|
![]() |
ya Utawa wa
Ndugu Wadogo wa Afrika
1. KUISHI KIINJILI KAMA FAMILIA YA
MUNGU
4. KUZAA KWA KUPENDANA NA MUNGU TU
7. KUISHI KIDUGU KATIKA JUMUIA
0.1.1. Yesu, Mwana pekee wa
Mungu, alikuja duniani aokoe kila kabila la watu na kuongozana na kila mmoja
katika safari ya maisha.
0.1.2.
Alikuja kutuangazia utamaduni tulioachiwa na wazee, ili tuone unavyomuelekea
yeye Adamu Mpya.
0.1.3.
Alikuja kutukusanya tena kwa njia ya Roho wake wa upendo, anayetufanya familia
ya Mungu Baba, jamaa ya wadogo wake walioshinda hofu na chuki kati yao, mfano wa
Utatu mtakatifu, ushirika kamili katika tofauti za nafsi, ambapo lugha zote
ziungane kutangazia maajabu aliyotutendea Mwenyezi Mungu.
0.2.1.
Kwa upendo wake alitaka Afrika iwe bara lake la pili, ambapo asalimike utotoni
na azidi kuwa Mwafrika kwa njia ya viungo vyake.
0.2.2.
Kanisa la bara letu, baada ya kutendewa naye makuu na kustawishwa kwa juhudi na
damu za wazee wetu katika imani, sasa linatakiwa kueneza wokovu hata miisho ya
dunia, lisitosheke na kazi ya kukidhi mahitaji ya majimbo yake tu.
0.2.3.
Kutuatana na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, Roho Mtakatifu katika Sinodi ya
Kwanza ya Afrika ameliambia Kanisa hilo anavyolitaka lijionyeshe familia ya
Mungu na kutangaza habari njema ya Yesu Kristo, aliye njia, ukweli na uzima kwa
Mwafrika na kwa yeyote duniani.
0.2.4.
Miaka ya elfu mbili, nafasi ya pekee ya kufikisha Injili kwa watu wote, ndiyo
saa yake tena.
0.2.5.
Ingawa Waafrika wengi wanazidi kuachwa nyuma kisiasa na kiuchumi, utamaduni wao
wa uzima na mshikamano unahitajiwa haraka na ulimwengu wote.
0.3.1.
Mtakatifu Fransisko wa Asizi alimshuhudia Kristo kwa upole na ushujaa mbele ya
Waislamu wa bara letu, akitamani kumwaga damu yake kwa wasiomjua bado.
0.3.2.
Mfano wake huo na karama aliyojaliwa, yenye sifa kuu mbili yaani udugu na udogo,
vinafaa sana kuchangia utekelezaji wa maazimio ya Sinodi hiyo.
0.4.1.
Tukizingatia hayo, sisi Ndugu Wadogo wa Afrika tunajisikia wito wa kutimiza
karama hiyo katika mazingira halisi ya Waafrika, kwa kudumisha, kustawisha na
kueneza tunu za utamaduni huo ambazo zinalingana na Injili.
0.4.2.
Hivyo tunatumaini kuwa nguvu ya Mungu, inayojionyesha wazi katika udhaifu wa
binadamu, itatutumia kwa ustawi wa Kanisa lote, ambao unategemea na kulenga
utakatifu, yaani kushiriki kikamilifu uzima wa Mungu.
0.5.1.
Utawa wetu wa Kifransisko wa kimisionari una makao makuu mjini Morogoro, ambapo
askofu wa jimbo, mhashamu Telesphore Mkude, katika juhudi zake za kueneza Injili,
ameuunda kama chama rasmi cha waamini kadiri ya kanuni 312 CIC.
0.5.2.
Ni juu ya askofu wa jimbo hilo kuzidi kufanya utambuzi wa karama hiyo ili aweze
kupendekeza utawa huo ukubaliwe kama aina mpya ya maisha yaliyowekwa wakfu,
kadiri ya kanuni 605 CIC, au aufute kwa sababu nzito.
0.6.1.
Mwenyewe amethibitisha katika hii itusaidie kumfuata kwa hakika Yesu na kutimiza
matakwa ya Baba kwetu.
0.6.2.
Tunaohusika nayo moja kwa moja ni sisi wanachama tuliojifunga kushika useja
mtakatifu, ufukara na utiifu kwa kuishi Injili kijumuia katika jamaa za kiume na
kike.
0.6.3.
Ni wanachama halisi pia makleri wanajimbo na walei wanaume na wanawake, waseja
na wenye ndoa, ambao kisha kupata malezi ya kufaa wanaishi ulimwenguni karibu na
jumuia mojawapo ya namna hiyo, wakishirikiana nayo katika maisha ya kiroho na ya
kitume: hao wanafuata kanuni na katiba za Utawa wa Kifransisko wa Ulimwenguni (S.F.O.)
kama washiriki wengine wa Utawa huo wa Kipapa.
0.7.1. Katiba hii ina mambo yale tu ya karama na taratibu zetu ambayo
hayatarajiwi kubadilika.
0.7.2. Hata hivyo tuzidi kuomba mwanga wa Mungu na kufaidi mang’amuzi yetu
ili tuelewe vizuri zaidi anataka nini kwetu, kwa kuzingatia ufuasi wa Kristo
kadiri ya Injili, hazina ya kiroho ya Kifransisko, malengo ya Kanisa na mahitaji
ya ulimwengu, tukiweka daima mbele ustawi wa roho zetu na wokovu wa watu.
0.8.1. Askofu wa Morogoro anaweza kuthibitisha marekebisho ya katiba
yaliyopitishwa na baraza pana kwa thuluthi mbili za kura, mradi yawe
yanahitajika kweli ili tuendelee kujenga juu ya misingi ileile.
0.8.2. Haja hiyo isipokuwepo, afadhali yaachwe, kwa sababu mabadiliko
yanadhoofisha sheria, na yale madogo yanachochea mengine makubwa, mpaka mfumo wa
utawa unakuwa mwingine na kusababisha utasa wake.
