HATUA TATU ZA MAISHA YA KIROHO |
YALIYOMO
0.
UTANGULIZI
1.
CHEMCHEMI NA LENGO LA MAISHA YA KIROHO
1.1. Uzima wa neema, mwanzo wa uzima wa milele
1.2. Maisha ya Kiroho na maongezi ya ndani na Mungu
1.3. Muundo wa Kiroho
1.3.1.
Maisha ya kimaumbile na yanayopita maumbile
1.3.2.
Maadili ya Kimungu
1.3.3.
Maadili ya kibinadamu
1.3.4.
Vipaji saba vya Roho Mtakatifu
1.3.5.
Neema za msaada na aina zake
1.4. Uwemo wa Utatu mtakatifu ndani mwetu kama chemchemi isiyoumbwa ya
maisha ya Kiroho
1.5. Kristo mkombozi anavyoathiri mwili wake wa fumbo
1.6. Msaada wa mama Maria
1.7. Ustawi wa uzima wa neema kwa njia ya stahili, sala na sakramenti
1.8. Ukamilifu wa Kikristo ni nini hasa?
1.9. Ukuu wa ukamilifu wa Kikristo na heri nane
1.10. Ukamilifu na ushujaa
1.11. Ukamilifu wa Kikristo na matakaso ya Kimungu
1.12. Ukamilifu na amri ya kumpenda Mungu
1.13. Ukamilifu na mashauri ya Kiinjili
1.14. Wajibu wa pekee wa mapadri na watawa wa kulenga ukamilifu
1.15. Hatua tatu za maisha ya Kiroho kadiri ya mababu na walimu wakuu
1.16. Somo la Kimungu
1.17. Uongozi wa Kiroho
2.
UTAKASO WA WANAOANZA
2.1. Hatua ya Kiroho ya wanaoanza
2.2. Fikra za kidunia na ufishaji kadiri ya Injili
2.3. Ufishaji kadiri ya mtume Paulo na sababu zinazofanya uwe wa lazima
2.4. Dhambi ambazo tuziepe: mizizi yake na matokeo yake
2.5. Kilema tawala, mdudu anayekula ndani kwa ndani
2.6. Maono ya kuratibiwa
2.7. Kujitakasa upande wa hisi
2.8. Kujitakasa upande wa ubunifu na kumbukumbu
2.9. Kujitakasa upande wa akili
2.10. Kujitakasa upande wa utashi
2.11. Kupona kiburi
2.12. Kupona uvivu wa roho
2.13. Sakramenti ya kitubio
2.14. Kushiriki misa, chemchemi ya utakatifu
2.15. Komunyo takatifu
2.16. Sala ya kuomba
2.17. Sala ya Kanisa
2.18. Sala ya moyo ya wanaoanza inavyozidi kuwa sahili
2.19. Kufikia maisha ya sala na kudumu ndani yake
2.20. Wachelewaji
3.
MWANGA WA WANAOENDELEA
3.1. Lugha ya walimu wa Kiroho ikilinganishwa na ile ya wanateolojia
3.2. Kuingia hatua ya mwanga
3.3. Wongofu wa pili kadiri ya walimu wengine
3.4. Kutakaswa upande wa hisi na kuingia hatua ya mwanga
3.5. Tufanye nini katika usiku wa hisi
3.6. Sifa kuu za hatua ya wanaoendelea
3.7. Jengo la Kiroho la wanaoendelea
3.8. Busara na maisha ya Kiroho
3.9. Haki, aina zake na kuunda utashi
3.10. Subira na upole
3.11. Usafi wa moyo, thamani na matunda yake
3.12. Unyenyekevu wa wanaoendelea
3.13. Unyenyekevu wa Neno aliyefanyika mwili na ule wa kwetu
unavyotakiwa kuwa
3.14. Roho ya ufukara
3.15. Ukuu wa utiifu
3.16. Usahili na unyofu
3.17. Roho ya imani na ustawi wake
3.18. Tumaini kwa Mungu na hakika yake
3.19. Upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu
3.20. Upendo wa kidugu, mng'ao wa upendo wa Mungu
3.21. Ari kwa utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu
3.22. Usikivu kwa Roho Mtakatifu
3.23. Upambanuzi wa roho
3.24. Sadaka ya misa na wanaoendelea
3.25. Komunyo ya wanaoendelea
3.26. Ibada ya wanaoendelea kwa bikira Maria
3.27. Kitabu cha "Kumfuasa Yesu Kristo" kinawaelekeza wote
njia ya mafumbo
3.28. Sala ya kumiminiwa
3.29. Uzushi wa Watulivu kuhusu sala ya kumiminiwa na kuhusu upendo safi
3.30. Ngazi za sala ya kumiminiwa kwa wanaoendelea
3.31. Maswala kuhusu sala ya kumiminiwa
3.32. Yaliyo mapya katika sala ya kumiminiwa
3.33. Ulinganifu na tofauti kati ya watakatifu Teresa wa Yesu na Yohane
wa Msalaba
4.
MUUNGANO WA WALIOKAMILIKA
4.1. Kuingia hatua ya muungano kupitia usiku wa roho
4.1.1.
Haja ya kutakaswa roho na utangulizi wa hatua ya muungano
4.1.2.
Ufafanuzi wa utakaso wa Kimungu wa roho
4.1.3.
Kinachosababisha roho kutakaswa
4.1.4.
Giza la mwanga mkali
4.1.5.
Miongozo kwa usiku wa roho
4.1.6.
Matokeo ya roho kutakaswa hasa upande wa maadili ya Kimungu
4.1.7.
Hatua ya waliokamilika: muungano wao na Mungu
4.1.8.
Aina mojawapo ya maisha makamilifu: njia ya utoto wa Kiroho
4.2. Ushujaa wa maadili
4.2.1.
Ushujaa wa maadili kwa jumla
4.2.2.
Imani ya kishujaa inayozama katika mafumbo
4.2.3.
Tumaini la kishujaa na kujiachilia kwa Mungu
4.2.4.
Upendo wa kishujaa
4.2.5.
Ushujaa wa maadili ya kibinadamu
4.2.6.
Upendo kwa Yesu msulubiwa na kwa Maria katika hatua ya muungano
4.3. Namna na ngazi za hatua ya muungano
4.3.1.
Maisha kamili ya kitume na sala ya kumiminiwa
4.3.2.
Maisha ya malipizi
4.3.3.
Roho Mtakatifu anavyomuathiri aliyekamilika
4.3.4.
Muungano mkavu na muungano wa kutoka nje ya nafsi
4.3.5.
Muungano unaotugeuza, utangulizi wa ule wa mbinguni
5.
NEEMA ZA PEKEE
5.1. Karama
5.2. Mafunuo na njozi
5.3. Maneno na miguso ya Kimungu
5.4. Madonda matakatifu na kudanganyika
5.5. Tofauti kati ya matukio hayo ya Kimungu na yale yatokanayo na
ugonjwa
5.6. Matukio ya Kishetani
6.
HATIMA
Mtu
akiacha kuongea na wenzake, mara anaanza kuwaza yanayomvutia zaidi. Mawazo
hayo yanatofautiana hasa kadiri ya umri na uadilifu wa watu. Kwa mtu
anayelenga ukweli na wema yanaelekea kugeuka maongezi
na Mungu, naye mwenyewe, badala ya kujipendea katika yote (yaani kujifanya
lengo la yote, ajue asijue) anamlenga Mungu katika kila jambo pamoja na
kumpenda na kuwapenda watu kwa ajili yake. Ndiyo maisha ya Kiroho.
Ni
jambo bora na la lazima kuliko elimu, sanaa, fasihi, siasa na mengineyo: wale
wasio na maisha ya Kiroho wakijihusisha na mambo hayo wanaonekana kutafuta
humo ukweli na wema, lakini utafiti wao unaathiriwa na umimi kiasi kwamba
tunapaswa kujiuliza kama utazaa matunda kwa uzima wa milele. Wengi wao
hawainuki juu ya utendaji wa kibinadamu tu na wa njenje, wala hawaishi kwa
jambo lililo bora kuliko wao, yaani kwa Mungu.
Maisha
ya Kiroho, yaani kuishi na Mungu, ndiyo kitu
pekee cha lazima kwa sababu kwa njia yake tu tunaelekea lengo letu kuu.
Tusiutenganishe wokovu na safari ya
utakatifu iliyo njia ya wokovu. Mbinguni
kutakuwa na watakatifu tu, wawe wameingia mara baada ya kufa, au wawe
wamehitaji kutakaswa toharani. Hakuna anayeingia mbinguni akiwa na doa lolote.
Ili aweze kufurahia daima uso wa Mungu, yaani kumjua na kumpenda kama mwenyewe
anavyojijua na kujipenda, ni lazima hatia yoyote hata ndogo iwe imefutwa, na
adhabu iliyostahili iwe imetimizwa au kuondolewa.
“Atafaidiwa
nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu
atatoa nini badala ya nafsi yake?” (Math. 16:26). Ikiwa tuko tayari kupoteza
vitu vingi ili kuokoa mwili, ambao kwa vyovyote utakuja kufa, kwa nini tusiwe
tayari kupoteza vyote ili kuokoa roho inayotakiwa kuishi milele? Je, binadamu
hapaswi kupenda roho kuliko mwili wake?
Hayo
tuliyoyasema ni ya kweli nyakati zote, lakini siku hizi yanahitaji kufikiriwa
zaidi, kwa sababu hakuna utulivu: wengi wamejitenga na Mungu, wakijitahidi
kupanga mbali naye maisha ya binafsi na ya jamii. Matatizo makuu yaliyowapata
daima binadamu yamepata sura mpya ya kutisha. Kwa kuwa Mungu ni mwanzo na
mwisho wa yote, mtu akitaka kutenda bila yake anajikuta vilindini mwa unyonge
mbaya kuliko utovu wa vyote. Hatimaye analazimika kutambua kuwa yote yanadai
azingatie sana swala la dini.
Mtu
asipotaka kutimiza wajibu wake kwa Mungu, aliye muumba na lengo lake kuu,
anajikuta akiabudu vingine, k.mf. sayansi au haki ya kijamii au kipeo chochote
cha kibinadamu, kwa kuwa hawezi kuishi bila ya dini. Hivyo anasogea mbali na
aliye Mkuu kabisa na kukabiliana na rundo la maswala ambayo, atake asitake,
hayana jibu lolote asiporudia swala la msingi la fungamano na Mungu.
Siku
hizi bingwa anaabudu taratibu za sayansi na kuzijali kuliko ukweli wenyewe.
Angefanya bidii hizohizo katika maisha ya Kiroho, angefikia mapema utakatifu.
Kumbe hiyo ibada ya sayansi lengo lake ni utukufu wa mtu badala ya upendo wa
Mungu. Vilevile siasa mara nyingi inajidanganya kuboresha maisha ya binadamu
kwa kukataa haki za Mungu.
Msingi
wa maswala yoyote ni swala la dini: hatuwezi kulipuuzia wala kuepa kusimama
ama upande wa Mungu ama dhidi yake. Historia ya karne ya 20 imetuonyesha hilo
waziwazi.
Mtu
akitaka kuishi bila ya Mungu, uzito wa
maisha unasogezwa kutoka upande wa dini kwenda upande mwingine. Lakini
baada ya muda analazimika kutambua kuwa yote yamevurugika.
Mali haiwezi kuwa yote ya wengi kwa wakati mmoja:
ndiyo sababu ya mashindano kati ya watu na kati ya mataifa, lengo kuu
likiwekwa katika mali. Kumbe mema ya
Kiroho yanaweza kuwa yote ya wote kwa wakati mmoja: tunaweza kuwa na
ukweli uleule, uadilifu uleule na Mungu yuleyule bila ya kunyang'anyana.
Bwana
ametuambia: “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote
mtazidishiwa” (Math. 6:33). Kukataa fundisho hilo ni kujitakia maangamizi:
"Bwana asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda
mji yeye aulindaye akesha bure" (Zab. 127:1).
Mtu
akijali sayansi au siasa kuliko dini, na akijitafutia utukufu badala ya
kumtafutia Mungu, maisha yatamfundisha mapema kuwa ameshika njia isiyofika
mahali. "Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu, na mtu asiyekusanya
pamoja nami hutapanya" (Math. 12:30).
Lakini
dini haiwezi kuwa jibu halisi la
maswala makuu ya leo isiposhikwa kwa dhati. Maisha ya Kiroho yanatakiwa kuwa
kweli muungano na Mungu ili dini idumu kuwa juu ya sayansi na siasa.
Lengo
ni kuwaalika watu kwenye muungano na Mungu, wakiepa hatari mbili.
Ya
kwanza ni kwamba leo kutofautisha fani kumezidi hata kufanya wengi wakose
mitazamo mipana inayohitajika ili kupima kwa busara mambo yoyote katika
uhusiano na mengine. Basi, katika maisha ya Kiroho pia kuzingatia madogomadogo
kusitusahaulishe jumla ya yote, la sivyo tutasogea mbali na hekima ya Kikristo.
Ya
pili ni kwamba vitabu vingi vya dini na vya ibada vinakosa msingi imara katika
imani na kurahisisha mno mafundisho ya Kiroho.
Maisha
ya Kiroho ni tawi la teolojia
linalohusika na utekelezaji wake katika kuongoza watu waungane kwa dhati na
Mungu likifafanua muungano huo ni nini na njia za kuufikia ni zipi. Hivyo
linafafanua taratibu za uzima wa neema kwa misingi ya teolojia likiilinganisha
na mang'amuzi ya watakatifu.
Maisha
ya Kiroho yanahitaji kuchambua mang'amuzi hayo kitaalamu, kwa kubainisha
taratibu zake kadiri ya saikolojia (k.mf. ukavu unaotakasa unavyohusiana na
muungano na Mungu). Somo hilo linakuwa la kiteolojia uchambuzi wa taratibu
hizo unapotegemea pia mafundisho ya imani. Ikiwa elimunafsia
ni ya lazima kwa maadilidini, ni ya
lazima zaidi kwa maisha ya Kiroho ambayo yanachunguza hatua zake ndani ya
mtu hadi muungano kamili.
Katika
ngazi ya chini, maadilidini yanatakiwa kuzungumzia sio tu madhambi ambayo
tuyaepe, bali pia maadili ambayo tuwe nayo na usikivu katika kumfuata Roho
Mtakatifu. Maisha ya Kiroho hayaenei kama maadilidini, lakini ni tawi la juu
yake kwa jinsi linavyolenga kufikisha hadi muungano
wa dhati na Mungu. Kwa njia yake teolojia inarudi ilipoanzia na kudumisha
umoja wake. Kwa hiyo linatakiwa kufuata mwanga
wa ufunuo wa Kimungu uliomo katika Maandiko na Mapokeo, ambao peke yake
unaweza kutujulisha uzima wa Kimungu na muungano wa roho na Mungu ambao
unapita maumbile.
Maisha
ya Kiroho yanatumia mawazo ya maadilidini, lakini kuhusiana zaidi na ustawi wa
uzima wa Kimungu rohoni. Utekelezaji wake, ambao ndio lengo la maisha ya
Kiroho kupitia uongozi wa mtu mmojammoja, una pande mbili: juhudi na mafumbo.
Upande wa juhudi maisha ya Kiroho yanazungumzia hasa namna ya kufisha vilema na kutekeleza maadili. Upande wa mafumbo yanazungumzia hasa usikivu kwa Roho Mtakatifu, neema ya kuzama katika mafumbo ya imani, na muungano unaotokana na neema hiyo, halafu karama ambazo pengine zinaongozana nayo.
Hapa
tutaeleza yaliyo ya lazima tu, kwa kukwepa aina mbili za upotovu ambazo ni
rahisi zitupate: moja kwa kuzingatia mafundisho ya imani na kupuuzia
mang'amuzi, nyingine kwa kuzingatia mang'amuzi na kupuuzia mafundisho ya
imani.
Tunapaswa
kuzungumzia maisha ya Kiroho kwa mwanga wa teolojia kuhusu neema ya utakaso,
maadili ya kujaliwa na vipaji saba; pasipo hayo tungekusanya tu dalili za hali
za Kiroho za juu, badala ya kuelewa kanuni za msingi za ustawi wa uzima wa Kimungu ambao hauwezi kung'amuliwa kwa kuwa si wa
kimaumbile. Pia tungetia maanani mno uhaba wa watu wanaofikia muungano wa
ndani na Mungu: hapo tungedhani kuwa walio wengi hawaitwi hata kwa mbali na
kwa jumla kufikia hatua hiyo; tungesahau maneno ya Bwana yanayokumbushwa na
walimu wa Kiroho kuhusu swala hilo: “Waitwao ni wengi, bali wateule ni
wachache” (Math. 22:14).
Upande
wa pili tunapaswa kuzingatia maelezo ya watakatifu kuhusu hatua mbalimbali za
maisha ya Kiroho, tukiyaangaza kwa imani ili kutambua katika mang'amuzi yao
yapi ni ya pekee na yapi ni ya juu, lakini yanakusudiwa kuwa ya kawaida. Upande huo hatari
nyingine ni kudhani kuwa neema ya kuzama katika sala ni ya wengi,
tukiichanganya na sala nyofu ya mapenzi ambao ni utangulizi wake tu. Kufuatana
na aina hizo mbili za upotovu, kuna makosa mawili ya kuepwa katika kuongoza
watu: kuwaachisha njia ya juhudi mapema mno au baadaye mno.
Basi,
tunapaswa kuchimba ukamilifu wa Kikristo ili kuona wazi lengo ambalo Mwokozi
amewawekea watu tusilipunguze. Halafu kuchambua mang'amuzi ili tutofautishe
yaliyo ya lazima na yaliyo ya ziada. Hatimaye kujumlisha hayo mawili ili kuona
yaliyo ya lazima au ya kufaa na ya
kutamaniwa kusudi tuufikie ukamilifu, na yale ambayo ni ya
pekee tu na hayahitajiki kufikia utakatifu mkuu.
Kutokana
na shida hizo mbalimbali, kusoma maisha ya Kiroho kunadai ujuzi wa teolojia (hasa
juu ya neema, maadili ya kumiminiwa, na vipaji vya Roho Mtakatifu kuhusiana na
mafumbo makuu ya Utatu, umwilisho, ukombozi na ekaristi) pamoja na ujuzi wa
walimu wa Kiroho, hasa wale ambao Kanisa limewataja kuwa viongozi katika
maswala hayo.
Kadiri
ya mapokeo (watakatifu Thoma wa Akwino, Yohane wa Msalaba na Fransisko wa
Sales) upande wa juhudi maisha ya
Kiroho yanazungumzia hatua ya utakaso
wa wanaoanza ambao, wakijua kwamba hawatakiwi kubaki nyuma na kupooza,
wanajitahidi kutekeleza maadili, lakini kwa
namna ya kibinadamu, yaani kwa nguvu zao zikisaidiwa na neema za kawaida.
Kumbe upande wa mafumbo unaanza mara
inapozungumziwa hatua ya mwanga ambapo
wanaoendelea, wakiangazwa na Roho Mtakatifu, wanatenda tayari, mara nyingi na
waziwazi kwa vipaji vyake saba; kwa
uongozi maalumu wa huyo mlezi wa ndani wanatenda kwa namna ipitayo maumbile ambayo kabla ya hapo ilikuwa imefichika au
kujitokeza mara mojamoja tu.
Walimu
hao wameonyesha kuwa mambo yanayopatikana upande wa mafumbo ni ya juu katika njia ya kawaida ya utakatifu, ila si ya pekee hasa (kama
njozi). Ndivyo ilivyo pia kwa wale wanaoitwa kufikia utakatifu katika utendaji
mwingi (kama mt. Visenti wa Paulo).
Basi,
kujua upande wa mafumbo hakufai tu kwa uongozi wa watu wachache wanaoitwa
kufuata njia za pekee, bali kwa uongozi wa watu wote wanaolenga ukamilifu na
muungano na Mungu katika maisha ya kila siku. Ujinga wa kiongozi wa Kiroho
kuhusu mambo hayo unaweza ukazuia wale anaowaongoza: kwa kuwa hapaswi kudhani
kila huzuni ya mtu aliyechoka kiakili ni takaso la Kimungu, lakini pia hapaswi
kudhani kuwa hilo likipatikana ni huzuni ya kinafsi tu.
Kutokana
na yote tuliyoyasema, ni wazi kwamba upande
wa juhudi unalenga upande wa mafumbo. Vilevile upande wa mafumbo
usipotanguliwa na juhudi za kufaa ni uongo mtupu.
Hatimaye
ni muhimu kuzingatia kuwa tukitazama njia ya utakatifu kuanzia maumbile
yetu, mafundisho yetu yataonekana yamepita kiasi. Lakini tukitazama njia
hiyo kuanzia mafumbo yapitayo maumbile
(uwemo wa Utatu mtakatifu ndani mwetu, umwilisho ulioleta ukombozi na ekaristi)
hapo tutaiona kwa hekima, yaani kutoka juu, badala ya kupima yote kutoka chini
unavyofanya upumbavu.
Ikiwa
kweli Utatu mtakatifu unaishi ndani mwetu, ikiwa kweli Neno alifanyika mwili
akafa kwa ajili yetu, yumo katika sakramenti kuu na kila siku anajitoa kwa
ajili yetu, basi hapo watakatifu tu,
wanaoishi kwa kujua na kama kung'amua mara nyingi uwemo huo wa Mungu, na kwa
kuupenda zaidi na zaidi katika magiza na matatizo ya maishani, ndio waliopo panapotakiwa. Hapo maisha
ya muungano wa ndani na Mungu yanaonekana kuwa peke yake ya
kawaida kweli. Kabla ya kufikia maisha hayo, tuko bado kama watu
waliosinzia, wasioishi vya kutosha kwa hazina ile kuu tuliyokabidhiwa na Mungu.
Utakatifu
ni muungano wa ndani na Mungu, yaani ukamilifu wa upendo kwake na kwa jirani,
ukamilifu ambao hata hivyo upo katika njia ya kawaida, kwa sababu amri ya
upendo inayowapasa wote haina mipaka. Utakatifu huo hauhitaji elimu ya juu,
wala utendaji mwingi wa nje, bali kuishi kwa ndani na Mungu.
Utakatifu
huo ni utangulizi wa kawaida wa uzima wa
milele; utangulizi huo unafanyika duniani au toharani, mpaka roho iwe imetakata kabisa iweze kukaribishwa kwenye heri ya kumuona Mungu.
Hatimaye,
tukisema kuzama katika mafumbo ya imani ni karibu jambo la lazima kwa kufikia
utakatifu, maana yake ni kwamba kwa kawaida pasipo hilo haiwezekani kufikia
utakatifu ambao unadai kutekeleza kwa namna bora maadili ya Kimungu na vipaji
vya Roho Mtakatifu vinavyoongozana nayo. Ndiyo tutakayoonyesha katika kozi hii.
1. CHEMCHEMI NA LENGO LA MAISHA YA KIROHO
Kwa
kuwa maisha ya Kiroho ni namna ambayo mtu mwenye bidii anaishi kwa neema
akizidi kujitambua, tutaongelea kwanza uzima
wa neema ili kuuthamini kikamilifu. Halafu tutazingatia muundo wa Kiroho
wa maadili ya kumiminiwa pamoja na vipaji vya Roho Mtakatifu, ambavyo vyote
vinatokana na neema ya utakaso katika kila mwadilifu. Hayo yote yatatuongoza
kuzungumzia uwemo wa Utatu rohoni
mwake, na athari ya kudumu ya
Bwana wetu Yesu Kristo, aliye mshenga pekee, na ya Maria
pamoja naye kwa roho hiyo.
Ndizo chemchemi za maisha ya Kiroho tunazoikuta juu sana, kuliko chemchemi za mito zinazotoka kwenye vilele vya milima mirefu. Kwa kuwa zinatoka juu, maisha ya Kiroho yanaweza kumrudia Mungu aliye juu na kuungana naye kwa ndani.
Katika
sehemu hii ya kwanza, kisha kuongelea chemchemi za maisha ya Kiroho,
tutazungumzia lengo lake, yaani ukamilifu
wa Kikristo na wajibu wa kuulenga, kila mmoja kadiri ya hali yake maishani.
Lengo ndilo la kwanza katika kupanga nia, ingawa ni la mwisho katika
utekelezaji. Ndilo tulilo na hamu nalo toka mwanzo, ingawa tunaweza kulipata
mwishoni tu. Ndiyo sababu Bwana alianza kuhubiri kwa kutuambia juu ya heri.
Maisha
ya Kiroho yanadai Mkristo awe na hali ya
neema ya utakaso, ambayo ni kinyume cha hali ya dhambi ya mauti. Kila mtu
yupo katika mojawapo kati ya hali hizo mbili, yaani ama anamuelekea Mungu kama
lengo kuu, ama amepotoka mbali naye. Hakuna anayeweza kuwa na hali ya
kimaumbile tu, kwa kuwa wote wanaitiwa lengo linalopita maumbile, yaani
kumuona Mungu uso kwa uso na hivyo kumpenda kabisa.
Ili
mtu awe na maisha ya Kiroho haitoshi awe na neema ya utakaso, kama vile mtoto
kisha kubatizwa au mtu aliyeondolewa dhambi katika kitubio. Zaidi ya hiyo,
maisha ya Kiroho yanadai vita dhidi ya yale yote yanayoweza kutuangusha
dhambini, na juhudi halisi katika kumlenga Mungu.
Tungeng'amua
kwa ndani hali ya neema, tungeona kwamba siyo tu mwanzo wa maisha matakatifu
bali pia ni mbegu ya uzima wa milele. Ni lazima tusisitize mapema jambo hilo,
tukikumbuka neno la mt. Thoma wa Akwino: “neema ya utakaso ya mmoja ni bora
kuliko mema ya kimaumbile ya ulimwengu wote”; kwa sababu neema hiyo ni mbegu
ya uzima wa milele, ambao una ubora usio na kifani kuliko uzima wa kimaumbile
wa kwetu na wa malaika.
Ndilo
linaloweza kutuonyesha vizuri kuliko yote thamani ya neema
ya utakaso, ambayo tunaipata katika ubatizo na kurudishiwa na kitubio ikiwa
tumeipoteza. Mwanzoni mwa kozi hii ni muhimu kuthamini kweli neema hiyo ambayo
Uprotestanti umeisahau, ukifuata wanafalsafa wengi wa karne ya XIV. Hatuwezi
kujua thamani ya mbegu tusipojua kinachoweza kutokana nayo. Upande wa binadamu,
tukitaka kuthamini roho ambayo imesinzia bado katika mtoto, ni lazima tujue
nguvu ya roho ya mtu aliyekomaa. Vilevile hatuwezi kuthamini neema ya utakaso
waliyonayo waadilifu, tusipozingatia ustawi wake kamili katika uzima wa milele.
Inafaa tuuzingatie kwa mwanga wa maneno ya Bwana, ambayo ni “roho, tena ni
uzima” (Yoh. 6:63) na yana ladha bora kuliko maelezo yoyote ya teolojia.
Lugha ya Injili na mtindo wa Bwana vinatuzamisha katika sala kuliko lugha ya
kitaalamu hata ikiwa na hakika ya juu. Hakuna kinacholeta wokovu kuliko
kupumua hewa safi ya vilele vile vinavyobubujika maji hai ya mafundisho ya
Kikristo.
Neno
“uzima wa milele” ni adimu katika Agano la Kale, ambamo yote yanaelekea
ujio wa Mwokozi aliyeahidiwa. Kumbe katika mahubiri ya Yesu yote yanaelekea
moja kwa moja uzima wa milele.
Tukizingatia kwa makini maneno yake tutaona jinsi uzima huo ulivyo tofauti na maisha yajayo yaliyozungumziwa na wanafalsafa bora (k.mf. Plato)
kama hali ya kimaumbile tu na isiyo ya hakika. Kumbe Mwokozi anaongea kwa
hakika juu ya uzima wa milele, bora, usio na jana, leo na kesho, unaopita
maumbile na usiopimika, kama ule wa ndani ya Mungu, kwa kuwa unashiriki
umilele wake usiobadilika.
Yesu
alifundisha kuwa “njia imesonga iendayo uzimani” (Math. 7:14) na kuwa
tukitaka kuupata ni lazima tuache dhambi na kushika “amri” za Mungu (taz.
Math. 19:17). Mara kadhaa alisema kuwa anayemwamini “yuna uzima wa milele”
(Yoh. 5:24; 6:40,47) maana yake anayemuamini kuwa ni Mwana wa Mungu kwa imani
hai, inayoambatana na upendo na utekelezaji wa amri, ameanza kuwa na uzima wa
milele. Ndivyo alivyotamka tangu mwanzo wa mahubiri yake: “Heri walio
maskini wa roho, maana ufalme wa
mbinguni ni wao... Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa...Heri
wenye moyo safi, maana hao watamwona
Mungu” (Math. 5:3-8). Basi, uzima wa milele ni kushiba huko na kumwona
Mungu katika ufalme wake. Kwa namna ya pekee, wanaoteswa kwa sababu ya kufanya
atakavyo Mungu wanaambiwa: “Furahini na kushangilia, kwa kuwa thawabu
yenu ni kubwa mbinguni” (Math. 5:12). Yesu akajieleza zaidi tena kabla
ya mateso yake aliposema: “Baba... ulimpa Mwanao mamlaka juu ya wote wenye
mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu: wakujue
wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:1-3).
“Wapenzi,
sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua
ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana
naye, kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yoh. 3:2), yaani si kwa
kuzingatia mng'ao wa sifa zake katika viumbe (vile vinavyoonekana na roho za
watakatifu zinazojitokeza katika maneno na matendo yao), bali moja kwa moja jinsi alivyo. “Wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa
jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso
kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua
sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1Kor. 13:12). Mtume hakusema
kuwa nitamjua ninavyojijua mpaka ndani; kwa sababu najifahamu kuliko wengine,
lakini mimi pia sielewi yote niliyonayo ndani, k.mf. siwezi kupima uzito wote
wa dhambi zangu. Mungu tu ananijua fika: siri za moyo wangu anazielewa
kikamilifu yeye tu. Mbinguni nitamjua anavyonijua, moja kwa moja, pasipo kupitia kiumbe chochote
au wazo lolote la kimaumbile, kwa sababu hakuna wazo la namna hiyo linaloweza
kumchora Mungu na ukweli wake usio na mipaka, nuru angavu ya milele. Kila wazo
la namna hiyo lina mipaka, linazingatia sifa mojawapo ya Mungu (k.mf. ukweli
au wema). Mawazo hayo mbalimbali hayatoshi kutujulisha undani wa Mungu, umoja
wake usiogawanyika kamwe. Mawazo hayo
yanahusiana na uzima wake wa ndani
kama vile rangi saba za upinde wa mvua zinavyohusiana na mwanga mweupe ambao
zinatokana nao. Hapa chini sisi ni kama watu tulioona hizo rangi saba tu na
sasa tunatamani kuona huo mwanga mweupe unaozisababisha. Kabla hatujaona umungu
wenyewe hatuwezi kuona ulinganifu wa ndani wa sifa zake, hasa huruma isiyo na
mipaka na haki isiyo na mipaka. Mawazo yetu ya kimaumbile kuhusu sifa za Mungu
ni vipande tu vya sura nzima, ambavyo vinaleta picha fulani ya Mungu
isiyopendeza vya kutosha. Tukifikiria haki yake, inaonekana ni kali mno, na
tukifikiria upendeleo wa huruma yake unaonekana ukienda kinyume cha haki.
Tukitafakari zaidi tunakiri kuwa ndani
ya Mungu haki na huruma ni kitu kimoja, hazitofautiani kweli. Huo ni
ukweli ambao tunauungama kwa hakika, lakini hatujaona ulinganifu
wa ndani wa sifa hizo, kwa kuwa unahitaji tutazame umungu jinsi ulivyo,
moja kwa moja, pasipo kutumia mawazo yoyote ya kimaumbile.
Mtazamo
huo ndio uzima wa milele. Nani anaweza kueleza ukuu usiopimika wa furaha na
upendo vitakavyokuwemo ndani mwetu kutokana na mtazamo huo? Upendo wa Mungu
wenye nguvu na wa moja kwa moja, hivi kwamba hakutakuwa na lolote litakaloweza
kuupunguza; upendo ambao tutafurahia hasa kuwa Mungu ni Mungu, mtakatifu,
mwenye haki na huruma pasipo mipaka, na ambao tutaabudu mipango yote ya
maongozi yake iliyolenga ufunuo wa wema wake. Tutazama katika heri yake,
alivyosema Mwokozi mwenyewe: “Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa
mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia
katika furaha ya bwana wako” (Math. 25:21,23). Tutamuona Mungu vile
anavyojiona moja kwa moja, ingawa
hatutaweza kumaliza vilindi vya hali yake, vya upendo wake na vya uweza wake.
Pia tutampenda anavyojipenda. Vilevile tutamuona Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo
heri ya milele yenyewe, mbali ya furaha ya ziada tutakayokuwa nayo kwa kuwaona
na kuwapenda Bikira Maria pamoja na watakatifu wote, hasa tuliowafahamu
duniani.
Huo
mtazamo wa moja kwa moja wa Mungu unapita uwezo wa kimaumbile wa akili yoyote
ya malaika na ya binadamu, kwa kuwa ungehitaji ulingane
na ule wa Mungu. Basi, akili ya kiumbe inaweza kupata mtazamo huo kwa
neema ya Mungu tu, ambayo ni kama kupandikiza chipukizi la mti bora katika
shina la mti mwitu ili uzae matunda mema. Malaika na binadamu hawawezi kumjua
na kumpenda Mungu kwa namna inayopita maumbile yao kabla hawajapandikiziwa neema
ya utakaso, ambayo ni kushiriki
umungu, yaani uzima wa ndani wa Mungu. Neema hiyo tu, ikipokewa rohoni
mwetu kama zawadi isiyolipika, inatuwezesha kutenda
Kimungu, yaani kumuona moja kwa moja vile anavyojiona, na kumpenda vile
anavyojipenda. Kwa maneno mengine, akili na utashi kushirikishwa umungu
kunategemea kushirikishwa umungu kwa
roho yenyewe iliyonavyo.
Neema
hiyo ikikamilika isiweze kupotezwa inaitwa utukufu,
ambao katika akili za watakatifu wa mbinguni unatia mwanga usio wa kimaumbile unaowawezesha kumwona Mungu, na katika
utashi wao unatia upendo wa kumiminiwa
unaowawezesha kumpenda Mungu hata wasiweze kuachana naye kamwe. Kwa ubatizo
sisi tumeshapokea mbegu ya uzima wa milele, kwa kupokea neema ya utakaso
inayouleta uzima huo: pamoja na neema ya utakaso tumepokea upendo wa
kumiminiwa unaokusudiwa kudumu milele. Ndivyo Mwokozi alivyomuambia mwanamke
Msamaria: “Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, ‘Nipe
maji ninywe’, ungalimwomba yeye, naye
angalikupa maji yaliyo hai… Yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa
mimi hataona kiu milele, bali yale maji
nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa
milele” (Yoh. 4:10,14).
“Atakayekunywa
maji hai ya neema yanayotolewa na Mwokozi hatatamani mengine, ila atatamani
kuyapokea hayohayo kwa wingi zaidi... Zaidi ya hayo, tofauti na maji ya
kawaida ambayo yanaelekea chini, yale ya Kiroho yanapanda juu. Ni maji hai
ambayo hayaachani kamwe na chemchemi yake na ambayo yanabubujikia uzima wa
milele ambao yanatustahilisha” (mt. Thoma wa Akwino). Hayo maji hai yanatoka
kwa Mungu, ndiyo sababu yanaweza kurudi juu kwake.
Siku
ya mwisho ya sikukuu ya Vibanda, Yesu alisimama hekaluni, “akapaza sauti
yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile
Maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” (Yoh.
7:37-38). Anayekunywa Kiroho kwa kumuamini Mwokozi, anaweza kuchota katika
chemchemi ya maji hai, siyo kwa ajili yake tu bali pia kwa ajili ya watu
wengine ili waokoke.
Yesu
alikariri: “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele” (Yoh. 3:36). Sio tu
atakuwa nao baadaye, bali kwa namna fulani anao tayari, kwa kuwa uzima wa
neema ni mwanzo wa uzima wa milele, kama vile mbegu inavyohusiana na mti wake.
