuna nafasi maalumu katika Kanisa na katika kushiriki utume wa maaskofu.

 

 

1.15.       WANDANI WA MUNGU

 

Ili tujaliwe kuwa kweli manabii, yaani kusema na wote kwa niaba ya Mungu, kwanza ni lazima tuwe wandani wake, wasikivu kwa Neno lake katika nafasi yoyote ya maisha, wenye utambuzi wa Kiroho na kupenda ukweli.

Basi, tuzidi kumuelekea Mungu, tukitafuta uso wake, tukiachana na mitazamo isiyolingana na ufunuo wake, halafu kubadili mwenendo wetu pia.

Tukiwa wanafunzi wa Neno linalotolewa na Kanisa, tunakua kumuelekea Kristo katika yote hata tufikie kimo cha utimilifu wake, tukizidi kujifunza fumbo la wokovu, kumuabudu Baba katika Roho na Ukweli, na kutekeleza ukweli kwa upendo.

 

 

1.16.       TOBA YA KUDUMU

 

Ili tuwe mashahidi halisi wa Kristo duniani kote, kwanza tunapaswa kuhakikisha tumeitwa na Mungu na kumtolea nafsi yetu pamoja na yote tuliyonayo, hasa yale yanayotuzuia tusimuitikie kikamilifu.

Wito wetu wa toba ya kudumu unataka turekebishe mfululizo uhusiano wetu na Mungu, na watu na ulimwengu ili Mungu atawale moja kwa moja maisha yetu.

Kwa ajili hiyo tukiri kwa moyo udhaifu, ujinga na uovu wetu, halafu tupambane navyo kwa roho na kwa mwili pia, tukifuata kwa uaminifu kanuni, katiba, ratiba na mbinu za kufanya juhudi.

 

 

1.17.       MAISHA YA KIROHO

 

Daima maisha ya Kiroho yawe na nafasi ya kwanza katika malezi yetu ili chama kiwe hasa shule ya Injili.

Ukarimu kwa fukara, uzazi wa kitume, mvutio kwa miito na vinginevyo vinategemea ustawi huo wa ndugu mmojammoja na wa jumuia nzima katika kuishi ndani ya Kristo kadiri ya Roho Mtakatifu kwa utukufu wa Baba.

Tunafanya safari hiyo ya uaminifu mkubwa zaidi na zaidi kwa Mungu Baba tukiongozwa na Roho anayetulinganisha na Yesu katika ushirika kamili wa Kanisa.

Safari hiyo inadai wongofu wetu wa binafsi na wa kijumuia usikome kamwe, bali uzidi kukamilika kwa kulipokea Neno la Mungu mpaka ndani ya moyo wetu na ya utendaji wetu, na kwa kuupokea uvuvio wa Roho Mtakatifu kadiri tulivyojaliwa na Baba, aliye asili na lengo la maisha yoyote.

 

 

1.18.       NENO LA MUNGU

 

Neno la Mungu ndilo chemchemi ya kwanza ya maisha ya Kikristo: linachochea uhusiano wa dhati na Mungu aliye hai na utekelezaji wa matakwa yake yenye kuleta wokovu na utakatifu.

Ndiyo sababu toka mwanzo watawa waliheshimu usomaji wake wa Kiroho, hata hekima ikaangaza maisha yao.

Uzoefu na Neno uliwapa mwanga unaohitajika kwa utambuzi, wasilingane na mitindo ya ulimwengu.

Kwa mfano wa mwanzilishi wetu, tuitafakari hasa Injili ili kuzingatia matendo na maneno ya Yesu, Maria na mitume.

Kutafakari Neno na mafumbo ya Kristo kunaleta ari katika sala na utume; pia kutumia muda wetu miguuni pake ndio namna wazi ya kumtangaza Yesu kuwa ni Bwana wetu na kuwa yu hai kati yetu.

 

 

1.19.       USHIRIKISHANO JUU YA INJILI

 

Kwa kuwa maisha yetu ni ya Kiinjili hasa, tutie maanani ushirikishano wa mawazo na mang'amuzi kuhusu Injili.