0.9.1. Ili tuwe na heri kwa kutekeleza kikamilifu yale tuliyoonyeshwa,
tujitahidi sura halisi ya utawa wetu ilingane na picha iliyochorwa katika katiba
tuliyojaliwa na Mungu kwa njia ya Kanisa lake.
0.9.2. Mkutano mkuu unaweza kutoa kwa kiasi sheria ndogondogo zinazohusu
jamaa nzima, na ambazo ziweze kurekebishwa nao inapotakiwa, mradi zilingane
daima na kanuni na katiba.
0.9.3. Halmashauri kuu inaweza kutoa maagizo maalumu yanayohusu baadhi tu ya
ndugu au jumuia, kadiri ya mahitaji yao na ya mazingira wanapoishi.
0.9.4. Lakini tutegemee uaminifu mnyenyekevu wa kila mmoja wetu kuliko wingi
wa sheria na juhudi za watumishi na walinzi.
0.10.1. Ukitokea wasiwasi kuhusu utekelezaji wa sehemu ya katiba hii,
halmashauri kuu iamue la kufanya, lakini baraza likikusanyika litoe maelezo
rasmi kwa kibali cha askofu wa Morogoro.
0.11.1. Ni juu ya askofu wa jimbo husika kusamehe ndugu wasitekeleze sehemu
fulani ya sheria zetu katika nafasi maalumu.
0.11.2. Ikiwepo sababu ya kutosha, watumishi na walinzi pia wanaweza
kuwasamehe ndugu walio chini yao, wale waliopo kwa muda na hata jumuia nzima,
isipokuwa katika yale yanayohusu miundo ya utawa wetu na kiini cha maisha yetu;
tena, ikihitajika ruhusa ya kudumu, itolewe na mtumishi tu.
0.11.3. Aliyesamehewa ajitahidi zaidi katika mengine anayoyaweza, akijua
urahisi wa ruhusa hizo unavyozima upesi hamu ya ukamilifu.
0.12.1. Hasa tujihadhari na kishawishi cha kuona sharti fulani la katiba hii,
eti ni gumu mno, au kuacha kulitimiza kwa makusudi au kwa ulegevu.
0.12.2. Tuamini kuwa wokovu umetokana na upumbavu wa msalaba, halafu tung’amue
jinsi mzigo wowote ulivyo mwepesi ukibebwa kwa ajili ya Yesu mpenzi ili kuungana
naye.
1 . KUISHI KIINJILI KAMA FAMILIA YA MUNGU
1.1. YESU NA INJILI YAKE
1.1.1. Yesu wa Nazareti ndiye mfano kamili wa Mungu asiyeonekana, na ndiye
anayetufumbulia kikamilifu ubinadamu wetu.
1.1.2. Injili takatifu, iliyo moyo wa Maandiko Matakatifu yote, inatufunulia
matendo na maneno yake, na hivyo inatuelekeza njia pekee ya kumfikia Baba katika
Roho Mtakatifu na ya kuwa watu waliokomaa anavyotutaka yeye.
1.1.3. Mzee wetu Fransisko wa Asizi tangu aanze kuongoka hakuwa kiziwi kwa
ujumbe wa Injili, bali kwa kuushika sawasawa alikuja kufanana na Yesu kwa namna
ya pekee.
1.1.4. Upendo wa Kristo uliotupata sisi pia, ndio asili ya maisha yetu yote
ambayo tunalenga ukamilifu wa Injili yake, kwa kushika sio tu amri za Mungu,
bali pia mashauri yanayotokana na mafundisho na mifano aliyotuachia, ili
tumfuate kwa karibu iwezekanavyo huyo Mwanakondoo kokote aendako.
1.1.5. Tuzingatie hivyo Injili zaidi kuliko mapokeo ya kibinadamu, hata kama
ni ya kitawa.
1.1.6. Kwa njia hiyo Roho Matakatifu atamfanya Yesu kuwa kiini cha maisha
yetu na kuunda upya utamaduni wetu ndani mwake, kwa sifa na utukufu wa Mungu
Baba.
1.2.
VIUNGO VYA MWILI WA KRISTO
1.2.1.
Kristo ameunganika kabisa na bibiarusi wake na kuishi ndani yake, kiasi kwamba
kushikamana na Kanisa na kushikamana naye ni mamoja.
1.2.2.
Tumtolee huyo Mama yetu maisha na moyo, maneno na matendo, muda na nguvu ili
sikuzote tuishi na kufanya kazi ndani yake na kwa ajili yake, tukiamini tunaye
Roho Mtakatifu kadiri tunavyolipenda Kanisa.
1.2.3.
Tushirikiane na vyombo vyake mbalimbali katika kazi na hasa katika adhimisho la
ekaristi, ili kuonyesha na kuimarisha umoja tulionao.
1.2.4.
Tutegemeze pia miundo yake ya lazima kwa njia ya sadaka na michango mbalimbali,
hasa kwa ajili ya mfuko wa pamoja kama umeanzishwa jimboni.
1.2.5.
Sisi watawa ni zawadi ambayo Baba amelijalia Kanisa ili kuwakumbusha watoto wake
undani wa miito yao maalumu, ambao kwa wote ni mmoja tu, yaani kuwa watakatifu
katika mwenendo wao wote.
1.2.6.
Kama vile sisi tunavyohitaji msaada wa waamini wenzetu, nao wanahitaji kuvutwa
na sisi ambao tumekataa tamaa za ulimwengu, na kuweka pembeni hata tunu kadhaa
za kidunia, ili kulenga moja kwa moja heri ya milele kwa kufuata njia
aliyoielekeza Yesu katika hotuba ya mlimani.
1.2.7.
Kwa mfano wa Maria wa Bethania, tumwage maisha yetu kama manukato ya miguu yake,
ili Kanisa lote lijae harufu nzuri ambayo imchochee kila Mkristo kusikiliza upya
Neno la uzima na kuchangia juhudi motomoto za familia yote ya Mungu katika
kutangaza, kuadhimisha na kutekeleza Neno hilo.
1.2.8.