Kwa undani ni uzima uleule wa Kimungu,
ambao hapa chini umo ndani ya Mkristo kama mbegu na ambao huko juu utachanua
kikamilifu katika watakatifu. Ndiyo maana Bwana aliongeza: “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho” (Yoh. 6:54). Ufalme wa Mungu umo ndani mwetu kama mbegu ya haradali,
kama chachu itakayoumua donge lote, kama hazina iliyositirika shambani.
Tunawezaje kujua
kama tumepokea tayari uzima huo unaokusudiwa kudumu milele? “Sisi tunajua ya
kuwa tumepita toka mautini kuingia
uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti…
Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna
uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu” (1Yoh. 3:14;
5:13).
Yesu
alisema: “Amin, amin, nawaambia: Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele” (Yoh. 8:51). Kwa kuwa, inavyosema liturujia,
“Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu”, tena
unastawi kikamilifu mbinguni tu. Hakika uzima wa neema hapa duniani ni mbegu
ya utukufu, hivi kwamba kiwango kidogo cha neema ya utakaso ni bora kuliko
mema ya kimaumbile ya ulimwengu wote na ya malaika pia, kwa sababu kinahusu
hali ya juu, yaani uzima wa ndani wa
Mungu; kwa hiyo ni bora kuliko miujiza yote na ishara nyingine za nje za
ufunuo wa Mungu.
Uzima
uleule unaopita maumbile, ndio unaopatikana duniani katika waadilifu na
mbinguni katika watakatifu. Ni pia upendo uleule wa kumiminiwa, isipokuwa
tofauti mbili. Hapa chini tunamjua Mungu si kwa kumtazama mwangani, bali
katika giza la imani ya kumiminiwa.
Halafu hapa chini, ingawa tunatumaini kuwa naye kikamilifu milele, tunaweza kupotewa
naye kwa kosa letu.
Kuna
tofauti hizo mbili zinazohusu imani na tumaini, hata hivyo ni uzima uleule na
upendo uleule ambavyo vinakusudiwa kudumu milele. Kwa mwanga huo tunapaswa
kuelewa maisha yetu ya Kiroho yanavyotakiwa kuwa na kustawi hapa chini yawe
utangulizi wa kufaa kwa uzima wa milele. Ikiwa neema ya utakaso, maadili ya
kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu kwa mfumo wake vinaulenga uzima wa
milele, je havikusudiwi kulenga pia muungano wa hali ya juu na Mungu?
Kwa
kweli neema ya utakaso na upendo, vinavyotuunganisha na Mungu katika maisha
yake ya ndani, ni bora, tena sana, kuliko neema za pekee (kama vile kutabiri
na kusema kwa lugha ngeni) ambazo ni ishara tu za kazi za Mungu lakini
hazituunganishi naye (taz. 1Kor. 12:28-13:13). Hali ya kuzama katika mafumbo
ni tunda la imani tuliyomiminiwa, ikiangazwa na vipaji vya akili na vya hekima:
hivyo inatokana na neema ya utakaso, ambayo inaitwa pia “neema ya maadili na
vipaji” na tunaipata wote katika ubatizo; haitokani na neema za pekee.
Kwa
kuwa neema ya utakaso kwa mfumo wake
inalenga uzima wa milele, inalenga pia
hali ile inayohitajika ili kupata mwanga wa utukufu. Hali hiyo ni upendo
kamili pamoja na hamu kubwa ya heri ya
kumuona Mungu; kwa kawaida hamu hiyo inatokana na neema ya kuzama katika
mafumbo. Hivyo basi kuzama huko si neema ya pekee kama ulivyo k.mf. utabiri,
bali ni hali ya juu iliyopo katika njia
ya kawaida ya utakatifu, ingawa ni adimu kama ulivyo adimu ukamilifu mkuu.
Hatimaye,
kwa vile neema ya utakaso kwa mfumo wake inalenga uzima wa milele, inalenga
pia kutuweka tayari kupata mwanga wa utukufu mara baada ya kufa bila ya
kupitia toharani, ambako ni adhabu,
maana yake kunatokana na kosa lisilotakiwa pamoja na malipizi yasiyotosha; ingekuwa
kawaida kutakaswa katika maisha haya kwa kujilimbikizia stahili na kukua
katika upendo, badala ya kutakaswa kisha kufa pasipo
stahili yoyote. Hali iliyo tayari kupokea mwanga wa utukufu mara
baada ya kifo inahitaji kwanza utakaso halisi unaolingana na ule wa roho
zinazotoka toharani zenye hamu kubwa ya kumwona Mungu.
Hamu
hiyo imedhihirishwa na mt. Paulo vizuri ajabu: “Katika nyumba hii twaugua,
tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni… twaugua, tukilemewa, si
kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa… Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya
neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho” (2Kor. 5:2-5).
Tukitaka
kujadili maswala ya maisha ya Kiroho jinsi inavyotakiwa, hatupaswi kusahau
vilele hivyo tunavyojulishwa na Maandiko na kuelezwa na teolojia ya walimu
wakuu. Hasa katika maisha ya Kiroho tunatakiwa kuzingatia watu sio walivyo tu
bali wanavyokusudiwa kuwa. Tunapaswa kupumua hewa bora ya vilele vya juu,
badala ya kuishia katika hali ya wastani ya binadamu. Heri watu ambao
wanajaribiwa hata wanakuta hewa ya kuwafaa upande wa Mungu tu na kumtamani kwa
hamu kuu.
1.2.
MAISHA YA KIROHO NA MAONGEZI YA NDANI NA MUNGU
Mtu anapoacha shughuli za nje na maongezi na wenzake na kubaki peke yake - hata kama ni katikati ya kelele za jiji - mara anaanza kuwaza kama kwa kuongea na nafsi yake. Akiwa kijana anafikiria ya kesho; akiwa mzee anafikiria ya zamani, na mang'amuzi aliyonayo sasa yanamfanya apime tofauti watu na matukio. Akiwa na umimi anafuata tamaa au kiburi na hivyo ndani yake anapata huzuni tu, ndiyo sababu anajaribu kujitoroka kwa kuzama katika mambo ya nje na anasa asahau utupu wa maisha yake yasiyo na maana. Kwa kufanya hivyo anakuja kujifahamu kwa namna fulani ya hali ya chini, na vilevile kujipenda visivyo. Sanasana anajifahamu upande wa hisi, alizo nazo sawa na wanyama; hivyo ana furaha na uchungu vya kihisi kadiri ya mabadiliko ya hali ya hewa au ya biashara yake. Anavyovitamani na anavyovichukia ni vya aina hiyohiyo, na akipingwa anakasirika kutokana na jinsi anavyojipendea.
Kumbe
anajifahamu kidogo tu upande wa roho, ambayo inalingana na malaika. Hata kama
anaamini ukuu wa roho (yenye akili na utashi) haishi katika ngazi hiyo: hana
mang'amuzi kuhusu sehemu hiyo bora ya utu wake, wala haipendi vya kutosha.
Angeijua angeona ndani yake sura ya Mungu na kuanza kujipenda kwa ajili ya
Mungu, si tena kujipendea kibinafsi. Hata akionyesha mara nyingi uwezo wa
kuelewa na kutenda kwa ujanja, akili yake inaelekea daima yaliyo ya chini
kuliko yeye. Ingawa ameumbwa ili kumtazama Mungu, ukweli mkuu, anafuata
udanganyifu hata kuutetea kwa kila njia. Maisha yasipofuata ubora wa mawazo,
mawazo yatafuata uduni wa maisha: yote yanafungamana, hata misimamo mizuri
aliyokuwa nayo inadhoofika zaidi na zaidi.
Hivyo
maongezi ya ndani yake yanaelekea mauti na hayastahili kuitwa maisha ya Kiroho.
Kujipendea kwake kunamfanya ajione kiini cha yote, na kuelekeza yote (watu na
vitu) kwake; lakini hiyo haiwezekani, ndiyo sababu mara nyingi anakata tamaa
na kuchukizwa, havumiliki kwake wala kwa wengine. Kwa kutaka kujipendea
mwishowe anajichukia pamoja na maisha, kwa kuwa katika maisha alitamani mno
yaliyo ya chini.
Kumbe
binadamu akianza kutafuta uadilifu, hata kama hajawa na neema ya utakaso,
maongezi yake na nafsi yake yanakuwa tofauti: k. mf. anazingatia
yanayohitajika ili aishi kwa haki na kutegemeza familia yake. Pengine mawazo
hayo yanamletea mahangaiko hata kumfanya atambue unyonge wake na haja ya
kumtegemea Mungu badala ya kujiamini tu. Akiwa na dhambi ya mauti isiyo dhidi
ya imani wala tumaini anaweza kuwa na maadili hayo yanayodumu ndani mwetu hata
baada ya kupoteza upendo. Kama ni hivyo pengine mawazo yake yanaangazwa na
imani ambayo mwanga wake unapita maumbile yetu; anaweza akawaza uzima wa
milele na kuutamani, ingawa si zaidi; tena pengine anajisikia msukumo wa
kwenda kanisani.
Hatimaye,
mtu huyo akijuta na kuondolewa makosa yake, anarudishiwa neema ya utakaso na
upendo kwa Mungu na kwa jirani. Kuanzia hapo, mawazo yake yanakuwa mengine.
Anaanza kujipenda kitakatifu, yaani si kwa ajili yake, bali kwa ajili ya Mungu, na kuwapenda watu pia kwa ajili ya Mungu;
anaanza kuelewa anavyopaswa kusamehe na kupenda maadui, na kuwatakia uzima wa
milele vile anavyojitakia. Lakini mara nyingi mawazo yake yanaendelea
kuchafuliwa na umimi, ubinafsi, tamaa na kiburi. Kwake makosa hayo si tena ya
mauti, lakini yakitokea mara nyingi yanamfanya arudie dhambi kubwa na mauti ya
roho. Hapo mtu atajaribu tena kujitoroka, kwa sababu haoni uzima ndani mwake;
ndiyo maana asipojifikiria upya atazidi kujitupa mikononi mwa anasa na kiburi.
Hata
hivyo maongezi ya ndani mwake yanaanza
tena yasiweze kuzuiwa na chochote, wala na yeye mwenyewe. Ndani mwa roho
mna haja inayodai kutimizwa. Mungu tu anaweza kufanya hivyo, kwa hiyo njia
pekee ni kumuendea yeye. Roho inahitaji
kuongea naye kwa sababu lengo lake kuu ni Mungu
aliye hai, hata isiweze kutulia isipokuwa ndani ya Mungu.
Basi,
maisha ya Kiroho ni maongezi ya kila mtu na nafsi yake kuinuliwa na kugeuka
sura mara yanapoanza kuwa maongezi na Mungu. Ni kwamba Roho wa Mungu
anawaonyesha zaidi na zaidi watu wenye mapenzi mema yale ambayo anayataka toka
kwao na yale anayotaka kuwazawadia. Lo, kama tungepokea kwa mikono miwili yale
yote Mungu anayotaka kutupatia!
Maonyesho
hayo hayafanyiki pasipo juhudi; tunapaswa kuokoka katika vifungo vitokanavyo
na dhambi, kufisha hatua kwa hatua “utu wa zamani” na kuunda “utu wa ndani”: “Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa
ndani; lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na
ile sheria ya akili zangu” (Rom. 7:22-23) “Utu wa ndani” ndio kilicho
bora ndani mwetu, yaani akili utashi ambavyo vinapaswa kutawala mwili, ulio
sawa kwa mtu na kwa mnyama.
“Kwa
hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu
wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku” (2Kor. 4:16). Nguvu za
Kiroho zinafanywa upya mfululizo kwa njia ya neema tunazozipokea kila siku.
“Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo
yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya
upate ufahamu sawasawa na mfano wake
yeye aliyeuumba” (Kol. 3:9-10). Baba “awajalieni, kwa kadiri ya
utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara
kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika
utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja
na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo na kina; na kuujua
upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate
kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef. 3:16-19).
Ndiyo
maisha ya Kiroho na vilindi vyake, maisha yale yanayolenga mfululizo
kulitazama fumbo la Mungu na kulifanya chakula chake katika muungano naye wa
ndani zaidi na zaidi. Mtume aliandika hayo kwa Wakristo wote, sio kwa
mmojammoja tu. Akaongeza: “Mfanywe
wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya
Mungu katika haki na utakatifu wa kweli… mkaenende
katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa
ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato”(Ef.
4:23-24; 5:2).
Kwa
kuzingatia maneno hayo ya Mungu tunaweza kufafanua maisha ya Kiroho kama
ifuatavyo: maisha ya Kiroho ni maisha
ambayo yanapita maumbile na kutuelekeza na kutufikisha kwenye muungano na
Mungu kwa njia ya kujikana na kusali kweli.
“Mafundisho
ya Yesu Kristo yanapita mafundisho yoyote ya watakatifu na mtu aliye na roho
yake anakuta humo mana iliyositirika. Lakini inatokea kuwa wengi, kwa kusikia
Injili mara nyingi, hawaguswi inavyotakiwa, kwa sababu hawana roho yake.
Mnataka kuelewa mpaka ndani na kufurahia maneno ya Yesu Kristo? Mjitahidi
kulinganisha maisha yenu yote na ya kwake” (Kumfuasa Yesu Kristo,
I,1:2).
Maisha
hayo yana hatua ya kwanza inayotawaliwa na utakaso, ya pili inayotarajia
mwanga mkubwa zaidi na zaidi, na lengo lake la mwisho ni kuungana na Mungu.
Ndivyo mapokeo yote yanavyofundisha, yakithibitisha uwepo wa hatua ya
kutakaswa kwa wanaoanza, hatua ya kuangazwa kwa wanaoendelea, na hatua ya
kuungana na Mungu kwa waliokamilika. Hivyo maisha ya ndani ya mtu yanakuwa
zaidi na zaidi maongezi na Mungu.
Kwa
namna hiyo, mtu anaanza kung'amua sehemu bora ya nafsi yake na kumjua Mungu.
Polepole mawazo ya nafsi yake aliyoifanya kuwa lengo la yote, yanaiachia
nafasi kumbukumbu ya kudumu ya Mungu. Vivyo hivyo kujipendea kunaacha nafasi
kwa upendo wa Mungu na wa watu kwa ajili yake. Maongezi ya ndani yanabadilika
hata kusema: “Sisi, wenyeji wetu uko mbinguni” (Fil. 3:20).
Katika
roho yenye neema ya utakaso, maisha ni hasa ya unyenyekevu, kujikana, imani,
tumaini na upendo, pamoja na amani inayotakana na kuweka miguso na matakwa
yote chini ya upendo wa Mungu atakayekuwa heri yetu. Basi, ili tuwe na maisha
ya Kiroho haitoshi tushughulikie sana utume wala kujua sana dini. Tena hayo si
ya lazima. Mtu aliyeanza tu kujikana na kusali kwa juhudi, anayo tayari maisha
ya Kiroho ambayo yanatakiwa kustawi zaidi na zaidi.
Katika
maongezi hayo yanayoelekea kuwa ya kudumu roho inasema kwa njia ya sala,
ambayo ingekuwepo hata kama Mungu angemuumba mtu mmoja au malaika mmoja tu.
Sala inaweza kuwa ya kuomba, ya kuabudu au ya kushukuru; lakini daima ni
kuinua roho kwa Mungu. Naye Mungu anajibu akitukumbusha yale ambayo tuliambiwa
katika Injili na yanatufaa kuitakasa nukta ya sasa hivi: “Huyo Msaidizi,
huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote,
na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yoh. 14:26)?
Hivyo
mtu anazidi kuwa mtoto wa Mungu, anatambua zaidi na zaidi kuwa Mungu ni Baba
yake na anazidi kujifanya mdogo mbele yake. Anaelewa yale Yesu aliyomuambia
Nikodemu, yaani kuwa ni lazima kurudi katika tumbo la Mungu ili kuzaliwa upya
Kiroho kila siku zaidi, k.mf. wa Neno kuzaliwa milele. Wenye heri wa mbinguni
wanabaki daima katika tumbo hilo.
Watakatifu
wanafuata njia hiyo, hata maongezi kati yao na Mungu hayana mwisho. Mt.
Dominiko hakuweza kusema isipokuwa juu ya Mungu au na Mungu; ndiyo sababu
alikuwa amejaa daima upendo kwa watu. Maongezi hayo na Mungu yanaundwa kwa
njia ya Kristo mshenga: “Ulimi hauwezi kusema, / wala maandishi kufafanua, /
aliyeng'amua tu anaweza kuamini / kumpenda Yesu ni nini” (Utenzi wa Jina
Takatifu la Yesu).
1.3.
MUUNDO WA KIROHO
Ili
tuelewe mbegu ya uzima wa milele iliyomo ndani mwetu ni nini, tunatakiwa
kuzingatia jinsi neema ya utakaso inavyoleta katika akili na utashi maadili ya
kumiminiwa na vipaji saba vya Roho Mtakatifu. Maadili hayo na vipaji hivyo ni
kama utendaji wa muundo uleule mmoja wa Kiroho unaokusudiwa kustawi hadi
tuingie mbinguni.
1.3.1. MAISHA YA KIMAUMBILE NA YANAYOPITA MAUMBILE
Kwanza
tutofautishe vizuri ndani ya roho yetu yale yaliyo ya kwake kwa jinsi
ilivyoumbwa, na yale ambayo ni zawadi tu ya Mungu. Hata malaika, ingawa ni
roho tu, ana maumbile ya chini kuliko neema ya utakaso.
Basi,
sisi binadamu tuna pande mbili tofauti:
upande wa hisi na upande wa akili. Wa
kwanza unalingana na wanyama, ukiwa na hisi za nje (milango ya fahamu),
hisi za ndani (ubunifu na kumbukumbu) na uwezo wa kupatwa na maono mbalimbali
(k.mf. pendo na chuki, hamu na hofu, furaha na huzuni, hasira).
Juu
ya sehemu hiyo, katika maumbile yetu ipo
nyingine inayolingana na malaika, ingawa ndani mwao ina nguvu na uzuri
zaidi. Upande huo roho inapita mwili, maana yake haitegemei mwili moja kwa
moja, kwa hiyo inaweza kudumu baada ya mwili kufa.
Kutokana
na maumbile ya roho upande huo wa juu tuna uwezo wa akili na wa utashi. Akili
inajua sio tu sifa ya viumbe zinazohisikana (rangi, sauti), bali undani wao na
kweli zisizobadilika kama vile: “Hakuna kinachotokea pasipo sababu, na hasa
pasipo sababu kuu, yaani Mungu”. “Tunapaswa kutenda mema na kuepa maovu”.
“Timiza wajibu wako, liwalo na liwe”. Mnyama hataweza kamwe kujua kweli
hizo.
Kwa
kuwa akili inaweza kujua sio tu yale yanayotupendeza au yanayotufaa bali pia
uadilifu (k.mf. kwamba ni “afadhali kufa kuliko kusaliti”), basi utashi unaweza kupenda huo uadilifu, kuutaka na kuutekeleza. Hivyo
unapata kutawala hisi na maono alivyonavyo mnyama pia. Kwa akili na utashi mtu
anafanana na malaika, ingawa katika maisha haya akili yetu, tofauti na malaika,
inazitegemea hisi katika kuanza kujua mambo.
Tunavyoona
katika watu kadhaa, akili na utashi vinaweza vikastawi, pasipo kufikia kujua
na kupenda maisha ya ndani ya Mungu,
ambayo ni ya ngazi tofauti, juu kupita maumbile ya malaika na ya binadamu. Hao
wanaweza kumjua kimaumbile Mungu kwa nje, kutokana na mng'ao wa sifa zake
katika viumbe, lakini haiwezi kuumbwa akili yenye nguvu ya kuyajua yaliyo ya
Mungu tu: “Ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya
binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo
ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1Kor. 2:11).
Kumbe
neema ya utakaso inatuingiza katika hiyo hali ya juu ya ukweli na uzima
inayopita maumbile yoyote. Ni uzima unaopita maumbile, kwa kuwa unashiriki
maisha ya ndani ya Mungu, ni hali ya Kimungu ambayo tangu sasa inatuandaa kumuona milele anavyojiona na kumpenda anavyojipenda.
“Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia
katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini
Mungu ametufunulia sisi kwa Roho”
(1Kor. 2:9-10).
Neema
ya utakaso inayotuwezesha kuanza kuishi maisha ya ndani ya Mungu, katika ngazi
ya juu kuliko maumbile ya malaika, ni kama chipukizi la Kimungu
lililopandikizwa ndani mwa roho ili kuinua uzima wake na kuifanya izae sio tu
matunda ya kimaumbile, bali matunda yanayopita maumbile, yaani matendo
yanayostahili uzima wa milele. Kupandikizwa huko kunapita miujiza
inayojulikana na hisi. Kwa mfano, ufufuo unaurudishia mwili uhai wa kimaumbile,
ndiyo sababu unaweza kujulikana na maumbile yetu; kumbe neema ya utakaso
inaipatia roho uzima usio wa kimaumbile, ndiyo sababu hauwezi kuhakikishwa na
maumbile yetu.
Tangu
sasa uzima huo wa neema unachanua ndani mwetu maadili
ya kumiminiwa na vipaji saba vya Roho Mtakatifu. Kama vile katika maumbile
yetu roho ina uwezo wa akili na kadhalika, katika ngazi inayopita maumbile
neema ya utakaso inaleta rohoni maadili na vipaji hivyo ambavyo, pamoja na
mzizi unaovisababisha, ndio muundo unaopita maumbile ambao tulijaliwa katika
ubatizo (na tunarudishiwa na ondoleo la dhambi ikiwa tuliupoteza).
Muundo huo wa Kiroho unaweza
kuonyeshwa na jedwali ifuatayo:
MAADILI
VIPAJI
Upendo
Hekima
YA
KIMUNGU
Imani
Akili
Tumaini
Elimu
Busara
Shauri
Haki
(Ibada)
Ibada
(Toba)
(Utiifu)
YA
KIBINADAMU Nguvu
Nguvu
(Subira)
Kiasi
Uchaji wa Mungu
(Upole)
(Unyenyekevu)
(Usafi wa moyo)
1.3.2. MAADILI YA KIMUNGU
Maadili
ya Kimungu ni maadili tunayomiminiwa yanayomhusu Mungu mwenyewe aliye lengo
letu kuu. Tofauti na hayo, maadili ya kibinadamu yanahusu njia za kufikia
lengo hilo.
Kati
ya maadili ya Kimungu, imani
inatuwezesha kusadiki yale yote ambayo
Mungu ametufunulia, kwa sababu ndiye ukweli wenyewe. Ni kama hisi ya
Kiroho inayotuwezesha kusikia muziki safi wa Kimungu usiojulikana kwa njia
nyingine yoyote, maana kuna tofauti kubwa kati ya kusoma Injili kihistoria au
kitaalamu na kuiamini kama Neno la Mungu, kwa kuwa kusadiki
ni tendo linalopita maumbile yetu na ya malaika, likituingiza katika
ulimwengu wa juu. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo
hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef. 2:8). Ndiyo msingi
wa kufanywa waadilifu, kwa kuwa inatujulisha lengo lipitalo maumbile
tunalopaswa kulikusudia. “Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa
haki” (Mwa. 15:6; Rom. 4:3,9). “Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu
kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi tutakaohesabiwa vivyo
hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu” (Rom.
4:23-24). Sisi tutaokoka tu kwa imani hiyo ambayo ni zawadi ya Mungu. Kanisa
lilitamka rasmi dhidi ya Wapelajiupande kwamba hata
mwanzo wa imani ni neema. Imani hiyo inapita
kabisa maumbile, siyo tu kama muujiza unaoonekana au kama utabiri wa tukio
la kawaida (k.mf. mwisho wa vita); kwa sababu imani inamhusu kwanza Mungu
mwenyewe katika maisha yake ya ndani, ambaye hawezi kujulikana kimaumbile,
tena kwa sababu tunasadiki kwa kutegemea mamlaka
ya Mungu aliyejifunua, ambayo pia haiwezi kujulikana na maumbile. Imani
inatufanya tushike kwa namna ipitayo maumbile na isiyoweza kukosa, yale
ambayo Mungu ametufunulia kadiri tunavyofundishwa na Kanisa
lililokabidhiwa ufunuo huo.
“Tazama,
msomi fulani anachimba mafundisho ya Kikatoliki bila ya kuyakataa kwa ukaidi,
bali anakariri, Heri nyinyi mlio na imani; mimi pia ninapenda kuwa nayo lakini
siwezi. Anasema ukweli: anataka asiweze (bado); kwa sababu kusoma na kuwa na
nia njema hakufikii daima kujua ukweli, ili ionekane wazi kuwa hakika
ya akili si hakika kuu inayotegemeza mafundisho ya Kikatoliki… Kinachotokea
ndani mwetu tunapoamini ni tukio la
mwanga wa ndani unaopita maumbile yetu... Mwongofu atawaambia, Nilisoma,
nilitafakari, nilitaka nisifike; lakini siku fulani, siwezi kusema vipi,
kwenye pembe ya njia, au nyumbani karibu na moto, sijui, sikuendelea kuwa
yuleyule, nimesadiki... Kilichotokea ndani mwangu katika nukta ya kupata
hakika kuu ni jambo tofauti kabisa na yale yote yaliyotangulia. Muwakumbuke
wanafunzi wale wawili waliokwenda Emau” (H. Lacordaire).
Imani
tunayomiminiwa ni kama uwezo wa kusikia ambao unapita maumbile na kutuwezesha
tusikilize sauti ya Mungu kupitia manabii na Mwanae mwenyewe, kabla
hatujakaribishwa kumuona uso kwa uso. Kati ya mtu anayesoma Injili bila ya
imani, na mwingine mwenye imani, tofauti ni kama ile iliyopo kati ya watu
wawili wanaosikiliza muziki fulani, lakini mmojawao ana karama ya muziki,
mwingine hana. Wote wanasikia noti zote, lakini yule wa kwanza tu anaelewa
undani na ujumbe wa muziki ule. Vivyo hivyo mwamini tu, hata kama hajui kusoma,
anashika Injili kwa namna ipitayo maumbile na kama Neno la Mungu linalopita maumbile, wakati msomi pamoja na elimu yake
yote hawezi kuishika hivyo pasipo imani ya kumiminiwa. “Yeye amwaminiye
Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa
mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe”
(1Yoh. 5:10).
Miaka
mia iliyopita mtu asiyejua redio angeshangaa kuambiwa siku moja ataweza
kusikia muziki unaochezwa wakati huohuo katika nchi nyingine. Kwa imani ya
kumiminiwa tunasikia muziki wa mbinguni. Nyimbo za muziki huo ni mafumbo ya
Utatu, umwilisho, ukombozi, misa na uzima wa milele. Kwa kusikiliza hayo mtu
anaongozwa zaidi na zaidi kwenye kilele kile kinachotoka muziki huo bora.
Ili
aelekee kweli lengo hilo na kulifikia, mtu amepewa mabawa mawili, tumaini na upendo. Pasipo
hayo anaweza kuelekea tu anapoelekezwa na akili yake; kumbe akiwa nayo
anarukia anapoelekezwa na imani. Kama vile akili yetu pasipo mwanga wa imani
haiwezi kujua lengo letu lipitalo maumbile, utashi wetu pia hauwezi kuelekea
lengo hilo nguvu zake zisipozidishwa na kuinuliwa kwenye ngazi ya juu.
Kwa tumaini
tunatamani kumpata Mungu, na kusudi tumfikie tunategemea si nguvu za maumbile
yetu, bali msaada aliotuahidia.
Tunamtegemea mwenyewe aliye tayari daima kusaidia wanaomuitikia.
Upendo ni kumpenda Mungu kwa namna bora zaidi,
isiyojitafutia faida tu; unatufanya
tumpende Mungu sio tu ili tumpate hapo baadaye, bali kwa ajili yake na kuliko tunavyojipenda, kutokana na wema wake usio
na mipaka, unaopendeza kuliko fadhili zake zote. Unatufanya tumpende Mungu
hasa kama rafiki aliyetangulia
kutupenda. Unamuelekezea vitendo vya maadili mengine yote ukiyahuisha na
kuyafanya yaweze kustahili. Ndio nguvu yetu kuu inayopita maumbile, nguvu ya upendo ambayo katika karne za dhuluma imeshinda vipingamizi
vyote, hata katika viumbe dhaifu kama watakatifu Anyesi na Lusia.
Hivyo
mwenye mwanga wa imani anamuelekea Mungu akiruka kwa mabawa ya tumaini na
upendo. Lakini akitenda dhambi ya mauti, mara anapoteza neema ya utakaso na
upendo, kwa kuwa anajitenga na Mungu akiacha kumpenda kuliko nafsi yake. Hata
hivyo huruma ya Mungu inamuachia imani na tumaini (mpaka atakapotenda dhambi
dhidi ya maadili hayo) awe bado na mwanga wa kumuelekezea njia na aweze bado
kutegemea huruma isiyo na mipaka ili kuomba neema ya uongofu.
Kati
ya maadili hayo ya Kimungu, upendo ndio la juu zaidi, nao utadumu milele
pamoja na neema ya utakaso, ambapo imani na tumaini vitakoma na badala yake
mtu atakuwa na Mungu akimjua waziwazi, bila ya hofu ya kupotewa naye (taz.
1Kor. 13:8,13). Ndio utendaji wa juu wa muundo wa Kiroho: maadili matatu ya
Kimungu ambayo yanastawi pamoja, halafu maadili ya kibinadamu yanayoendana
nayo.
1.3.3. MAADILI YA KIBINADAMU
Ili
tuzielewe taratibu za muundo wa Kiroho, ni muhimu tujue vizuri maadili ya
kibinadamu, yaliyo chini ya yale ya Kimungu. Jina linavyosema, ya kwanza
yanapatikana kwa kurudiarudia vitendo vyake; yalijulikana na wapagani pia kwa
kuwa yana lengo linalojulikana na akili.
Baadhi
ya watu waliojitoa kwa Mungu hawajali vya kutosha maadili hayo katika ujana
wao; kinyume chake wengine wenye umri mkubwa zaidi, kisha kutambua umuhimu wa
maadili hayo hawajali tena vya kutosha maadili ya Kimungu, ambayo ni bora
pasipo mfano, kwa kuwa ndiyo yanayotuunganisha na Mungu.
Basi
tupande ngazi kwa ngazi kutoka uadilifu wa kimaumbile hadi ule unaopita
maumbile. Tuangalie kwanza mtu mwenye dhambi ya mauti anavyoweza kuwa na maadili
ya uongo, k.mf. kiasi cha mchoyo; yeye anakitekeleza si kwa kupenda
uadilifu, bali kwa kupenda fedha. Vilevile akilipa madeni si kwa kutekeleza
haki bali kwa kukwepa gharama za kesi.
Juu
kuliko hayo maadili ya uongo, mtu mwenye dhambi ya mauti anaweza kuwa na maadili
halisi ya kibinadamu aliyojipatia. Wako wengi wanaofuata kiasi ili kuishi
akili inavyotaka, na kwa ajili hiyohiyo wanalipa madeni na kuwalea vizuri
watoto wao.
Lakini
mpaka mtu anapozidi kubaki katika dhambi ya mauti, hayo maadili halisi hayana
msimamo, kwa kuwa utashi wake haumuelekei Mungu: badala ya kumpenda kupita
yote, anajipenda kuliko Mungu. Ndiyo sababu ni dhaifu katika kutekeleza
uadilifu, hata ule wa kibinadamu. Zaidi ya hayo, maadili halisi yanayopatikana
katika mtu mwenye dhambi si imara kwa kuwa maadili mengine yanayotakiwa
kuyasaidia hayapo, hivyo hayawezi
kushikamana. Anayeendesha gari la kukokotwa na farasi kadhaa, anahitaji
kila mmoja wao awe amezoea kazi hiyo: vilevile adili moja haliwezi kwenda bila
ya lingine; yote yanahusiana na kuongozwa na busara.
Basi,
ili maadili ya kibinadamu yawe imara
ni lazima yashikamane, na hiyo inadai mtu asibaki katika dhambi ya mauti, bali
utashi wake ulenge kweli kuishi na Mungu; ni lazima ampende kuliko nafsi yake,
jambo ambalo haliwezekani pasipo neema ya utakaso na upendo.
Akipata
hayo, hapo maadili yote yanaweza kushikamana na kuwa imara; nayo chini ya
upendo yanakuwa chanzo cha matendo yanayostahili uzima wa milele. Maadili ya
Kimungu yanatuinua na kuturekebisha kuhusu lengo lipitalo maumbile na kuhusu njia
zipitazo maumbile zinazoweza kutufikisha kwenye lengo hilo kuu. Bila ya
hayo, maadili ya kibinadamu hayatoshi: kuna tofauti
ya dhati kati ya kiasi walichokieleza wapagani na kile cha Kikristo (k.mf.
kati ya ufukara wa mwanafalsafa na ule wa Kiinjili), kwa sababu kanuni na lengo ni tofauti
: cha kwanza kinataka mtu ale tu kipimo cha wastani ili
kufuata akili, kutodhuru afya au kuweza kutumia akili yake vizuri. Kumbe
kiasi cha Kikristo kinataka mtu ajipatie chakula ili
kuishi kama mtoto wa Mungu, akielekea uzima wa milele unaopita maumbile;
hivyo kinadai maisha magumu zaidi; kinadai mtu autese mwili wake “na
kuutumikisha” (1Kor. 9:27), kusudi asiwe tu raia mwadilifu wa nchi yake,
bali pia mwenyeji “pamoja na watakatifu” na mtu “wa nyumbani mwake Mungu”
(Ef. 2:19).
Tofauti
hiyohiyo ipo kati ya adili la ibada linalotakiwa kumpatia Muumba heshima
anayostahili, na adili la ibada la Mkristo linalomtolea Mungu asili ya neema,
sadaka ya misa ipitayo maumbile. Ni tofauti ya ngazi, hivi kwamba aina ya
kwanza inaweza kustawi mfululizo kwa kurudiarudia vitendo vyake, lakini bila
ya kufikia kiwango kidogo cha aina ya pili iliyoinuliwa na neema ya utakaso.
Kinachoongoza maadili hayo mawili yenye jina lilelile moja ni tofauti: upande
mmoja ni akili ya binadamu, upande wa pili ni imani iliyomiminwa na Mungu.
Ni
malengo mawili tofauti na nia mbili tofauti, ambapo busara haijui nia zipitazo
maumbile, ila ikiangaziwa na imani inakuja kuzijua kwa kujua ukuu usio na
mipaka wa lengo letu, yaani kumuona Mungu uso kwa uso; hapo inakuja kujua uovu
wa dhambi ya mauti, thamani ya neema ya utakaso na ya neema za msaada ambazo
ziombwe kila siku, na hazina ya sakramenti zilizowekwa kwa faida yetu.
Vilevile
kuna tofauti kubwa kati ya utaratibu ulioelezwa na mwanafalsafa Aristotle na
unyenyekevu wa Kikristo unaozitegemea kweli za imani. Kuna tofauti kubwa kati
ya ubikira wa wanawake waliokabidhiwa kuchochea daima moto wa miungu, na ule
wa Mkristo aliyejiweka wakfu mwili na moyo kwa Mungu ili kumfuata Yesu
kikamilifu zaidi.
Upendo
unapoturekebisha tulenge uzima wa milele upitao maumbile, unarekebisha maadili
pia kuhusu njia zipitazo maumbile za kufikia wokovu. Kumbe katika dhambi ya
mauti mtu anajipenda kuliko Mungu na kwa umimi anaelekea kutotimiza wajibu
wake wa kiutu pia.
Katika
utekelezaji walioendelea Kiroho wanaongozwa zaidi na kwa namna wazi na hiyo
nia ipitayo maumbile, kumbe ni nia ya kibinadamu inayozidi kuwaongoza wengine.
Maadili
ya kibinadamu yanasimama katikati ya
pande mbili tofauti, ambazo mmoja umezidisha na mmoja una upungufu. Kwa mfano,
adili la nguvu linatufanya tusimame katikati ya woga (unaokimbia hatari bila
ya sababu yenye msingi) na ushupavu (unaotaka kuvunjika kichwa bila ya sababu
ya kutosha). Lakini, ebu! hiyo katikati isieleweke vibaya. Wanaopenda anasa na
watu vuguvugu wanataka kusimama katikati si kwa kupenda uadilifu, bali kusudi
waepe matatizo ya vilema vinavyopingana pande hizo mbili. Hao wanachanganya
hiyo katikati na ule wastani ambao
haupatikani katikati ya vilema viwili vinavyopingana bali katikati ya njia
inayoongoza kutoka uovu kwenda uadilifu.