Kuitafakari kijumuia kuna thamani kubwa kwa kutufanya tuchange kwa furaha utajiri tuliochota humo ili tukue pamoja na kusaidiana kidugu katika maisha ya Kiroho.

Tena, ushirikishano juu ya Neno unalisha imani na tumaini, kuheshimiana na kuaminiana, kupatana na kushikamana katika sala.

Halafu zoezi hilo linatusaidia kulieneza kati ya viungo vingine vya taifa la Mungu.

Tutafute namna za kuwafanya wote wajifunze kushirikishana kwa unyofu.

Vilevile ugumu wa mtu fulani kushirikisha ulio na mzizi wa kisaikolojia usiwe kisingizio cha kutomjali, bali wote wapokee toka kwake pia yale anayotaka kuyatoa kwa maneno na matendo.

 

 

1.20.       LITURUJIA

 

Tuwe na hakika ya kuwa jumuia inajengwa na liturujia, hasa ekaristi na upatanisho.

Maajabu hayo ya Mungu yanasababisha sifa, shukrani, furaha, umoja wa mioyo, nguvu za kukabili matatizo ya kila siku na kutegemezana katika imani.

Yesu anazidi kutuita pamoja kila siku hasa katika ekaristi ili aseme nasi na kutuunganisha naye na kati yetu: ndio moyo wa maisha ya Kanisa na ya utawa vilevile.

Ekaristi inafungamana na juhudi za wongofu zinazokamilika katika kupokea mara nyingi upatanisho, ili tuwe wazi na waaminifu katika uhusiano na Mungu.

 

 

1.21.       EKARISTI

 

Sisi tuliomfanya Yesu awe maana pekee ya maisha yetu, tunavutwa kutamani tuzidi kumshiriki kwa njia ya sakramenti inayomfanya awepo kati yetu, ya sadaka anayojitoa kwa upendo kwetu, na ya meza anayotulisha safarini.

Kwa njia hiyo tunaitwa kuishi fumbo la Pasaka tukiungana naye katika kujitoa kwa Baba kwa nguvu ya Roho.

Tumuabudu mara nyingi na kwa muda mrefu katika ekaristi ili tufurahie na kutamani zaidi zawadi hiyo.

Hata tusipoweza kuhudhuria Misa kila siku, kiini cha maisha yetu kiwe ni fumbo hilo la Bwana kuwepo hai ndani ya jumuia.

Katika kulea roho ya kijumuia tuanze daima hapo, kwa kuwa ekaristi ikiadhimishwa au kuabudiwa na kuliwa ndipo umoja wa mioyo unapojengwa.

 

 

1.22.       SALA YA JUMUIA

 

Pamoja na ekaristi, Sala ya Kanisa inatokeza wito wetu wa kuinua daima mioyo kwa Mungu ili kumtolea sifa na maombezi.

Adhimisho lake linahuisha mfululizo sala yetu kwa kutuletea Neno kadiri ya mzunguko wa mwaka wa liturujia na linatufanya tujisikie washiriki wa taifa la Mungu.

Sala ni zawadi ya Mungu inayotupasa tuipokee na kuistawisha kwa bidii, mafunzo na uaminifu.

Hasa walelewa waongozwe kuthamini zaidi na zaidi nafasi za sala ya jumuia zinazoongoza mwendo wa siku zetu, ili wazitumie zote kwa bidii walau kuanzia zoezi, wakidumu katika uchipukizi na baadaye.

Kila ndugu apate ujuzi wa kitaaluma, wa Kiroho na wa kichungaji kuhusu Maandiko na liturujia utakaomwezesha kulishwa navyo na kuwasaidia waamini wengine wavumbue hazina hizo na kufaidika nazo.

Ili jumuia itimize wajibu wa kulea katika sala, ndugu wote watoe mchango wao kwa kujenga mazingira yanayofaa, kwa kujiandaa, kuwahi na kusali vizuri.

 

 

1.23.       SALA NA KIMYA

 

Sala ieleweke kuwa ni muda wa kukaa na Mungu aweze kufanya kazi ndani mwetu na kuenea katika maisha yetu, akitufariji na kutuongoza kati ya uchovu na mawazo ya kila aina, kusudi hatimaye tuwe wake tu.