Hivyo katika Mwili wa Kristo tutashika nafasi yetu hasa, yaani kuwa moyo wa
maisha yake, wa utakatifu wake na wa utume wake.
1.3.
MAKANISA MAALUMU
1.3.1.
Kanisa Katoliki linaishi katika Makanisa maalumu ya Mashariki na ya Magharibi,
yenye sura mbalimbali kadiri ya mazingira, historia na utamaduni wa watu wake.
1.3.2.
Tuthamini utajiri huo wote na kuuzingatia hasa tunapohamia jimbo fulani ili
karama yetu istawi humo kama mahali pake, na kulijenga kweli.
1.3.3.
Popote pale tutekeleze kwa ushujaa karama yetu ya kinabii, tukitenda na kusema
kwa niaba ya Mungu, bila ya kufuata mkondo au kutaka kuwapendeza watu; lakini
kwa unyenyekevu pia, tukikubali waandamizi wa Mitume waifanyie utambuzi.
1.3.4.
Tukiongozwa na imani tuwapende na kujali kazi zao tatu za kutufundisha,
kututakasa na kutuchunga.
1.3.5.
Tuwe tayari kushirikiana nao katika ziara rasmi wanazotufanyia kwa maendeleo ya
utawa wetu ndani ya Kanisa.
1.3.6.
Tuwaone mapadri wao kuwa ni kaka zetu katika Kristo na tupokee kwa shukrani
huduma zao, hasa za maparoko wetu na za wale ambao askofu wa jimbo kwa
kushauriana na watumishi amewateua kuwa washauri na waungamishi wetu utawa
usipojitosheleza.
1.4
UMOJA WA KANISA
1.4.1.
Umoja wa Mungu katika nafsi tatu ni asili, kielelezo na lengo la familia yake
inayounganishwa na Roho wa upendo.
1.4.2.
Ubora wa Kanisa unategemea mafungamano yetu watoto wake, yaani jinsi
tunavyotunzana na kushikamana na kupendana, tunavyokaribishana na kujadiliana na
kuaminiana.
1.4.3.
Kwa ajili hiyo askofu wa Roma amekabidhiwa kundi lote la Kristo duniani, kusudi
alichunge kwa upendo, na kuliimarisha katika imani liwe nguzo na msingi wa
ukweli.
1.4.4.
Kwa ahadi yetu tunawajibika kuwapenda na kuwatii kwa namna ya pekee yeye na
Kanisa lake, tukijitahidi kujua na kutekeleza hati zote wanazozitoa.
1.4.5.
Sisi tunaoshuhudia uzuri wa kuishi kidugu, tujenge madaraja kati ya makleri,
walei, watawa na miundo yao pia, ili tufanye kwa nguvu ya umoja kazi ile kubwa
ajabu tuliyoagizwa na Yesu.
1.4.6.
Vilevile tujadiliane na kufahamiana, tushirikiane na hasa tusali na kutubu
pamoja na ndugu zetu wa madhehebu mbalimbali, kusudi ushuhuda wetu kwa Kristo,
amani yetu, uweze kuaminika hadi mafarakano yoyote yaishe kabisa.
1.5. TOBA YA KIFRANSISKO
1.5.1. Yesu Kristo akitangaza utawala wa Mungu aliwaita watu kuupokea kwa
kufanya mapinduzi ndani mwao, wakianza kuwaza, kupima mambo na kupanga maisha
kulingana na upendo wa Baba aliotufunulia.
1.5.2. Mwenyewe akamtuma mzee wetu Fransisko ili kwa mfumo wake alirekebishe
Kanisa ambalo ni takatifu, lakini pia linahitaji siku zote utakaso na
matengenezo, ili waamini wote watekeleze maishani sakramenti zilizowaweka wakfu.
1.5.3. Tuzingatie hazina ya kiroho ya mtakatifu huyo, kwa kuitimiza,
kuilinda, kuichimba na kuikuza moja kwa moja, halafu kwa kuwashirikisha watu
wowote ili wapate wokovu na utakatifu.
1.5.4. Ndani ya Kanisa jumuia zetu zijengeke kama mazingira ya toba juu ya
msingi wa ubatizo unaowezesha maisha yote yawe Pasaka, tukizidi kufia dhambi ili
kufufuka na Kristo kwenye uzima mpya.
1.5.5. Ingawa hatujui mwaliko wa Yesu wa kupoteza maisha yetu nyuma yake
utatufikisha wapi, tusifadhaikie mambo ya hesko, ila tumuachie Mungu wa faraja
zote na kusaidiana kidugu kubeba msalaba siku kwa siku.
1.5.6. Baada ya kufunga safari ya kuufikia upendo kamili, tushinde
kishawishi cha kujipongeza kwa urahisi na kusimama katikati, tukijua kwamba
tusiposonga mbele, tunarudi nyuma tu.
1.5.7. Kama alivyofanya mtakatifu Fransisko, kwa uongozi wa Roho na vipaji
vyake, tuvue utu wa zamani na vilema vyake, tukamvae Kristo na maadili yake,
hata kuchuma matunda ya Roho na kuonja heri za Yesu, malimbuko ya uzima wa
milele.
1.6. MFUASI MKAMILIFU WA YESU
1.6.1. Vizazi vyote vinamshangilia Maria mwenye heri kwa jinsi alivyosadiki
Neno la Mungu na alivyokubali kujiliwa na Roho Mtakatifu: hivyo amekuwa
kielelezo cha namna ya kupokea neema na kujiweka wakfu kwa Mungu.
1.6.2. Vilevile, akishiriki toka mwanzo maisha yaliyofichika ya Mwanae,
halafu akihudhuria matukio makuu ya utume wake, ametuonyesha namna ya kuungana
naye, hasa kwa kuyaweka na kuyatafakari katika moyo safi yale yote yanayomhusu
Yesu.
1.6.3.
Maisha yetu ya kiroho, ya kijumuia na ya kitume yawe na tabia hiyo ya Maria hasa,
ili tuweze kukua katika imani, tumaini na upendo tunavyofundishwa na Injili.