Wastani huo unakimbia uadilifu wa juu ukijisingizia kuwa “pengine yaliyo
bora yanazuia yaliyo mema”, ukiwa na maana ya kwamba, eti “mara nyingi au
daima yaliyo bora yanazuia yaliyo mema”.
Kumbe
hiyo katikati halisi ya uadilifu haisimami tu katikati ya vilema viwili
vinavyopingana, bali juu ya hivyo kama kilele. Inainuka juu ya upotovu wa
pande hizo mbili tofauti: busara halisi iko juu ya upumbavu na ujanja; ukarimu
uko juu ya choyo na ubadhirifu; adili la ibada liko juu ya dharau ya dini na
ushirikina.
Tena
hiyo katikati ambayo ni pia kilele inaelekea
kuinuka pasipo kupotoka upande mmoja wala upande mwingine kadiri
uadilifu unavyokua, kwa kufuata kanuni ya juu na lengo la juu.
Hatimaye,
tuzingatie kuwa Injili na walimu wa kiroho wanasisitiza baadhi ya maadili ya kibinadamu ambayo yanahusiana zaidi na Mungu na
kulingana zaidi na maadili ya Kimungu, nayo ni: ibada na toba (zinazompatia
Mungu heshima na malipizi anavyostahili), upole (ukiambatana na subira), usafi
kamili (au ubikira) na unyenyekevu ambao ni adili la msingi kwa kuwa unashinda
kiburi kilicho chanzo cha dhambi zote. Unyenyekevu ukituinamisha mbele ya
Mungu unatuinua juu ya ufinyu wa moyo na juu ya kiburi na kutuelekeza kuzama
katika mambo ya Mungu na kuungana naye. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu,
kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini
mwenu” (Math. 11:29). Yesu tu, kwa jinsi alivyojijenga katika ukweli,
aliweza kusema juu ya unyenyekevu wake pasipo kuupoteza papohapo.
Maadili ya kibinadamu na yale ya Kimungu ambayo yanayaongoza, ni utendaji wa aina mbalimbali wenye kulingana vizuri ajabu, dhambi nyepesi isipokuja kuvuruga. Ni lazima tukeshe kitu chochote kisije kikaharibu ulinganifu wa muundo huo, kama inavyotokea kwa wale ambao wanadumu katika neema ya utakaso lakini wanajali elimudunia na mafungamano na watu kuliko ustawi wa imani, tumaini na upendo wa Mungu. Halafu haiwezekani kuwa na upendo mkubwa pasipo unyenyekevu mkubwa, kama vile tawi la juu la mti linazidi kwenda juu kadiri mzizi unavyozidi kupenya ardhi.
Sehemu zote za muundo huo wa Kiroho zinakua pamoja kama vidole vitano vya mkono mmoja. Kutokana na mshikamano uliopo maadili yote yanakua pamoja na upendo, lakini hasa maadili ya Kimungu kwa kuwa yale ya kujipatia pengine yanastawi kwa kasi ndogo zaidi yasipofanyiwa mazoezi.
1.3.4. VIPAJI SABA VYA ROHO MTAKATIFU
Kusudi
tujue kweli muundo wa Kiroho, haitoshi kuyajua maadili. Ni lazima tuseme pia
juu ya vipaji saba vya Roho Mtakatifu, pasipo kusahau namna mbalimbali za
kupata msaada wa Mungu.
Ufunuo
kuhusu vipaji vya Roho Mtakatifu unapatikana hasa katika dondoo la Isaya 11:2
ambalo linamhusu kwanza Masiha, halafu kwa kumshiriki yeye linawahusu
waadilifu wote ambao Yesu aliahidi kuwapelekea Roho Mtakatifu. Maneno yenyewe
ni haya: “Roho ya Bwana atakaa juu yake, roho
ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya
kumcha Bwana”. Kipaji cha ibada hakitajwi katika lugha asili ya Kiyahudi,
bali katika tafsiri za Septuaginta na Vulgata, na kuanzia karne ya tatu
mapokeo yanashika idadi ya vipaji saba. Halafu, Isaya 11:3 kwa Kiyahudi
inataja tena “kumcha Bwana”, ambapo katika Agano la Kale “kumcha
Bwana” na “ibada” ni maneno mawili yenye maana karibu ileile.
Katika
kitabu cha Hekima tunasoma: “Naliomba,
nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua
kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu
ikilinganishwa nayo; wala sikuifananisha na kito cha thamani, mradi dhahabu
yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama
udongo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru
nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo
nikajiliwa na mema yote jamii… ingawa sijajua ya kama yeye ndiye aliyeyazaa…
Maana yeye amekuwa hazina kwa wanadamu isiyowaishia; nao wale waitumiao
hujipatia urafiki na Mungu… na tangu
kizazi hata kizazi huwaingilia roho takatifu, huwafanya wanadamu kuwa
rafiki za Mungu na manabii” (Hek. 7:7-11,12,14,27).
Ufunuo
wa Agano la Kale umetimilizwa na Mwokozi: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.
Nami nitamwomba Baba, naye atawapa
Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli…
anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu… huyo Roho
Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yoh.
14:15-17,26). Yohane, akitaka kuwakinga waamini dhidi ya wazushi akaongeza:
“Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu… Nanyi, mafuta yale
mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha;
lakini kama mafuta yake
yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo”
(1Yoh. 2:20,27).
Katika Maandiko yapo pia madondoo kuhusu vipaji kimojakimoja.
Mababu
wa Kanisa waliyafafanua mara nyingi maneno hayo ya Maandiko, na kuanzia karne
ya tatu mapokeo yanatamka wazi kuwa vipaji saba vya Roho Mtakatifu vimo ndani
ya waadilifu wote. “Hivyo vipaji vya Roho Mtakatifu kwetu ni kama chemchemi
ya Kimungu tunapochota ujuzi hai wa amri za maisha ya Kikristo, na kwa njia ya
hivyo tunaweza kujua pia kama Roho Mtakatifu anakaa ndani mwetu au la” (Katekisimu
ya Mtaguso wa Trento).
Ushuhuda
wa Mapokeo kuhusu vipaji saba unapatikana katika liturujia ya Pentekoste, hasa
katika sekwensya “Uje Roho Mtakatifu”: “Wape waamini wako, / wenye
tumaini kwako, / paji zako zote saba”. Tunaukuta vilevile katika utenzi
“Uje Roho Muumbaji”: “Mtoa wa vipaji saba... / tia nuru akilini / na
upendo mioyoni”.
Ushuhuda
wa Mapokeo ulielezwa vizuri na Leo XIII: “Mwadilifu
anayeishi kwa neema ya utakaso na kutenda kwa njia ya maadili kama kwa viungo
mbalimbali (vipya), anahitaji kabisa
vipaji saba, ambavyo vinaitwa kikamilifu zaidi vipaji vya Roho Mtakatifu. Kwa
vipaji hivyo roho ya mtu inainuliwa na kuwezeshwa kutii kwa urahisi na mapema
zaidi miangaza na misukumo ya Roho Mtakatifu. Nguvu ya vipaji hivyo ni
kubwa hata kumwongoza mtu kwenye utakatifu wa hali juu; vyenyewe ni bora hivi
hata vinadumu mbinguni pia, ingawa kwa kiwango cha juu zaidi. Kwa njia yake
roho inaongozwa na kuhimizwa kujipatia
heri za Kiinjili, ambazo ni maua yanayochanua kwa wakati wake, dalili
tangulizi za heri ya milele... Kwa kuwa vipaji ni vikubwa hivyo navyo
vinaonyesha wema mkuu wa Roho Mtakatifu kwetu, vinatudai
tumuonyeshe heshima na utiifu mkuu kabisa. Tutafikia kwa urahisi hatua
hiyo tukijitahidi zaidi na zaidi kumjua, kumpenda na kumuomba... Tunapaswa
kumpenda Roho Mtakatifu kwa kuwa ni Mungu... na pia kwa kuwa ni upendo wenyewe,
asili, wa milele, kwa sababu hakuna kinachopendeza kuliko upendo... Yeye
atatujalia kwa wingi zawadi zake za kimbingu, hasa kwa sababu utovu wa
shukrani unafunga mikono ya mfadhili, lakini moyo wa shukrani unaifungua tena...
Tunapaswa kumuomba mfululizo na kwa
tumaini kubwa atuangaze zaidi na zaidi na kuwasha ndani mwetu moto wa upendo
wake, ili kwa kutegemea imani na upendo tutembee kwa ari kuelekea tuzo la
milele, kwa kuwa ndiye amana ya urithi
wetu”.
Mwalimu
huyo wa Kanisa ametufundisha hasa matatu: 1° kwamba vipaji ni misimamo ya
kudumu, lakini tofauti na maadili; 2° kwamba ni vya lazima kwa wokovu; 3°
kwamba vinashikamana na upendo na kukua pamoja nao.
1°
“Ili kutofautisha vipaji na maadili mbalimbali tunapaswa kufuata lugha ya
Biblia inayoviita si vipaji bali roho” ili tuelewe kuwa vinapatikana ndani
mwetu kwa uvuvio wa Mungu au msukumo
kutoka nje na wa juu wa Roho Mtakatifu. Ni lazima tuzingatie kwamba binadamu
anasukumwa na mambo mawili
yanayomwongoza: moja limo ndani mwake, yaani akili, lingine liko nje,
yaani Mungu. “Inaeleweka mara moja kwamba chombo kinachosukumika kinatakiwa kulingana
na kinachokisukuma; na ukamilifu wa
kinachosukumika ni urahisi wa
kusukumwa na kinachokisukuma. Basi, kadiri hicho cha mwisho kilivyo bora,
ni lazima kinachosukumwa kiwe kikamilifu zaidi ili kupokea msukumo wake.
Hatimaye ni wazi kwamba maadili ya
kibinadamu yanamkamilisha mtu katika kujiongoza kwa akili yake katika maisha ya ndani na ya nje. Basi inahitajika
iwemo ndani mwake misukumo ya juu inayomuandaa kusukumwa Kimungu, na namna hizo kamilifu zinaitwa vipaji siyo tu
kwa kuwa tunamiminiwa na Mungu, bali pia kwa sababu kwa njia yake mtu
anakuja kuweza kupokea mara uvuvio wa Kimungu, alivyosema Isaya: ‘Bwana
Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma’
(50:5). Ndiyo sababu wengine wanasema kuwa vipaji vinamkamilisha binadamu
vikimuandaa kutenda mambo bora kuliko ya maadili”.
Hapo
tunaona kuwa vipaji vya Roho Mtakatifu si matendo wala si misukumo au misaada
ya kupita ya neema, bali ni misimamo ya kudumu tunayomiminiwa, inayotuweka
tayari kupokea uvuvio wa Mungu, kama vile tanga zinavyowezesha chombo kwenda
kwa nguvu ya upepo. Kwa utayari huo wa kupokea misukumo vinatusaidia kutenda
mambo yale bora yanayoitwa heri kutokana na ukamilifu wake unaoonyesha kwamba
yanategemea vipaji kuliko maadili. Mfano huo ulitolewa na Bwana mwenyewe
aliliposema, “Upepo huvuma upendako,
na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na
hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh. 3:8). Hatujui vizuri
upepo unaovuma umetokea wapi na utasikika mpaka wapi; vilevile hatujui vizuri
uvuvio wa Kimungu unaanzia wapi, na utatufikishia ngazi gani ya ukamilifu
tukiufuata kwa uaminifu moja kwa moja. Tusiwe kama wanamaji ambao kwa uzembe
hawatweki tanga wakati wa kufaa.
Wanateolojia
wengi wanamuunga mkono mt. Thoma wa Akwino anaposema kuwa vipaji vinatofautiana
kweli na maadili ya kumiminiwa, kama vile wanavyotofautiana wanaoviongoza,
yaani Roho Mtakatifu na akili iliyoangazwa na imani; hiyo ni miongozo na kanuni tofauti. Utendaji wa kibinadamu unatokana na kanuni ya
kibinadamu, utendaji upitao maumbile unatokana na kanuni ya Kimungu, yaani
uvuvio wa Roho Mtakatifu. Hata busara iliyoinuliwa na upendo inafanya kazi kwa
kuzingatia mafuatano ya mawazo, tofauti na kipaji cha shauri kinachotuandaa
kupokea uvuvio maalumu usioyahitaji. Kwa mfano, tukiulizwa swali linalohusu
siri fulani, busara inasita kuhusu namna ya kutunza siri hiyo bila ya kusema
uongo, kumbe uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu unaondolea wasiwasi (taz. Math.
10:19). Vilevile, imani inaambatana
tu na kweli tulizofunuliwa, kumbe kipaji cha akili kinatuwezesha kuona
ndani ya vilindi vyake, na kile cha hekima kinatuwezesha kuonja
utamu wake. Basi vipaji vinatofautiana na maadili.
2°
Vipaji vya Roho Mtakatifu ni vya lazima
kwa wokovu wa milele. “Maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima”
(Hek. 7:28). “Miongoni mwa ndugu awatawalaye ana heshima, bali machoni pa
Bwana ni wao wamchao” (YbS. 10:20). Sasa kipaji bora ni hekima, na cha
mwisho ni uchaji wa Mungu.
Hata
maadili ya Kimungu yanajilinganisha na namna
ya kibinadamu ya akili na utashi wetu, na hivyo yanatuacha katika hali
isiyotosha kwa lengo letu kuu lipitalo maumbile, ambalo tunatakiwa kulijua kwa
namna iliyo hai, inayochimba na kuonja, na ambalo tunatakiwa kulilenga kwa ari
zaidi.
Imani
hata ikiwa kubwa inaendelea kuwa na upungufu kwa sababu tatu za msingi: 1) kwa
kuwa yale inayoyaamini ni giza, nayo
haiyafikii moja kwa moja, ila inayona “kwa kioo kwa jinsi ya fumbo” (1Kor.
13:12); 2) inayafikia kwa njia ya matamko
rasmi mbalimbali ya Kanisa, kumbe umoja wa Mungu haugawanyiki; 3)
inayafikia kinadharia, kwa kukiri na
kukanusha maneno fulanifulani, kumbe Mungu aliye hai ni mwanga wa uzima ambaye
anatakiwa kujulikana kama kwa mang'amuzi.
Tumaini
linashiriki upungufu wa imani, na vilevile upendo, kwa kuwa imani ndiyo
inayoupatia la kupenda. Zaidi tena busara ina upungufu, kwa kuwa inahitaji
kufuata mawazo, kutafuta sababu za kutenda, ili kuelekeza maadili ya
kibinadamu; mara nyingi inasita isijue la kufanya, ila unahitajika mwanga
kutoka juu, k.mf. ili kushinda vishawishi kadhaa visivyotambulikana, au vikali
na vya muda mrefu.
“Akili
ya binadamu, hata baada ya kukamilishwa na maadili ya Kimungu, haiwezi kujua
yale yote inayohitaji kuyajua, wala haiwezi kuepuka kila upotovu. Mungu tu
aliye na ujuzi wote na uwezo wote anaweza kufidia ujinga na upumbavu wetu,
ugumu wa moyo na kasoro nyingine za namna hiyo. Ni kwa ajili ya kutuondolea
kasoro hizo kwamba tumejaliwa vipaji vya Roho Mtakatifu, vinavyotuwezesha
kupokea vizuri uvuvio wa Kimungu”. Ndiyo maana vipaji ni vya lazima kwa
wokovu wetu. “Kwa njia ya maadili ya Kimungu na ya kibinadamu, mtu
hajakamilika kuhusu lengo lake kuu linalopita maumbile asihitaji daima
kusukumwa na Roho Mtakatifu kutoka juu”. Kwake haja hiyo ni ya kudumu, ndio
sababu vipaji ni misimamo ya kudumu tunayomiminiwa.
Sisi
tunatumia vipaji kwa mfano wa adili
la utiifu, ili kupokea vizuri agizo kutoka juu, na kutenda kulingana nalo,
lakini hatuwezi kuwa na uvuvio huo kila tunapotaka. Upande huo vipaji
vinatufanya tusiweze kutenda wenyewe, ila kwa msukumo wa Roho Mtakatifu. Hivyo
ni wazi zaidi kuwa vipaji, kama vile utiifu, ni misimamo ya kudumu ya
mwadilifu.
Tunaweza
kuona vizuri zaidi tunavyohitaji vipaji hivyo, tukizingatia jinsi kila kimoja
kinavyokamilisha akili au utashi na hisi:
KIPAJI
ADILI
ili
kupenya ukweli
akili
imani
akili
iliyoangazwa na imani
mambo ya Mungu hekima
upendo
ili kuamua kuhusu mambo
yetu shauri
busara
Vipaji
vinakamilisha
malimwengu
elimu
tumaini
ili tumuabudu Mungu ipasavyo
ibada
ibada
utashi na hisi
ili tusiogope hatari
nguvu
nguvu
ili
tushinde tamaa mbaya
uchaji
kiasi
3°
Hatimaye, kwa kuwa vipaji ni vya lazima kwa wokovu, basi vinahusiana
na upendo. Roho Mtakatifu haji ndani mwetu pasipo vipaji vyake saba,
vinavyoendana na upendo na kwa hiyo vinapotezwa pamoja na upendo kwa dhambi
yoyote ya mauti.
Basi,
vipaji ni sehemu ya muundo wa Kiroho wa neema ya utakaso; ndiyo maana hiyo
inaitwa “neema ya maadili na vipaji”. Kame vile maadili ya kumiminiwa
yanavyokua pamoja kwa mfano wa vidole vya mkono, vipaji pia vinakua pamoja.
Hakuna mwenye kiwango kikubwa cha upendo
wa Mungu, inavyotakiwa na ukamilifu, asiye na vipaji
vya Roho Mtakatifu kwa kiwango hichohicho.
Tutazungumzia
mbele usikivu kwa Roho Mtakatifu, lakini tangu sasa tunaona thamani ya huo
muundo wa Kiroho ambao ni chanzo cha
uzima wa milele: ni thamani kubwa kuliko ile ya macho, ya afya, na ya
akili kwa maana mwadilifu akipotewa na akili hapotewi na hazina hiyo ambayo
kifo chenyewe hakiwezi kumnyang'anya. Neema ya maaadili na vipaji ina thamani
kubwa kuliko karama (za kufanya miujiza, kutabiri n.k) kwa kuwa hizo ni alama
za nje tu ambazo zinaweza kuelekeza njia ya kumfikia Mungu, lakini haziwezi
kutuunganisha naye inavyofanya neema ya utakaso.
Ili
tuone vizuri zaidi utendaji wa muundo huo wa Kiroho, inatupasa bado tuseme juu
ya neema za msaada zinazohitajika ili kutekeleza maadili na vipaji.
1.3.5. NEEMA ZA MSAADA NA AINA ZAKE
HAJA YA NEEMA ZA MSAADA
Hakuna
kiumbe kinachotenda pasipo nguvu ya Mungu, aliye chanzo cha utendaji wote wa
miili na wa roho: “Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa
na uhai wetu” (Mdo 17:28). Zaidi upande wa maisha yapitayo maumbile, ili
tutende kadiri ya maadili ya kumiminiwa na ya vipaji, tunahitaji msukumo wa Kimungu unaoitwa neema
ya msaada.
Ni
ukweli wa imani kwamba pasipo neema hiyo hatuwezi kujiandaa kuongoka, wala
kudumu muda mrefu katika kutenda mema, wala hasa kudumu katika neema ya
utakaso mpaka kufa. Pasipo neema ya msaada hatuwezi kuzaa tendo lolote (hata
dogo) linalostahili wokovu, wala zaidi hatuwezi kuufikia ukamilifu. Kwa maana
hiyo Yesu alisema, “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote”(Yoh.
15:5). “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu
wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu” (2Kor. 3:5). “Kwa maana
ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa
kulitimiza kusudi lake jema” (Fil. 2:13), akisukuma hiari yetu bila ya
kuilazimisha. Ndiye anayetujalia kujiandaa kupokea neema ya utakaso na halafu
kustahili uzima wa milele.
Ndiyo
sababu tunapaswa kusali daima. Haja ya
kusali inatokana na haja ya kupata neema za msaada. Mbali na neema ya
kwanza tunayojaliwa bure pasipo sisi kuomba (kwa kuwa ndio chanzo chenyewe cha
sala), sala ndiyo njia ya kawaida, ya
hakika na ya jumla ambayo Mungu anataka tupate neema tunazozihitaji. Ndiyo
sababu Bwana wetu ametusisitizia: “Ombeni,
nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana
kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa” (Mt.
7:7-8). Kuna haja hiyo hasa katika kishawishi: “Kesheni, mwombe, msije
mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Math. 26:41).
Tunaposali tunapaswa kuamini kuwa Mungu ndiye asili ya mema yote, kwa hiyo
tegemeo lolote lisilo na msingi katika sala ni la kipumbavu tu.
“Mungu
haagizi kamwe yasiyowezekana, bali akiagiza anatuambia tufanye
tunayoyaweza, tuombe tusiyoyaweza, naye mwenyewe anatusaidia ili tuweze” (Mtaguso
wa Trento), tena kwa neema ya msaada anatusaidia kusali pia. Kuna neema kadhaa
tusizoweza kuzipata isipokuwa kwa kusali. Haitatosha kamwe kusisitiza jambo
hilo, kwa kuwa wengi mwanzoni wamejaa mawazo ya kibinadamu tu wakidhani
inawezekana kufanya lolote kwa utashi na bidii, pasipo neema za msaada. Lakini
watang'amua mapema ukweli wa maneno ya Yesu na ya mt. Paulo tuliyodondoa. Basi
tunapaswa kuomba neema za msaada ili tushike vizuri zaidi na zaidi amri za
Mungu, hasa ile kuu ya upendo.
Neema
za msaada zina namna nyingi tofauti ambazo inafaa kuzijua, kwa kukumbushwa
wazi iwezekanavyo kweli kadhaa ambazo ni za hakika, ingawa zinatokeza fumbo
mojawapo la imani ambalo kuliko mengine mengi lina mchanganyiko wa mwanga na
giza kwetu.
Mara
nyingi tunapewa neema ya mwanga, yaani
tunaangaziwa kwa ndani; k.mf. wakati wa masomo ya misa tunaangazwa kuelewa
maana yake. Hiyo inafuatwa na neema ya
mvutio, yaani tunavutiwa na tendo fulani, k.mf. katika kuzingatia upendo
wa Mwokozi kwetu, tunajisikia kumrudishia upendo. Neema ya msaada ya namna
hiyo inatenda katika utashi na kuusukuma upendo utende, hata kujitoa kwa Mungu,
tayari kupokea mateso yoyote na kufa kwa ajili yake ikiwa ni lazima. Hapo si
neema ya mvutio tu, bali neema ya
ushujaa ambayo mara nyingi tunaipokea pasipo kuing'amua, lakini
inatuwezesha kustahimili ukavu wa roho. Kati ya neema hizo, nyingi
hazitambulikani na yule anayezipokea, kwa kuwa zinapita maumbile, hivyo
zinapita njia zetu za kujua mambo.
Neema
ya msaada inayogusa utashi inaweza kuwa na sauti kuhusu matakwa yake kwa namna
mbili: kwa kuupendekezea jambo
ambalo liuvutie, na kwa kuusukuma kwa
ndani. Bila ya shaka Mungu anaweza kuelekeza utashi wetu upande wa
uadilifu kwa kuupendekezea jambo fulani, k.mf. ahadi ya heri ya milele, au
ustawi wa upendo. Ndivyo mama anavyomvuta mtoto wake atende mema kwa
kumpendekezea jambo la kuvutia au kwa kumshauri. Hata malaika mlinzi anaweza
kufanya hivyo kwa kututia mawazo mazuri.
Lakini
kitu ambacho Mungu tu anaweza kukifanya ni kuusukuma kwa ndani utashi wetu
utende mema. Mungu yumo ndani mwetu kuliko nafsi yetu, ndiye anayedumisha roho
yetu, pamoja na akili na utashi alivyoviumba; ndiyo sababu anaweza kuvisukuma
kwa ndani, kadiri ya maelekeo ya kimaumbile viliyonayo, pasipo kuvilazimisha,
ila kwa kuvipa nguvu mpya. Kwa mfano, mama akitaka kumfundisha mtoto kutembea
anamsaidia sio tu kwa sauti huku akimuonyesha kitu ambacho akifikie, bali pia
kwa mikono akimuinua. Mungu anaweza kufanya hivyo upande wa roho, akiinua
utashi wetu ufikie uadilifu. Ndiye
Muumba wa utashi wetu; ameupa elekeo la ndani la kulenga uadilifu, naye
peke yake anaweza kuusukuma kwa ndani kadiri ya elekeo hilo. Ndivyo
anavyotenda kazi ndani mwetu akitufanya tutake na kutenda. Naye atafanya hivyo
kadiri tutakavyomuomba kwa ukakamavu atustawishie upendo tunaopaswa kuwa nao
kwake.
Neema
ya msaada inaitwa ya kutangulia
ikisababisha ndani mwetu wazo jema au mguso mwema, kabla hatujafanya lolote la
kusababisha kitu hicho. Tusipoikaidi Mungu anatuongezea neema ya kuchangia itakayousaidia utashi wetu kutekeleza tendo
linalohitajika ili kutimiza mpango wetu mzuri.
Halafu
inafaa kutambua kwamba Mungu anatusukuma, mara kutenda
kufuatana na uamuzi tulioukata kwa utaratibu wa kibinadamu, mara kutenda
kwa uvuvio maalumu kutoka juu, bila ya sisi kukata shauri kwa utaratibu
huo wa kawaida. Mfano wa namna ya kwanza ni pale ninapoamua kwenda kusali
rozari saa niliyozoea kufanya hivyo; hapo natenda kwa neema ya msaada ya
kawaida inayoitwa ya kushiriki tendo kwa kuwa inashirikiana nami katika kutenda kwa
namna ya kibinadamu ya kuamua. Mfano wa namna ya pili ni pale ambapo ghafla,
wakati wa kazi nzito, najisikia uvuvio
maalumu wa kusali kidogo, nami nafanya hivyo mara: neema hiyo inaitwa ya
kutenda, kwa kuwa inatenda ndani mwangu pasipo mimi kukata shauri, ingawa
sio pasipo kukubali mwenyewe kwa hiari na kwa kustahili tuzo.
Kwa
namna ya kwanza Mungu anatusukuma kwa kawaida kutenda namna ya kibinadamu ya maadili. Kwa namna ya pili anatusukuma
kutenda namna inayopita utu ya vipaji
vya Roho Mtakatifu: hapo chombo chetu kinakwenda sio tu kwa kasia, bali
kwa msukumo wa upepo, tunatendewa kuliko kutenda wenyewe. Hapo kazi yetu hasa
ni kukubali ile ya Mungu, kuacha Roho Mtakatifu atuongoze, kufuata mara na kwa
juhudi uvuvio wake wowote. Lakini hata tukiwa na neema ya kushiriki tendo tu,
kila tendo letu linalostahili tuzo ni lote
la Mungu kama asili kuu, na lote la
kwetu kama asili ya pili.
Ni
muhimu tuwe waaminifu kwa neema, tena kuwa waaminifu zaidi na zaidi kwa neema
ya msaada ya sasa hivi, ili tutimize wajibu wa dakika hiyo unaotudhihirishia
matakwa ya Mungu kwetu. Tukumbuke maneno ya mt. Augustino, “Aliyekuumba bila
yako, hatakufanya mwadilifu bila yako” kwa kuwa ni lazima ukubali na kuzitii
amri. Yeye aliongeza kuwa tunapewa msaada wa Mungu si kusudi utashi wetu
usifanye chochote, bali kusudi utende kwa kustahili wokovu.
Mungu
anatutolea mfululizo neema za msaada ili tutimize wajibu wa sasa hivi, kama
vile hewa inavyoyafikia mapafu yetu tuweze kupumua kila sasa. Kama
tunavyotakiwa kuingiza hewa inayosafisha damu, tunatakiwa pia kupokea kwa
mikono miwili neema inayozifanya mpya nguvu zetu za Kiroho ili tumuelekee
Mungu. Kama vile asiyepumua anakufa, vivyo hivyo roho isiyopokea neema inakufa
kwa kukosa hewa yake.
“Nasi
tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure”(2Kor.
6:1). Tunapaswa kuiitikia na kushirikiana nayo kwa bidii. Ndio ukweli mwepesi
ambao tukiutekeleza siku hadi siku unatufikisha kwenye utakatifu.
Kwa
hakika Mungu ndiye wa kwanza kupiga hatua kwetu kwa neema ya kutangulia;
halafu anatusaidia kuikubali. Anatuongoza katika njia zetu zote hadi saa ya
kufa.
Upande
wetu tunapaswa kuwa waaminifu. Namna gani? Mosi kwa kupokea kwa furaha mianga
ya kwanzakwanza ya neema; halafu kwa kufuata kwa makini yale inayotuambia;
hatimaye kwa kufanya juu chini kuyatekeleza, bila ya kujali gharama. Hapo
tutashiriki kazi ya Mungu, na utendaji wetu utakuwa tunda la neema yake na
papohapo la hiari yetu.
Neema
ya kwanza inayotuangaza kwa kusababisha wazo jema ndani mwetu inatosha kufanya utashi ukubali kutenda kwa adilifu, kwa maana
inatupa uwezo wa kulitenda. Lakini tukikaidi wazo hilo tunajinyima neema ya
msaada ambayo ingesababisha kwa hakika
tulikubali. Ukaidi unaangukia neema ya kutosha kama vile mvua ya mawe
inavyonyeshea maua yanayotarajiwa kuzaa matunda mengi: maua yanaangamizwa na
hivyo matunda hayatazaliwa kamwe. Neema ya hakika inatolewa kwetu katika ile
ya kutosha kama tunda katika ua; ni lazima tusiangamize ua ili tupate tunda.
Tusipoikaidi neema ya kutosha tutapewa ile ya hakika na kwa njia yake
tutaendelea bila ya wasiwasi katika njia ya wokovu. Hivyo neema ya kutosha
inatufanya tusiweze kujisingizia, na ile ya hakika haituruhusu tujivunie; kwa
njia yake tunasonga mbele kwa unyenyekevu na juhudi.
Ndilo
fumbo la neema ambalo mwanga wake umo katika kweli mbili, wakati giza lake
limo katika namna ya kuzilinganisha. Upande mmoja Mungu haagizi
kamwe yasiyowezekana (angekuwa hana haki wala huruma), bali kwa upendo anawawezesha
kweli wote watimize wajibu wao. Hakuna mtu mzima anayenyimwa neema ya
lazima kwa wokovu asipoikataa kwa kukaidi mwaliko wa Mungu. Upande mwingine,
“kwa kuwa upendo wa Mungu kwetu ni
asili ya mema yote, hakuna mtu anayeweza kuwa mwema kuliko mwingine
asipopendwa zaidi na Mungu” (mt. Thoma wa Akwino). Kwa maana hiyo Yesu
alisema kuhusu wateule: “Hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba
yangu” (Yoh. 10:29). “Ikiwa baadhi wanaokolewa ni kwa zawadi ya Mwokozi:
ikiwa wengine wanapotea ni kwa kosa lao” (Mtaguso wa Quiercy wa mwaka 853).
Kukaidi neema ni ovu linalotokana na sisi wenyewe tu. Kutoikaidi
kwenyewe ni jema linalotokana na Mungu, chemchemi ya mema yote. Maneno
hayo ndiyo sura mbili za fumbo lilelile; kila moja ni la hakika, kama lile la
kwamba wote wanaweza kuokoka, na lile la kwamba hakuna aliye bora kuliko
mwenzake isipokuwa kwa sababu amependwa zaidi na Mungu. Lakini hayo mawili
yanawezaje kulingana? Hakuna kiumbe anayeweza kuona ulinganifu huo kabla
haijakaribishwa kumuona Mungu mbinguni, kwa sababu ni sawa na kuona jinsi haki
isiyo na mipaka, huruma isiyo na mipaka, na hiari yake kuu zinavyolingana
katika ubora wa Umungu.
Tusikatae
ukarimu wa Mungu ambaye ametujalia neema ya utakaso, maadili ya kumiminiwa na
vipaji, tena kila siku anatuvuta kwake. Tusiridhike na maisha ya wastani na
kuzaa matunda yasiyoiva, wakati Mwokozi wetu mwema alisema, “Mimi nalikuja
ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh. 10:10) hadi kufurahia milele
heri yake. Mungu ana moyo mkuu, basi tuwe nao sisi pia.
Uaminifu
huo unahitajika kwanza ili kutunza
uzima wa neema, na kukwepa dhambi ya mauti. Uzima huo una thamani kubwa pasipo
kifani, hata Mwokozi alikabili kifo ili kuturudishia. Tungejaliwa kuona wazi
mng'ao wa ajabu wa neema ya utakaso, tungejisahau. Uaminifu unahitajika pia
ili tustahili na kupata ustawi wa
uzima huo ndani mwetu, unaotakiwa kukua mpaka tutakapoingia mbinguni, kwa
sababu tunapohiji kuelekea umilele hatuwezi kusonga mbele isipokuwa kwa kukua
katika upendo wa Mungu.
Kwa
hiyo tunahitaji kutakasa matendo yetu
yote, hata la kawaida zaidi, tukiyatenda kwa nia safi na kwa lengo
lipitalo maumbile. Tungekuwa waaminifu toka asubuhi hadi jioni, siku zetu
zingejaa na kufurika matendo ya upendo kwa Mungu na kwa jirani, katika nafasi
yoyote, ya furaha na ya uchungu, na kufikia jioni muungano wetu na Mungu
ungekuwa wa ndani na imara zaidi. Kwa watu wowote hakuna njia rahisi na ya
hakika ya kupata utakatifu kuliko ile ya kuinua kila tendo juu kuliko maumbile,
kwa kumtolea Mungu pamoja na Yesu, kwa utukufu wake na kwa wokovu wa watu.
1.4.
UWEMO WA UTATU MTAKATIFU NDANI MWETU
KAMA
CHEMCHEMI ISIYOUMBWA YA MAISHA YA KIROHO
Sasa
inafaa tuzingatie chemchemi isiyoumbwa ya maisha yetu ya Kiroho, yaani Utatu
mtakatifu uliomo ndani ya waadilifu wote wa duniani, toharani na mbinguni.
USHUHUDA
WA MAANDIKO MATAKATIFU
Maandiko
yanatufundisha kuwa Mungu yumo katika
viumbe vyote kwa namna fulani inayotokana na hali yake ya kutokuwa na
mipaka: “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko”
(Zab. 139:7-8). “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye,
kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi… hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa
maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu” (Mdo.
17:24-28). Kwa hakika, Mungu anaona vyote, anadumisha vyote, na kukiongoza
kila kiumbe kitende inavyokifaa.
Lakini
Maandiko yanasema pia juu ya uwemo wa pekee wa Mungu katika waadilifu. “Mtu
akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja
kwake, na kufanya makao kwake” (Yoh. 14:23). Nani atakuja? Mambo yaliyoumbwa
tu, kama vile neema ya utakaso, maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho
Mtakatifu? Hapana, watakaokuja ni walewale wanaopenda, Baba na Mwana
wasiotenganika na Roho Mtakatifu, ambaye Bwana alimuahidi na kumtuma wazi
kwenye Pentekoste: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba,
naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae
nanyi hata milele… Ndiye Roho wa kweli… anakaa kwenu, naye atakuwa ndani
yenu…” (Yoh. 14:15-17). Hao watakuja si kwa muda, bali watafanya
makao yao ndani ya mwadilifu mpaka atakapodumu katika upendo.
Maneno
hayo hayakuwahusu mitume tu: “Mungu ni upendo, naye akaaye
katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh.
4:8). Huyo anaye Mungu moyoni mwake, lakini hasa Mungu anaye huyo ndani mwake
akimdumishia sio tu uhai wa kimaumbile, bali pia ule mpya wa neema na upendo.
“Pendo
la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho
Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom. 5:5). Hatukujaliwa tu upendo ulioumbwa,
bali Roho Mtakatifu mwenyewe, aliye Upendo-Nafsi. Hao wamo ndani mwetu, lakini
tutafananishwa nao kikamilifu kwa kupokea tu mwanga wa utukufu.
“Hamjui
ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani
yenu?... Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani
yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe” (1Kor. 3:16;
6:19). Hivyo Maandiko yanafundisha wazi kuwa Nafsi tatu za Mungu zinaishi
katika waadilifu wote.