Sala ya pamoja inazaa kadiri inavyoshikamana na ile ya binafsi: toka mwanzo wa malezi yetu tusisitize umuhimu wa kuhusiana kwa dhati na Baba, wa kuongea na Bwanaarusi na rafiki moyo kwa moyo, wa kuchimba yaliyoadhimishwa katika Roho Mtakatifu, na wa kutunza kimya cha ndani na cha nje kama nafasi ya Roho na Ukweli kutuhuisha kabisa.

Kusikia na kuitikia wito wa utakatifu kunadai kimya hicho ambacho kimejaa uwepo wa Mungu tu, na kinatuwezesha kuelewa anapotaka na anavyotaka kusema nasi.

Hivyo tuzoee mapema kimya na upweke: upweke wa hiari unaelekeza kwenye kimya cha ndani, nacho kinadai kimya cha nje.

Tufurahi kuwaruhusu ndugu waliokwishaonyesha ukomavu fulani katika maisha ya kijumuia waweze kujipatia nafasi zaidi za upweke na sala.

Nyumba zetu ziwe tayari kupokea watu kwa ukarimu, hasa kwa sala, lakini bila ya kuvuruga hali ya kimya, nafasi ya faragha na mengine ya kitawa.

 

 

1.24.       SALA NA KUMSHIRIKI YESU

 

Tukipanda mlima wa sala pamoja na Yesu, kama walivyofanya Petro, Yakobo na Yohane, tunafunuliwa fumbo lake katika utukufu wa Utatu na katika ushirika wa watakatifu, tukatamani kukaa naye moja kwa moja; pia tunaandaliwa kushuka naye kati ya watu tukabili shughuli za kila siku na kushiriki msalaba wake bila ya kukwaza nao.

Daima watu wa sala ndio waliofanya makuu, kwa kuelewa na kutekeleza vizuri matakwa ya Mungu.

Sala inakusudiwa kutuathiri hata kila wazo, neno na tendo letu, katika nafasi muhimu na za kawaida vilevile, lionyeshe tunavyofanana na Yesu katika kujitoa mhanga.

Ushirika naye utuongoze kujiunga na kila jambo ambalo mwenyewe aliunganika nalo kwa dhati: na Baba aliyemtuma ulimwenguni, na Roho aliyemsukuma maishani, na Kanisa alilojitoa kwa ajili yake, na binadamu wote, hasa wenye hali ngumu zaidi ambazo alipenda kuzishiriki kama kaka yao.

Tusichoke kuhimizana ili wakati wa shughuli tudumishe ile roho ya sala inayotakiwa iwe lengo la malimwengu yote, hivi kwamba siku nzima na kazi zake mbalimbali zigeuke kuwa nafasi za kuungana na Bwana.

Maisha hayo ya ndani yanaleta furaha ya Kifransisko ambayo ni nguvu ya kushinda mabaya na kuzidi kujitoa maisha yote.

 

 

1.25.       MALEZI YA SALA

 

Katika malezi ya sala tuelekeze:

- kuunda moyo safi unapoweza kung'aa uzuri wa Mungu;

- kutambua daima uwepo wa Mungu na matakwa yake;

- kustawisha uwezo wa kuyashangaa maajabu yake katika uumbaji na ukombozi;

- kuzoea kusikiliza Neno la Mungu na kutumia sala za Biblia ili kumuonja Mungu na kuingia katika historia ya wokovu;

- kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Kanisa kadiri ya mwaka wa liturujia ili kuishi mafumbo makuu ya ukombozi;

- kufuata vema ratiba ili kudumisha sala hata isipojibubujikia;

- kuwa na moyo mpana ambao unasali na kuishi ukishiriki furaha na huzuni za wote;

- kujua jinsi watu mbalimbali wa zamani na wa siku hizi walivyong'amua fumbo la Mungu;

- kumpenda kitoto Mama wa Mungu aliyekingiwa dhambi asili.