2.1 NJIA YETU
2.1.1. Roho Mtakatifu anawaongoza watoto wa Mungu kumfuata Yesu kwa namna
maalumu na kuunda ndani ya Kanisa familia za kiroho zenye karama za aina nyingi.
2.1.2. Kwa neema yake sisi tunawajibika katika familia ile iliyoanzishwa na
mzee wetu Fransisko katika matawi mbalimbali, ili mataifa yote yazidi kushuhudia
utakatifu wa Kiinjili unaopatikana kwa kufuata nyayo za Yesu fukara tena
msulubiwa.
2.1.3. Ndiye kitabu kikuu ambamo Roho Mtakatifu anatufundisha maana na namna
ya kuishi, kupenda na kuteseka, hata kupokea kwa amani matakwa ya Baba katika
nafasi ngumu zaidi za maisha.
2.1.4. Kwa upendo wa pekee Mungu Baba anawavuta mfululizo wale anaowataka
waache vyote wakaungane kabisa na Mwanae kiroho na kimaisha, hasa kwa njia ya
utiifu, ufukara na useja mtakatifu, ambayo ni yake kabisa na ambayo yalimfaa
sana ayashike duniani.
2.1.5. Kama vile upendo huo, mambo hayo pia yanahusu maumbile yetu mpaka
ndani kabisa, tunapojisikia misukumo ya kujifanyia mipango, kumiliki vitu na
kupendana kijinsia.
2.1.6. Sisi tuliojaliwa karama hiyo hatuwezi kuithamini vya kutosha, lakini
tuipokee kwa shukrani na kumrudishia Mungu utu wetu wote ili uwezo wake
uuzidishe kwa manufaa ya umati.
2.1.7. Hivyo tutawaelekeza watu kushinda tamaa za utawala, mali na anasa,
ambazo zimo mioyoni mwa wote kutokana na dhambi ya asili, na ambazo zinawapeleka
kwenye maangamizi.
2.2. MIITO
2.2.1. Maisha ya Bwana na agizo lake vinaonyesha kwamba toka mwanzo swala la
miito mitakatifu ni la msingi kwa Kanisa, na kwamba sala ndiyo njia ya
kulikabili kwa hakika kabisa.
2.2.2. Tushiriki katika kazi za Kanisa kwa ajili hiyo, tukiwafundisha hasa
vijana waiombee miito, tukikaribisha na kuchambua wanaojisikia wito ili
tuwatagemeze waitikie vizuri, tukionyesha kwa matendo ubora wa kuishi na Yesu na
tukitambulisha karama yetu.
2.2.3. Kila wito ni mwaliko maalumu wa Mungu kwa mtu fulani ambao unaleta
furaha na tumaini kwake na kwa jamaa, na kudai zifanyike juhudi mpya uweze
kustawi kwa uaminifu wa wote.
2.2.4. Padri au shemasi asipokewe kabla mtumishi hajashauriana na askofu
wake; aliyewahi kuwa mtawa au mseminari asipokewe pasipo taarifa ya mkuu wa
shirika au gombera wa seminari husika.
2.2.5. Wafuatao hawawezi kabisa kupokewa: wenye umri chini ya miaka 18;
wasiopata ubatizo, kipaimara na ekaristi; wasio ndani ya ushirika kamili wa
Kanisa; wanaoingia utawani kwa kulazimishwa au kwa hofu kubwa au kwa udanganyifu;
wanaopokewa na mtumishi kwa misingi hiyo; wenye madeni yanayowashinda; wenye
mwenzi wa ndoa; wenye nadhiri za kitawa na wanashirika wa aina nyingine;
waliowahi kuwa na ahadi ya daima katika jamaa yoyote ya utawa watu.
2.2.6. Ni lazima hatua za kuingizwa katika maisha yetu, ambazo ni utakaji,
zoezi na uchipukizi, zifanyike chini ya walezi, ambao wawasaidie ndugu wapya
kupata kwa taratibu ujuzi na mang’amuzi vinavyohitajika ili waendelee na
safari ya kiroho kwa uhuru wa ndani ulio mkubwa zaidi na zaidi.
2.2.7. Kumrudisha nyumbani mtakaji na mwanazoezi asiyefaa ni juu ya mtumishi
tu, ila kwa sababu nzito za haraka ni pia juu ya mlezi akiwa na kibali cha
halmashauri ya jumuia husika.
2.3. MALEZI KWA JUMLA
2.3.1. Tangu mtu aingie utawani hadi kufa kwake anahitaji malezi ya
Kifransisko kamili iwezekanavyo kuhusu utu, Ukristo, utawa na umisionari, ili
asaidiwe kushiriki upendo wa Yesu hata msalabani kwa tumaini la kutimilika
kabisa katika ufufuko.
2.3.2. Papo hapo malezi yanalenga kumfikisha kwenye ukomavu wa kibinadamu
kama msingi ambao umwezeshe kujenga utawa, Kanisa na jamii.
2.3.3. Wakimtegemea Roho Mtakatifu, aliyetumwa kuwa
mtendaji mkuu wa malezi, wahusika wote, yaani ndugu wenyewe waliopokea wito,
baraza na halmashauri ya jamaa, walezi na viongozi wa kiroho, tena jumuia nzima,
wawe na nia moja na moyo mmoja, wakishiriki vizuri kwa kuwajibika.
2.3.4. Wenyewe wajitahidi mfululizo kuitikia wito na kutumia vema misaada
wanayopewa ili kulingana na Yesu, katika nafasi muhimu za maisha na katika zile
za kawaida, katika utamu na ugumu wa kuishi pamoja na katika juhudi za kitume.
2.3.5. Ingawa maisha na malezi yetu yanategemea na kulenga moja kwa moja
tuambatane naye kuliko kufuata mwongozo wenye vipengele vingi, hata hivyo baraza
liandae mpango mzuri kwa kazi hiyo yote ambao utimilizwe na maandishi mengine
maalumu kwa kila hatua na nyumba ya malezi.
2.3.6. Utekelezaji wake uhesabiwe na baraza kuwa ndio wajibu wake wa kwanza,
hasa kwa kuwaandaa katika kila jamaa ndugu wa kutosha kwa kazi hiyo muhimu kama
nini ya kuwalea na kuwafundisha wenzao.