USHUHUDA
WA MAPOKEO
Mwanzoni
mwa karne ya pili, mt. Inyasi wa Antiokia aliwaita Wakristo halisi
“theophoroi” (= waleta Mungu) kwa kuwa wana Mungu ndani mwao. Mt. Lusia
alikiri ukweli huo mbele ya mahakimu: “Ndio, wale wote wanaoishi kwa usafi
na imani ni mahekalu ya Roho Mtakatifu”. Mt. Atanasi alisema kuwa Nafsi tatu
za Mungu zimo ndani mwetu. Mt. Bazili alitamka kuwa Roho Mtakatifu kwa kukaa
ndani mwetu anatufanya tuwe watu wa Kiroho zaidi na kufanana na Mwana Pekee.
Mt. Sirili wa Aleksandria pia alisema juu ya muungano huo wa ndani kati ya
mwadilifu na Roho Mtakatifu. Upande wa Magharibi, mt. Ambrosi alifundisha kuwa
tumempata katika ubatizo tena zaidi katika kipaimara. Mt. Augustino
alithibitisha kwa shuhuda za mababu waliomtangulia kwamba hatupewi neema tu,
bali tunajaliwa Mungu mwenyewe, yaani Roho Mtakatifu na vipaji vyake saba.
Ukweli
huo uliofunuliwa unawekwa tena machoni petu na Ualimu wa Kanisa. Mtaguso wa
Trento ulisema: “Anayetufanya waadilifu ni Mungu ambaye kwa huruma yake
anatutakasa bure na kutufanya watakatifu, akitupaka mafuta na kututia muhuri
wa Roho Mtakatifu tuliyeahidiwa ambaye ni dhamana ya urithi wetu (taz. Ef.
1:13-14)”. Leo XIII alifafanua zaidi: “Inafaa sana kukumbuka maelezo
yaliyotolewa na walimu wa Kanisa kadiri ya mafundisho ya Maandiko matakatifu:
Mungu yumo katika vitu vyote kwa uwezo
wake, kwa sababu vyote viko chini yake; halafu kwa
uwepo wake, kwa sababu vyote viko wazi mbele yake; tena kwa undani wake, kwa sababu yumo ndani ya viumbe vyote kama chanzo
cha uwepo wao. Lakini katika binadamu Mungu hayumo tu kwa namna ile ambayo
yumo katika vitu vyote, bali zaidi kwa
kujulikana na kupendwa naye, kwa sababu maumbile yetu wenyewe yanatufanya
tupende, na kutamani na kufuata yaliyo mema. Kwa
neema yake Mungu anakaa katika roho adilifu kama hekaluni kwa namna ya ndani
na ya pekee kabisa. Ndipo kinapotokea kile kiungo cha upendo
kinachofungamanisha roho na Mungu kuliko mtu na rafiki yake mkuu na
kinachoifanya imfurahie kwa ukamilifu wote. Muungano huo wa ajabu, unaoitwa uwemo
ndani na unaotofautiana na hali ya wenye heri wa mbinguni kwa namna yake
tu, unasababishwa kwa ukweli wote na uwemo wa Utatu mzima: ‘tutakuja kwake,
na kufanya makao kwake’ (Yoh. 14:23). Hata hivyo unasemwa kuwa ni hasa kazi
ya Roho Mtakatifu, kwa kuwa tunaona alama za uwezo na za hekima ya Mungu hata
katika mtu mwovu, lakini mwadilifu tu anashiriki upendo,
ambao ni sifa ya Roho Mtakatifu...
Wingi wa mema ya kimbingu unaosababishwa na uwemo wa Roho Mtakatifu katika
roho adilifu unajitokeza kwa namna mbalimbali... Kati ya zawadi hizo zimo
tahadhari za siri, na mialiko ya kifumbo ambavyo roho zinajaliwa kwa njia ya
Roho Mtakatifu, na ambavyo visipokuwepo hatuwezi kujitahidi katika maadili,
wala kuendelea, wala kufikia wokovu wa milele”.
UFAFANUZI
WA TEOLOJIA KUHUSU FUMBO HILO
“Mbali
ya neema ya utakaso hakuna lingine linaloweza kuangaza jambo hilo, kwamba
Nafsi ya Kimungu iwemo ndani mwetu kwa namna mpya... Halafu, ili tuwe
nalo ni lazima tuweze kulifurahia
na kulitumia. Sasa hatuwezi kufurahia Nafsi ya Kimungu isipokuwa kwa neema ya
utakaso na upendo” (mt. Thoma wa Akwino).
Ni
kwamba pasipo hayo Mungu hakai ndani
mwetu. Haitoshi kumjua kimaumbile (kifalsafa), wala kwa imani iliyokufa (anavyomjua
mwamini mwenye dhambi ya mauti). Ni lazima tumjue
kwa imani hai na vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyohusiana na upendo. Hiyo
namna ya mwisho ya kumjua Mungu inampata
si kama jambo la mbali lililochorwa tu kwetu, bali kama jambo lililopo, tulilonalo na ambalo tunaweza kulifurahia
tangu sasa. Ili Nafsi za Kimungu zikae
ndani mwetu, inatakiwa tuweze kuzifahamu
kama kwa mang'amuzi ya kimapenzi,
ambayo msingi wake ni upendo tuliomiminiwa unaotulinganisha
na maisha ya ndani ya Mungu.
Lakini
ili Utatu mtakatifu ukae ndani mwetu si lazima tumjue hivyo kila
sasa; inatosha tuweze kufanya
hivyo kwa njia ya neema ya maadili na vipaji. Basi uwemo wa Utatu mtakatifu
unadumu katika mtu mwadilifu hata usingizini mpaka atakapodumu katika neema ya
utakaso. Ila mara mojamoja inatokea kuwa Mungu anatambulikana nasi kama kiini
cha roho yetu, kama uhai wa maisha yetu, alivyosema mt. Paulo: “Mlipokea
roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu”
(Rom. 8:15-16). Mt. Thoma wa Akwino alifafanua: “Roho Mtakatifu
anathibitishia roho yetu kwa kusababisha ndani mwetu upendo
kama wa mwana kwa Baba”. Upendo huo ni ishara inayotuwezesha kuwa na
hakika fulani ya kwamba tuna neema ya utakaso.
Kufuatana
na mafundisho hayo, Utatu mtakatifu unakaa katika roho adilifu vizuri kuliko
mwili wa Mwokozi unavyokaa katika umbo la mkate lililogeuzwa, walau kwa namna
fulani. Yaani Yesu yumo kweli katika maumbo ya ekaristi, lakini hayo hayamjui
wala hayampendi. Kumbe Utatu mtakatifu umo ndani ya mwadilifu kama katika
hekalu hai linaloujua na kuupenda (kwa kiasi tofautitofauti). Umo katika wenye
heri wa mbinguni wanaoutazama moja kwa moja, hasa katika roho takatifu ya
Mwokozi ambayo Neno ameungana nayo katika Nafsi moja. Kuanzia dunia hii,
katika mwanga/giza la imani, Utatu mtakatifu unakaa ndani mwetu, ingawa
hatuuoni, ukitustawishia uhai zaidi na zaidi hadi saa ya kuingia katika
utukufu.
Uwemo
huo wa Roho Mtakatifu hautuondolei haja ya kukaribia ekaristi, kwa kuwa Utatu
mtakatifu unakaa ndani ya Kristo kuliko unavyokaa ndani mwetu. Ikiwa
tunafaidika na kumkaribia mtakatifu wa Mungu, jinsi gani tutafaidika
tukimkaribia Mwanae!
YATOKANAYO
KWA MAISHA YA KIROHO
Ikiwa
uwemo wa Utatu mtakatifu ndani mwetu unatuwezesha
kumjua Mungu kama kwa mang'amuzi, maana yake ujuzi huo si jambo la pekee (kama
njozi) bali lipo katika njia ya kawaida ya utakatifu. Ujuzi huo unatokana na imani
iliyoangazwa na vipaji vinavyohusiana
na upendo. Kama ni hivyo, basi, kwa kawaida unatakiwa kustawi kadiri
upendo unavyostawi. Tutaona kuwa sala ya kumiminiwa, ambayo ni kuchanua kwa
aina hiyo ya ujuzi/mang'amuzi, inaanza katika hatua ya mwanga na kukamilika
katika hatua ya muungano. Ujuzi huo wa Mungu na wa wema wake utakua pamoja na
ule wa unyonge wetu.
Jambo
lingine linalotokana na hayo tuliyosema ni kwamba upendo uliomo ndani mwetu
unapostawi sana, nafsi za Kimungu
zinakuwemo mwetu kwa undani zaidi, yaani kirafiki zaidi. Ndivyo
inavyotokea k.mf. wakati wa uongofu wa pili ambao ni mwanzo wa hatua ya mwanga.
Hatimaye
hao Watatu wamo ndani mwetu sio tu kusudi tuwafahamu na kuwapenda kwa namna
ipitayo maumbile, bali wamo kama asili
ya vitendo vinavyopita maumbile, kama Yesu alivyosema, “Baba yangu
anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi” (Yoh. 5:17), hasa katika kiini
cha roho.
Lakini
kiutendaji ni lazima tukumbuke kwamba kwa kawaida Mungu anajitoa kwa kiumbe
chake kadiri hicho kilivyo tayari kumpokea. Mtu akiwa safi zaidi, ndani mwake
Nafsi za Kimungu zinakuwemo na kufanya kazi zaidi. Hapo Mungu
ni wetu nasi ni wake, na tunatamani kuliko yote tuendelee katika upendo
wake. “Hilo ni mojawapo kati ya mambo yanayotusukuma zaidi kuendelea Kiroho,
kwa sababu linaifanya roho iwe daima na juhudi kwa maendeleo yake, iwe macho
ili kuzaa mfululizo vitendo vyenye nguvu na motomoto zaidi na zaidi kuhusu
maadili yote, ili kwa kukua katika neema, ustawi huo umlete upya Mungu ndani
mwake… kwa ajili ya muungano wa ndani zaidi, wa kudumu zaidi na imara zaidi”
(L. Chardon).
TUNA
WAJIBU GANI KWA MGENI WETU WA KIMUNGU?
Mgeni
huyo anatuambia: “Mwanangu, nipe moyo wako” (Mith. 23:26). “Tazama,
nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango,
nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” (Ufu.
3:20). Roho ya mwadilifu inafanana na mbingu, kwa sababu Utatu mtakatifu umo
ndani mwake, lakini bado kuna giza, na siku fulani tu itajaliwa kuuona
waziwazi ndani mwake.
Kwa
kifupi wajibu wetu kwake ni kama ifuatavyo: kumfikiria mara nyingi, kwa
kujiambia, “Mungu anaishi ndani mwangu”. Kumwekea wakfu siku zetu, tena
kila saa, kwa kusema: “Kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.
Kukumbuka kwamba kwetu yeye ni chemchemi ya mwanga, ya faraja na ya nguvu.
Kumuomba kadiri ya neno la Bwana: “Wewe usalipo, ingia katika chumba chako
cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye
sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Math. 6:6). Kumuabudu kwa
kusema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu,
Mwokozi wangu” (Lk. 1:46-47). Kumuamini, kumtumainia, kumpenda kwa upendo
unaozidi kuwa safi, mkarimu, wenye nguvu. Kumpenda kwa kumuiga hasa katika
wema: “Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk. 6:36).
“Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako,
hao nao wawe ndani yetu” (Yoh. 17:21).
Hayo
yote yanatufanya tuone kwamba maisha ya
Kiroho upande wa mafumbo (ambapo ujuzi/mang'amuzi ya Mungu kuwemo ndani
mwetu ni ya sasa hivi) kwa yenyewe si ya pekee, bali ni
ukamilifu wa kawaida. Watakatifu tu,
ambao wanayo kikamilifu, wapo kweli
wanapotakiwa. Kabla hatujaona muungano huo wa ndani na Mungu, sisi ni kama
tumesinziasinzia: bado fumbo tamu la
uwemo wa Utatu mtakatifu tunalijua kijuujuu mno, kumbe ndilo uzima tele
tuliokaribishwa; hatujamuabudu wala kumpenda Mungu inavyotakiwa, na mara
nyingi tunahesabu kile ambacho pekee ni cha lazima kama kwamba kwetu si muhimu
kuliko vyote; vilevile hatujaelewa kwa undani ukuu wa zawadi tuliyopewa katika
ekaristi, wala Mwili wa fumbo wa Kristo ni nini.
Roho
Mtakatifu ndiye roho ya Mwili wa fumbo ambao Yesu ndiye kichwa chake. Kama
vile roho nzima imo katika mwili wote na katika kila kiungo, nayo inafanya
kazi bora kichwani, vivyo hivyo Roho Mtakatifu yumo mzima katika Mwili wote wa
fumbo, naye anafanya kazi bora katika roho takatifu ya Mwokozi na kwa njia
yake kwetu pia. Kiini cha uhai
kinachounganisha hivyo Mwili wa fumbo kina
nguvu ya kuunganisha zaidi kuliko roho inavyounganisha mwili wake, na
kuliko umoja wa familia au taifa fulani. Hivyo vinaunganishwa na namna fulani
ya kutazama, kupima, kuhisi, kupenda, kutaka na kutenda. Roho anayeunganisha
Mwili wa fumbo ana nguvu pasipo mfano, kwa kuwa ni Roho aletaye utakatifu, ni
chemchemi ya maji hai yanayobubujikia uzima wa milele. Mto wa neema zote
unaotokana na Roho Mtakatifu unapanda juu tena kumrudia Mungu kwa namna ya
ibada, sala, stahili na sadaka. Ndiyo mambo yapitayo maumbile tunayopaswa
kuyajua vizuri zaidi na zaidi. Upande wa
mafumbo tu ndipo roho inapozinduka kweli, na kutambua zawadi ya Mungu ilivyo,
kwa namna ile hai, ya ndani na angavu tunayohitaji ili kumrudishia
kikamilifu Mungu upendo alio nao kwetu.
1.5. KRISTO MKOMBOZI ANAVYOATHIRI MWILI WAKE WA FUMBO
Tumeona
jinsi Utatu mtakatifu uliomo ndani ya kila mwadilifu ulivyo chemchemi
isiyoumbwa ya maisha yetu ya Kiroho. Lakini utakatifu wetu unategemea pia
nguvu zinazomtoka mfululizo Kristo Mkombozi ambaye, kwa njia ya sakramenti na
hata nje ya hizo, anatushirikisha neema alizotustahilia alipoishi duniani na
hasa wakati wa mateso yake. Basi, tuongelee sasa nguvu hizo zinazotuletea
utakatifu hasa kwa njia ya sakramenti kuu kuliko zote, yaani ekaristi.
JINSI
MWOKOZI ANAVYOTUSHIRIKISHA NEEMA ALIZOTUSTAHILIA
Anafanya
hivyo kama chombo hai kilichounganika moja kwa moja na umungu, chemchemi ya
neema zote. “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema
juu ya neema” (Yoh. 1:16). Yesu mwenyewe alituambia: “Kaeni ndani yangu,
nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani
ya mzabibu, kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu, ninyi ni
matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo
mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote… Ninyi mkikaa ndani yangu, na
maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo
hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu”
(Yoh. 15:4-8).
Mt.
Paulo alitoa mfano mwingine wa kushangaza, akisema Kristo ni kama
kichwa kinachovishirikisha viungo vyote uhai wa roho; Kanisa ndilo mwili wa fumbo wa Kristo, na Wakristo ndio viungo vya
mwili huo. “Ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake”
(1Kor. 12:27). “Tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye
katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa
na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila
sehemu mojamoja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo” (Ef.
4:15-16).
Kufuatana
na hayo, Mwokozi anatushirikisha nguvu hai za neema kama vile kichwa
kinavyovishirikisha viungo vyake uhai ambao roho ndiyo asili yake. Ili tuelewe
vizuri tunapaswa kutofautisha umungu na ubinadamu wa Yesu Kristo. Kama Neno yeye anakaa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu katika kiini cha
roho yetu akiidumishia uzima wake wa kimaumbile na ule upitao maumbile;
anaiongoza kufanya yale makuu na ya ndani zaidi isiyoweza kufanya peke yake.
Kuhusu ubinadamu wa Mwokozi ndio
chombo kilichounganika na umungu moja kwa moja ambacho tunashirikishwa neema
zote. Huo ubinadamu haukai rohoni mwetu, kwa kuwa mwili wake hauwezi kuwemo
rohoni mwetu, ila uko mbinguni kwa namna ya mwili na umo katika ekaristi kwa
namna ya sakramenti. Hata hivyo roho adilifu inapokea mfululizo nguvu za
ubinadamu wa Yesu, kwa sababu kila neema inatolewa kwa njia yake tu. Halafu,
kwa kuwa kila sasa tuna wajibu fulani wa kutimiza, ubinadamu wa Mwokozi
unatushirikisha nukta baada ya nukta neema ya msaada ya sasa hivi, kama vile
hewa inavyoingizwa mfululizo mapafuni.
Mungu,
asili ya neema, anatumia ubinadamu wa Mwokozi ili kutujalia neema, kama vile
mwanamuziki bora anavyotumia ala ili kutushirikisha aliyonayo moyoni, au kama
vile mwanafalsafa bora anavyotumia ufasaha wa lugha yake ili kutokeza mawazo
yake. Ubinadamu wa Mwokozi ni chombo bora, chenye kujua na kutaka kutumika,
kilichounganika moja kwa moja na umungu ili kutushirikisha neema zote
tunazojaliwa, ambazo zote alitustahilia msalabani.
Hivyo
kwa Mwokozi vinatoka mianga yote ya akili, neema zote za mvutio, za faraja na
za ushujaa, tunazozihisi na tusizozihisi. Ni nguvu ya mfululizo inayochangia
kila tendo linalostahili wokovu kuliko mama bora anavyoweza kumsaidia mwanae
anapomfundisha kusali. Utendaji huo wa Mwokozi unawashirikisha wasioamini
mianga ya imani, na Wakristo wakosefu neema ya kujuta inayowaalika kwenye
kitubio. Lakini nguvu hiyo inatumika hasa katika ekaristi, kwa kuwa sakramenti
hiyo haina neema tu, bali inaye mwenyewe aliye asili ya neema, tena ni sadaka
yenye thamani isiyo na mipaka. Jambo hilo linatakiwa kusisitizwa, tunapoongea
juu ya chemchemi ya maisha ya Kiroho.
NGUVU
YA KUTAKASA INAYOTOKA KWA MWOKOZI KATIKA EKARISTI
Ili
tufaidike zaidi na kumshukuru Bwana ni afadhali tutumie maneno yenyewe ya
Injili. Tukumbuke alivyotuahidia
kwanza ekaristi kwa upendo; alivyotupatia
katika karamu ya mwisho, alipoweka upadri; anavyoifanya
upya kila siku katika misa; anavyotaka kubaki kati yetu kwa
kudumisha uwemo wake halisi katika sakramenti; hatimaye anavyojitoa kwetu
katika komunyo ya kila siku, hadi ile ya mwisho tunayotumainia kuipokea
kabla hatujafa. Ukarimu huo wote wa Kimungu unatokana na upendo mmoja na
kulenga ustawi wa utakatifu wetu.
Maneno
aliyotuahidia ekaristi (taz. Yoh. 6:26-69) yanatuonyesha kwa namna bora hizo
nguvu hai za Mwokozi zinazotakiwa kutufanyia kazi na jinsi sisi tunavyotakiwa
kuzipokea. Baada ya kuzidisha mikate, alisema: “Msikitendee kazi chakula
chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana
wa Adamu atawapa. Kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani Mungu...
Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana
chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima”.
Basi wakamuambia: “Bwana, sikuzote utupe chakula hiki”. Yesu akawaambia:
“Mimi ndimi chakula cha uzima...
Lakini niliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini... Amin, amin, nawaambia:
yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu
waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni
chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi
ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula
hiki, ataishi milele. Na chakula
nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu...
Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni
kinywaji cha kweli... Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”.
Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena.
Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?”.
Simoni Petro akamjibu, “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima
wa milele”. Ahadi hiyo ya ekaristi inadokeza yale yote ambayo sakramenti
hiyo inakusudiwa kuzaa ndani mwetu.
Simulizi
la kuiweka linatuonyesha uzito wa ahadi hiyo: “Walipokuwa wakila, Yesu
alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, ‘Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu’. Akakitwaa kikombe,
akashukuru, akawapa, akisema, ‘Nyweni
nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa
ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi’” (Math. 26:26-28). Maneno ya
ahadi yanaangazwa na hayo yaliyomtuza mt. Petro kwa sababu alisema kwa imani,
“Wewe unayo maneno ya uzima wa milele”. Hakika Yesu karamuni alikuwa na
neno lenye nguvu kuliko kawaida, neno lenye
kugeuza undani wa mkate kuwa mwili wake ili abaki kati yetu kisakramenti.
Papohapo
aliweka upadri ili kudumisha
kisakramenti sadaka ya msalabani mpaka mwisho wa nyakati. Kwa kusema, “Fanyeni
hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk. 22:19; 1Kor. 11:24-25) aliwapa mitume
uwezo wa kugeuza, wa kutolea sadaka ya ekaristi inayodumisha ile ya msalabani,
ili watushirikishe matunda, stahili na malipizi yake mpaka mwisho wa dunia.
Kuhani mkuu ni Bwana wetu, anayeendelea kujitoa; “maana yu hai sikuzote ili
awaombee” (Eb. 7:25). Anafanya hivyo hasa katika sadaka takatifu, ambayo ina
thamani isiyo na mipaka, kutokana na kuhani mkuu anayeitoa, sadaka inayotolewa,
na damu azizi inayomwagwa kisakramenti. Papohapo Yesu anamtolea Baba yake
ibada, dua, malipizi na shukrani zetu, yaani kwa jumla matendo yote ya Mwili
wake wa fumbo yanayostahili wokovu.
Upendo
wa Kristo umetupatia ekaristi si mara moja tu, bali kila
siku upya. Angeweza kuamua misa iadhimishwe mara moja au mbili tu kwa
mwaka mahali fulani patakatifu ambapo waamini waende kutoka nchi za mbali.
Kumbe kila nukta misa kadhaa zinatolewa duniani kote. Hivyo analijalia Kanisa
lake neema linazozihitaji kulingana na nyakati linazoishi, tuwe na nguvu ya
kukabili hatari kubwa tulizonazo.
Kristo
anarudi kila siku, kweli, kati yetu, si kwa muda wa saa moja, tunapoadhimisha
sadaka ya ekaristi, bali kusudi abaki
nasi mfululizo katika tabenakulo kama mwenzetu hapa uhamishoni,
akitungojea kwa hamu ya kutusikiliza, na kumtolea daima Baba yake ibada yenye
thamani isiyo na mipaka.
Hatimaye
komunyo ni utimilifu wa kujitoa
zawadi. Wema kwa jinsi ulivyo unaelekea kuenea; unavutia na kujishirikisha.
Hiyo ni kweli hasa kwa wema mwangavu wa Mungu na Kristo wake. Katika komunyo
Mwokozi anatuvuta kwake na kujitoa kwetu, sio sote kwa jumla, bali tukitaka
kwa kila mmoja wetu, tena tukiwa waaminifu kwa ndani zaidi na zaidi. Anajitoa
si kusudi alingane nasi bali sisi tuzidi kulingana naye. “Mkate ule tuumegao,
si ushirika wa mwili wa Kristo?”
(1Kor. 10:16). Tunaupokea uhai wenyewe.
Ushirika
huo unatakiwa kutuunganisha na Kristo zaidi na zaidi, ukikuza ndani mwetu
unyenyekevu, imani, tumaini na hasa upendo, ili moyo wetu ulingane na ule wa
Mwokozi aliyekufa kwa upendo wake kwetu. Kwa maana hiyo komunyo zetu
zinatakiwa kuwa na upendo mwingi zaidi na zaidi, kwa kuwa kila mojawapo
inatakiwa sio tu kutunza, bali kustawisha upendo wa Mungu ndani mwetu na hivyo
kutuandaa kumpokea Bwana kesho yake kwa utashi motomoto zaidi (bila ya kujali
umotomoto wa hisi ambao ni wa ziada tu: tunaweza kupokea vizuri ekaristi
katika ukavu mkubwa wa hisi, kama ilivyokuwa bora sala ya Yesu bustanini).
Inatakiwa kuwa kama mbio ya kumuendea Mungu ambayo izidi kuwa ya kasi: kama
vile vitu vinavyozidi kuanguka kwa kasi kadiri vinavyokaribia ardhi
inayovivuta, roho zinatakiwa kumwendea Mungu kwa kasi kadiri wanavyomkaribia
na kuvutiwa naye.
“Ninakuabudu
Mungu wangu, / unayejificha altareni. / Ninakutolea moyo wangu, / usiofahamu
siri yako... / Ewe Yesu nipe pendo lako, / tumaini kwako na imani. / Umeteswa
nini, Bwana mwema, / kwa kunipa mkate wa uzima? / Yesu unifiche ndani yako, /
ili nilionje pendo lako. / Yesu pelikane nitazame, / na kwa damu yako nitakase.
/ Tone moja ndilo linatosha, / na dunia yote yaokoka. / Ndani ya mafumbo Yesu
yumo. / Atafumbuliwa kwangu lini? / Nikuone, Yesu, uso wako, / nishiriki nawe
heri yako” (mt. Thoma wa Akwino).
Mtu
akiishi hivyo ekaristi kila siku, atafikia urafiki wa ndani naye, na kuzama
zaidi na zaidi katika fumbo kuu la altare na kulionja, ikiwa ni pamoja na
thamani isiyo na mipaka ya misa, chemchemi ya neema mpya daima, ambayo vizazi
vyote vinatakiwa kutuliza kiu yao na kupata nguvu ya kufikia mwisho wa safari
ya kuelekea uzima wa milele. Nabii Eliya alipoishiwa nguvu alizipata upya kwa
kula mkate kutoka mbinguni, akatembea mpaka mlima Horebu, unaomaanisha kilele
cha ukamilifu.
Katika
ushirika mtakatifu Kristo anatuambia kama alivyomuambia mt. Augustino:
“Ndimi mkate wa watu wa uzima... Kua, nawe utanila; lakini hutanigeuza ndani
mwako, kama chakula cha mwili wako; bali wewe utageuzwa ndani mwangu”.
Anayemshiriki kweli Kristo anakuja kuunganishwa naye zaidi na zaidi, hata
kuishi kwa mawazo yake na kwa upendo wake; hapo anaweza kusema: “Kwangu mimi
kuishi ni Kristo, na kufa ni faida” (Fil. 1:21), kwa kuwa ni mlango wa uzima
usio na mwisho.
KUZIDI
KUUNGANA NA KRISTO NA UTAKATIFU
Mafundisho
hayo kuhusu kuungana na Kristo zaidi na zaidi yana uwezo mkubwa ajabu wa
kumfaidisha anayeamua kuyaishi.
Kwanza
ili tufie dhambi na matokeo yake tukumbuke kwamba “tulizikwa
pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake… ili mwili wa dhambi
ubatilike, tusitumikie dhambi tena” (Rom. 6:4-6); “hao walio wa Kristo
Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake” (Gal.
5:24). Ndiyo kufia dhambi kwa ubatizo na kitubio.
Halafu,
kwa mwanga wa imani na uvuvio wa Roho Mtakatifu, Mkristo anatakiwa kuvaa
“utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye
aliyeuumba... Basi… jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole,
uvumilivu… Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu”
(Kol. 3:10-14). Ndiyo hatua ya kuangazwa ya wanaomuiga Yesu Kristo kwa
kujipatia msimamo wake, roho ya mafumbo yake, ya mateso, kifo na ufufuko wake.
Ndiyo njia waliyoifuata watakatifu wote, kufuatana na maneno ya mtume:
“Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa
kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya
mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo” (Fil. 3:8).
Njia
hiyo inaelekeza kwenye muungano kama wa kudumu na Mwokozi:
“Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo
aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikiri yaliyo juu, siyo yaliyo
katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika
Mungu” (Kol. 3:1-3). Hapo amani ya Mwokozi itatawala roho ya mtu anayependa
kumuambia, “Bwana, nipe nafsi yako, pokea nafsi yangu”. Elekeo la roho
kwake linamuambia tunatamani nini, likimtolea udhaifu wetu, nia yetu njema,
azimio letu la uaminifu, kiu yetu ya nafsi yake. Ndiyo hatua ya kuzama kwa
upendo katika mafumbo, kama utangulizi wa heri ya kuonana na Mungu uso kwa uso
mbinguni.
Wengi
wanadanganyika kuwa wanaweza kufikia muungano na Mungu pasipo kumkimbilia
mfululizo Bwana wetu: hao watafikia tu ujuzi wa mbali wa Mungu, sio ule
mtamu unaoitwa hekima ambayo ni kama mang'amuzi ya Mungu na ya maongozi yake
katika mambo yote, hata yale madogo. Tusiache kamwe kwa makusudi kuzingatia
ubinadamu wa Mwokozi katika sala: kwa kuwa ndiye njia inayoelekeza kwa umungu
wake. Tufikirie mara nyingi utajiri wa Kiroho wa Yesu, wa akili, utashi na
hisi zake, ili tuzidi kuelewa neno lake: “Mimi
ndimi njia, na kweli, na uzima” (Yoh. 14:6).
1.6. MSAADA WA MAMA MARIA
Tunaposema
juu ya misingi ya maisha ya Kiroho, hatuwezi kuzungumzia kazi ya Kristo
mshenga juu ya mwili wake wa fumbo tusidokeze pia juu ya msaada wa mama Maria.
Wapo Wakatoliki kadhaa wasioamini vya kutosha haja ya kumkimbilia Maria ili
kuungana na Mwokozi kwa undani zaidi. Mt. Alois Maria Grignion de Montfort
alisema juu ya “walimu wanaomjua Mama wa Mungu kinadharia tu, kwa namna kavu,
tasa na baridi; wanaoogopa ibada kwa Bikira mtakatifu itatumika vibaya hivi
hata kwa kumheshimu mno Mama mtakatifu Bwana atachukizwa. Wakiongelea ibada
kwa Maria ni kwa kuzuia namna zake zisizofaa kuliko kwa kuihimiza”; hata
tunaweza kudhani wanamuona Maria kama kizuio kwa kufikia muungano na Mungu!
Akasema ni kiburi kutowajali wasaidizi tuliopatiwa na Mungu kutokana na
udhaifu wetu. Muungano wa ndani na Bwana katika sala unasaidiwa na ibada
halisi na kubwa kwa Maria.
Mt.
Thoma wa Akwino aliandika: “Kazi ya mshenga ni kuwasogeza na kuwaunganisha
wale ambao amewekwa katikati yao: kwa kuwa pande mbili zinaungana kwa njia ya
mshenga. Basi, kuunganisha watu na Mungu ni kazi hasa ya Kristo, kwa kuwa
ndiye aliyewapatanisha na Mungu alivyosema mt. Paulo: ‘Mungu alikuwa ndani
ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake’ (2Kor. 5:19). Kwa hiyo
mshenga kamili kati ya Mungu na watu ni Kristo tu, kwa sababu kwa kifo chake
amawapatanisha watu na Mungu. Hata mt. Paulo aliposema: ‘mpatanishi kati ya
Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu’ akaongeza, ‘ambaye
alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote’ (1Tim. 2:5-6). Hata hivyo
hakuna kinachozuia wengine wasiitwe kwa namna fulani washenga kati ya Mungu na
watu kwa kuwa wanachangia muungano wa Mungu na watu kama wahudumu katika
ugawaji”. Kwa maana hiyo manabii na makuhani wa Agano la Kale wanaweza
kuitwa washenga; kama vile mapadri wa Agano Jipya, walio wahudumu wa mshenga
halisi. Mwalimu huyo akaongeza kuwa “ni
kwa ubinadamu wake kwamba Kristo ni mshenga:
kwa sababu ni kama binadamu kuwa yeye yupo kati ya pande mbili: chini ya Mungu
kwa maumbile, juu ya watu kwa ukuu wa neema na utukufu. Tena kama binadamu
anawaunganisha watu na Mungu akiwatolea amri na zawadi za Mungu, na kutoa
fidia na kusali kwa ajili yao”. Yesu alitoa fidia na kustahili kama binadamu,
ambaye fidia na stahili zake zilikuwa na thamani isiyo na mipaka kutokana na
nafsi yake ya Kimungu. Hapo tuna ushenga wa aina mbili, wa kushuka na wa
kupanda, maana yake wa kuwapa watu mwanga na neema ya Mungu na wa kumtolea
Mungu ibada na malipizi anayostahili kwa ajili ya watu. Basi, hakuna
kinachozuia uwepo wa washenga washiriki
chini ya Kristo. Mt. Alberto alisema juu ya ubora wa ushenga wa Maria: “Yeye
hakuingizwa na Bwana kwenye huduma, bali kwenye ushirika na msaada, kadiri ya
maneno, ‘nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’ (Mwa. 2:18)”. Maria
alichaguliwa na Bwana si kuwa mhudumu, bali awe mshiriki wa pekee na wa ndani
wa ukombozi wa wanadamu.
Maria
kama Mama wa Mungu, je, hakukusudiwa
kuwa mshenga kwa wote na yote? Kuwa
kati ya Mungu na watu? Kwa hakika Maria yuko chini kuliko Mungu na Kristo kwa
kuwa ni kiumbe; lakini pia ameinuliwa juu kuliko watu wote kwa neema ya kuwa
Mama wa Mungu, na kwa ukamilifu wa neema aliyojaliwa tangu achukuliwe mimba
hali amekingiwa dhambi asili, ukamilifu ambao ukaongezeka moja kwa moja hadi
kifo chake. Naye hakuchaguliwa tu awe mshenga kutokana na umama wake wa
Kimungu, bali kweli alikabidhiwa na kutekeleza kazi hiyo ambayo inamfaa kwa
sababu kuu mbili: 1° kwa kuwa alichangia sadaka ya msalabani kwa malipizi na stahili zake;
2° kwa kuwa haachi kutuombea, kutupatia
na kutugawia neema zote tunazopokea. Ndio ushenga wa kupanda na kushuka
tunaopaswa kuuzingatia ili kuufaidi kila siku zaidi.
Maisha
yake yote bikira Maria alichangia sadaka ya Mwanae hadi aliposema,
“Imekwisha” (Yoh. 19:30).
Kwanza
ilihitajika ridhaa yake, aliyoitoa siku ya kupashwa habari na malaika, ili
fumbo la umwilisho lifanyike, kama kwamba Mungu alisubiri kibali cha binadamu
kwa sauti ya Maria. Kwa njia hiyo alichangia sadaka ya msalabani kwa kutupatia
kuhani na sadaka yake.
Aliichangia
pia kwa kumtolea Mwanae hekaluni kama sadaka safi, mzee Simeoni alipoona kwa
mwanga wa kinabii kuwa mtoto wake ndiye wokovu ulioletwa na Mungu “tayari
machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa
watu wako Israeli” (Lk. 2:31-32). Maria akiwa ameangaziwa kuliko yeye,
alimtoa Mwanae na kuanza kuteseka pamoja naye, akitabiriwa kwamba mtoto
amewekwa “kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni
mwako” (Lk. 2:34-35).
Hasa
chini ya msalaba Maria alichangia sadaka ya Kristo, akiungana naye katika
malipizi na stahili kwa undani kuliko tunavyoweza kueleza. Baadhi ya
watakatifu, hasa waliotiwa madonda ya Yesu, waliungana kwa namna ya pekee na
mateso na stahili za Mwokozi. Lakini hayo ni madogo yakilinganishwa na
muungano wa Maria aliyemtoa Mwanae kama mwenyewe alivyojitoa. Yesu angeweza
kuzuia kwa urahisi ukatili wa watesi wake usimuue, lakini alitoa kwa hiari
uzima wake: “Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao
uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena” (Yoh. 10:18). Alijinyima
haki ya kuishi, akijitoa mhanga kwa wokovu wetu. Basi, Maria alisimama
“penye msalaba wake Yesu” (Yoh. 19:25), akiungana naye kwa undani katika
mateso na kujitoa, “akijinyima haki zake za kimama kuhusu Mwanae kwa ajili
ya wokovu wa watu wote” (Benedikto XV). Alikubali kifodini cha Kristo na
kukitoa kwa ajili yetu. Kadiri ya upendo wake alihisi uchungu wa Mwanae katika
mwili na katika roho. Maria alionja kuliko wote uchungu wa Mwokozi; alisikitishwa
na dhambi kadiri ya upendo wake: kwa Mungu, anayechukizwa nayo; kwa Mwanae, aliyesulubiwa nayo; kwa
watu ambao roho zao zinaangamizwa nayo. Upendo wa Bikira ulipita ule wa
watakatifu wowote.