 

 

1.26.       UDUGU

 

Mang'amuzi ya dhati ya Mungu kuwa ni Baba yalimuongoza mzee wetu Fransisko kutambua na kuishi upya udugu wake na watu wote, hasa na wale aliojaliwa na Baba awe nao njia moja.

Tukishiriki karama yake, tuwapokee na kuwapenda wenzetu kama zawadi ya Bwana.

Tumetumwa kushuhudia udugu wa Kikristo kwa kuwaona wote kuwa ni wana wa Mungu tayari, au walau wanaitwa wawe hivyo, na kwa kujitoa kwa upendo kwa kila mmojawao, hasa wale wa mwisho.

Jina la chama lina uzito mkubwa na linadai tuwe:

- wadogo wa Yesu, wenye uhusiano wa dhati naye, aliye kaka wa wengi;

- ndugu sisi kwa sisi kwa kupendana na kufanya kazi pamoja;

- ndugu wadogo wa kila mmoja kusudi tustawishe udugu ndani ya Kanisa na ya jamii, tukishuhudia upendo wa Kristo kwa wote na kuwakumbusha ukweli huu wa msingi: "Nyinyi nyote ni ndugu".

 

 

1.27.       KUIMARISHA UDUGU

 

Ili tuhifadhi na kuimarisha maisha ya kidugu kadiri ya Injili:

- tujiite na kuwazoesha wote watuite "ndugu";

- tunapoeleza karama yetu ili kuchochea miito na kuingiza utawani, tuyakazie mambo makuu ya maisha hayo (kuishi kijumuia, kuwa wadogo wa wote n.k.) kuliko kazi au hadhi fulani (upadri n.k.);

- kwa kuwa wito wetu kimsingi ni uleule, malezi ya utakaji na zoezi yalingane kwa wote; baadaye tu ndugu wapewe nafasi ya kujiendeleza kadiri ya uwezo wao na ya udogo wetu;

- tutoe huduma za kutufaa zaidi kama wadogo (kutangaza Neno, kufundisha sala, kutekeleza matendo ya huruma, kufanya kazi za mikono n.k.);

- tuwe watu wa haki na amani, tukiwasaidia wote kuunda dhamiri zao kuhusu tunu hizo;

- tuchangie pia maendeleo halisi ya jamii kuendana na Injili na katiba yetu ili tuwe watu wa Mungu wasio mbali na mashaka ya maisha ya watu.

 

 

1.28.       UPENDO WA KRISTO

 

Kristo katika fumbo la Pasaka ndiye kielelezo cha kudumu cha namna ya kujenga umoja, tena ndiye chemchemi na kipimo cha upendo unaohitajika.

Ili tufaulu kuishi kidugu ni lazima Roho wake atuwezeshe kupendana kama Yesu alivyopenda.

Akiwa ni upendo wake uliomiminwa mioyoni mwetu, anatusukuma tupende wote kwa kubeba udhaifu wao na matatizo yao hata kujitoa mhanga kwa ajili yao.

Hasa kuishi na ndugu ambao hawajisikii vizuri, na hivyo wanasababisha uchungu kwa wenzao na kuvuruga maisha ya jumuia, ni fursa ya kukomaa kiutu na Kikristo.

Safari hiyo ya ukombozi wa moyo inadai tujikane ili tumpokee mwingine alivyo, pamoja na tofauti na mipaka yake, sifa na kasoro vilevile, kuanzia yule aliyepewa uongozi, tusije tukamdai mno.

Moyo huo tu, ambao unatokana na upendo na kulenga ustawi wa upendo ndani mwetu na mwa wenzetu, utatuwezesha kutegemezana, kukosoana, kujishtaki hadharani, kukagua na kupanga maisha kwa pamoja n.k.: namna hizo zote tuzing'amue kuanzia utakaji.

Ikiwa ndugu atajisikia anapokewa alivyo, hapo tu ataondoa kinga zake na hofu zinazomfunga akapokea ukosoaji na shauri na kukua vema.

 

 

1.29.       JUMUIA NA UKOSEFU

 

Kwa kuwa maisha na malezi yetu yana elekeo la kidugu, kumuingiza mtu katika utamu na ugumu wa kuishi pamoja kunafanyika katika jumuia.