2.3.7. Halmashauri ya jamaa inapowatuma ndugu kuanzisha jumuia katika nchi
nyingine ihakikishe baadhi yao wafae kuwa walezi.
2.3.8. Wajue vizuri hasa njia ya Mungu ili kuweza kuwaongoza wale
waliokabidhiwa na jamaa; halafu wasilemewe na kazi mbalimbali wasije wakashindwa
kuwashughulikia ipasavyo.
2.3.9. Wawaonyeshe vizuizi vya wazi na vilivyofichika, haja ya kujikaza
mfululizo, lakini hasa uzuri wa lengo na thamani ya karama inayofikisha huko.
2.3.10. Walau katika nyumba za utakaji, zoezi na uchipukizi, halmashauri ya
jamaa iwateue pia wale wanaofaa zaidi kuwa vyombo vya Mungu kwa uongozi wa
kiroho, kutokana na uzoefu wao wa kusikiliza Neno lake, kutumia vipaji vya Roho
Mtakatifu na kufanya utambuzi.
2.3.11. Wanajumuia wengine wanapaswa kuwasaidia ndugu wapya kwa kuwapokea
kwa upendo, kuwaombea na kuwatolea mifano bora.
2.4. UTAKAJI
2.4.1. Utakaji lengo lake ni kuziba mapengo ya malezi ya awali ya mtu ili
wito wake uweze kueleweka, naye akiendelea nasi aifaidi hatua ya zoezi.
2.4.2. Mbali ya muda unaotumika pengine kufuata masomo kwenye shule na vyuo
mbalimbali, mtakaji aishi katika jumuia zetu kati ya mwaka mmoja hadi mitatu.
2.4.3. Wakati huo ajichunguze na kuchunguzwa kuhusu ukomavu wa kibinadamu na
wa Kikristo, yaani ushirikiano wa kidugu, bidii ya kufanya kazi, msimamo wa
kijinsia na wa kimapenzi, imani halisi ya Kikatoliki, juhudi za kiroho na hamu
ya kuokoa watu.
2.4.4. Baada ya kuvumbua maana ya utawa na aina zake, mtakaji aiombe kwa
maandishi halmashauri ya jamaa husika aanze zoezi la kujipatia mpaka ndani sura
hiyo.
2.5.
ZOEZI
2.5.1.
Katika mazingira ya imani, sala na kuhudumiana kidugu, wanazoezi wajifunze elimu
ya upendo ili kuwa na msimamo uleule wa Yesu: kujikana kwa furaha na kuwa
wanyenyekevu na wapole kwa wote na katika hali yoyote.
2.5.2.
Wasaidiwe kufanya hivyo kwa mafundisho ya Kikristo na ya Kifransisko, na hasa
kwa maongezi ya binafsi na mlezi, kusudi watambue wanavyopendwa jinsi walivyo,
pamoja na wanavyoweza kukomaa.
2.5.3.
Zoezi hilo linachukua miaka mitatu, ila kama pengine utahitajika mwaka wa nne
uongezwe.
2.5.4.
Mwaka wa pili mtumishi, kwa ombi la mlezi, anaweza kuwapeleka wanazoezi wakaishi
kijumuia sehemu nyingine, au anaweza kuwaruhusu wauruke wakikusudia kuweka ahadi
ya muda.
2.5.5.
Kwa vyovyote katika hatua hiyo utiliwe mkazo juu ya kusali na kutafakari kama
Yesu alivyofanya Nazareti alipojiandaa kujitoa kabisa kwa Baba ili kuondoa
dhambi ya ulimwengu.
2.5.6.
Miezi mitatu hivi kabla muda wa zoezi haujaisha, kila mmoja aiombe kwa maandishi
halmashauri ya jamaa aweke ahadi kwa siku zote za maisha yake au kwa muda
usiopungua mwaka.
2.5.7.
Kisha kupata taarifa ya mlezi ikiwa ni pamoja na maoni ya jumuia, halmashauri
hiyo ijadili ombi hilo na kulipigia kura za siri, ikizingatia kama kuweka ahadi
kutamsaidia mwanazoezi kupenda zaidi au kutamuelemea.
2.5.8. Mwanazoezi akikubaliwa,
kabla hajaweka ahadi ya muda amuachie mtu yeyote kusimamia na kufaidi mali zake
binafsi, pia aandike wasia wake; baada ya hapo atahitaji sababu zinazoeleweka na
ruhusa ya mlinzi ili kubadili alivyoviamua.
2.6. KUWEKA AHADI
2.6.1. Siku ya kuweka ahadi,
mhusika awe ametimiza miaka 23 na kushauriana na ukoo wake walau kwa njia ya
barua; kwa ahadi ya daima awe amepata kibali cha ndugu zake wanaohusika zaidi.
2.6.2. Wakati wa Misa
atimilize ahadi za ubatizo kwa kujifunga hadharani kushika Injili kijumuia
kadiri ya Kanuni na Maisha ya Ndugu wa Kiume na wa Kike wa Utawa Hasa wa Tatu wa
Mtakatifu Fransisko, iliyokubaliwa na papa Yohane Paulo II, na kadiri ya katiba
hii.
2.6.3. Ahadi hiyo kwa Mungu
haimwajibishi aliyeiweka tu, bali pia jamaa iliyoipokea kwa niaba ya Kanisa,
kuhusu kuyafikia malengo ya wito wake, hasa kwa kumpatia mazingira na malezi ya
kufaa.
2.6.4. Kwa kuweka ahadi ya
muda tunataka kufuata njia ya upendo kamili bila ya vipingamizi kusudi tuungane
zaidi na Yesu ili azae matunda mengi ya utakatifu ndani mwetu; vilevile tuungane
zaidi na Kanisa na umisionari wake kadiri ya wito wetu.
2.6.5. Ahadi ya muda inaweza
kurudiwarudiwa bila ya mwisho: pia inaweza kuwa nafasi ya kukomaa ili baadaye
tujitoe mpaka kufa.