Alichangia
sadaka ya msalabani kama malipizi
kwa kumtolea Mungu kwa niaba yetu, kwa uchungu mwingi na upendo mkuu, uhai wa
Mwanae mpenzi, aliyemuabudu na kumpenda kuliko nafsi yake mwenyewe. Saa hiyo Mwokozi
alikuwa akilipa kwa niaba yetu, kwa matendo yake ya kibinadamu
yaliyoshiriki thamani isiyo na mipaka ya nafsi yake ya Kimungu, yenye uwezo wa
kufidia dhambi zote na zaidi tena. Upendo wake ulimpendeza Mungu kuliko
anavyochukizwa na dhambi zote. Ndio kiini cha fumbo la ukombozi. Akiungana na
Mwanae huko Kalivari, Maria alilipa kwa niaba yetu si kwa
msingi wa haki yenyewe, bali wa
urafiki wa ndani au upendo uliomuunganisha na Mungu. Mwanae alipokuwa
akifa msalabani kama mtu aliyeshindwa na kutupwa, yeye hakuacha hata kidogo
kumuamini. Ndilo tendo kuu la imani; ndilo pia tendo kuu la upendo baada ya
lile la Kristo mwenyewe. Tendo hilo limemfanya Maria malkia
wa mashahidi, kwa kuwa sio tu shahidi kwa ajili ya Kristo, bali pamoja
naye, hivi kwamba msalaba mmoja tu uliwatosha Mwana na Mama aliyesulubiwa
kwa namna fulani kutokana na upendo wake kwake. Hivyo akawa mkombozi
mshiriki kwa maana alikomboa binadamu pamoja na Kristo, kwa njia yake na
ndani mwake.
Kwa
sababu hiyohiyo, yale yote ambayo Kristo msalabani alitustahilia kwa msingi wa
haki, Maria alitustahilia kwa msingi wa upendo uliomuunganisha na Mungu.
Kristo tu, akiwa ni kichwa cha binadamu wote, aliweza kustahili kwa haki
tushirikishwe uhai wa Kimungu, lakini ilifaa kwamba Mungu azingatie pia
stahili za Maria aliyeungana naye katika kazi ya wokovu. Mapokeo yote ya
Mashariki na Magharibi yanamuita Eva mpya, Mama wa watu wote upande wa roho,
kama vile Eva alivyokuwa upande wa mwili. Basi Mama
wa Kiroho wa watu wote anatakiwa kuwapa uzima wa Kiroho, ingawa si kama
asili yake kuu. Msingi wa mafundisho hayo ni maneno ya Yesu kufani:
“alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, ‘Mama, tazama mwanao’. Kisha akamwambia yule
mwanafunzi, ‘Tazama mama yako’. Na tangu saa ile mwanafunzi yule
akamchukua nyumbani kwake” (Yoh. 19:26-27). Maana yenyewe ya maneno hayo
yanamhusu Yohane, lakini kwa Mungu matukio na watu wana maana nyingine pia;
hapo Yohane aliwakilisha watu wote waliokombolewa na sadaka ya msalabani.
Mungu anasema sio tu kwa maneno, bali pia kwa matukio na watu ambao mikononi
mwake wanamaanisha yale anayoyataka. Kama vile neno la Yesu lilivyosababisha
ndani ya Maria mapendo makubwa ya kimama kwa mwanafunzi mpendwa, vilevile hayo
mapendo yakaenea kwa wote na kumfanya kweli mama wa Kiroho wa watu wote. Basi,
ikiwa mama mwema anaweza kuwastahilia watoto wake neema nyingi kutokana na
maadili yake, zaidi Maria anaweza kuwastahilia watu wote kutokana na ukamilifu
wa upendo wake unaomuunganisha na Mungu, ingawa
si kustahili kwa msingi wa haki.
Ndio
ushenga wa kupanda wa Maria, ambao akiwa na Bwana wetu alitoa sadaka ya
msalabani kwa ajili yetu; sasa tuzingatie ushenga wa kushuka ambao anatugawia
zawadi za Mungu.
Akiwa
ni Mama wa watu wote, Maria anashughulikia wokovu wao, akiwaombea na kuwapatia
neema zile wanazojaliwa. Ndiyo sababu Kanisa linamuelekea ili kupatiwa neema
za kila aina, za kimwili na za Kiroho, zikiwa ni pamoja na wongofu na kifo
chema, bila ya kusahau zile zinazohitajiwa na mabikira ili kutunza ubikira wao,
na wachungaji kwa ajili ya utume wao, na wafiadini ili wadumu katika kukiri
imani. Kwa namna fulani hata neema za sakramenti zinagawiwa kwa njia yake, kwa
kuwa alitustahilia hizo huko Kalivari akiwa ameunganika na Bwana wetu, halafu
kwa sala zake anatuandaa kuzipokea vema; tena pengine anatutumia padri ili
tuweze kufaidi huduma hiyo. Imani ya Kanisa inasali mfululizo atuombee “sasa
na saa ya kufa kwetu”; kwa maneno hayo tunajiombea neema
ya sasa hivi, ambayo ni ya pekee kwa kuwa ni tofauti kwa kila mtu na kwa
kila nukta aliyonayo. Ikiwa sisi tunatamka maneno hayo bila ya kuyazingatia,
Maria ni tofauti, hasinzii: anajua mahitaji yetu ya Kiroho ya kila nukta, na
kutuombea na kutupatia neema zile tunazojaliwa.
Msingi
wa imani hiyo umo katika Maandiko na Mapokeo. Maria aligawa neema kuanzia
wakati wa maisha yake duniani. Kwa njia yake Yesu alimtakasa Yohane mtangulizi
wake, akaimarisha imani ya wanafunzi kwenye arusi ya Kana. Kwa njia yake Roho
Mtakatifu alimiminwa juu ya mitume, alipokuwa akisali pamoja nao. Zaidi tena,
baada ya kupalizwa mbinguni, akiwa ni Mama mwenye heri ya milele, anajua
mahitaji ya watoto wake aliowaacha duniani. Basi, kwa upendo wake mkuu
anatuombea, na kwa uwezo wake mkuu juu ya moyo wa Mwanae anatupatia neema zote
tunazojaliwa, zile zote wanazozipata wasiofanya moyo wao kuwa mgumu. Ndiyo
sababu alifananishwa na mfereji unaoleta maji, pia na shingo la Mwili wa
Kristo.
Tutakaposema
juu ya sala ya wanaoendelea tutaongelea ibada halisi kwa bikira Maria. Lakini
tangu sasa tunaona umuhimu wa kufanya mara nyingi sala
ya washenga, yaani kuanza kuongea na Maria kwa tumaini kubwa ili
atufikishe hadi kuungana na Mwanae kwa undani, halafu kwa njia ya Mwokozi
tuinuke hata muungano na Mungu.
1.7. USTAWI WA UZIMA WA NEEMA
KWA NJIA YA STAHILI, SALA NA SAKRAMENTI
Hatuwezi
kusema juu ya chemchemi ya maisha ya Kiroho bila ya kusema juu ya ustawi wa
neema ya utakaso na wa upendo. Hakuna wokovu bila ya adili hilo la Kimungu,
lililo kuu kuliko yote na linalotakiwa kuyaongoza na kuyahuisha mengine pia.
Tena halitakiwi kubaki lilivyo, bali kukua
ndani mwetu hadi siku ya kufa. Fundisho hilo linaweza tena linapaswa kuangaza
maisha yote ya Kiroho, kwa kuwa ni msingi wa himizo lolote la kusonga mbele
kwa unyenyekevu na moyo mkuu, kwa kutamani muungano wa ndani na Mungu, kwa
kujitahidi kuupata pamoja na kuuomba. Basi, tuone kwanza kwa nini upendo unatakiwa kustawi daima, halafu jinsi
unavyostawi.
KWA
NINI UZIMA WA NEEMA NA UPENDO USTAWI NDANI MWETU HADI KUFA?
Hata
katika kiwango kidogo upendo halisi (ambao tuliupokea kwa ubatizo na pengine
kurudishiwa kwa upatanisho) unampenda tayari Mungu Mwokozi kuliko yote, na kwa
ajili yake unampenda jirani kama mtu mwenyewe anavyojipenda. Kiwango hicho cha
upendo uliomiminwa rohoni kinapita tayari bila ya kifani pendo la kimaumbile
tunaloweza kuwa nalo kwa Muumba na kwa watu; hakimbagui yeyote, kwa kuwa ubaguzi huo ungekuwa dhambi ya mauti
ambayo ingeufuta upendo. Lakini upendo huo wa wanaoanza uko mbali na ushindi
juu ya umimi wowote. Unaendana bado na kujipendea ambako, ingawa si dhambi ya
mauti, kunasababisha dhambi nyepesi nyingi na hivyo kuzuia upendo usiweze
kutenda na kupamba vizuri.
Bila
ya shaka, upendo huo wa kiwango cha chini unatakiwa kustawi: “Hii ndiyo dua
yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” (Fil. 1:9). “Bwana
awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote,
kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila
lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu” (1Thes. 3:12-13).
“Mwenye haki na azidi kufanya haki, na mtakatifu azidi kutakaswa” (Ufu.
22:11). “Njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata
mchana mkamilifu” (Mith. 4:18). Ni kwamba hapa duniani Mkristo ni msafiri
anayemuelekea Mungu. Anamkaribia kwa vitendo vya upendo ulio kamili zaidi na
zaidi, kwa “hatua za upendo” (mt. Gregori Mkuu). Upendo unaweza na kupaswa
kustawi mfululizo, la sivyo Mkristo badala ya kusafiri anasimama kabla
hajafika. Lengo la njia ni kutembea, si kulala. Kila mtu anayeelekea uzima wa
milele anatakiwa kukua katika upendo ili azidi kumkaribia Mungu: sio tu
wanaoanza na wanaoendelea, bali hata waliokamilika. Tena hao wa mwisho
wanapaswa kwenda kasi zaidi kadiri
wanavyomkaribia na kuvutwa naye; nguvu ya maisha yao ya Kiroho inaongezeka
zaidi na zaidi, elekeo la roho yao linainuka zaidi na zaidi; kwao hakuna
machweo: mwili tu unadhoofika kwa uzee.
Juu
ya hayo Bwana alisema: “Mimi nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu”
(Yoh. 12:32). “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba
aliyenipeleka” (Yoh. 6:44). Mungu ndiye anayetufanya twende, na anakotuvuta
ni kwake: ndiye mwanzo na mwisho wa yote, ndiye wema mkuu unaovuta upendo kwa
nguvu kadiri tunavyomkaribia. Ndiyo sababu katika maisha ya watakatifu, ustawi
wa upendo miaka yao ya mwisho ni mkubwa sana; ingawa wanabeba uzito wa uzee na
wa udhaifu fulani upande wa hisi (k.mf. kumbukumbu) wanang’amua ukweli wa
maneno ya Zaburi (103:5): “Ujana wako unarejezwa kama tai”. Maendeleo hayo
ya kasi zaidi na zaidi yalikuwepo hasa katika bikira Maria, kwa kuwa ndani
mwake hayakuzuiwa na chochote, tena yalikuwa ya haraka kadiri ilivyokuwa kubwa
neema ya kwanza aliyojaliwa. Basi, upendo ndani mwetu unatakiwa sio tu kustawi
hadi kufa, bali kustawi zaidi na zaidi, kama vile kasi ya kitu kinachoanguka
inavyozidi hadi kikafika ardhini.
Ikiwa
ni hivyo, upendo unastawi vipi ndani
mwetu? Kwa kuwa hata katika kiwango cha chini unampenda tayari Mungu kuliko
yote, na jirani kwa jumla bila ya kubagua yeyote, hauwezi kuenea
zaidi: lakini unaweza kuongezewa
nguvu na kutia mizizi ndani ya utashi wetu zaidi na zaidi. Upendo
hauongezeki kama nafaka, yaani haukui kwa wingi, bali kwa ubora, kwa
kuongezewa nguvu katika utashi, ukizidi
kuuelekeza kwenye mema yapitayo maumbile na kuuepusha na maovu. Mfano wake
ni elimu ya msomi ambayo haipati daima taarifa mpya, ila inazidi kuchimba na
kuwa na hakika; vivyo hivyo upendo unastawi ndani mwetu, ukitufanya tuwapende kwa
namna kamili na safi zaidi na zaidi Mungu kwa ajili yake mwenyewe na
jirani kwa ajili ya Mungu. Tukielewa mafundisho hayo, tunaona haja ya roho kutakaswa
kila uchafu na kudhihirisha jinsi maadili makuu yanavyolenga ukweli na wema wa
Mungu. Basi, upendo kama joto, unastawi kwa ubora, kwa kupata nguvu zaidi na
zaidi; na hiyo inafanyika kwa namna tatu: kwa stahili, kwa sala na kwa
sakramenti.
Tendo
linalotokana na upendo (au adili lolote linaloongozwa na kuhuishwa na upendo)
linastahili tuzo linalopita maumbile, hasa ustawi wa upendo wenyewe. Stahili
hazisababishi zenyewe ustawi huo, kwa kuwa upendo si adili
la kujipatia, bali ni adili la
kumiminiwa. Kama vile Mungu tu anaweza kuuweka ndani mwetu (kwa kuwa ni
kushiriki uzima wa ndani mwake mwenyewe), yeye tu anaweza kuustawisha: “Mimi
nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye
kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu
akuzaye… ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu” (1Kor. 3:6-9).
Yeye “atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya
haki yenu” (2Kor. 9:10).
Ingawa
matendo ya upendo hayawezi kusababisha
ustawi wa adili hilo, yanauchangia
kwa namna mbili, yaani kwa kuustahili na
kwa kutuandaa kuupokea.
Stahili
ni haki ya kupata tuzo; hailisababishi ila inalipata. Mwadilifu kwa matendo
yake mema yanayopita maumbile anastahili upendo wake ustawi, ilivyofundishwa
na Mtaguso wa Trento. Bwana kabla hajampa tuzo la mbinguni anampa hapa duniani
lile la kukua katika upendo wa Kimungu. Wazushi walioitwa Watulivu walidharau
tuzo la Mungu wakijidai eti, hawajitafutii faida; kumbe kadiri
roho inavyojipenda, inatamani zaidi tuzo hilo: kumpenda Mungu kwa nguvu na kwa
usafi mkubwa zaidi na zaidi, jambo lisilotenganika na ustawi wa maadili
mengine ya kumiminiwa na wa vipaji vya Roho Mtakatifu.
Matendo
ya upendo na ya maadili yanayoongozana nao, sio tu kwamba yanastahili ustawi
wa upendo, bali pia yanaandaa
kuupokea, kama kwa kufungua na kupanua akili na utashi ili uzima wa Kimungu
uweze kuvipenya zaidi, na kwa kuvitakasa uviinue juu zaidi. Hiyo ni kweli hasa
kwa matendo motomoto ya upendo. Tendo la ukarimu mkubwa la upendo wa Mungu
linaathiri pengine maisha yote ya baadaye na kustahili ustawi mkubwa wa upendo,
likituandaa kupokea ustawi huo. Ni kama kwamba tunainuliwa hadi
ghorofa ya juu, ambapo tuna mtazamo mpya wa mambo ya Mungu na mvutio mkubwa
zaidi kwa mambo hayo. Aliyekuwa na talanta mbili anaongezewa, yaani Roho
Mtakatifu anakuwemo ndani mwake kwa namna mpya inayofanya kazi zaidi. Kwa
kawaida Roho Mtakatifu anamsukuma mtu kulingana na kiwango cha maadili na
vipaji alichonacho au kulingana na usikivu wake. Kama angemsukuma bila ya sababu atende kwa upungufu, maana yake ingekuwa amepokea bure
kiwango kikubwa cha maadili na vipaji. Basi, mwadilifu asipozuia
kazi ya Mungu, atapokea neema kubwa zaidi na zaidi apande kwa ukarimu
kumuelekea Mungu.
Wanateolojia
kadhaa wamefundisha kuwa Mungu anatukuzwa na tendo moja la upendo la talanta
kumi kuliko anavyotukuzwa na vitendo kumi vya upendo vya talanta mojamoja;
vilevile kuwa mwadilifu mmoja aliye
mkamilifu anampendeza Mungu kuliko wengine wengi wanaobaki katika wastani. Ubora
ni muhimu kuliko wingi. Ndiyo sababu ukamilifu wa Maria unapita ule wa
watakatifu wote, kama vile almasi moja ina thamani kuliko vito vingine vingi.
Basi,
upendo unatakiwa kustawi kwa njia ya stahili zetu hadi tutakapokufa; pamoja na
adili hilo utakua pia utayari wetu wa kupokea ongezeko lingine: moyo unapanuka
zaidi na zaidi na ujazo wake wa Kimungu unaongezeka: “mioyo yetu
imekunjuliwa… Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa… nanyi pia mkunjuliwe
mioyo” (2Kor. 6:11,13).
Mara
nyingi tunasahau tuko safarini kuelekea uzima wa milele, na tunajaribu
kustarehe katika maisha ya hapa duniani kama kwamba yangedumu moja kwa moja.
Ni kama maabiria wa treni bora ambamo wanakula na kulala kama hotelini hata
wakasahau wako safarini; pengine wakiangalia dirishani wanaona mandhari
ikibadilika haraka na baadhi ya wenzao wakiteremka: hapo wanajisemea kuwa wao
pia watawahi kufikia mwisho wa safari. Shida ni kwamba, ingawa tunaona wengi
kufa, hatupati hakika ya ndani kuwa siku fulani itakuwa zamu yetu. Basi,
tuishi kwa kukazia macho mwisho wa safari, kusudi tusipoteze tena muda
tuliojaliwa, bali tuujaze iwezekanavyo matendo ya kustahili uzima wa milele.
Ustawi
wa upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji vinavyoongozana nao)
unapatikana si kwa njia ya stahili tu, bali kwa sala pia. Ustawi huo unaombwa
na Kanisa linaposali hivi, “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani,
matumaini na mapendo” (Jumapili ya 30 ya mwaka).
Tukumbuke
tofauti iliyopo kati ya kuomba na kustahili: asiye na neema ya utakaso hawezi
kustahili (kwa kuwa neema hiyo ndiyo asili ya stahili yoyote ipitayo maumbile);
lakini kwa neema ya msaada anaweza kuomba (k.mf. neema ya wongofu) na akiomba
kwa unyenyekevu, imani na udumifu, atapata. Stahili
inahusu haki ya Mungu; kumbe sala inaelekea
huruma ya Mungu ambayo mara nyingi inanyanyua walioanguka na kusikiliza ombi
lao lisilostahili chochote. Mtu duni kuliko wote, aliyetumbukia katika vilindi
ambamo hawezi kustahili tena, anaweza kulilia huruma ya Mungu: “Kilindi
chapigia kelele kilindi” (Zab. 42:7), yaani kilindi cha unyonge kinalilia
kile cha huruma; mkosefu akisihi kwa moyo wote anasikilizwa, roho yake
inanyanyuliwa, na Mungu anatukuzwa. Nguvu ya sala haitegemei tu neema ya
utakaso iliyo ya lazima ili kustahili.
Tukishaongoka
na kufanywa waadilifu, tunaweza kustawishiwa uzima wa neema kwa njia ya
stahili na kwa sala pia. Hiyo ikiwa na unyenyekevu, imani na udumifu,
inatupatia ustawi wa maadili ya Kimungu tunaoomba katika maombi matatu ya
kwanza ya Baba Yetu. Sala ya mwadilifu, anayependa kutafakari polepole na
kujilisha kwa undani maombi yake (hata kusimama pengine nusu saa kuzamia
mojawapo kwa upendo), inastahili pamoja na kuomba neema: inampa haki ya
kustawishiwa upendo ulioisababisha, na kwa nguvu ya ombi inapata
zaidi kuliko inavyostahili. Tena, ikiwa ni motomoto kweli, inapata mara tu. Hapo tunaweza kuona matunda ya sala na jinsi
inavyomvuta Mungu ajitoe kwetu kwa undani, nasi tujitoe kwake. Hapo moyo
unazidi kupanuka upokee neema kwa wingi zaidi; roho inajitenga na malimwengu
na kumtamani zaidi Mungu, ambaye ndani yake inakuta yale yote yanayostahili
kupendwa, tena kwa ngazi ya juu. Haitatosha kamwe kuyaishi hayo katika sala ya
moyo, k.mf. katika kimya kikubwa cha usiku, ambapo mtu yuko peke yake na Mungu,
Muumba na Mwokozi wake. Hapo anang’amua kuwa Mungu ni mwema kupita kiasi, na
sala ni mwanzo wa uzima wa milele.
Tena,
kwa njia ya sala mwadilifu anaweza kupata neema kadhaa ambazo hawezi
kuzistahili, hasa ile ya kudumu mpaka mwisho. Hawezi kustahili zawadi hiyo
kwa kuwa ni kudumu kwa hali ya neema ambayo ni chanzo chenyewe cha stahili
kisichoweza kustahiliwa. Hata hivyo neema hiyo ya kifo chema inaweza
kupatikana kwa sala nyenyekevu, yenye imani, ya kila siku. Kanisa linatualika
kukariri kwa bidii: “Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu,
sasa na saa ya kufa kwetu. Amina”.
Vivyo
hivyo tunaweza kumuomba Mungu neema ya kumjua kwa ndani zaidi na zaidi, yaani
ya kuzama katika sala, ambayo matokeo yake ni kuungana na Mungu kwa namna
imara na yenye matunda mengi zaidi: “Neno moja nimelitaka kwa Bwana, nalo
ndilo nitakalolitafuta: nikae nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana na kutafakari hekaluni mwake” (Zab. 27:4), yaani
kuona kila siku vizuri zaidi jinsi wema wake usivyo na mipaka kwa wale ambao
wanamtafuta na kumpata.
Hatimaye,
upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji saba) unastawi ndani mwetu kwa
njia ya sakramenti, hasa ekaristi. Stahili na sala za mwadilifu zinapata
zawadi za Mungu kulingana na imani na upendo alivyonavyo; kumbe sakramenti
zinaleta neema kwa nguvu zake zenyewe katika wale wasioweka kizuio. Yaani zenyewe
zinasababisha neema kwa kuwa ziliwekwa ili kutugawia stahili za Mwokozi.
Zinaleta neema bila ya kutegemea sala na stahili za yule anayeziadhimisha na
yule anayezipokea. Padri mwovu, na hata mtu asiye Mkristo, anaweza kuadhimisha
ubatizo halisi mradi awe na nia ya kufanya Kanisa linavyofanya.
Hata
hivyo sakramenti zinaleta neema kwa kiasi tofauti kulingana na juhudi za yule
anayezipokea. Mtaguso wa Trento umefundisha: “Kila mmoja anapokea uadilifu
kadiri Roho Mtakatifu anavyomtakia kulingana na utayari wake”. Kama vile
moto unawaka wenyewe, lakini sisi tunafaidi joto lake kadiri tunavyoukaribia,
upande wa roho tunafaidika na sakramenti kadiri imani yetu ilivyo hai na
utashi wetu ulivyo motomoto. Kwa msingi huo Mkristo mkosefu anajipatia neema
kadiri ya majuto yake wakati wa kupokea ondoleo la dhambi. “Inatokea kwamba
nguvu ya majuto ya mwenye kuungama ni kubwa, sawa au pungufu kuliko kiwango
cha neema alichokipoteza; hapo anapata tena neema kwa kiwango kikubwa, sawa au
pungufu kuliko awali” (mt. Thoma wa Akwino). Kwa mfano, aliyekuwa na talanta
tano kabla hajazipoteza kwa dhambi ya mauti, akija kuwa na majuto kama ya
talanta mbili, anapata tena neema, lakini kwa kiasi kidogo kuliko awali.
Kinyume chake, kwa majuto makubwa anaweza kuipata kwa kiwango kikubwa zaidi.
Hilo ni muhimu kwa wale wanaokuja kuanguka wakati wa kupanda mlima; wanaweza
kuinuka kwa bidii na kuendelea na safari yao kuanzia pale walipoanguka. Lakini
wakiinuka kwa kuchelewa na bila ya bidii inawatokea kwamba wanajikuta chini,
badala ya kuendelea tu kupanda.
Kwa
msingi huohuo komunyo moja yenye bidii inafaa kuliko nyingi vuguvugu. Kadiri
tunavyomkaribia Yesu katika ekaristi kwa imani hai, tumaini imara na upendo
motomoto (upande wa utashi, si wa hisi) tunafaidi joto lake, yaani neema za
mwanga, upendo na ushujaa za kututosha sisi hata kuwashirikisha wengine.
Kinyume
chake, tunda la komunyo linaweza kuwa dogo tukikaribia meza takatifu kwa namna
ambayo inatosha tu tusikufuru. Hiyo inatakiwa kutufikirisha tuking’amua kuwa
hatuendelei kweli baada ya kukomunika kila siku kwa miaka kadhaa. Ingawa
tunapaswa pia kuzingatia kwamba mtu akiendelea, kadiri anavyokuja kujua ukuu
wa Mungu anazidi kufahamu vilevile unyonge wake mwenyewe. Inaweza kututokea
kwamba, kwa kuambatana na dhambi fulani nyepesi, tunda la komunyo ya kila siku
lizidi kupungua, kama kasi ya jiwe lililorushwa hewani wima ambayo inapungua
zaidi na zaidi mpaka jiwe likaanguka tena ardhini. Mungu atuepushe!
Tunatakiwa
tuwe na bidii nyingi kutosha itutokee kama katika maisha ya watakatifu: kwamba
kila komunyo yetu iwe na upendo mkubwa
na matunda mengi kuliko ile iliyotangulia. Kumbe mara nyingi uzembe na
uvuguvugu yanazuia ustawi huo.
Baada
ya kuongelea chemchemi za maisha ya Kiroho, tunapaswa kuzingatia lengo lake:
si lengo kuu tulilokwishalizungumzia tukisema kuwa maisha ya Kiroho ni mwanzo
wa uzima wa milele, ila lengo lile linaloweza kufikiwa duniani, yaani
ukamilifu wa Kikristo.
Zamani
watu wasiostaarabika waliona ukamilifu wa binadamu unategemea hasa ushujaa. Wengi kati ya wanafalsafa wa Kigiriki waliona unategemea
hasa hekima. Kumbe Injili inatuambia
kuwa unapatikana hasa katika upendo. Tuzikumbuke
kwa ufupi dhana hizo mbili za kwanza, tukitambua sura zilizonazo siku hizi.
Hivyo tutaweza kuthamini zaidi ukuu wa ile ya tatu, pia kwa sababu hizo mbili
zina chembe za ukweli ambazo chini ya upendo zinaweza kupata thamani kubwa.
Makabila
yasiyostaarabika waliweka ukamilifu wa binadamu hasa katika nguvu,
moyo, uhodari, tunavyoona katika hadithi zao. Pengine utaifa unaelekea
kuwarudisha watu kwenye kipeo hicho, kinachotukuza mambo yaliyo magumu, ambayo
yanahitaji nguvu nyingi na kuhatarisha uhai, k.mf. vitani. Ni mtazamo wa
askari, mpelelezi na rubani. Umechanganyikana na kiasi kikubwa cha kiburi, na
pengine cha utovu wa haki, tena hautoshi ili kumweka binadamu mahali pake
mbele ya Mungu na ya jirani.
Kuna
watu motomoto wanaosafisha dhana hiyo na kuihamisha upande wa roho
wakimfikiria Mkristo kuwa askari wa
Kristo na kujali mno kifodini. Kumbe ubora wa kifo hicho hautokani na kuwa
tendo la uhodari, bali na kuwa ishara angavu ya upendo mkuu. Karne tatu za
dhuluma za Kanisa la mwanzoni zilikuwa za uhodari, lakini hasa za upendo
mkubwa: ndio unaotofautisha wafiadini wa Kikristo na mashujaa wa kipagani.
Kwa
mtazamo unaofanana na huo kuna watu wanaoona ukamilifu umo hasa katika ugumu wa maisha (mafungo, makesha n.k.): huo unaweza kuhitajika kwa
utawa unaokusudia hasa sala na sadaka ambazo ni ishara za upendo. Ila
tusiufanye ugumu huo kuwa lengo wakati
ni njia tu ya maendeleo. La sivyo
maisha makamilifu zaidi yangekuwa yale magumu zaidi, si yale yenye lengo bora
na njia za kufaa zaidi kulifikia. Maisha ya Kiroho yanahusu uadilifu kuliko
ugumu. Kwanza si kila tendo gumu ni adilifu: pengine ni juhudi ya ushupavu tu.
Halafu uadilifu ni mgumu mara nyingi,
lakini si daima: vitendo kadhaa vya upendo vinatendeka pasipo shida, kwa
msukumo mkubwa wa roho, hata hivyo vina stahili kubwa kwa kuwa vinatokana na
upendo mkubwa. Je, nguvu ndio adili bora? Ndio sifa muhimu ya askari, lakini
je, ndio ukamilifu wa mtu kama mtu na wa Mkristo kama Mkristo?
Jibu
ni kwamba nguvu ni ya lazima kwa ukamilifu, lakini juu yake kuna haki
kuhusu wengine, kuna busara inayoongoza
maadili yote ya kibinadamu, na hasa kuna maadili
ya Kimungu yanayomlenga Mungu moja kwa moja: imani, tumaini na upendo.
Basi, hatuwezi kukubali kuwa ukamilifu wa mtu na wa Mkristo umo hasa katika
nguvu. Hiyo si ukamilifu wa akili yetu kuhusu ukweli mkuu, wala si ukamilifu
wa utashi wetu kuhusu wema mkuu, ila ni adili linaloshinda hofu tu ili tuzidi
kufuata njia nyofu hata tukiwa kwenye shida na hatari.
Ikiwa
ukamilifu haumo hasa katika ushujaa, je, utapatikana katika hekima?
Ndivyo walivyodhani wanafalsafa wengi, wakisema binadamu anatofautiana na viumbe vilivyo chini yake kwa akili
aliyonayo, kwa hiyo ukamilifu wake kama binadamu ni hasa ule wa akili yake,
yaani hekima au ujuzi mkuu.
Hakika
hekima inahitajika kwa ukamilifu,
lakini si kweli kwamba kumjua kimawazo Mungu kunafuatwa
daima na upendo kwake. Mwanafalsafa, hata kama ana akili na wazo sahihi
kuhusu Mungu kama asili na lengo kuu la
ulimwengu, anaweza akawa mwovu. Ukweli ni ukamilifu wa akili, lakini si
ukamilifu wa mtu mzima, wala si jema pekee la binadamu.
Elimu
inaweza kuwepo pasipo upendo kwa Mungu na kwa jirani, na hapo “huleta
majivuno” (1Kor. 8:1). Ukamilifu wa mtaalamu kama mtaalamu si ule wa
binadamu kama binadamu, wala ule wa Mkristo kama Mkristo. Tusichanganye
ukamilifu wa akili na ule wa mtu mzima unaohitaji kunyosha utashi kuhusu lengo
kuu. Utashi unakusudiwa kuelekezwa kwenye ustawi wa mtu
mzima, sio wa akili tu. Uadilifu unadai utashi
unyoshwe, tofauti na sanaa na sayansi. Hapo tu mtu anaitwa mtu mwema moja
kwa moja, sio tu mchoraji mzuri, mjenzi mzuri au mganga mzuri.
Hatimaye
hapa duniani kumpenda Mungu ni bora kuliko kumjua. Ujuzi unamvuta kwetu na
kumlazimisha ndani ya mipaka ya mawazo yetu finyu; kumbe upendo wa Mungu
unatuvuta kwake na kutufanya tupende ndani mwake hata yale tusiyoweza kuyajua
sawasawa, kwa sababu tuna hakika ya kuwa maisha yake ya ndani yaliyofichika
kwetu yanapendeza kupita kiasi.
Dhana
ya kuwa hekima ndiyo ukamilifu inajitokeza leo katika wale wanaojali elimu kuliko yote. Hata baadhi ya Wakristo wanaelekea kudhani
inawezekana kuufikia ukamilifu haraka kwa kusoma maandishi mengi ya watakatifu,
bila ya kujitahidi zaidi katika utekelezaji wa maadili yao, wala kukumbuka vya
kutosha kuwa sala ya kujaliwa kuzama
ndani ya Mungu inatakiwa kujaa upendo upitao maumbile na kujikana.
Tutaona
mbele kuwa sala hiyo sio ukamilifu hasa, bali huo umo katika kuungana na Mungu
kwa upendo; ila kumtazama kwa upendo ni njia
iliyounganika na lengo hilo kwa sababu
kunatuandaa moja kwa moja tuungane naye. Lengo letu lisiwe hasa sala hiyo,
bali Mungu mwenyewe ambaye apendwe kuliko yote.
Basi,
kwa ukamilifu vinahitajika kweli ushujaa na hekima, yanahitajika pia maadili
yote ya Kimungu na ya kibinadamu, pamoja na vipaji saba vya Roho Mtakatifu. Je,
ukamilifu umo katika jumla ya maadili? Ndiyo, mradi jumla hiyo iwe imepangwa vizuri kama muundo hai na kati ya maadili liwepo moja
lenye kuyatawala, kuyaongoza na kuyahuisha yote na kuelekeza juhudi zake zote
kwenye lengo kuu. Kama ni hivyo, ukamilifu umo hasa katika adili hilo kuu
ambalo mengine yote yanapaswa kulisaidia. Lenyewe ni lipi?
Bwana
ametukumbusha kwa namna mbalimbali kwamba amri inayotawala amri na mashauri
yote ni ile ya upendo iliyotajwa tayari katika Agano la Kale: “Mpende Bwana,
Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”
(Kumb. 6:5). “Umpende jirani yako kama nafsi yako. Mimi ndimi Bwana” (Law.
19:18). Ndicho kipeo kikuu kuliko ushujaa na hekima. Ndani yake mna nguvu ya
aina nyingine, tena mna hekima ya kweli na ya juu zaidi.
“Kwa
kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema,
utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana… Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu” (Kol.
3:12-14)”. Upendo ndio kifungo cha
ukamilifu kwa kuwa ni adili bora ambalo linatuunganisha na Mungu na kudumu
milele; ndio unaohuisha maadili mengine yote yawe na stahili kwa kuyalengesha
kwa Mungu mpendwa kuliko yote.
Mt.
Paulo alikuwa na hakika kuhusu upendo kuwa bora kuliko maadili mengine yote na
vipaji vya Roho Mtakatifu na karama mbalimbali: “Nijaposema kwa lugha za
wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu
uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote,
nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina
upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena
nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu”
(1Kor. 13:1-3). Pasipo upendo karama za pekee hazisaidii kitu kwa uzima wa
milele. Kwa sababu nisipokuwa na upendo sitekelezi amri ya kwanza ya Mungu,
silinganishi matakwa yangu na ya kwake, napotoka mbali naye, nimeshika njia
isiyoelekea kwenye moyo wa Mungu. Basi, katika wokovu “kama sina upendo, si
kitu mimi”, sistahili kitu ingawa ninaweza nikawasaidia wengine kuokoka kwa
mahubiri na kwa miujiza.
Kwa
maana hiyo, mt. Augustino alisema, “Penda,
halafu tenda lolote utakalo”, nalo litakustahilisha uzima wa milele.
Lakini uwe na upendo halisi, kwa sababu hakuna lililo baya kuliko upendo wa
bandia (unaofumba macho usitimize wajibu wake dhidi ya maovu: huo ni udhaifu,
ni ule upole wa kulaumiwa wa watu wasiomchukiza yeyote kwa kuwa wanaogopa. Au
ni miguso ya kibinadamu tu inayotaka kukubaliwa na upendo halisi na
kuuambukiza). Kati ya mapambano makuu ya leo, mojawapo ni lile kati ya upendo
halisi na upendo wa bandia, ambao unatukumbusha Makristo wa uongo
wanaozungumziwa na Injili. Uharibifu
mbaya zaidi ni ule unaohusu yaliyo bora, kama vile upendo ulio adili kuu.
Kwa kuwa yale yanayoonekana tu mema ni ya hatari kadiri yalivyo bora mema
halisi yanayoigizwa nayo (k.mf. kipeo cha wanaotaka kuunganisha madhehebu ya
Kikristo kwa kupunguza kweli za imani). Ikiwa kwa upumbavu au woga wale
wanaotakiwa kuwakilisha upendo halisi wanayakubali kwa namna moja au nyingine
yale yanayoficha upendo wa bandia, yanaweza kutokea mabaya yasiyopimika,
makubwa kuliko yale yanayoweza kusababishwa na watesi waliojitokeza ambao ni
wazi kuwa hatuwezi kushirikiana nao.