Wengi wanavutiwa nayo, lakini kudumu ndani yake katika hali halisi ya maisha kunaweza kukawa mzigo mzito: mtu wa kawaida, akipenda umoja, hataki kuugharimia mwenyewe kwa kuwajibika.

Kwa hiyo toka mwanzo tujulishe kwamba maisha ya jumuia yanadai sadaka, lakini kujiangamiza kwa ajili ya wenzetu ndiyo njia ya wokovu: Injili inataka watu ambao, sawa na chembe ya ngano, wanajua kujifia ili udugu ustawi.

Hivyo jumuia inakuwa shule tunapojifunza kumpenda kweli Mungu kwa kuwapenda ndugu aliowaweka karibu nasi, na binadamu wote, hasa wanaohitaji zaidi huruma ya Mungu na mshikamano wa kidugu.

Jumuia kamili haipatikani duniani, ambapo Kanisa lenyewe, pamoja na miundo na utakatifu wake, linajengwa juu ya udhaifu wa binadamu.

Hata hivyo kwa msaada wa Mungu tunaweza daima kuongoka na kujenga kwa pamoja jumuia juu ya msamaha na upendo.

Umoja tunaoulenga unategemea upatanisho: kwa hiyo utovu wetu wa ukamilifu usitukatishe tamaa, mradi tushike upya kila siku njia tuliyoelekezwa na Neno.

 

 

1.30.       NJIA ZA UMOJA

 

Umoja halisi ni zawadi ya Mungu kwa wanaosikiliza Injili na kuishika.

Ili tupendane kama watoto wa Baba mmoja:

- tukuze hali ya kifamilia, ya furaha na ya unyofu kati yetu;

- tuzidi kuaminiana, kuelewana, kuthaminiana;

- tuelezane shida zetu;

- tuimarishane wakati wa taabu na wa kuvunjika moyo;

- tupendane bila ya masharti;

- tutumikiane kwa ukarimu;

- tutiiane kwa upendo;

- tusihukumiane;

- tuzoee kuvumilia na kusamehe sabini mara saba;

- tukosoane kidugu tukilenga daima wongofu;

- tupambane na ugeugeu wetu na misukosuko ya kujianzia;

- tuachane na chochote kinachoweza kuvuruga maisha ya kidugu;

- tushirikishane kila kitu.

Pasipo juhudi hizo, umoja haupatikani.

 

 

1.31.       FUMBO LA JUMUIA

 

Ushuhuda wa kidugu unadhoofishwa na shughuli nyingi mno zikituzuia tusishiriki kwa kawaida sala za pamoja, maisha ya jumuia na huduma za nyumbani.

Basi, ratiba ya kila siku isipangwe kwa kujali utendaji wa kitume kuliko maisha ya kidugu, bali jumuia ijipatie muda wote unaohitajika ili kuboresha maisha hayo yasiwe ya kuhangaika hata kujichosha bure.

Tuelewe mapema kuwa ushirika wa kidugu sio tu njia ya kufanya vizuri kazi yetu, bali ni mahali pa kung'amua uwepo wa Yesu hai kati yetu, tena pa kuushuhudia Utatu, yaani Baba anayetaka kuwafanya watu wote kuwa familia moja, Mwana aliyekusanya waliotawanyika, na Roho anayewaunganisha katika upendo.

Umoja hautegemei raha ya kulingana kwa mawazo, kwa tabia na kwa machaguo, bali wito wa Bwana aliyetuweka wakfu namna moja ili tuishi pamoja na kufanya utume mmoja.

Hasa mfano wa jumuia za kimataifa unaweza ukasaidia makabila mbalimbali kushirikiana, kutajirishana na kurekebishana.

Lakini umoja kati ya watu tofauti si rahisi: unadai nia imara upande wa wote, na utambuzi upande wa viongozi na walezi.

Juhudi za kuwatii kwa imani, za kupokeana wenyewe kwa wenyewe na za kutatua matatizo katika jumuia mchanganyiko zinadhihirisha kwamba tuko pamoja kwa jina la Bwana.