2.6.6. Atakayeweka ahadi ya
daima baada ya kuweka ile ya muda ili ajiaminishe kwa Mungu kama sadaka ya
kuteketezwa kwa wokovu wa watu wote, ajiandae kwa miezi miwili ya kukusanya
mawazo na kusali kama Mitume walivyojiandaa kumpokea Roho Mtakatifu awafanye
mashahidi wa Kristo mpaka mwisho wa dunia.
2.6.7. Kwa ahadi ya daima
tunaitikia kwa moyo usiogawanyika upendo wa Mungu Baba, kwa mfano wa Mwanae
aliyependa upeo na kwa karama maalumu ya Roho Mtakatifu; tunawekwa wakfu kwa
namna mpya na ya pekee kwa njia ya Kanisa; pia tunapokewa na utawa moja kwa moja
kama familia yetu mpya, na kujitoa kikamilifu kwake, tayari kutumwa kokote
duniani.
2.6.8. Kabla ya kuweka ahadi
ya daima ndugu aandike hati ya kujinyima moja kwa moja mali yoyote, kwa kupanga
namna ya kuwagawia maskini vyote alivyo navyo na vile vitakavyopatikana baadaye
kwa kurithi; hati hiyo iwe na nguvu kuanzia siku ya kuweka ahadi hiyo.
2.6.9. Mtu ambaye alimaliza
zoezi au kuweka ahadi ya muda, halafu akaacha vilivyo utawa, akiomba kwa
maandishi kupokewa tena, halmashauri ya jamaa ikimkubalia impangie muda na
masharti ya jaribio, ambalo likienda vizuri imkubalie kuweka ahadi ya muda,
baadaye akipenda ile ya daima.
2.7. UCHIPUKIZI
2.7.1. Miaka mitatu inayofuata
zoezi itumike kuendelezea malezi kuhusu Neno la Mungu na maisha ya kiroho,
pamoja na ndugu kuzoea polepole kazi mbalimbali ndani na nje ya jumuia.
2.7.2. Hizo zipangwe na
kutekelezwa hasa kwa manufaa yao, si kulingana na mahitaji ya sasa hivi ya jamaa
au ya watu wa nje, wasije wakalemewa.
2.7.3. Mwelekeo wa sala na
toba utawale hatua hiyo pia, ili wazidi kujitoa kwa upendo kadiri ya ahadi yao,
na kujiandaa kukabili yale yote yatakayoweza kutokea maishani, hasa katika
mazingira magumu.
2.7.4. Ihakikishwe kuwepo kwa
nyakati maalumu za watawa chipukizi kukaa faraghani ili kusali, kutafakari na
kuchimba mafundisho waliyoyapata.
2.8. MALEZI MAALUMU
2.8.1. Mungu ameunda utawa
watu naye anaufanya upya siku kwa siku kwa kutuangazia tuyashike maisha ya
Kiinjili ya Kifransisko, ambayo ni lengo kamili tena ni lazima liwe la kwanza
kwa yeyote anayejiunga nasi.
2.8.2. Pamoja na hayo, ikiwa
ndugu ameitwa kweli awe pia padri au shemasi au kutoa kuduma nyingine ya
Kikanisa, mtumishi ampatie malezi yanayotakiwa awe mhudumu kadiri ya moyo wa
Mungu, aliye tayari kumwakilisha Kristo kwa uaminifu na ukarimu; uamuzi wa
mwisho ni juu ya askofu, lakini daraja inakusudiwa kutolewa kwa maisha na
umisionari wa utawa wetu, sio kwa ajili ya jimbo lake tu.
2.8.3. Vilevile ikihitajika
mmoja wetu akasome fani fulani, halmashauri ya jamaa imteue ndugu ambaye kwa
ukomavu wake anatumainisha kwamba ataendelea kuwa kielelezo cha wito wetu.
2.8.4. Chini ya mlezi hao wote
wakabili matatizo ya kipindi cha masomo, wakiangalia hasa yasidhuru roho ya
ibada na sala, wala yasiwavimbishe, bali yawaongoze kumshiriki zaidi Mungu
anayejifunua kwa wadogo, na yawaandae kuwahudumia watu vizuri zaidi.
2.9. MALEZI YA KUDUMU
2.9.1. Utawa unapaswa
kuwasaidia ndugu wote kwa mwendo wake wa kila siku na pia kwa njia ya kozi,
semina, mikutano na mang’amuzi mbalimbali ili wito wao wa Kifransisko ustawi
mfululizo na utume wao ufae daima katika mabadiliko ya mazingira.
2.9.2. Kila mmoja wetu, kadiri
ya uwezo na majukumu aliyonayo, awajibike kujiendeleza katika yale yanayomhusu,
kwanzia maisha ya kiroho ambayo ni ufunguo wa malezi yote kwake na kwa wengine.
2.9.3. Tuamini kuwa Mungu Baba
anailisha familia yake kwanza kwa Maandiko Matakatifu, ambamo anaongea nasi
mfululizo ili kutuingiza katika ushirika naye na kutujulisha matakwa yake kwa
maisha yetu.
2.9.4. Kila siku tushike
mikononi Biblia takatifu, tukilenga kwa unyenyekevu kuielewa kulingana na imani
ya Kanisa na mazingira yetu, ili tumfahamu Kristo ambaye ndiye Neno.
2.9.5. Halafu tupendelee
kusoma maandishi ya Ualimu wa Kanisa, ya mababu wake, ya walimu wakuu wa maisha
ya kiroho na habari za watakatifu, hasa Wafransisko, tukijitahidi kutekeleza.
2.9.6. Tushibe hayo kwa pamoja
walau mchana au jioni tunapolisha miili yetu, isipokuwa kwenye Jumapili, sherehe
na nafasi nyingine za kufaa.
2.9.7. Kwa mwanga huo wa
Kiinjili Roho wa hekima atatuwezesha kutambua hali ya ulimwengu na dalili za
nyakati zetu, kuchambua yanayotokana naye na yanayopingana naye, na kufurahia
jinsi Baba anavyoongoza yote ili mabaya pia yaweze kuleta mema.