Tofauti
na upendo wa bandia, ndani ya ule halisi yamo maadili yote nayo yako chini
yake hivi kwamba yanaonekana kama namna na sura mbalimbali za upendo kwa Mungu
na kwa jirani. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo
hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni
uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo
haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo
lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika… Maana wakati wa sasa
tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso… Basi,
sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni
upendo” (1Kor. 13:4-8,12-13). Imani itatoweka kwa kumuona Mungu, tumaini kwa
kumpata, lakini upendo utadumu milele.
Kwa
upendo huo tunakuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Kadiri tunavyompenda Mungu
tunamfahamu na kama kumng’amua kwa ujuzi upitao maumbile, jina lake hekima
ya Kimungu. “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa
na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu
wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate
kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef. 3:17-19).
Mafundisho
hayohayo tumepewa na mt. Yohane: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo,
hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake… Yeye ampendaye Mungu,
ampende na ndugu yake” (1Yoh. 4:16,21). Mt. Petro aliandika vilevile:
“Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana, kwa sababu upendano
husitiri wingi wa dhambi” (1Pet. 4:8). Alivyosema Yesu: “Amesamehewa
dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk. 7:47).
Kadiri
ya mafundisho hayo, ukamilifu haumo hasa
katika unyenyekevu na ufukara, wala katika ibada, bali katika upendo kwa Mungu
na kwa jirani unaofanya matendo ya maadili mengine yote yastahili. Ufukara sio
ukamilifu, ila ni njia ya ukamilifu.
Basi, njia haitafutwi kwa ajili yake, bali kwa ajili ya lengo, nayo ni bora si kulingana na ukubwa wake, bali kulingana na jinsi
inavyolingana na lengo, kama vile daktari mzuri ni yule anayetoa matibabu
yanayoponya, si anayeyatoa mengi zaidi. Ni vivyo hivyo kuhusu unyenyekevu
unaotuinamisha mbele ya Mungu ili kupokea kwa mikono miwili msaada wake ambao
utuinue hadi kwake. “Unyenyekevu ni adili la msingi kwa kuwa unaondoa kizuio
kikuu, yaani kiburi, lakini umo chini ya maadili ya Kimungu yanayotuunganisha
na Mungu” (mt. Thoma wa Akwino). Hata adili la ibada, linalompatia Mungu
ibada inayompasa, liko chini ya maadili ya Kimungu; halistahili lisipohuishwa
na upendo. Si adili la Kimungu kwa sababu halimhusu Mungu moja kwa moja, ila ibada
yake. Tukisahau ukweli huo tunaweza tukazingatia liturujia kuliko Mungu
mwenyewe, mifano kuliko ukweli, namna ya kusali Baba Yetu kuliko maana yake:
hapo utumishi wa Mungu ungepiku upendo wake.
“Kila
kiumbe ni kamili kadiri kinavyofikia lengo
lake ambalo ndio ukamilifu wake wa mwisho. Sasa, lengo kuu la maisha ya
binadamu ni Mungu, na upendo ndio unaotuunganisha naye, kadiri ya neno la mt.
Yohane: ‘Kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu,
na Mungu anaishi katika muungano naye’. Basi, ukamilifu wa maisha ya
Kikristo umo hasa katika upendo” (mt. Thoma wa Akwino). Imani na tumaini
haviwezi kuwa kiini cha ukamilifu, kwa sababu vinaweza kuwepo katika mtu
ambaye kwa dhambi ya mauti amepotosha utashi wake mbali na Mungu, aliye lengo
lake kuu. Vinabaki ndani mwake kama mzizi wa mti uliokatwa na ambao unaweza
kuchipua tena.
Mt.
Thoma akaongeza: “Ukamilifu umo hasa
katika upendo kwa Mungu, halafu katika upendo kwa jirani, kwa kuwa ndio
amri kuu za sheria ya Kimungu”. Hatutaweza kamwe kusisitiza mno neno la
Bwana: “Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama
vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote
watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa
ninyi” (Yoh. 13:34-35). Ndiyo dalili kuu ya ustawi wa upendo wa Mungu
mioyoni mwetu: “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake,
yumo gizani hata sasa… Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia
uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.
Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana
uzima wa milele ukikaa ndani yake” (1Yoh. 3:14-15).
Sasa
tuzingatie mambo mawili yanayotofautisha ukamilifu wa duniani na ule wa
mbinguni.
Ni
lazima tusisitize neno hilo la mt. Thoma wa Akwino. Yeye alikubali kuwa akili
ni bora kuliko utashi unaoongozwa nayo, kuwa ni uwezo wa kwanza wa binadamu
unaomtofautisha na mnyama, kuwa mbinguni heri yetu itatokana hasa na akili kumuona Mungu uso kwa uso, kwa kuwa ndiyo njia ya kumpata
milele: kuzamisha akili yetu katika vilindi vya maisha yake ya ndani yakiwa
wazi tu. Hivyo Mungu atajitoa moja kwa moja kwetu, nasi tutajitoa kwake; sisi
tutakuwa naye kama mali yetu, nasi tutakuwa mali yake, kwa kuwa tutamfahamu
kama anavyojifahamu na anavyotufahamu. Upendo
wenye heri utakuwa matokeo ya huo mtazamo wa moja kwa moja wa umungu, tena
matokeo ya lazima, kwa kuwa utashi wetu utavutwa moja kwa moja na
uzuri wa Mungu. Tutaona wema wake mkuu kwa namna iliyo wazi hivi hata tusiweze
kutompenda; hatutaweza kuona kisingizio
chochote cha kusimamisha kwa nukta moja tu tendo hilo la upendo lililo juu
kuliko hiari yetu, na ambalo halitapimwa na muda, bali na umilele tulioshirikishwa, ile nukta pekee isiyokwisha kamwe ya Mungu
kuwepo pasipo badiliko. Mbinguni upendo kwa Mungu na furaha ya kuwa naye kama
mali yetu vitatokana kwa lazima na heri ya kumuona iliyo kiini cha heri yetu
yote.
Kama
ni hivyo, basi, mwalimu huyo aliwezaje kusema ukamilifu
wa Kikristo hapa duniani umo hasa
katika upendo ambao ni adili la utashi, badala ya kuwemo hasa katika
hekima au katika sala ya kumiminiwa ambazo zinahusu akili? Jibu alilolitoa ni
zito tena muhimu.
Kwa
ufupi alisema kuwa kipawa fulani kinaweza kuwa bora kuliko kingine kwa
maumbile yake, lakini tendo fulani la hicho cha pili linaweza kuwa bora kuliko
mojawapo la hicho cha kwanza. Kwa mfano uwezo wa kuona ni bora kuliko ule wa
kusikia, na kuwa kipofu ni tatizo kubwa kuliko kuwa kiziwi; lakini kusikiliza
muziki bora kuna thamani kuliko kuona vitu vya kawaida. Vivyo hivyo, ingawa
kwa maumbile yake akili ni bora kuliko utashi, hapa duniani kumpenda Mungu ni
bora kuliko kumjua. Basi, ukamilifu unapatikana hasa katika kumpenda, hivi
kwamba mtakatifu ambaye hana elimu lakini ana upendo mkubwa kwa Mungu kwa
hakika ni mkamilifu kuliko mwanateolojia mkuu mwenye upendo mdogo. Jambo hilo,
ambalo Wakristo wote wanalielewa kwa urahisi, tukilifikiria kwa makini
linaonekana ukweli wa thamani unaoweza kuthibitishwa na madondoo mengi ya
Biblia na ya walimu wa Kiroho.
Huo
ubora wa upendo hapa duniani unatokana na kwamba “kazi ya akili yetu
inafanyika kwa kujichorea ukweli
uliojulikana, kumbe utashi wetu unavutwa
na upendo kukiendea kilichopendwa jinsi kilivyo. Alivyosema mwanafalsafa,
wema ulio lengo la utashi umo ndani ya vitu, kumbe ukweli umo hasa katika roho
yetu” (mt. Thoma wa Akwino). Kwa hiyo tunapomjua
Mungu, kwa namna fulani tunambana ndani ya mipaka ya mawazo yetu finyu ili
tujichoree alivyo; kumbe tunapompenda, sisi ndio tunaovutwa naye na kuinuliwa
kwake jinsi alivyo kweli. Basi, duniani na toharani upendo kwa Mungu ni
bora kuliko kumjua; unahitaji kumjua kwanza, lakini unapita ujuzi huo.
Tena
tokea hapa duniani upendo wetu unamfikia
Mungu na kuambatana naye moja kwa moja: “Ujuzi wetu unainuka kwa Mungu
kutoka kwa viumbe, kumbe upendo wetu kutoka kwa Mungu unawashukia viumbe” (mt.
Thoma wa Akwino).
Hatimaye,
sisi tunapenda ndani ya Mungu hata yale
tusiyoyajua, kwa sababu tuna hakika ya kuwa yeye ndiye wema wenyewe. Kwa
maana hiyo tunaweza kumpenda Mungu
kuliko tunavyomfahamu; tena ndani mwake tunapenda zaidi yale yaliyofichika,
kwa kuwa tunaamini ndiyo maisha yake ya dhati yanayopita uwezo wowote wa kujua.
Basi, hapa duniani upendo kwa Mungu unashinda ujuzi unaomhusu. Hilo ni ajabu
linalotuonyesha ukuu wa upendo juu ya imani na tumaini, juu ya ujuzi wowote
tunaoweza kuwa nao duniani, na hata juu ya tendo la kuzama katika sala, kwa
kuwa hata hilo halimpati bado Mungu jinsi alivyo, na utamu ulilonalo unatokana
na upendo unaoliongoza.
Ndiyo
sababu upendo ni kifungo cha ukamilifu: hakuna adili linalotuunganisha na
Mungu kwa undani kuliko hili, tena maadili mengine yote yanaongozwa na
kuhuishwa na kulengeshwa na upendo kwa Mungu anayependwa kuliko yote.
Tunapaswa
kukariri pamoja na mapokeo yote ya Kanisa kwamba ukamilifu wa Kikristo umo
hasa katika upendo wa vitendo ambao
unatuunganisha kweli na Mungu katika ukavu kama katika faraja, na kuzaa
kila aina ya vitendo vyema. Kwa usahihi zaidi ukamilifu haumo hasa katika
adili lenyewe la upendo, bali katika utekelezaji wake ambao katika
waliokamilika ni wa kudumu. Kwa sababu lengo la adili ni kutekelezwa, na
ukamilifu umo katika muungano wa kudumu na Mungu. Kumbe Watulivu walikataa
utendaji wowote ili wamuachie Mungu tu kutenda; hali yao ya kutotenda ilikuwa
ya kujitakia kwa kujizuia, si ya kujaliwa: ilikuwa kama kusinzia tu! Hivyo
walifuta juhudi na kupotosha hali za juu za kujaliwa. Kinyume chao, ni wale
wanaodhani ukamilifu umo katika kuwasaidia watu, wakisahau kuwa upendo kwa
Mungu ni wa juu kuliko ule kwa jirani ambao ni ishara na tunda lake tu. Hivyo
wanapindua mpangilio wa upendo. Wengine tena, wanaozingatia zaidi maisha ya
Kiroho, wanazidisha matendo ya sala badala ya kulenga sala sahili ya kimapenzi
ambayo ni kama tendo moja tu linalodumu kwa muda fulani.
Basi
upendo unatakiwa kushika nafasi ya kwanza rohoni mwetu, juu kuliko hamu ya
ujuzi na ya maendeleo ya kibinadamu ya aina yoyote; hapo upendo wenyewe
utazidisha nguvu zetu kwa kumtumikia Mungu na jirani.
Mungu
tu anaweza kujipenda anavyostahili, kama vile mwenyewe tu anaweza kujifahamu
kikamilifu; lakini watakatifu wa mbinguni, ingawa hawampendi anavyostahili, wanampenda
kwa nguvu zao zote, kwa upendo wa kudumu moja kwa moja. Hiyo haiwezekani
hapa duniani, hasa kutokana na usingizi.
Ukamilifu
unaowezekana hapa duniani ni ule unaozuia
yale yote yanayopinga upendo wa Mungu (yaani dhambi ya mauti) na
yale yote yanayofanya upendo usimuelekee kikamilifu. Waadilifu wanaoanza
maisha ya Kiroho na wale wanaoendelea wanalenga huo muungano na Mungu ambao ni
maalumu wa waliokamilika. Kwao ukamilifu wa upendo unazuia
sio tu dhambi ya mauti na dhambi nyepesi za makusudi, bali pia kasoro za hiari, k.mf. juhudi chache katika kumtumikia Mungu, na mazoea
ya kutenda kwa namna pungufu (kulingana na talanta zao) na
ya kupokea sakramenti pasipo utashi kutamani kweli. Upendo wa
waliokamilika kwa jirani unaenea si
kwa wote jumla tu, bali ikipatikana nafasi kwa kila mmoja wa wale ambao wana
fungamano lolote nao: sio kwa marafiki tu, bali kwa wengine wowote na hata kwa
maadui. Tena ndani mwao upendo huo wa kidugu una
nguvu hata ya kujitolea mali na uhai kwa ajili ya watu, kwa kuwa Bwana
ametuambia, “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yoh.
15:12). Ndiyo sababu mt. Paulo aliandika: “Nami kwa furaha nyingi
nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu” (2Kor. 12:15).
Ili
tufikie hatua hiyo vinahitajika: kazi kubwa juu ya nafsi zetu, mapigano halisi,
moyo wa kujikana na kujikatalia hivi kwamba mapendo yetu yaache kuteremka
kuelekea vitu vya dunia au ubinafsi, na badala yake yazidi kuinuka kwa Mungu
kwa usafi na nguvu. Maisha ya roho
yakiacha kushuka, yanapanda juu kwa Mungu. Hapa duniani roho haiwezi
kubaki pale ilipo; sheria yake, kama ile ya moto, ni kupanda, si kushuka.
Hapa
duniani upendo wa waliokamilika, ingawa si wa kudumu moja kwa moja kama ule wa
mbinguni, unatenda karibu mfululizo na kwa namna ya ajabu: “Upendo ni jambo
kubwa sana; ni jema kushinda mema yote. Upendo peke yake hugeuza mazito kuwa
mepesi, hubeba magumu kwa urahisi… Upendo una hamu ya kupaa, hautaki kuzuiwa
na mambo ya chini… Upendo umetoka kwa Mungu, hauwezi kutulia isipokuwa kwa
Mungu peke yake mbali na viumbe vyote. Mwenye upendo huenda kama kuruka,
huenda mbio kwa furaha, yu huru, hazuiliki, hutoa yote kusudi apewe yote;
katika mambo yote yeye hupata yote, kwa sababu humtegemea yule aliye juu
kabisa, ndiye asili panapotokea mema yote… Mara nyingi hupendo haujui kiasi,
huchemka kupita kiasi chochote… Upendo hukesha unapolala, hausinzii usingizi;
unapochoka haupumziki… Kama moto unaoteketea, kama mwenge unaowaka huruka
juu, hupenya kila mahali” (Kumfuasa Yesu Kristo III,5:3-5).
Hayo
ndiyo maisha ya watakatifu. Ndiyo wito wetu, kwa kuwa tunaitwa kuishi mbinguni,
ambapo wapo watakatifu tu. Ili tufike huko tunapaswa kutakasa kila tendo la
siku zetu, tukikumbuka kwamba juu ya mfululizo wa matukio ya kila siku (ya
kupendeza na ya kuchukiza, yaliyotarajiwa na yasiyotarajiwa) kuna mfululizo sambamba wa neema za msaada tunazojaliwa dakika baada ya
dakika ili tufaidi upeo matukio hayo. Hapo tutayaona sio tu upande wa hisi au
wa akili iliyopotoshwa na umimi, bali upande wa roho kwa imani. Hapo matukio
hayo yatakuwa kama mafundisho ya mambo ya Bwana, utekelezaji wa mafundisho ya
Injili, na polepole kati yake na sisi yataanza maongezi ambayo karibu hayana
kikomo: ndiyo maisha halisi ya Kiroho na kama mwanzo wa uzima wa milele.
Ukamilifu
wa Kikristo umo hasa katika upendo unaotuunganisha na Mungu. Lakini baadhi ya
wanateolojia waliwahi kujiuliza kama ukamilifu huo unadai upendo mkubwa au
unaweza kupatikana pasipo kiwango kikubwa cha adili hilo. Jibu la hakika ni
kwamba, kama vile utu uzima unadai nguvu za mwili nyingi kuliko za mtoto (ingawa
kwa nadra watoto wenye afya wana nguvu kuliko watu wazima kadhaa), hata hali
ya waliokamilika inadai upendo mkubwa kuliko ule wa wanaoanza (ingawa
watakatifu kadhaa, mwanzoni mwa maisha ya Kiroho, wana upendo mkubwa kuliko
baadhi ya wazee waliokamilika).
Fundisho
hilo lina msingi katika mahubiri ya Mwokozi, hasa aliposema juu ya heri
zinazofafanua ukuu wa ukamilifu wa Kikristo ambao Yesu anawaitia wote. Hotuba
ya mlimani ni muhtasari wa mafundisho aliyoyatoa ili kutimiliza sheria ya Musa
na kusahihisha ufafanuzi wake usiofaa. Heri nane zilizotangazwa mwanzoni mwa
hotuba hiyo zinajumlisha vizuri ajabu kipeo cha maisha ya Kikristo zikionyesha
ukuu wake wote.
Neno
la kwanza la Yesu ni kuahidi heri na kuelekeza njia za kuzipata. Alianza na
heri kwa sababu kila mtu kwa maumbile yake anaitamani: ndiyo lengo ambalo wote,
watake wasitake, wanalitafuta katika yote. Lakini mara nyingi wanatafuta heri
mahali isipokuwepo, ambapo watakuta tu mahangaiko na unyonge. Tumsikilize
Bwana ambaye anatuambia heri halisi ya kudumu na lengo
la maisha yetu viko wapi, tena anatupatia njia za kuvipata.
Lengo
linaelekezwa na kila neno la heri, na kwa majina mbalimbali ni ile heri ya
milele ambayo waadilifu wanaweza kuanza kuionja hapa duniani: ni ufalme wa
Mungu, nchi ya ahadi, faraja kamili, utimilifu wa hamu zote zilizo halali na
takatifu, rehema kuu, kumuona Mungu Baba yetu. Njia zinakwenda kinyume cha
maelekezo ya dhana za ulimwengu, kwa kuwa lengo lenyewe ni tofauti mno.
Mpangilio
wa heri nane unaanzia chini kwenda juu (kinyume
na sala ya Baba Yetu ambayo kutoka kuzingatia utukufu wa Mungu inateremkia
mahitaji yetu). Heri tatu za kwanza ni zile zinazopatikana
katika kukwepa dhambi na kukombolewa: katika ufukara uliopokewa kwa upendo
wa Mungu, katika upole na katika machozi ya majuto. Heri mbili zinazofuata ni
zile za maisha ya utendaji ya
Kikristo: zinahusu kiu ya haki na utekelezaji wa huruma kwa jirani. Halafu
zinakuja zile za kuzama katika mafumbo
ya Mungu: usafi wa moyo unaotuandaa kumuona na amani inayotokana na hekima
ya kweli. Heri ya mwisho na bora kuliko zote ni ile inayoziunganisha
zilizotangulia hata wakati wa kudhulumiwa
kwa ajili ya haki.
Hizo
zinahusu hatua ya utakaso, ambayo ni maalumu kwa wanaoanza.
Wakati
ulimwengu unasema kuwa heri inapatikana katika wingi wa mali, utajiri na
heshima, Bwana amesema waziwazi, kwa hakika tulivu ya ukweli mkuu, “Heri
walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Math. 5:3).
Kila heri ina viwango mbalimbali:
heri walio fukara bila ya kunung’unika, kwa uvumilivu, bila ya wivu, hata
wakikosa chakula, na ambao wanafanya kazi wakimtegemea Mungu tu. Heri
waliobahatika zaidi, lakini hawana roho ya utajiri, fahari, kiburi, wala
hawashikamani na mali. Heri zaidi walioacha vyote ili kumfuata Yesu,
waliojifanya fukara kwa hiari na kuishi kweli wito huo; hao watapata mara mia
hapa duniani halafu uzima wa milele. Fukara hao ni wale ambao, kwa kuvuviwa kipaji cha uchaji, wanafuata njia ambayo ni nyembamba mwanzoni,
lakini baadaye inakuwa barabara kuu ya mbinguni, ambapo roho inapanuka zaidi
na zaidi, wakati njia pana za ulimwengu zinaelekea maangamizi: “Ole wenu
ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa” (Lk. 6:25). Kinyume chake,
ufukara wenye heri unatufungulia ufalme wa Mungu, ulio bora kuliko mali yoyote,
yanavyoonyesha maisha ya mt. Fransisko wa Asizi. Heri wanyenyekevu wa moyo,
wasiojitwalia mema ya kimwili wala ya Kiroho, wala heshima wala upendo, na
ambao hawatafuti chochote isipokuwa ufalme wa Mungu.
Wakati
tamaa ya utajiri inawatenga watu na kusababisha ugomvi, mashtaka, kesi,
dhuluma na hata vita kati ya mataifa, Yesu amesema, “Heri
wenye upole, maana hao watairithi nchi” (Math. 5:5). Heri
wasiowakasirikia ndugu zao, wasiotafuta kulipa kisasi wala kuwatawala wengine,
wasiohukumu bila ya msingi, wasiomuona jirani kama adui wa kushindana naye,
bali kama ndugu wa kusaidiwa, mtoto wa Baba yuleyule wa mbinguni. Kipaji cha ibada ndicho kinachotutia upole huo kwa mapendo ya kitoto
hasa kwa Mungu, Baba yetu sote. Walio wapole hawashikamani mno na mtazamo wao
wala hawaoni haja ya kuapa kwa chochote kile. Ili tuwe wapole hivyo, hata kwa
wanaotutendea kwa ukali, tunahitaji kuungana na Yesu aliyesema, “Mjifunze
kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Math. 11:29). Yeye
hakuvunja “mwanzi uliopondeka” wala kuzima “utambi utokao moshi”
(Math. 12:20) hata alifananishwa na “mwanakondoo apelekwaye machinjoni”
asifunue “kinywa chake” (Isa. 53:7; Mdo. 8:32). Upole huo si ule
usiomchukiza yeyote kwa sababu unaogopa, bali ni adili linalotegemea upendo
mkubwa kwa Mungu na kwa jirani: unazidisha thamani ya huduma unayotoa, unaweza
kusema lolote na kufanya mashauri yake yapokewe, na hata lawama kwa kuwa
anayeambiwa anatambua kuwa vinatokana na upendo mkubwa. Heri walio wapole,
maana watairithi nchi halisi ya ahadi; na tangu sasa wanajipatia kitakatifu
mioyo ya wale wanaojiaminisha kwao.
Wakati
ulimwengu unasema furaha imo katika anasa, Yesu amesema, “Heri
wenye huzuni, maana hao watafarijika” (Math. 5:4). Tajiri alijibiwa
vilevile: “Wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro
vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa”
(Lk. 16:25). Heri yao wale ambao, kama Lazaro, wanateseka kwa subira, bila ya
kufarijiwa na watu; ila Mungu anaona machozi yao. Wenye heri zaidi wanaolia
juu ya dhambi zao, ambao kwa kipaji cha
elimu wanang’amua kwamba dhambi ndiyo baya kubwa kuliko yote, na kwa
kulia machozi wanajipatia msamaha. Hatimaye wana heri zaidi wanaolia kwa
upendo wakizingatia huruma na hisani visivyo na mipaka vya mchungaji mwema
aliyejitoa sadaka kwa kondoo zake. Hao wanapokea farajia isiyo na kifani
kuanzia hapa duniani.
Furaha
nyingine takatifu zimeandaliwa kwa mwadilifu ambaye, kisha kuopolewa katika
maovu, anajitahidi kutenda mema kwa moyo wote.
Mtu
mwenye shughuli nyingi anayetawaliwa na kiburi anamuita mwenye heri yule
anayeishi na kutenda anavyotaka, asiyekaa chini ya wengine bali anawashinda.
Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye njaa
na kiu ya haki, maana hao watashibishwa” (Math. 5:6). Maana pana ya hilo
neno “haki” ni kumpatia Mungu yale anayostahili; hapo kwa upendo wake hata
kiumbe anapatiwa anayostahili: kama malipo Mungu anajitoa kwetu. Ndio
utaratibu kamili, katika utiifu kamili, ambao unaongozwa na upendo unaopanua
moyo. Wenye heri wanaotamani haki hiyo hadi kuwa na njaa na kiu nayo. Kwa
namna fulani hao watashibishwa kuanzia hapa duniani, kwa kugeuka waadilifu na
watakatifu zaidi. Kiu hiyo ina heri kweli: “Mtu akiona kiu, na aje kwangu
anywe… mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” (Yoh. 7:37-38). Lakini
ili kudumisha kiu hiyo hata hisi zikiwa zimepoa Kiroho, au katikati ya
upinzani, vizuio, kukata tamaa, ni lazima tupokee kwa mikono miwili kipaji
cha nguvu, ambacho kinatuzuia tusishindwe wala tusikate tamaa, na
kinatutia moyo katika matatizo. “Bwana anataka tuitamani haki hiyo hivi
kwamba tusishibe kamwe hapa duniani, kama vile mwenye uroho asivyoshiba
kamwe… Watashiba watakapomuona Mungu milele… na tangu sasa katika mema ya
Kiroho… Watu wakiwa katika dhambi, hawasikii njaa ya Kiroho, lakini
wanapoacha dhambi hapo wanaisikia” (mt. Thoma wa Akwino).
Lakini
njaa na kiu za haki hazitakiwi kuendana na ari chungu kuhusu wakosefu: “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math. 5:7).
Katika maisha yetu, kama vile kwa Mungu, haki inapaswa kuungana daima na
huruma. Hatuwezi kuwa wakamilifu tusipomsaidia mwenye uchungu au ugonjwa kama
alivyofanya Msamaria mwema. Bwana atawalipa wanaojitolea bilauri ya maji kwa
upendo wake, wanaokaribisha mezani pao fukara, walemavu na vipofu. Mkristo
anapaswa kufurahia zaidi “kutoa kuliko kupokea” (Mdo. 20:35), tena
kusamehe (kwa Kilatini “kutoa zaidi”) waliomchukiza, kusahau dharau na
kupatana na nduguye kabla hajatolea altareni sadaka yake. Kipaji cha shauri kinatuelekeza kwenye huruma, na kutufanya tutambue
mateso ya wenzetu pamoja na dawa yake, yaani pengine neno la kuwainua na
kuwafariji.
Kama
utendaji wetu utafuata mara nyingi maadili hayo mawili ya haki na huruma,
pamoja na vipaji vinavyohusiana nayo, roho zetu zitajaa furaha takatifu tokea
hapa duniani na kuwa tayari kuingizwa katika mafumbo ya Mungu.
Baadhi
ya wanafalsafa walidhani kuwa heri imo katika kujua ukweli, hasa ukweli mkuu,
lakini hawakujali usafi wa moyo; kwa hiyo katika mambo kadhaa maisha yao
yalikuwa yakipingana na mafundisho yao. Kumbe Yesu amesema, “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu” (Math. 5:8).
Hakusema wana heri walio na akili sana pamoja na muda na njia ya kuistawisha,
bali walio na moyo safi, hata kama kimaumbile akili yao ni ndogo kuliko ya
wengine. Wakiwa na moyo safi watamuona Mungu: ni kama maji safi ya ziwa ambamo
uangavu wa anga unarudishwa, au kama kioo cha Kiroho ambamo sura ya Mungu
inaonekana. Lakini usafi halisi wa moyo unadai kujifisha kwa bidii: “Jicho
lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe… Na mkono wako wa
kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe” (Math. 5:29-30). Tunapaswa
kuangalia hasa tuwe na nia njema: si
kutoa sadaka mbele ya watu ili kuonekana nao, wala kusali ili kusifiwa nao,
bali kutafuta tu tumpendeze Baba wa mbinguni “aonaye sirini” (Math.
6:4,6,18). Hapo tu yatatimia maneno ya Mwalimu: “Taa ya mwili ni jicho; basi
jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru” (Math. 6:22). Tokea
hapa duniani Mkristo atamuona Mungu kwa namna fulani katika jirani yake, hata
katika watu kadhaa ambao mwanzoni aliwaona wanampinga; atamuona katika
Maandiko, katika maisha ya Kanisa, katika nafasi mbalimbali za maisha yake
mwenyewe, hata katika majaribu, ambapo atajifunza maongozi ya Mungu. Ndipo
sala ya kumiminiwa inapopatikana kwa msaada wa kipaji
cha akili, tunapojiandaa kumuona Mungu uso kwa uso, wema wake, uzuri wake
usiopimika; hapo hamu zetu zote zitatimia, nasi tutakuwa kama tumelewa na mto
wa vitamu vya Kiroho.
Tangu
hapa duniani huko kuzama ndani ya Mungu kunazaa matunda; kunaleta amani
angavu, inavyotangaza heri ya saba: “Heri
wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Math. 5:9). Heri hiyo
inahusiana na kipaji cha hekima kinachotufanya
tuonje mafumbo ya milele, na kuona kwa namna fulani mambo yote ndani ya Mungu.
Miangaza ya Roho Mtakatifu, ambayo kipaji hicho kinatusaidia kuipokea kwa
mikono miwili, inatuonyesha polepole utaratibu mzuri ajabu wa maongozi ya
Mungu, pengine palepale – na hasa palepale – tulipopatwa kwanza na mshtuko
mkubwa katika matukio machungu yasiyotarajiwa ambayo Mungu aliyaruhusu kwa
manufaa makubwa zaidi. Haiwezekani kung’amua hivyo anavyoongoza maisha yetu
bila ya kufaidi amani kubwa ambayo ni utulivu wa utaratibu. Ili tusifadhaishwe
na matukio ya namna hiyo, bali tuyapokee yote mikononi mwa Mungu kama njia ya
kumuendea, ni lazima kujiachilia kwa Roho Mtakatifu, anayetaka kutujalia hatua
kwa hatua kutazama mambo ya Kimungu, ambako ni sharti la kuungana naye. Ndiyo
sababu tumejaliwa kipaji cha hekima. Miangaza yake inatupatia amani angavu,
sio tu kwa ajili yetu, bali kwa jirani pia; inatufanya wenye amani; inatusaidia kuwapa amani watu wasiotulia, kuwapenda
maadui, kusema maneno ya upatanisho yanayomaliza ugomvi. Hiyo amani ambayo
ulimwengu hauwezi kuitoa, ndiyo ishara ya watoto
halisi wa Mungu ambao hawaachi kumfikiria Baba yao wa mbinguni. Heri hizo
ni mwanzo fulani wa heri ijayo.
Hatimaye,
katika heri ya nane, Bwana ameonyesha kwamba yale yote aliyoyasema
yanathibitishwa hasa na majaribu yaliyovumiliwa kwa upendo: “Heri
wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Math.
5:10). Hasa ndiyo majaribu ya mwisho yaliyo masharti ya utakatifu. Neno la
kushangaza kama hilo halijasikika: halituahidii tu heri milele, bali pia wakati
wa uchungu na dhuluma. Ni heri isiyo ya kimaumbile hata kidogo, haieleweki
kweli isipokuwa na wale walioangazwa na Mungu. Lakini ndani yake kuna ngazi
nyingi, kuanzia ile ya Mkristo anayeanza kuteseka kwa kuwa ametenda mema,
ametii, ametoa mfano mzuri, hadi ile ya mfiadini. Heri hiyo inamhusu
aliyeongoka anayepingwa tu katika mazingira yao; pia mtume ambaye kazi yake
inazuiwa na walewale anaotaka waokoke, wasiokubali kumsamehe kwa kuwaeleza
wazi kweli za Injili. Pengine makabila mazima yanapaswa kustahimili dhuluma za
namna hiyo. Heri hiyo ni kamili kuliko zote kwa kuwa ni ya wale wanaofanana
zaidi na Yesu aliyesulubiwa kwa ajili yetu. Kudumu wanyenyekevu, wapole na
wenye huruma wakati wa dhuluma, hata kwa watesi wenyewe, na sio tu kuendelea
kuwa na amani, bali kuwashirikisha wengine pia, huo ndio ukamilifu wa
Kikristo. Si watakatifu wote walifia dini, lakini kwa viwango tofauti wote walidhulumiwa
kwa ajili ya haki na kujua walau kidogo ule ushahidi wa moyoni uliomfanya
Maria Mama wa huzuni. Yesu alisisitiza tuzo waliloahidiwa watu hao: “Heri
ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa
ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa
mbinguni” (Math. 5:11-12). Kutokana na maneno hayo mt. Inyasi wa Antiokia na
wengineo walitamani kufia dini. Ndiyo sababu wakawa “chumvi ya dunia”,
“nuru ya ulimwengu” (Math. 5:13-14), na nyumba yao, iliyojengwa kwenye
mwamba, sio katika mchanga, ilistahimili dhoruba zote isianguke.
Heri
hizo ni matendo bora ya maadili yaliyokamilishwa na vipaji, hivyo zinapita
juhudi zetu. Kwa maneno mengine, ukamilifu wa Kikristo unategemea mafumbo, ni
mwanzo wa uzima wa milele, ambapo Mkristo atakuwa mkamilifu kama Baba,
akimuona na kumpenda kama mwenyewe anavyojiona na kujipenda.
Mt. Teresa aliandika, “Vitabu kadhaa vinasema tusijali mabaya yanayosemwa juu yetu, bali tuyafurahie kuliko maneno ya sifa, tusijali sana heshima tunayopewa, tusishikamane na ukoo… na sijui mambo mangapi ya namna hiyo… Nionavyo mimi, hayo ni zawadi za Mungu tu, ni mema yanayopita maumbile”, yaani yanapita uwezo wa juhudi zetu katika kutekeleza maadili; ni matunda yanayozaliwa na usikivu mkubwa kwa Roho Mtakatifu. Mwenyewe aliandika pia, “Tukipenda heshima na tunu za kidunia, hata tukifanya sala, au afadhali niseme tukitafakari miaka na miaka, hatutaendelea kweli kamwe. Kumbe sala kamili inatukomboa kutoka kasoro hizo”. Maana yake pasipo sala ya kumiminiwa hatutaweza kamwe kuufikia ukamilifu.
Ndivyo
ilivyoandikwa katika Kumfuasa Yesu Kristo: “Utakapofaulu kujidharau kabisa,
uwe na hakika kwamba umepata kuonja amani yote inayowezekana hapa duniani”
(III,25:3). Kwa sababu hiyohiyo, mwanafunzi anaomba kumiminiwa
sala: “Mungu wangu, nahitaji sana neema kubwa zaidi, yakinipasa kufika
katika hali njema, hata nisiweze kuzuiwa tena na mtu yeyote wala na kiumbe
chochote… Mtu mmoja aliyekuwa na pupa ya kuruka hivi afike kwako, alisema,
Nani atanipa mabawa kama ndege nipate kuruka na kufika mustarehe? Mtu
asiyevunja vifungo vinavyomfunga pamoja na viumbe, hatapata nafasi ya
kumfikiri Mungu na mambo yake. Ndiyo maana hatuoni watu wengi wa kuzama ndani
ya Mungu, kwa kuwa wenye kujitenga kabisa na mambo mapotevu ya dunia au hata
na viumbe vyote huwa wachache. Kufanya hivi hutaka neema kubwa sana, yenye
kuinua roho na kuivuta hata ipae juu ya hali yake. Lakini kama mtu hapandi
vile rohoni mwake kwa kujiambua na viumbe vyote akiambatana na Mungu tu, yote
ayajuayo na yote awezayo hayana maana” (III,31:1-2). Ndio ustawi kamili wa
muundo wa Kiroho, yaani neema ya maadili na vipaji, nao unaonyeshwa kwetu
katika heri nane si kinadharia tu, bali katika utekelezaji wake.
Ili
tukamilishe tuliyoyasema kuhusu ukuu wa ukamilifu wa Kikristo, tunapaswa kuona
kama wenyewe unadai upendo mkubwa pamoja na ushujaa katika maadili yote.