2.9.8. Tutatambua pia tukabili
vipi matukio yoyote, kwa kumtumainia kama kwamba yote yanamtegemea yeye tu, na
kwa kuwa kuwajibika kama kwamba yote yanatutegemea sisi.
2.9.9. Kwa ajili hiyo, vitabu
na magazeti machache vyenye msimamo wa Kikatoliki kweli viwepo tayari kwa faida
ya wote.
2.10. UAMINIFU
2.10.1. Kila mtawa wetu ana
wajibu na haki ya kutimiza wito wake, na kushiriki katika maisha na utendaji wa
jamaa na ngazi zake, kadiri ya katiba hii.
2.10.2. Adili la ibada na amri
ya kwanza ya Mungu vinatudai tutekeleze yale tuliyomuahidia ili kumuonyesha
heshima na upendo inavyotupasa.
2.10.3. Ili tutamani zaidi
kufanya hivyo na kuwajibika kulingana na sheria ya moyoni, ambayo ni Roho
Mtakatifu mwenyewe, kila siku tusome kwa pamoja sehemu ya katiba; halafu mara
moja kwa mwezi turudie ahadi yetu baada ya kusoma kanuni nzima, onyo na laana
vya mtakatifu Fransisko.
2.10.4. Tujiombee neema za
kuzishika, tuzitafakari mara nyingi na kuziongelea katika mikutano yetu, ili
zipenye zaidi na zaidi maisha ya kila mmoja na ya jumuia nzima na kutusaidia
kulenga utakatifu na kufanya utume anavyotutaka Mungu.
2.10.5.
Kwa uaminifu wake yeye hawezi kughairi kuhusu wito bora aliotujalia; vilevile
sisi tuwe waaminifu kwake tukitegemea neema tusiyoweza kupungukiwa, mradi
tukeshe na kusali pasipo kuchoka.
2.10.6.
Kwa hakika kizo tupige mbio kwenye njia nyembamba ya uzima, ili kujinyakulia
taji lisiloharibika, tukijua wengi wanaingia uwanjani bila ya kufanikiwa.
2.10.7.
Tujihadhari na uvuguvugu ambao ni mwanzo wa uasi, tena tusifuate mitindo ya
ulimwengu, bali tuzidi kujitoa kama sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu.
2.10.8.
Kanzu tunayoivaa usiku na mchana, na mtindo wetu wa kifukara kwa jumla,
vimekusudiwa kutusaidia tudumu katika wito wetu, halafu kushtua na kufikirisha
watu.
2.10.9.
Hivyo tusivionee aibu ila tuangalie moyo wetu ulingane na sura ya nje kadiri
inavyoonyesha unyenyekevu na usafi.
2.11.
KUTENGANA NA UTAWA
2.11.1.
Ndugu mwenye ahadi akiwa na shida anaweza kuomba kwa maandishi muda wa kujitenga
na jamaa; baada ya mtumishi kuongea naye na kumpa nafasi ya kufikiri,
halmashauri ya jamaa ikate shauri kwa upendo na busara, ambalo liandikwe katika
rejesta na kuarifiwa kwa ndugu mhusika; hapo haki na wajibu vilivyotokana na
ahadi yake vinasimamishwa, isipokuwa haruhusiwi kufunga ndoa; muda aliopangiwa
ukiisha anaweza kuomba apokewe tena; asipoomba au asipokubaliwa, atoke moja kwa
moja utawani inapoelezwa hapa chini.
2.11.2.
Muda wa ahadi ukiisha, ndugu ana hiari ya kuacha utawa, na vilevile halmashauri
inaweza kumkatalia asiirudie au asiweke ahadi ya daima zikiwepo sababu zenye
msingi.
2.11.3.
Mwenye ahadi ya daima ambaye kwa sababu nzito anataka kuacha utawa, kisha
kushauriana na mtumishi wake, amuombe askofu wa jimbo anamoishi kitawa, ambaye
anaweza kumruhusu kwa kuwasiliana na halmashauri ya jamaa.
2.11.4.
Ndugu ambaye ameasi kabisa imani au amejitenga au ametengwa rasmi na ushirika
kamili wa Kanisa au ametoroka utawani, amepoteza papohapo kazi alizokuwanazo
utawani na haki zake kama mwanajumuia; mtumishi ajitahidi kumrudisha kwa kuwa
anapaswa bado kutimiza ahadi yake; ikishindikana amtumie barua ya tahadhari
kwamba ataondoshwa, ambayo isipoleta mafanikio baada ya mwezi mmoja halmashauri
ya jamaa imuondoe rasmi; aliyeachishwa anaweza kumkimbilia askofu wa jimbo
alimokuwa anaishi kitawa, na hivyo kusimamisha utekelezaji wa uamuzi huo, mradi
asichelewe zaidi ya siku kumi baada ya kuarifiwa.
2.11.5.
Kwa sababu nyingine nzito, wazi, zenye dhambi na thibitisho, zilizoorodheshwa
katika sheria zetu ndogondogo, mtumishi afungue kesi mbele ya halmashauri yake,
akimpa mhusika nafasi ya kujitetea, halafu awasilishe hati zote kwa askofu wa
jimbo anamoishi kitawa ili aondoshwe.
2.11.6.
Aliyetengana moja kwa moja na utawa kwa namna yoyote ile, hana tena wajibu na
haki vilivyotokana na ahadi yake, wala hawezi kudai chochote kwa kazi
alizozifanya utawani.
2.11.7.
Upande wake jamaa iwajibike kutumia upendo na usawa kwa ndugu yeyote aliyeiacha,
hasa kwa aliyekaa muda mrefu, ikimsaidia kukabili maisha na kuendelea katika
safari ya kiroho.
2.12. BIKIRA
MWAMINIFU
2.12.1.
Kisha kumfuata Yesu mpaka Kalivari, Maria alituzaa kwa uchungu na kufanywa na
Mwanae kuwa mama wa kila mmoja wetu, hasa wa wale aliowapenda zaidi.
2.12.2.
Toka mwanzo wa kukaa utawani tumpokee upya kama mama tukimpenda na kumuiga,
tukimfunulia siri za maisha yetu na kumuomba atulee kama alivyomlea Yesu.
2.12.3.
Kwa hisani yake atatushirikisha upendo ule unaowezesha kumtolea Mwanae maisha
yote bila ya kujitwalia tena hata chembe; kujiaminisha kwa Baba na kwa matakwa
yake hata msalabani; halafu kufurahia maajabu anayotutendea kwa Roho Mtakatifu.
2.12.4.
Furaha hiyo kudumu katika majaribu kutahakikisha ubora wa kuishi kwa ajili ya
Mungu tu, kutavuta miito mingine, na kuuelekeza ulimwengu njia za kugeuka sura
uwe ufalme wake.
3.1.MUUNGANO
NA MUNGU
3.1.1. Kwa kuwa Yesu alidumu
moja kwa moja katika muungano wake na Baba, aliingiza duniani ile ibada kamili
katika Roho na ukweli inayompendeza.
3.1.2. Mwenyewe anaendelea
kufanya hivyo kwa njia ya Kanisa lake, akitupelekea Roho Mtakatifu atusaidie
sisi viungo vyake katika udhaifu wetu, na kutuongoza hata hali ya juu ya
muungano na Mungu, kama alivyomjalia Fransisko, mtu aliyefanyika sala, ambaye
alikuwa akimuona Mungu ndani ya vyote na vyote ndani ya Mungu.
3.1.3. Kwa kuwa tumeitwa
kufuata nyayo zake, tuchague kile ambacho peke yake ni cha lazima: kumjua kweli
Yesu anayetuvutia kumpenda na kumtangaza ulimwenguni kote, kwa kuwa ni mzuri
kuliko wanadamu wote na hakuna mwingine aliyewahi kusema vema kama yeye.
3.1.4. Katika sala tuzingatie
hasa alivyojishusha kwa ajili yetu, akikabili magumu yoyote hadi kilele cha
maisha yake msalabani, ambapo upendo wa moyo wake safi ulifikia upeo, ufukara
wake ulikuja kukosa yote kabisa, na utiifu wake ulijitoa mhanga.
3.1.5. Sala zetu zote
zilingane na liturujia, zitokeze karama ya udugu na udogo, na kuzilisha roho
zetu kwa mapokeo bora ya Kifransisko.
3.1.6. Tunasali kweli kama
ndugu tukiwa roho moja na mojo mmoja: na kama wadogo tukishiriki hali ya
wanaodhulumiwa na kumlilia Mungu usiku na mchana awapatie upesi haki zao.
3.1.7. Tuwaombee wenzetu wote,
wazima na wafu, pasipo kubagua maadui, kwa kuwa nguvu ya sala ni upendo.
3.1.8. Tuwavute waamini kwenye
maji hai ya sala ili maisha yao ya kiroho yastawi kweli, kwa kuwa anayesali
ataokoka, lakini asiyesali atapotea kwa sababu anabaki pweke na unyonge wake.
3.2 LITURUJIA
3.2.1. Sala, ambayo ni pumzi
ya roho zetu na ya jumuia pia, kiini chake kiwe liturujia, na hasa ekaristi, kwa
kuwa ndimo kazi ya wokovu inamozidi kutendeka.
3.2.2. Upande wetu liturujia
ni jibu la kijumuia kwa Mungu, kilele cha utendaji wa Kanisa na chemchemi ya
uwezo wake wote.
3.2.3. Ukweli wa maneno hayo
unategemea jinsi imani inavyozingatia mafumbo yanayoadhimishwa; pia unachangiwa
na ubora wa ibada.
3.2.4. Mtindo mwepesi wa
Kifransisko unaosisitiza upendo kuliko fahari za ibada, uendane daima na heshima
inayodaiwa na kazi hiyo ya Kimungu.
3.2.5. Kwa kuwa liturujia
ndiyo uwanja wa kwanza wa urekebisho na utamadunisho wa Kanisa, tutie maanani
uzuri wa ishara zake mbalimbali, tukihusisha mwili na hisi zake; tufanye
mabadiliko yale yanayokubalika na kutumia nafasi za kimya; tuimbe kwa moyo na
sauti, tukipiga ala zetu za muziki za kuadhimishia ushindi wa uzima dhidi ya
mauti.
3.2.6. Kila siku tushiriki
kijumuia sadaka ya Misa au walau meza ya ekaristi, ambapo tujitoe kabisa kwa
Yesu anayejitoa kwetu kwa upendo mnyenyekevu, ili tupate nguvu mpya za
kumtumikia maishani.
3.2.7. Kwa ajili hiyo
tujiandae kwa makini, halafu tukae tukimshukuru kwa muda usiopungua dakika
ishirini, ili tuimarishe muungano wetu naye.
3.2.8. Zaidi tena, matunda
tunayoweza kuchuma humo yanategemea usafi wa upendo wetu; basi, tuadhimishe kwa
imani na unyofu sakramenti ya upatanisho kila baada ya wiki moja au mbili, ili
kutengeneza upya roho na jumuia zetu.
3.2.9. Ili maisha yetu yote
yawe wimbo wa kushangilia uzima mpya tuliojaliwa, mwendo wa kila siku wa jumuia
zetu zote uongozwe na maadhimisho ya pamoja ya vipindi vyote vya Sala ya Kanisa
vinavyompasa padri.
3.2.10. Tusali kila kipindi
kwa wakati wake na kuamka usiku wa manane kwa Kipindi cha Masomo.
3.2.11. Tunatakiwa kusali kila
mtu peke yake vipindi vile ambavyo tumeshindwa kuviadhimisha pamoja na ndugu
zetu.
3.2.12. Hivyo tutakuwa mfano
wa Kanisa ambalo linamsikiliza Mungu na kufanya ukumbusho wa fumbo la wokovu,
likimsifu na kumuomba kwa umoja kwa ajili ya wote.
3.3. SALA YA MOYO
3.3.1. Katika kushiriki kabisa
liturujia tujifunze kustawisha zaidi na zaidi uongofu wetu na sala ya moyo.