Kanisa
linafundisha hivyo kwa kuwa ukamilifu huo unapatikana tu baada ya utekelezaji
wa muda mrefu wa maadili ya kumiminiwa na ya kujipatia; kwa utekelezaji
huo maadili hayo yanastawi zaidi na zaidi. Na ikiwa mwanzoni “upendo wa
kiwango cha chini una uwezo wa
kushinda vishawishi vyote” (mt. Thoma wa Akwino), baadaye unavishinda kweli
na kuzidi kuwa na nguvu. Basi, haiwezekani kumfikiria Mkristo
aliyekamilika, aliye juu kuliko wanaoanza na wanaoendelea, asiye na upendo
mkubwa, ingawa kupima kiwango cha upendo kinachotakiwa ni kazi ya Mungu tu.
Mfano wake ni utu uzima, ambao kwa kawaida unadai nguvu za mwili nyingi kuliko zile za ubalehe, lakini bila ya kipimo
maalumu.
Fundisho
hilo msingi wake mwingine ni kwamba upendo
unastawi kwa nguvu kuliko kwa uenezi. Viwango
vitatu vya upendo vinavyowafaa wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika, ni
viwango vya nguvu ya adili hilo, ambalo linazidi kuzuia dhambi nyepesi za
makusudi na kututenganisha na malimwengu ili tuambatane na Mungu. Hata hivyo
mtu mmoja anakwepa dhambi hizo kuliko mwingine mwenye kiwango kilekile cha
upendo, kwa sababu kwa wakati huo ana juhudi nyingi zaidi au halazimiki
kupambana zaidi na tabia yake, uchovu na upinzani. Mt. Teresa wa Yesu
alipokuwa katika nafasi zisizotazamiwa nje ya monasteri ilimtokea kutenda
dhambi nyepesi nyingi zaidi, lakini pia kujipatia stahili nyingi zaidi
kutokana na majaribu aliyoyashinda. Ni kama katika mtu kupanda mlima mrefu,
inamtokea kuanguka kuliko mahali tambarare, lakini ana stahili ya kutenda kazi
ngumu kwa kupanda.
Basi,
ukamilifu unadai upendo mkubwa unaopatikana tu kwa kushinda kwanza vishawishi
vingi na kujipatia stahili nyingi. Fundisho hilo limethibitishwa na mt. Yohane
wa Msalaba: “Kuna watu wanaoridhika na aina yoyote ya kukusanya mawazo na ya
kuongoka; wengine wanaishia katika kutekeleza maadili kwa ukamilifu mkubwa au
mdogo, na kuwa waaminifu katika sala na kujinyima. Wanachokosa ni kujishusha,
kuwa fukara, au kujikana na kuwa safi Kiroho… Kinyume chake wanakwepa
msalaba ambao ungewalinganisha na Bwana wetu Yesu Kristo. Wanajifanya
lengo ndani ya Mungu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha upendo… Ningependa
kuweza kuwathibitishia watu wote wa Kiroho ukweli huu: kwamba njia ya Mungu
haimo katika kuzidisha mawazo, mbinu na maonjo, ingawa kwa namna fulani
wanaoanza wanayahitaji hayo. Lakini jambo moja tu ni la lazima kabisa, yaani
kuweza kabisa kujikana kwa ndani na kwa nje, kujitoa mhanga kwa Yesu Kristo
kama sadaka kamili ya kuteketezwa. Katika zoezi hilo tu tutayakuta mengine
yote na mengi zaidi tena. Kumbe, tukipuuzia zoezi hilo, ambalo ni muhtasari na
mzizi wa maadili, tutakuta tu vitu visivyo muhimu, na maendeleo yatakwama,
hata tukiwa na mawazo na neema za kimalaika… Mtu wa Kiroho akifaulu
kujiangamiza, yaani kutekeleza unyenyekevu kamili, hapo muungano wake na Mungu
utatimia, nao ndio hali bora tena kuu tunayoweza kuifikia katika maisha
haya”. Hali hiyo inadai upendo mkubwa, pamoja na unyenyekevu kamili: “Ukamilifu
umo katika kumpenda kikamilifu Mungu na kujidharau”.
Mafundisho
hayo yanalingana na yale ya mt. Thoma wa Akwino alipoeleza ukamilifu kuwa ni
“hali ya wale ambao wanalenga hasa kuambatana na Mungu na kumfurahia, na
ambao wanatamani kufa ili kuishi na Kristo”, wakikabili magumu kwa utukufu
wa Mungu na wokovu wa watu. Basi, pasipo juhudi kubwa haiwezekani kufikia
upendo mkubwa, hata kwa miaka ya kukomunika kila siku na kutenda mema yenye
stahili pungufu. Kwa njia hizo tunaweza kujidumisha katika neema ya utakaso au
kuinuka mapema baada ya kutenda dhambi ya mauti, lakini hatutafikia kamwe
kiwango kikubwa cha upendo.
Ikiwa
upendo kwa nchi yetu unatudai ushujaa ikipatwa na hatari, bila ya shaka
ukamilifu wa Kikristo unadai ushujaa katika maadili, walau upande wa nia;
yaani Mkristo anapaswa kuwa tayari, kwa msaada wa Mungu, kuuawa kwa ajili ya
imani, kama atajikuta katika nafasi ya kulazimika kuchagua kati ya kuikana na
kuteswa. Ushujaa huo wa lazima kwa wokovu unadaiwa zaidi na ukamilifu. Mkristo
akiwa mwaminifu katika wajibu wowote wa kila siku, awe na hakika kuwa katika
nafasi ngumu zaidi Bwana atamsaidia kulingana na ukuu wa wajibu wa dharura:
“Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa
pia” (Lk. 16:10). “Msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu
au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ileile yawapasayo
kuyasema” (Lk. 12:11-12). Tunapaswa pia kuwapenda maadui wetu na kuwasaidia
wakiwa na shida kubwa.
Vipaji
vya Roho Mtakatifu ni vya lazima kwa wokovu ili tupokee kwa dhati na kwa
mikono miwili uvuvio wake wa pekee pale ambapo maadili hayatoshi, kutokana na
nafasi kuwa ngumu zaidi. Ikiwa kila Mkristo anapaswa kukubali kifodini kuliko
kuikana imani, padri aliyewekwa wakfu na Mungu awachunge watu anapaswa
kuhatarisha uhai wake ili kuwaletea sakramenti wakiwa na shida kubwa nazo
(k.mf. kwenda kuwaungamisha wenye tauni). Zaidi tena askofu, katika nafasi
kadhaa anapaswa kutoa uhai wake kwa ajili ya kundi lake. Lakini kuwa tayari
rohoni kutekeleza maadili kwa ushujaa huo ni tofauti na kuwa
nayo kwa kiwango cha ushujaa.
Katika
sura ijayo tutaona kuwa ukamilifu unadai Mungu atutakase hisi na roho ili
kufuta kasoro za wanaoanza na za wanaoendelea. Mt. Yohane wa Msalaba
alifafanua matakaso hayo yanavyowatokea wanasala wanaoitiwa ukamilifu mkuu kwa
njia ya mkato; lakini mambo ya namna hiyo yanawatokea wengine pia ambao kwao
matakaso hayo ya ndani yanaendana na huzuni na shida za utume. Katika majaribu
hayo si kwa nadra mtu anatakiwa kushinda kishujaa vishawishi dhidi ya usafi wa
moyo na subira, halafu dhidi ya imani, tumaini na upendo. Upande huo ukamilifu unadai ushujaa fulani katika maadili, ambao baadaye
unaweza na kutakiwa uongezeke.
Hatimaye,
upendo wa Kikristo, kwa kuwa
unalenga kutulinganisha na Mwokozi aliyesulubiwa kwa ajili yetu, unatakiwa kulenga ushujaa katika maadili. Hiyo inatokana na yale
tuliyoyasema kwanza: tendo la kishujaa linalompasa Mkristo yeyote, k.mf. la
kukubali kuuawa kuliko kuikana imani, si chini ya lengo la upendo, yaani kumpenda Mungu kuliko yote. Kwa maumbile
yake, upendo huo unampenda Mungu kuliko uhai wa mwili, kwa hiyo unapaswa kuwa
tayari kutoa uhai wake unavyodaiwa na nafasi kadhaa. “Upendo wa Mungu
unafanya tutende bila ya kikomo na kuvumilia bila ya kuchoka” (mt. Bernardo)
hasa katika tabu za ndani na za nje ambazo watumishi wa Mungu wanapaswa
kustahimili kwa utakaso wao na kwa kuchangia wokovu wa watu kwa mfano wa
Mwokozi.
Mtu
anaweza akapinga mafundisho hayo akisema eti, yangekuwa kweli Wakristo
wanaofikia ushujaa wangekuwa wengi zaidi, kumbe ushujaa ni adimu. Mt. Thoma wa
Akwino alijibu hoja ya namna hiyo kuhusu idadi ya wateule: “Jema
linalolingana na hali ya kawaida ya maumbile ya kibinadamu kwa kawaida
linafikiwa; lakini si hivyo kuhusu jema linalopita hiyo hali ya kawaida”. Ni
adimu kudumu maisha yote katika neema ya utakaso, bila ya kutenda dhambi ya
mauti baada ya ubatizo. Hata hivyo kwa mfumo wake neema ya utakaso inalenga
uzima wa milele, kwa hiyo idumu milele bila ya kuangamizwa kamwe na dhambi
ya mauti. Ila tumepokea hazina hiyo katika chungu ya udongo, hivyo tamaa na
kiburi vinaweza kufanya tuipoteze. Wengi wanaishi kijuujuu tu, wakifuata hisi,
na wachache tu wanafuata akili nyofu; hata hivyo kwa maumbile yake roho ya
binadamu ina akili, nayo neema inatakiwa kuifanya iishi Kimungu kweli. Vivyo
hivyo upendo ukiwa ni mbegu ya uzima wa milele, kwa mfumo wake unalenga
ushujaa ili kudumu katika uaminifu kwa Mungu.
Kuhusu
utakatifu mkubwa, huo unadhihirika hasa katika ulinganifu
wa maadili yote, hata yale yaliyo mbalimbali zaidi. Mmoja anaweza kuelekea
kimaumbile upande wa nguvu, lakini si wa upole; mwingine ni kinyume. Kwa namna
fulani maumbile yanaelekea daima upande mmoja, hivi kwamba yanahitaji
kukamilishwa na maadili mbalimbali. Muungano wa nguvu kubwa na upole kamili,
wa upendo motomoto kwa ukweli na haki pamoja na huruma kubwa kwa waliopotoka,
unathibitisha muungano wa dhati na Mungu, kwa kuwa yaliyogawanyika katika
ulimwengu huwa yameunganika katika ufalme wa Mungu, na hasa ndani mwake
mwenyewe. Utakatifu ni mfano mzuri wa muungano wa sifa mbalimbali za Mungu, wa
haki isiyo na mipaka na huruma isiyo na mipaka ndani ya ukuu wa Umungu.
Tumeshaona
kuwa ukamilifu wa Kikristo umo hasa katika upendo, unaotuunganisha na Mungu na
jirani kuliko adili lingine lolote. Tunatakiwa bado kusema unavyodai pia
matendo ya maadili mengine na ya vipaji vya Roho Mtakatifu. Hata katika swala
hilo watu walipotoka pande mbili. Watulivu waliyapuuzia mno maadili hayo na
kufuta utekelezaji wa kujinyima na wa kuwatendea mema majirani. Kinyume chao,
wengine walisisitiza matendo ya toba, ibada na huruma wasitambue vya kutosha
ukuu wa upendo wa Mungu, na hivyo wakazingatia juhudi zao na utume wa njenje
kuliko mafumbo.
Ukamilifu
wa Kikristo unadai matendo ya maadili
mengine yaliyo ya amri na ambayo yanatakiwa kuangazwa, kuhuishwa na
kustahilishwa na upendo. Tutaona kuwa amri kuu inatudai tukue zaidi na zaidi
katika maadili hayo kama vile katika upendo.
Kutokana
na yale tuliyokwishasema kuhusu muundo wa Kiroho, ukamilifu unadai maadili
yote ya kumiminiwa na ya kujipatia, halafu vipaji saba vinavyohusiana na
upendo hivi kwamba vinakuwa pamoja nao. Lakini kwa kawaida upendo wa
waliokamilika unapaswa kuwa mkubwa na
motomoto kuliko ule wa wanaoanza na wanaoendelea. Basi, ukamilifu unadai
utekelezaji wa maadili yote na wa vipaji saba pia. Mtu hawezi kuwa mkamilifu
bila ya kupenya mafumbo ya imani kwa kipaji cha akili, wala kuwa na kipaji cha
hekima kwa kiwango kinacholingana na upendo (ingawa kipaji hicho kinaelekea
sala hasa katika watakatifu kadhaa na utendaji zaidi katika wengine).
Upendo
ndio kiungo cha ukamilifu huo wa
maadili na vipaji, ambavyo kwa pamoja ni kama fungu la maua linalotolewa kwa
Mungu. Basi, ukamilifu umo hasa katika
upendo, ingawa unadai pia maadili mengine na vipaji saba. Vilevile na
binadamu ambaye mwili ni sehemu ya utu wake, ingawa utu umo hasa katika roho
inayomtofautisha na wanyama.
Neema
ya utakaso na upendo wa wanaoanza havitoshi kuunda ukamilifu, mpaka vikue hadi
kufikia hatua ya waliokamilika. Ili tuifikie tunahitaji kujikana,
kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu kwa njia ya vipaji saba, na kupokea
kwa mikono miwili misalaba au matakaso yanayokusudiwa kufisha ndani mwetu
umimi na kuhakikisha nafasi ya kwanza ishikwe moja kwa moja na upendo wa Mungu
wenye kuangaza na kuwaka zaidi na zaidi.
Tusisitize
tangu sasa jambo hilo kufuatana na yale yaliyosemwa na mt. Paulo: “Kwa ajili yake (Kristo) nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu
kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena
nionekane katika yeye… ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika
wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote
kuufikia ufufuo wa wafu. Si kwamba
nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo
ili nipate kulishika lile ambalo, kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu.
Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja
tu: nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo,
niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu, katika Kristo Yesu. Basi
sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo… Lakini, hapo tulipofika na tuenende
katika lilo hilo” (Fil. 3:8-16). Ndio ukamilifu wa Kikristo kweli, si wa kifalsafa
tu; nao tumependekezewa sisi sote tunaolishwa na Maandiko hayo hadi mwisho wa
dunia.
Watu
kadhaa walisema eti, mt. Thoma wa Akwino alizungumzia kidogo tu matakaso ya
Kiroho. Basi, msome alivyofafanua maneno hayo kwa Wafilipi kuhusu kushiriki
mateso ya Kristo walau kusudi tusipoteze misalaba yetu, tufanane naye na
kuwaokoa watu pamoja naye (maana ulimwengu umejaa misalaba tasa, kama ule wa
mwizi wa pili aliyesulubiwa pamoja na Yesu: njia ya kuifanya ilete faida ni
kuibeba kwa uvumilivu na upendo pamoja naye). Msome pia alivyofafanua maneno
ya Yesu kuhusu mzabibu wa kweli ambao Baba anausafishia
kila tawi lizaalo: “Ili waadilifu wanaozaa matunda wazae kwa wingi
zaidi, Mungu anapogolea ndani mwao yaliyo ya ziada; anawatakasa kwa kuwatumia
tabu na kuruhusu washambuliwe na vishawishi ambavyo katikati yake wazidishe
nguvu na juhudi. Hapa duniani hapana mtu
safi kiasi kwamba asihitaji kutakaswa zaidi”. Ndiyo matakaso ya Kimungu
yaliyokuja kuelezwa zaidi na mwalimu wa Kanisa aliyeyachimba kuliko wote,
yaani mt. Yohane wa Msalaba. Katika mafundisho yake tunapata pia mwanga mkubwa
ili kutofautisha hatua tatu za maisha ya Kiroho.
Sasa
tunapaswa kuona yale yanayohitajika ili tufikie kilele
cha ustawi wa kawaida wa upendo.
Tunaposema kilele tusisahau neno kawaida; vilevile tunaposema kawaida
tusisahau neno kilele. Mara nyingi mno tunaita “ya kawaida” yale ambayo
wengi wanayafikia kweli, bila ya kujiuliza vya kutosha juu ya yale ambayo wangetakiwa kuyafikia kama wangekuwa waaminifu. Haifai kutamka eti,
muungano wa karibu mfululizo na Mungu uko juu
kuliko kilele cha ustawi wa kawaida wa upendo, kwa sababu tu wengi
hawaufikii. Tusichanganye yanayotakiwa
kuwa na yale yaliyopo maishani,
la sivyo tutasema uaminifu halisi hauwezekani duniani, kwa kuwa walio wengi
wanafuata faida yao (k.mf. pesa na
anasa) kuliko uadilifu. Wengi
wanajiongoza kwa kufuata yale yasiyo
mabaya mno badala ya wajibu wao unaowadai
juhudi kubwa katika mazingira ambamo yote yanawaelekeza kudidimia; wanafuata
mkondo kadiri ya sera ya kujitahidi kidogo iwezekanavyo. Sio tu kwamba
wanayavumilia yasiyo mabaya mno, bali
wanayatenda na mara nyingi
wanayaunga mkono kwa mashauri yao ili wadumishe hali yao. Wanasiasa wengi
wanasema kuwa wanafanya hivyo ili kuepa mabaya makubwa zaidi ambayo wengine
wangeyafanya mahali pao kama wenyewe wangepotewa na wadhifa wao kwa
kutowapendeza watu. Hivyo, badala ya kuwasaidia kupanda
juu tena wanawasaidia kudidimia, wakijitahidi
tu kupunguza kasi ya anguko. Kuna kitu cha namna hiyo katika maisha ya Kiroho
pia.
Tunapaswa
kukumbuka kwamba sheria kuu ya
ustawi wa kawaida wa upendo ni tofauti na ile ya maumbile yetu yaliyoanguka.
Hata baada ya ubatizo hayo yanaendelea kuwa na madonda na hivyo yanatuelekeza
kudidimia, kumbe neema inayotuumba upya hatua kwa hatua inatufanya tupande
daima. Tunapongojea uzima wa milele, maisha yetu yanatushangaza kwa jinsi
yalivyo na mwanga na giza pamoja: “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa
maana hizi zimepingana” (Gal. 5:16-17). Tabia mbovu inabaki hata ndani
ya waliobatizwa. Upendo wa Kristo uliomo ndani mwetu haujashinda umimi wetu
moja kwa moja, bali unahitaji bado kushindana nao kwa nguvu. Unahitajika
utakaso mkubwa; sio tu ule tunaotakiwa kujipatia kwa kujifisha, bali ule
tunaopatiwa na Mungu anapokuja kupogolea matawi ya mzabibu yazidi kuzaa.
“Ili
tufikie nuru ya Kimungu na muungano kamili wa upendo na Mungu – nayasemea
yanayowezekana duniani – roho inapaswa kupitia usiku
wenye giza… Kwa kawaida, wateule wanapojitahidi kufikia hiyo hali
ya ukamilifu wanakuta magiza makubwa, na kupaswa kuteseka katika mwili na
roho hivi kwamba ujuzi wa kibinadamu hauwezi kueleza hata kidogo… Picha zake
hazijulikani na mtu isipokuwa na wale waliyoyang’amua wenyewe” (mt. Yohane
wa Msalaba). Tawi ambalo Mungu analisafisha si hai tu, bali anajitambua pia,
na ili mtu aweze kujua huko kupogolewa ni nini anatakiwa kukupata mwenyewe.
Kila mmoja anapaswa kubeba msalaba wake,
lakini hajui msalaba ni nini kabla hajaubeba kwa upendo.
Bila
ya tabu hatufikii kushinda kikamilifu umimi,
tamaa ya anasa, uvivu, hasira, wivu, kijicho, utovu wa haki katika kuhukumu,
kujipendea, kujidai kipumbavu, kujifanya
lengo hata la ibada, hamu kubwa mno ya kufarijika, kiburi upande wa akili
na wa roho, yale yote yanayopingana na imani na tumaini kwa Mungu, ili
tumpende Bwana kikamilifu “kwa
moyo wote, kwa akili yote, kwa nguvu zote, kwa roho yote” na kumpenda
jirani, hata adui, tunavyojipenda.
Tunahitaji kwa wingi imani, subira, ustahimilivu ili kudumu katika upendo kwa
vyovyote, yanapotimia maneno ya mt. Paulo: “Naam, na wote wapendao kuishi
maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2Tim. 3:12).
Kwa
hiyo mt. Yohane wa Msalaba, akielekeza njia inayofikisha kwa hakika na haraka
zaidi kwenye ukamilifu wa Kikristo,
alisema hatuwezi kuufikia Mungu
asipotutakasa hisi – ndiyo ishara ya kuingia hatua ya mwanga – na asipotutakasa roho – kwenye kizingiti cha hatua ya muungano. Kujitakasa
hakutoshi: “Mtu, hata akiwa na juhudi namna gani, hawezi kufaulu kujitakasa
kikamilifu: hawezi kabisa kujiandaa
kuungana na Mungu kwa upendo kamili. Ni lazima Mungu mwenyewe
ashughulike na kumtakasa kwa moto
ambao ni giza kwa roho… Roho zinaanza kuingia katika huo usiku wa giza
Mungu mwenyewe anapowakomboa polepole kutoka hali ya wanaoanza, ambapo wanatafakari katika njia ya Kiroho, ili
awaingize katika hali ya wanaoendelea,
ambayo ni ile ya wanasala. Wanapaswa kupitia njia hiyo ili wawe wakamilifu,
maana yake wafikie muungano wa Kimungu”.
Kwanza
tunaachishwa faraja za kihisi, ambazo zinafaa kwa muda, lakini zinakuwa kizuio
zikitafutwa kwa zenyewe. Ndiyo sababu tunahitaji kutakaswa hisi kwa ukavu na
kuongozwa kwenye maisha ya Kiroho yasiyotegemea mno hisi, ubunifu na mafuatano
ya mawazo. Hapo kwa vipaji vya Roho
Mtakatifu, ingawa kuna giza la kusumbua, tunapata ujuzi wa kuangaziwa
unaotuingiza kwa undani katika mambo ya Mungu, pengine tuyapenye kwa nukta
moja kuliko kwa miezi au miaka ya kutafakari. Ili kushinda vishawishi dhidi ya
usafi wa moyo au ya subira, vinavyotokea mara nyingi wakati wa usiku wa hisi,
unahitajika pengine ushujaa mkubwa unaoleta faida baadaye.
Katika
usiku huo hisi zinatupwa kwenye giza na ukavu kwa kutoweka kwa neema za kihisi
ambazo roho ilikuwa inaziishia kwa kuzifurahia kwa umimi. Lakini katika giza
hilo, akili na utashi vinaanza kuangazwa na mwanga wa uzima unaopita
kutafakari kwa mafuatano ya mawazo na ambao unaelekeza kumkazia Mungu macho ya
upendo katika sala. “Basi, roho imetoka, na kuanza kupenya njia ya roho
wanayoifuata wale wanaoendelea, njia
inayoitwa ya kuangazwa au ya kujaliwa kuzama katika sala” (mt. Yohane wa Msalaba).
Baada
ya hayo yote utahitajika utakaso
mwingine wa kujaliwa ili kuokoa roho kutoka kasoro za wanaoendelea ambazo “haziponyeki
kadiri hao wanaoendelea wanavyodhani ni mema kamili ya Kiroho… Basi,
anayetaka kusonga mbele kweli, ni lazima
apitie utakaso wa usiku wa roho. Hapo tu roho itaweza kuona njia ya kufaa
ya kuungana na Mungu” (mt. Yohane wa Msalaba). Utakaso huo unapatikana
katika walioendelea zaidi ambao wanatamani mema lakini wanadai yafanywe nao na
kwa namna yao wenyewe. Hao wanapaswa kutakaswa kila namna ya kushikilia
kibinadamu akili yao na matendo yao, namna yao binafsi ya kuona, kutaka na
kutenda. Utakaso huo ukivumiliwa vizuri, katikati ya vishawishi dhidi ya
maadili ya Kimungu, unazidisha mara mia imani, tumaini na upendo wao.
Jaribu
hilo la kutakaswa linajitokeza kwa namna tofauti katika maisha ya sala tu na
katika yale ya kitume. Pia ni tofauti kadiri linavyolenga kumfikisha mtu
kwenye ukamilifu mkuu kuanzia hapa duniani au linavyotokea mwishoni tu mwa
maisha haya ili kumsaidia kutakaswa walau
kwa kiasi fulani kabla hajafa, akijipatia
hivyo stahili kwa ustawi wa upendo, badala
ya kutakaswa toharani asipoweza kustahili. Hivyo dogma ya toharani
inathibitisha haja ya matakaso hayo.
Hapo
mchanganyiko wa mwanga na giza ni
mkubwa kuliko ule wa usiku wa hisi. Roho inaonekana imekosa mianga na urahisi
wa kusali na kutenda ambao ilikuwa inaufurahia mno kutokana na baki la
kujipendea na kiburi. Lakini katikati ya huo usiku wa roho unaonekana mwanga
mkuu zaidi; polepole, katikati ya vishawishi dhidi ya imani na tumaini,
zinajitokeza sababu zenyewe za maadili ya Kimungu, ambazo ni kama nyota kuu
tatu: ukweli asili wenye kufunua, huruma yenye kusaidia na wema mkuu wa Mungu.
Mtu anafikia kumpenda Mungu kwa usafi mkubwa na kwa uwezo wake wote.
Tutayaeleza
hayo kirefu mwanzoni mwa sehemu ya tatu na ya nne. Hapa yalihitajika tusije
tukapunguza ukuu wa ustawi kamili wa
kawaida wa maisha ya Kikristo. Kama tulivyokwishaona, kilele hicho
kinachoweza kufikiwa duniani ni kile alichotuonyesha Bwana katika heri
nane za Kiinjili: hizo, na hasa zile za mwisho, zinapita taratibu za
juhudi tu na kupatikana upande wa mafumbo, kama hayo matakaso ya Kimungu.
Fundisho
la kwamba ukamilifu unadai matakaso ya Kimungu ya hisi na roho lina mengi
yanayotokana nalo.
Kwanza
kuwa sala ya kumiminiwa, yaani
kuzama katika mafumbo ya imani, imo katika njia ya kawaida ya utakatifu, kwa
sababu inaanza katika ukavu wa utakaso wa hisi. Ingekuwa kosa kubwa
kuchanganya sala hiyo na faraja ambazo hazifuatani nayo daima.Usemi wa kuwa
mizizi ya ujuzi ni michungu lakini matunda yake ni matamu unafaa kuhusu mizizi
na matunda ya sala ya kumiminiwa.
Pili,
siku hizi hakuna tena mtu anayesema kuzama katika mafumbo ya imani ni karama
tu, kama ile ya unabii au ile ya kusema kwa lugha ngeni. Wote wanakubaliana
sala hiyo inahusiana na neema ya utakaso, yaani neema ya maadili na vipaji.
Hatimaye,
tusipoweza kustahili neema ya hakika ya kuzama katika sala, maana yake si
kwamba haipo katika njia ya kawaida ya utakatifu. Mwadilifu hawezi kustahili
vilevile neema ya kufa katika neema ya utakaso, ingawa ni ya lazima kwa uzima
wa milele. Wala hawezi kustahili neema ya hakika inayomkinga dhidi ya dhambi
ya mauti adumu katika neema ya utakaso. Lakini zawadi hizo ambazo hawezi kuzistahili,
anaweza kuzipata kwa sala nyenyekevu,
yenye tumaini na udumifu.
Tusichanganye
maswali mawili yafuatayo: “Je, sala ya kumiminiwa ipo katika njia ya kawaida
ya utakatifu? Je, waadilifu wote wanaweza kuifikia, bila ya tofauti ya
mazingira, malezi na uongozi?”. Kama vile isivyofaa kuchanganya haya
yafuatayo: “Je, neema ya utakaso ni mbegu ya uzima wa milele? Je, kati ya
wale walioipokea kwa ubatizo au kati ya waliodumu nayo miaka kadhaa, wataokoka
wote au walau wengi wao?”.
Kwa
nini wanasala hasa ni wachache hivi? Kwa sababu wachache tu wanajua kujitenga
na viumbe. Wengine wanaweza wakawa na nia njema, lakini hawana juhudi zile zote
zinazohitajika ili kufikia ukamilifu. Tena
ili kuufikia ni muhimu kupata malezi mazuri na uongozi mzuri, ingawa Mungu
anafidia kwa watu kadhaa wenye juhudi nyingi.
Tusisahau
pia kuwa wito wa kuwa mwandani wa Mungu, kama ule wa kuishi Kikristo, unaweza
kuwa wa jumla na wa mbali tu, au maalumu na wa jirani. Tena huo wa pili
unaweza kuwa wa kutosha au wa hakika. Hatimaye huo wa hakika unaweza kuhusu
viwango vya chini au vile vya juu vya muungano na Mungu.
Hatutakiwi
kupunguza ukuu wa lengo tunalotaka
kulifikia. Kuhusu njia zake, busara
inapaswa kuzipendekeza kulingana na
hali mbalimbali walizonazo watu, na kadiri hao walivyo kati ya wanaoanza au
wanaoendelea. Hivyo vinahakikishwa ukuu wa lengo, na uongozi wa kufaa
kulifikia.
Baada
ya kuona ukamilifu wa Kikristo umo hasa katika upendo, inafaa tujiulize kama
ukamilifu huo ni shauri tu au amri
inayowalazimisha Wakristo wote kuulenga. Ni sawa na kujiuliza maana halisi
na upana wa amri ya upendo.
Baadhi
ya watu wanadhani si lazima kuwa na upendo mkubwa ili kutimiza kikamilifu amri
kuu; kwao ukamilifu haulengi amri
hiyo, bali unahusika na utekelezaji wa mashauri kadhaa yaliyo juu ya amri
yenyewe. Mt. Thoma wa Akwino alijibu kwa unyofu na undani kwamba wote wanapaswa kulenga ukamilifu, kila mmoja kadiri ya hali yake, ingawa
hawapaswi kuwa wakamilifu tayari. Akaonyesha kuwa amri kuu inatulazimisha wote kwa jumla kulenga ukamilifu wa upendo, walau kwa
kufuata njia ya kawaida, ingawa
nadhiri za kitawa zinawalazimisha tu wale walioziweka waulenge kwa kufuata njia
ya pekee ya wito wao. “Ukamilifu wa upendo, ambao unafanya maisha ya
Kikristo yawe kamili, umo hasa katika kumpenda Mungu kwa moyo wote na jirani
kama nafsi yetu. Kwa hiyo ukamilifu umo hasa katika kushika amri”, si katika
kutimiza nadhiri.
Kimsingi ukamilifu
wa Kikristo umo katika upendo, kwanza
kwa Mungu halafu kwa jirani; tungejidanganya kama tungedhani huo upendo unaagizwa
kwa kiwango fulani tu, halafu unakuwa shauri.
Amri hiyo inadai wazi ukamilifu: “Mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako
zote, na kwa akili zako zote”. Mipaka iko wapi? Vilevile: “na
jirani yako kama nafsi yako” (Lk. 10:27). Kila mmoja anajipenda
iwezekanavyo, tena kwa upendo anapaswa kujitakia uzima wa milele si kwa
kiwango cha chini tu, bali pasipo kujiwekea mpaka fulani, kwa sababu hatujui
Mungu anataka kutufikishia wapi.
Ni
hivyo kwa kuwa upendo ndio lengo la amri
yoyote, na katika utashi lengo halipatikani kwa kiwango fulani tu, bali
katika ukamilifu wake, tofauti na njia za kulifikia. Lengo tunalitaka au
hatulitaki; hatuwezi kulitaka nusu. Daktari
hawezi kutaka mgonjwa apone nusu; anapima dawa, lakini analenga afya pasipo kipimo. Basi, ukamilifu umo hasa katika amri.
“Kwa nini ukamilifu huo usiagizwe kwa binadamu, ingawa hakuna anayeweza kuwa
nao katika maisha haya?” (mt. Augustino). Maana yake, ukamilifu wa mbinguni
unadaiwa na amri ya kumpenda Mungu si kama kitu cha kutimizwa mara moja, bali
kama lengo ambalo wote wajiwekee.
Amri
nyingine zilizo chini ya amri kuu, lengo lake ni kuondoa vile ambavyo
vinapinga upendo na kutaka kuuangamiza; kumbe mashauri ya Kiinjili, lengo lake
ni kusukumia mbali vinavyoweza vikazuia utekelezaji
kamili wa upendo, ingawa haviupingi, k.mf. ndoa, shughuli za kidunia n.k.
“Amri… na mashauri… vinashikwa vizuri vinapotimizwa ili kumpenda Mungu
na kumpenda jirani kwa ajili ya Mungu, katika ulimwengu huu na ule ujao”
(mt. Augustino). “Ndiyo sababu katika Mafundisho ya Wazee, abati Musa
alisema: Mafungo, makesha, kutafakari Maandiko, kwenda uchi na kukosa vitu si
ukamilifu, bali vifaa au njia za ukamilifu; huo haumo ndani ya mambo hayo, ila kwa njia yake
unafikiwa kwa kasi na kwa hakika zaidi” (mt. Thoma wa Akwino). Ndiyo njia
inayoelekea ukamilifu; lakini wenyewe ni kumfuata Yesu kwa upendo. Kwa maana
hiyo alisema, “Ukitaka kuwa mkamilifu,
enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina
mbinguni, kisha njoo unifuate”
(Math. 19:21). Tunaweza kuwa fukara kwa hiari kutokana na sababu isiyo ya
kidini (k.mf. kwa kudharau utajiri kifalsafa) au kwa upendo wa Mungu; kwa
vyovyote si jambo la lazima kwa ukamilifu. Huo umo hasa katika kutekeleza
vizuri zaidi na zaidi amri kuu isiyo na mipaka: Wakristo wote waliopewa amri
hiyo wanapaswa walau kulenga ukamilifu huo, kila mmoja kadiri ya hali
yake (k.mf. ndoa au utawa), kama si kuwa nao tayari. Kwao wote kulenga upendo
kamili si afadhali tu, bali ni
wajibu sawa na ule wa kuelekea mbinguni, ambapo upendo wa Mungu utatawala
kikamilifu, kisiwepo kitu kinachoweza tena kuupunguza.
Fundisho
la kuwa amri kuu haina mipaka kwa jinsi ilivyotolewa linathibitishwa kwa
kuzingatia kuwa lengo tunalolizungumzia hapa si la katikati (kama vile afya),
bali ni lile kuu, yaani Mungu mwenyewe, aliye wema
usio na mipaka. Ikiwa mgonjwa anajitakia afya pasipo kiwango, zaidi sisi
tunapaswa kutamani upendo wa Mungu pasipo kiwango, kwa kuwa hatujui ni kipi
ambacho Mungu anataka kutufikishia na kweli atatufikishia tukiwa waaminifu. “Binadamu hawezi kamwe kumpenda Mungu anavyotakiwa kupendwa; kama vile
hatutaweza kamwe kumuamini na kumtumainia tunavyopaswa” (mt. Thoma wa
Akwino). Tofauti na maadili ya kibinadamu, yale ya Kimungu, lengo lake, sababu
yake na kipimo chake halisi ni Mungu mwenyewe, yaani ukweli wake na wema wake
usio na mipaka. Kwa hiyo hatuwezi kumuamini mno na kumtumainia mno; hatutaweza
kamwe kumpenda anavyostahili. Hivyo tunaona vizuri kuwa amri kuu haina mipaka:
inawadai wote hapa duniani waulenge upendo wa Mungu ulio safi na wenye nguvu
zaidi na zaidi.
Tumaini
linapatikana kati ya kukata tamaa ya wokovu na kuudai kipumbavu, lakini si
kwamba anayetarajia kipumbavu kuokoka anamtumainia mno Mungu, bali anabadili
sababu ya kutumainia, akitumaini kile ambacho Mungu hawezi akaahidi, k.mf.
msamaha pasipo majuto halisi. Vilevile kilema cha wepesi wa kuamini hakimo
katika kumuamini mno, bali katika kusadiki mambo yaliyobuniwa na binadamu kama
kwamba yamefunuliwa na Mungu.
Kusahau
kuwa katikati adilifu ni pia kilele, na kudhani maadili ya Kimungu yamo hasa
katikati sawa na maadili ya kibinadamu, ndiko sifa ya mtu wa wastani
anayejisingizia kuwa na kiasi. Mtu wa namna hiyo yupo katikati ya uadilifu na
uovu, tena anakaribia uovu kuliko uadilifu: “Mtu wa wastani kweli
anapendezwa na kila kitu, lakini hapendezwi na chochote hata achangamke…
Anachukia tamko lolote, kwa kuwa kila tamko linapinga tamko lingine tofauti.
Kumbe ukijifanya kidogo rafiki na kidogo adui wa kila jambo, atakuona mwenye
busara na kiasi. Mtu wa wastani anasema katika yote kuna mchanganyiko wa mema
na mabaya, kwa hiyo tusiwe na msimamo mkali katika kupima mambo. Ukisisitiza
ukweli kwa nguvu, mtu wa wastani atasema unajiamini mno. Mtu wa wastani
anasikitika kuwa Ukristo una dogma; angependa ufundishe maadili tu; ukimuambia
kuwa maadili ya Ukristo yanatokana na dogma zake kama matokeo na sababu yake,
atakujibu umezidisha chumvi… Kama neno ‘kuzidisha’ lisingekuwepo, mtu wa
wastani angelitunga… Kwa kawaida mtu wa wastani anaonekana mtaratibu; hawezi
kuwa mnyenyekevu, la sivyo angeacha kuwa wa wastani. Mnyenyekevu anakataa
uongo, hata kama ungetukuzwa na ulimwengu wote, naye anaupigia magoti
ukweli… Mtu mwenye upendo hawezi kamwe kuwa wa wastani” (E. Hello).
Sababu
ya mwisho ya amri ya upendo kutokuwa na mipaka ni kwamba tunasafiri
kuelekea uzima wa milele, nasi tunasafiri vizuri kadiri tunavyokua katika
upendo wa Mungu na wa jirani. Upendo wetu unatakiwa
kustawi mfululizo mpaka mwisho wa safari. Hilo si shauri tu, yaani jambo
bora la hiari, bali ni agizo,
linatakiwa, hivi kwamba mtu ambaye hapa duniani hataki kukua katika upendo
anamchukiza Mungu. Njia ya uzima wa milele haikusudiwi kwa kusimama wala
kulala, bali kwa kutembea tu. Kwa msafiri ambaye hajafikia mwisho wa lazima wa
safari yake, kusonga mbele si shauri, ni sharti. Basi, tunaposafiri kumuelekea
Mungu, tunasonga mbele si kimwili, bali Kiroho, kwa kukua katika upendo ambao
uwe safi na wa nguvu zaidi na zaidi. Ndivyo tunavyotakiwa kuomba, na ndiyo
maombi matatu ya kwanza ya Baba Yetu.
Ikiwa
ni hivyo, tusipotimiza bado kikamilifu amri hiyo, je, tunaivunja?
Jibu la hakika ni hapana, kwa kuwa “ili tukwepe uvunjaji huo inatosha
kushika kwa namna fulani sheria ya upendo kama wanavyofanya wanaoanza” (mt.
Thoma wa Akwino). Ni kweli kwamba upendo wa Mungu unaingia wote kabisa katika lengo la amri hiyo; hata ukamilifu wa mbinguni
hauwekwi kando, kwa kuwa ndio lengo ambalo tulikusudie, lakini hatuivunji amri
tukitimiza upendo kwa kiasi fulani. Sasa, kiwango cha chini cha kumpenda Mungu ni kutopenda chochote kuliko
yeye, au kinyume chake au sawa naye; asiye na kiwango hicho hatimizi amri.
Kinyume na hicho, kuna kiwango cha upendo kisichoweza kufikiwa hapa duniani,
isipokuwa mbinguni, nacho ni kumpenda Mungu hivi kwamba upendo wetu umlenge
kweli mfululizo. Kwa hiyo hatuvunji amri kwa sababu hatujafikia ukamilifu
huo, wala hatuivunji kama hatujafikia viwango vya katikati, mradi tuwe na
kiwango cha chini. Lakini tukisimama katika kiwango hicho hatutimizi
kikamilifu amri kuu.
Ni
kosa kudhani kuwa upendo huo tu usiokamilika ni wa lazima, na kuwa viwango
vyake vya juu ni vya shauri tu. Hivyo vinaagizwa walau kama lengo, hata ikiwa
si kwa sasa hivi. Ni sawa na mtoto ambaye asipokua kadiri ya taratibu za
ukuaji wake, hatabaki mtoto, bali atakuwa mbilikimo. Upande wa roho pia sheria
ya ukuaji ina masharti makali: ikiwa mbegu ya Kimungu tuliyotiwa kwa
ubatizo haistawi, ina hatari kubwa ya kufa, ya kusongwa na magugu. Hakika
katika njia ya wokovu, watu walio tofauti na vile wanavyotakiwa kuwa si wale
waliozama katika mafumbo, bali ni wachelewaji
na watu vuguvugu.
Yapo
matatu yatokanayo na ambayo tutayafafanua hapo mbele:
1°
Katika njia ya Mungu, asiyesonga mbele, anarudi nyuma: kwa sababu
kwetu ni sheria kusonga mbele mfululizo, na asiyefanya hivyo anakuwa mchelewaji,
kama garimoshi linalosimama mno kwenye stesheni lisifuate ratiba, au kama
mtoto asiyekua anavyotakiwa na hivyo anakuwa mbilikimo.
2°
Ustawi wa upendo unatakiwa kuwa ya kasi zaidi na zaidi kadiri tunavyomkaribia
Mungu na kuvutwa naye. Ndivyo jiwe linavyoanguka kasi zaidi kadiri
linavyokaribia ardhi na kuvutwa nayo.
3°
Hatimaye, ikiwa ndio ukuu wa amri wa upendo, hatuwezi kuwa na wasiwasi kuhusu kuzidi kutolewa neema za msaada ili tulifikie lengo hilo, kwa sababu
Mungu haagizi kamwe yasiyowezekana. Anatupenda mno, kuliko tunavyoweza
kudhani. Ni juu yetu kuitikia. Baada ya kumpenda kwa moyo wote, kihisi pia, kwa mapenzi, tunapaswa
kumpenda kwa akili yote, kwa upendo
mtendaji, kwa nguvu zetu zote saa ya
kujaribiwa inapotufikia, na hatimaye kwa
roho yetu yote, iliyoachana na mahangaiko ya hisi, ili tumuabudu “katika
rono na kweli” (Yoh. 4:23,24).
Fundisho
hilo kwa jumla linatuonyesha kuwa haifai kutenganisha utakatifu na wokovu wa
milele, kama wanavyofanya wanaosema, eti, “Mimi sitakuwa mtakatifu kamwe;
kwangu inatosha niokoke”. Mtazamo huo ni kosa kubwa. Kujipatia utakatifu
zaidi na zaidi ndiyo njia ya wokovu wa milele; mbinguni kutakuwa na watakatifu
tu, na kwa maana hiyo wote, na kila mmojawetu, tunapaswa kulenga utakatifu.
Tumeona
kuwa waamini wote wanapaswa kulenga
ukamilifu wa upendo, na kuwa hawawezi kuufikia wakiishi duniani kama kwamba
ndiyo maskani yao ya milele, pasipo roho
ya mashauri ya Kiinjili, yaani kutoambatana na ulimwengu. Kutokana na amri
kuu huo ni wajibu wa wote, kila
mmoja kadiri ya hali yake maishani. Lakini, kutokana na wito wa pekee, baadhi
wana wajibu maalumu wa kulenga
ukamilifu katika maisha ya pekee, kama vile padri ili awe mhudumu mwadilifu wa
Bwana, na kama vile mtawa kufuatana na nadhiri au ahadi zake za kutekeleza mashauri ya ufukara, useja na utiifu. Kwanza
tutazungumzia utekelezaji huo kuhusiana na ukamilifu wa Kikristo na uponyaji
wa madonda yetu ya rohoni.
Yesu
alipomualika tajiri akauze vyote ili kumfuata katika ukamilifu, “yule kijana
alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali
nyingi” (Math. 19:22). Utekelezaji wa vitendo wa mashauri ya Kiinjili si
wajibu wala si sharti la kufikia ukamilifu tunaopaswa kuulenga; ila ni njia ya
kufaa tulifikie lengo hilo kwa hakika na kasi zaidi, tusije tukasimama njiani.
Ni vigumu kuwa na roho ya kutoambatana na malimwengu tusipoitekeleza kwa
vitendo, tunavyoona katika huyo aliyeshindwa. Mkristo anayeishi ulimwenguni
yuko katika hatari ya kuzama katika mahangaiko ya kujipatia nafasi nzuri au
kuwatafutia ndugu zake, na hivyo kusahau kwamba anapaswa kuelekea nchi
nyingine, na kwamba ili aifikie anahitaji sio akili kuhusu shughuli za
kidunia, bali msaada wa Mungu (ambao ajiombee) na tunda la neema (yaani
stahili). Pia katika maisha ya kifamilia anaelekea kukwama katika mafungamano
yanayomtimizia haja ya mapendo, na hivyo kusahau wajibu wa kumpenda Mungu
kuliko viumbe vyote. Mara nyingi upendo wake si mwali hai unaoinuka kwa Mungu
ukihuisha mapendo mengine yote, bali ni kama makaa madogo yanayozidi kuzimika
chini ya majivu: ndiyo sababu anaweza akatenda dhambi kwa urahisi, asifikirie
kuwa anasaliti urafiki wa Mungu. Hatimaye yuko katika hatari ya kufuata
matakwa yake na, kisha kusali kifupi, kupanga maisha yake upande wa maumbile
tu, akiathiriwa na umimi, mawazo ya kibinadamu na madai ya mazingira. Hapo
akili inahangaikia maswala ya kidunia na pengine michezo, halafu yakitokea
matatizo makubwa yanayohitaji nguvu nyingi za Kiroho anakuja kutambua imani
yake ni haba mno: kwake kweli kuu za imani hazina nguvu kiutendaji, ziko mbali
angani zisiingie ndani ya roho. Anakosa imani yenye vitendo ambayo ilete nuru
ya mafumbo ya wokovu katika maisha ya kila siku.
Ndizo
hatari zinazomkabili Mkristo asipojitahidi kutekeleza mashauri ya Kiinjili
kadiri anavyoweza. Akiteleza kwenye mteremko huo, anapotea na kuzidi kupatwa
na maradhi matatu yanayopingana moja kwa moja na hayo mashauri matatu: “Kila
kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha
uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia” (1Yoh. 2:16). Hayo ni
madonda matatu yenye usaha yanayoziathiri roho na kuziua kwa kuzisogeza mbali
na Mungu.
Madonda
hayo yameenea ulimwenguni kufuatana na dhambi ya mtu wa kwanza pamoja na
dhambi zetu tulizozirudiarudia. Ili tuelewe ubaya wake tunapaswa kukumbuka
kuwa kwa wengi yanashika nafasi ya ule ulinganifu
uliokuwepo katika hali ya uadilifu asili pande zote tatu, na ambao Mwokozi
anataka kuturudishia kwa njia ya mashauri yake.
Mtu
alipoumbwa kulikuwa na ulinganifu kamili kati ya Mungu na roho, kati ya roho
na mwili, kati ya mwili na vitu vya nje. Kulikuwa na ulinganifu
kati ya Mungu na roho, kwa sababu roho imeumbwa ili kumjua, kumpenda na
kumtumikia Mungu, na kwa njia hiyo kupata uzima wa milele. Mtu wa kwanza,
aliyeumbwa katika utakatifu na uadilifu, alikuwa kama mwanasala mwenye kuongea
kirafiki na Mungu akijilisha hasa mambo ya Kimungu, akizingatia yote katika
mwanga huo na kumtii.
Kutokana
na ulinganifu huo wa juu kulikuwa na ule kati
ya roho na mwili, ulioumbwa ili utumikie roho. Roho ikiwa chini ya Mungu
kikamilifu iliutawala mwili wake, maono na maelekeo ya hisi yakifuata kwa
makini uongozi wa akili (yenye kufuata busara na kuangazwa na imani) na
msukumo wa utashi (uliohuishwa na upendo).
Hatimaye
kulikuwa na ulinganifu kati ya mwili na
vitu vya nje, dunia ikizaa yenyewe pasipo haja ya kulimwa kwa jasho la
uso; vilevile wanyama walikuwa wakimtii mtu aliyepewa kuwatawala, au walau
hawakumdhuru.
Dhambi
ilivuruga ulinganifu huo wote ikiangamiza ule wa juu: mtu aliasi sheria ya
Mungu, na tangu hapo roho yake inaelekea
kiburi na kukariri, “Sitatii”. Imeacha kujilisha ukweli wa Kimungu
ijitungie mawazo yake finyu, danganyifu, geugeu, na kujitengenezea ukweli wake
yenyewe na kujiongoza kwa kuiwekea mipaka mamlaka ya Mungu, badala ya kupokea
toka kwake uongozi ule ambao peke yake unafikisha kwenye uzima.
Kwa
kukataa kumtii Mungu, roho imepoteza utawala wake juu ya mwili na juu ya maono
yake yaliyokusudiwa kutii akili na utashi. Tena mara nyingi imejifanya mtumwa
wa mwili na silika zake za kinyama: ndizo tamaa
mbaya za mwili. Watu wasio na idadi wanasahau lengo lao la Kimungu na
kushughulikia kutwa kucha mwili wao kama mungu wao. Maono yanaitawala roho
hata isipotaka, kwa kuwa ndani yake pendo, wivu, hasira na chuki vinajitokeza
vikipambana na kuipeleka huko na huko kama farasi wasiokubali lijamu wala
hatamu.
Hatimaye
mwili, badala ya kufaidika na vitu vya nje, umekuwa mtumwa wa vitu hivyo:
unajichosha ili kuvipata kwa wingi, unajizungushia fahari ya bure kwa hasara
ya maskini wenye njaa, unajiona na haja na vile vyote vinavyong’aa na
kuonekana na kuthaminika: ndizo tamaa za
macho. Kisha kujilimbikizia vitu, hangaiko la kuvidumisha na kuvizidisha
tena linakuwa wazo kuu kwa umati wa watu ambao, kama watumwa wa shughuli hizo,
hawana kamwe muda wa kusali na kusoma Injili ili kujilisha rohoni; wanajijenga
hapa duniani kama kwamba wataishi hapa milele yote, wasiwazie wokovu wao.
Utumwa
huo wa pande tatu, ulioshika nafasi ya ulinganifu asili pande zote tatu, ni
kinyume cha utaratibu. Mwokozi alikuja kuurudisha, na kwa ajili hiyo
ametupatia mashauri matatu.
Yesu
katika ubinadamu wake ndiye kielelezo cha maadili yote, mfano bora wa
utakatifu wote. Utu wake uliwekwa wakfu kwa Mungu tangu achukuliwe mimba,
kutokana na umoja wake na nafsi ya Neno; kwa sababu hiyo ulipokea utakatifu wa
kuzaliwa nao, usioumbwa. Haiwezekani kuwaza muungano na Mungu ulio wa ndani na
wa kudumu kuliko huo unaounganisha utu na umungu katika nafsi ya Neno
aliyefanyika mwili. Kutokana nao utu wa Mwokozi umewekwa wakfu kwa vipawa
vyake vyote na kwa matendo yake yote, hata akili yake isiweze kudanganyika,
utashi wake usiweze kufanya kosa na hisi zake safi zisiweze kuvurugwa na
lolote. Matendo yake yote ni ya Mungu, yanatokana na Mungu na kumuelekea
Mungu; hapana pengine popote utawala wa Aliye Juu ulipotimia kikamilifu hivyo.
Kwa kuwa utu wa Yesu umewekwa wakfu namna hiyo bora, ukuu wake umemtenga na
roho ya ulimwengu na yale yote yaliyo maovu au yasiyo mema tu, naye akatolewa
kwa ulimwengu ili kuukomboa kutoka upofu wa tamaa na kiburi.
Kwa
ukuu huo wa asili, Yesu alitengana na mali, heshima, shughuli za kidunia:
kielelezo cha ufukara, hakuwa na mahali “pa kujilaza kichwa chake” (Lk.
9:58). Kwa ukuu huo, Yesu hakuambatana na furaha za dunia, alikuwa huru kuhusu
madai ya familia ili aiunde nyingine ya kimataifa, yaani Kanisa: hivyo ni
kielelezo cha useja mtakatifu, wenye uzazi wa Kiroho usio na mipaka. Hatimaye,
kwa ukuu wake upitao maumbile, Yesu hakuambatana na matakwa yake yoyote: akiwa
na umri wa miaka kumi na miwili alitamka kwamba ”imenipasa kuwamo katika
nyumba ya Baba yangu” (Lk. 2:49), halafu “akawa mtii hata mauti, naam,
mauti ya msalaba” (Fil. 2:8).
Kwa
kuwa Mwokozi ametoka juu, hakuwa wa ulimwengu huu, bali alitolewa auokoe, ukuu
wake wenyewe ulimtenga na yale yote yaliyo ya chini aweze kuufanyia kazi
ulimwengu kutoka juu ili kazi hiyo ifike popote na ipenye zaidi, kama vile jua
likifika kwenye kilele cha mzunguko wake. Kwa kuwa huru kutoka vifungo vyote
vya binadamu (mali, familia na mawazo finyu), Yesu aliweza kuwashughulikia
binadamu wote akiwaletea uzima wa milele. Injili yake haizeeki, ni ya kisasa
daima, vile Mungu alivyo. Hivyo katika Bwana tunaona urekebisho wa ulinganifu
asili pande zote tatu, urekebisho bora kuliko ukamilifu wa Adamu: “dhambi
ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi” (Rom. 5:20).
Urekebisho huo unatakiwa kuendelea katika Kanisa, linalopaswa kung’aa kwa utakatifu. Sifa yake hiyo inatakiwa kuwa wa ajabu na kuonekana, sio tu mara mojamoja katika watu shujaa (k.mf. wafiadini na watakatifu waliotangazwa rasmi), bali mfululizo katika familia za kitawa ambamo idadi kubwa ya watu inafuata shule ya utakatifu na kutamka hadharani nia ya kumfuata Bwana kwa kuungana na Mungu wasiambatane na malimwengu. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya Bwana na watu hao, hata wakiwa na juhudi za namna gani: yeye ametoka juu, hao wametoka chini, katika dhambi na udanganyifu, na wanapaswa kujitenga navyo zaidi na zaidi ili kujiweka wakfu kwa Mungu kwa ndani zaidi na zaidi.
Wale
waliopokea wito huo wa pekee, Mwokozi anawapendekezea waishi sio tu kwa
kufuata roho ya mashauri matatu ya Kiinjili, bali kwa kuyatekeleza kweli,
akiwaahidia mara mia zaidi. Anawaalika wajitenge
pande tatu ili kujiweka wakfu pande tatu na hivyo kuhakikisha ustawi wa
maadili bora hadi muungano na Mungu. Katika kutumia malimwengu anawashauri wabane kwa kujinyima wasije wakavutwa kuzidisha.
Anawaalika
kutekeleza ufukara, kujitenga na
matumizi huru na hata umilikaji wa vitu ili kuviweka wakfu kwa Mungu visiwe
tena vizuio, bali vyombo kwa safari ya kuelekea uzima wa milele. Anawaalika
kuishi kwa usafi kamili, yaani
kujinyima furaha za jinsia na kuuweka moyo wao wakfu kwa Mungu, usiwe tena
kizuio, bali chombo ambacho upendo unakifanya kuwa cha Kimungu ili kuungana na
Mungu kila siku kwa dhati na nguvu zaidi. Hatimaye anawaalika kwenye utiifu mtakatifu, kujikomboa kutoka matakwa yao yoyote, yaliyojaa
ugeugeu na ukaidi, ili utashi wao usiwe tena kizuio, bali chombo ambacho
upendo unazidi kukifanya cha Kimungu ili kuungana na Mungu kwa undani na nguvu
kila siku zaidi.
Utekelezaji
wa maadili hayo matatu na wa nadhiri zake una shida, lakini unaondoa shida
nyingine nyingi. Ndege anainua mabawa, lakini ni kweli zaidi kuwa mabawa
yanamuinua ndege; vilevile maadili ya kitawa na nadhiri zake vinamletea mtu
wajibu wa pekee, lakini hasa vinamleta kwenye ukamilifu wa upendo kwa haraka
na hakika zaidi.
Maadili
ya ufukara, useja na utiifu yako chini ya adili
la ibada ambalo linampa Mungu ibada inayotupasa, kwa hiyo ni kuu kuliko
maadili mengine ya kibinadamu, likifuata mara yale ya Kimungu. Lenyewe
linamtolea Mungu vitendo vya kitawa. Ili mtawa awe na msimamo wa kutorudi
nyuma anajifunga kwa nadhiri, akiwajibika kuyatekeleza hayo matatu mpaka kufa
kwa mfano wa Bwana: anajitoa pamoja naye kwa maisha mazima ya sadaka; na kwa
kuwa anapaswa kutoa yote (vitu, mwili na moyo, matakwa) asijichukulie tena,
jina la sadaka ya kuteketezwa linafaa kweli.
Sadaka
hiyo itimizwe kwa dhati kila siku; hapo itatupatia mara mia zaidi. “Amin,
nawaambieni: hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au
mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya
Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu
wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu
ujao uzima wa milele” (Mk. 10:29-30). Tutaona hapo mbele kwamba: imani
ndiyo uhai wa utiifu mtakatifu, na utekelezaji wa adili hilo unakuza roho
ya imani; tumaini ndilo uhai wa ufukara
mtakatifu, unaotufanya tuzidi kumtumaini Mungu; na upendo ndio uhai wa useja mtakatifu ambao unapotekelezwa kikamilifu
unastawisha ndani mwetu upendo kwa Mungu na kwa watu kwa ajili yake.
1.14. WAJIBU WA PEKEE WA MAPADRI NA WATAWA
WA KULENGA UKAMILIFU
Baada
ya kueleza wajibu wa jumla unaowapasa Wakristo wowote wa kulenga ukamilifu
kutokana na amri kuu ya upendo, inafaa tuzungumzie wajibu wa pekee wa kufanya
hivyo unaompasa kila padri, awe ameweka nadhiri za kitawa au sivyo. Tunatakiwa
hasa kuonyesha jinsi adili la ibada linavyohitaji kuhuishwa zaidi na zaidi na
upendo kwa Mungu ambao uzidi kuwa safi na wa nguvu.
Msingi
wa wajibu huo ni nadhiri za kitawa, ambazo neema zake si za muda, bali za
kudumu tukizidi kuwa waaminifu. “Kwa kusema kwa usahihi, wengine wako katika
hali ya ukamilifu, sio kwa kufanya tendo la upendo kamili, bali kwa kujifunga moja kwa moja, kwa fahari fulani, kushika kile
kinachoelekeza kwenye ukamilifu… Hiyo ni kweli kwa watawa na kwa
maaskofu. Kwa kuwa watawa wanajifunga kwa nadhiri kujinyima malimwengu ambayo
wangeweza kuyatumia kwa hiari, nao wanafanya hivyo ili kushughulikia mambo ya
Mungu kwa urahisi zaidi… Vilevile maaskofu wanajifunga kushika mambo ya
ukamilifu wanapokubali daraja ya uaskofu, kwa sababu mchungaji anapaswa kutoa
uhai wake kwa ajili ya kondoo zake” (mt. Thoma wa Akwino).
Mtawa
anatamka kuwa atalenga ukamilifu: “Si kwamba nimekwisha kufika, au
nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali
nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo, kwa ajili yake, nimeshikwa na
Kristo Yesu” (Fil. 3:12). Hatendi kosa la unafiki kwa kutokuwa bado
mkamilifu, ila analifanya asipolenga ukamilifu kwa unyofu. Kwake wajibu huo wa
pekee ni mamoja na ule wa kushika nadhiri zake na kanuni aliyoahidi. Lakini
wajibu huo uzingatiwe daima katika uhusiano wake na ule wa jumla unaotokana na
amri kuu ya upendo; hapo utawa hautapotewa na ukuu wake kwa kutazamwa upande
wa sheria tu, bali utaonekana katika upana wa maana yake ya Kiroho.
Kwa
mtazamo huo unaeleweka uzito halisi wa neno la mt. Thoma wa Akwino: “Kufanya
tendo kwa nadhiri kunastahili kuliko kulifanya bila ya nadhiri”. Si kwamba
tuzidishe nadhiri ili kustahili zaidi, bali kwamba mtawa atekeleze nadhiri
zake vizuri zaidi na zaidi, akizidi kuchimba sababu tatu alizozitoa mtakatifu
huyo katika ufafanuzi wake:
1°
Nadhiri ni tendo la adili la ibada, ambalo
ni bora kuliko yale ya utiifu, ufukara na usafi wa moyo ambayo linamtolea
Mungu yawe ibada.
2°
Kwa nadhiri ya daima mtu anamtolea Mungu si tendo mojamoja, bali uwezo wenyewe wa kutenda, na kwa hakika ni afadhali kutoa mti na
matunda yake kuliko kutoa matunda tu.
3°
Kwa nadhiri utashi unaimarishwa katika
kutenda mema, na kwa hakika kutenda kwa msimamo kunastahili zaidi, kama vile
ni vibaya zaidi kutenda dhambi kwa utashi ulioimarika katika nia mbovu.
Tukiishi
kwa roho hiyo tunaelewa kwa namna hai fundisho la kwamba, kwa kujifunga
kushika mashauri matatu, zilizo kiini chenyewe cha utawa, mtu anajitenga na yale yanayoweza yakazuia mapendo yake yasimuelekee
Mungu tu, halafu asipofuta uamuzi huo anajitoa
kwa Bwana kama sadaka ya kuteketezwa. Hivyo hali yake ni ya kujitenga na
ulimwengu na kuwekwa wakfu kwa Mungu.
Hasa
mambo matatu yanaweza kuzuia mapendo yake yasimuelekee Mungu: tamaa za macho
(yaani za vitu), tamaa za mwili na kiburi cha maisha (yaani kupenda kuwa huru
tu). Mtawa anayakataa hayo matatu kwa nadhiri zake, kwa sababu anamtolea Mungu
mali kwa ufukara, mwili na moyo kwa useja mtakatifu na matakwa yake kwa
utiifu. Asipojitwalia tena chochote, tena akitekeleza vizuri zaidi na zaidi,
kwa upendo mkubwa, maadili matatu yanayohusiana na nadhiri za kitawa, basi
anamtolea kweli Mungu sadaka ile kamili inayostahili kuitwa ya kuteketezwa.
Hapo maisha yake yanatolewa kila siku
pamoja na sadaka ya misa kwa adili la ibada. Ni hivyo hasa kama mtawa
anarudia mara nyingi ahadi zake kwa namna inayostahili kuliko alipozitoa kwa
mara ya kwanza. Stahili zinakua ndani mwake pamoja na upendo na maadili
mengine, hivyo hali yake ya kuwekwa wakfu kwa Mungu inazidi kuwa ya dhati na
kamili.
Lengo
la kujinyima hivyo pande tatu na kujitoa hivyo pande tatu ni kuungana na Mungu
kila siku kwa ndani zaidi, kama utangulizi wa uzima wa milele. Mtawa anapaswa
kuufikia muungano huo kwa kumuiga Yesu Kristo aliye “njia, na kweli, na
uzima” (Yoh. 14:6). Yeye, katika ubinadamu wake, alitenganika
na roho ya ulimwengu akaunganika na
Mungu vizuri iwezekanavyo. Mtawa anatamka hadharani nia ya kumfuata,
lakini Yesu alitoka juu, kumbe mtawa ametoka duniani, palipotawaliwa na
dhambi, hivyo anapaswa kujitenga zaidi na zaidi na mambo yote ya kidunia ili
kujiweka wakfu kwa Mungu kwa ndani zaidi na zaidi. Hapo ndani mwake yatatimia
maneno haya: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo
juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikiri yaliyo juu, siyo
yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai
wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa,
aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”
(Kol. 3:1-4). Mt. Thoma wa Akwino alifafanua hivi: “Msionje malimwengu kwa
kuwa mmefia ulimwengu; uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo; mwenyewe
amefichika kwetu, kwa kuwa yuko katika utukufu wa Mungu Baba yake, na hivyo
uhai… tulionao kutoka kwake umefichika, kadiri ya maneno ya Maandiko
matakatifu, Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako ulizowawekea wakuchao;
ulizowatendea wakukimbiliao mbele ya wanadamu! (Zab. 31:19). Yeye ashindaye
nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa (Ufu. 2:17)”. Hiyo mana ya Kiroho,
ambayo ile ya jangwani ilikuwa mfano wake tu, ndiyo malisho ya roho: kujaliwa
kuzama katika mafumbo kwa imani hai iliyoangazwa na vipaji vya Roho Mtakatifu.
Hivyo maisha ya utendaji (yaani utekelezaji wa maadili ya kibinadamu)
yanaandaa kwa maisha ya sala ya kumiminiwa (yaani muungano na Mungu); kwa
namna ya pekee “ubikira unalenga ustawi wa roho katika maisha ya kuzama
katika sala” (mt. Thoma wa Akwino). Hivyo maisha ya kitawa yanalenga
utekelezaji mkamilifu zaidi na zaidi wa amri ya upendo na undani wa muungano
na Mungu.
Basi,
inafaa kuzingatia daima wajibu wa pekee alionao mtawa wa kulenga ukamilifu
kuhusiana na wajibu wa waamini kwa jumla unaotegemea amri kuu ya upendo. Amri
hiyo inatawala mashauri ya Kiinjili, kwa kuwa hayo ni njia na vyombo tu kwa
ajili ya kufikia kwa kasi na hakika zaidi ukamilifu wa upendo, yaani muungano
wa dhati na Mungu unaostawisha zaidi na zaidi ule na jirani.
Hivyo,
kwa mwanga wa maadili matatu ya Kimungu yanatekelezwa kikamilifu maadili
matatu ya kitawa. Kati ya hayo linaundwa fungamano la ndani, hivi kwamba
tumaini la heri ni kama uhai wa ufukara unaoachana na mali ya dunia ili kupata
ya milele; upendo ndio uhai wa useja unaojinyima pendo la chini ili kupata
upendo wa juu kabisa; imani ndiyo uhai wa utiifu unaotekeleza maagizo ya
wakubwa kama kwamba yamefunuliwa na Mungu. Hivyo maisha ya kitawa yanafikisha
kwenye sala ya kumiminiwa na muungano wa ndani na Mungu.
Ikiwa
bradha na sista wana wajibu wa pekee wa kulenga ukamilifu, zaidi tena anao
padri, hata kama si mtawa. Utawa
ni hali
ya kulenga ukamilifu; maaskofu
wako katika hali ya kutekeleza
ukamilifu; ndiyo sababu inafaa wawe katika hatua ya muungano ya
waliokamilika. Padri wa ulimwenguni anajiongezea stahili mpya akiingia
utawani. Lakini kwa vyovyote anapaswa tayari alenge ukamilifu kutokana na
sakramenti ya daraja na kazi zake takatifu. Wajibu huo maalumu hautofautiani
na ule wa kutimiza kitakatifu majukumu mbalimbali ya kipadri. Kutokana na amri
kuu anapaswa kuyatimiza vizuri zaidi na zaidi, kadiri upendo unavyostawi hadi
kufa kwake.
Upadirisho unadai, sio tu hali ya neema ya utakaso na vipaji vya pekee, bali mwanzo wa ukamilifu, maisha bora kuliko yanayotakiwa kwa mtu anayeingia utawani. Kwa kuwa padri anapaswa kuwaangaza wengine, inafaa awe katika hatua ya mwanga. Tena matokeo ya upadirisho ni alama isiyofutika ambayo inamshirikisha moja kwa moja ukuhani wa Kristo, pamoja na neema ya sakramenti inayomwezesha kutimiza kazi za kipadri inavyomfaa mtumishi wa Kristo. Hiyo neema ya sakramenti inatimiliza neema ya utakaso na kumpa padri haki ya kupokea misaada inayohitajika ili atimize kitakatifu zaidi na zaidi matendo ya kipadri. Ni kama sehemu ya sura ya Kiroho ya padri, ambaye anapaswa kuelewa zaidi na zaidi ukuu na masharti ya upadri wake. Kwa hakika upadirisho ni bora kuliko nadhiri za kitawa, na wajibu maalumu wa kulenga ukamilifu unaotokana nao ni mkubwa kuliko ule unaotokana na nadhiri.
“Umekuwa
padri, umepakwa mafuta ili umtolee Mungu sadaka ya misa. Fanya sasa kwa bidii,
kwa uaminifu, kila wakati inapofaa. Sasa uwe na mwendo mzuri bila ya hitilafu.
Usidhani kwamba u huru kuliko watu wengine, bali umefungwa kifungo cha sheria,
hata imekupasa kutafuta ukamilifu mkubwa zaidi. Ni lazima padri awe mtu
aliyepambwa fadhila zote, kusudi awape watu wengine mfano wa maisha mema.
Mazoea yake siyo waliyozoea watu wa dunia, watu wa chini, bali yafuatana na
malaika wa mbinguni; rafiki zake ndio watu watimilifu walioko duniani”
(Kumfuasa Yesu Kristo, IV,5:2). Kazi za kipadri, kuhusiana na Mwokozi aliomo
katika ekaristi na Mwili wake wa fumbo, zinatuonyesha kuliko upadirisho
wenyewe wajibu wake wa pekee wa kulenga ukamilifu.
Padri
anapoadhimisha misa ni mfano wa yule anayesema kwa niaba yake, yaani Kristo
aliyejitoa kwa ajili yetu. Anapaswa kuelewa ukuu wa kazi yake na kuzidi
kuungana kwa dhati na kuhani mkuu ambaye ni kafara pia. Ni unafiki, au walau
ni uzembe wenye kosa, kupanda altareni bila ya nia imara ya kupanda juu katika
ngazi ya upendo. Mtumishi wa Kristo anapaswa kusema kila siku kitakatifu
zaidi, “Huu ndio mwili wangu… Hiki ni kikombe cha damu yangu”. Kila siku
zaidi komunyo yake inatakiwa kuwa motomoto kwa utashi kuwa tayari kumtumikia
Mungu, kwa sababu ekaristi inatakiwa kukuza upendo ndani mwetu, si kuutunza
tu. “Kwa ukuu wa kazi ambayo padri altareni ni mtumishi wa Kristo, unadaiwa
utakatifu wa ndani ulio mkubwa kuliko ule unaodaiwa na utawa” (mt. Thoma wa
Akwino). Hivyo, mambo yakilingana, tendo dhidi ya utakatifu ni dhambi kubwa
zaidi likitendwa na padri kuliko likitendwa na bradha. “Padri mwenye
kumtolea Mungu sadaka ya misa, humsifu Mungu, huwafurahisha malaika,
huthibitisha Kanisa, husaidia walio hai, hutuliza marehemu, hupewa mwenyewe
neema zote” (Kumfuasa Yesu Kristo, IV,5:3). Anapaswa pia kuadhimisha Sala ya
Kanisa kwa makini na ibada halisi. Sala hiyo kuu inatangulia na kufuata misa;
ni wimbo wa bibi arusi wa Kristo kwa usiku na mchana, hivyo ni heshima kubwa
kuhusika nao. Tusali hivyo tukizingatia nia kuu za Kanisa, kama vile
kupatanisha ulimwengu kwa kueneza utawala wa Mungu.
Hatimaye
padri ana wajibu wa pekee wa kulenga ukamilifu ili atimize vizuri kazi zake
kwa ajili ya Mwili wa fumbo wa Kristo. “Hakuna kinachofaa zaidi kuwaongoza
waamini kwenye ibada halisi kuliko mfano mwema wa padri. Macho ya watu
yanamuelekea yeye, kama kioo cha ukamilifu ambao waige. Kwa hiyo, basi,
anatakiwa kupanga maisha yake, sura yake ya nje, mwendo wake na, matendo yake
hivi kwamba adumishe daima uzito, utaratibu na tabia ya kidini ambavyo
anapaswa kuwa navyo” (Mtaguso wa Trento). Padri wa ulimwenguni halazimiki
kuweka nadhiri ya ufukara, lakini anatakiwa kutoshikamana na malimwengu kwa
kuwa radhi kuwapa maskini; anatakiwa pia kumtii askofu wake na kuwa kama
mtumishi wa waamini, bila ya kujali matatizo na pengine masingizio anayoweza
akakabiliana nayo.
Haja
ya ukamilifu huo ni wazi kuhusu mahubiri, maungamo na uongozi wa Kiroho. Ili
mahubiri yawe hai na kuzaa matunda, ni lazima padri aseme “yaujazayo moyo
wake” (Math. 12:34). Tena mt. Thoma wa Akwino alisema yanatakiwa “kutokana
na utimilifu wa sala ya kumiminiwa”, na imani hai yenye kupenya na kuonja
fumbo la Kristo, thamani isiyo na kifani ya misa, ya neema ya utakaso na ya
uzima wa milele. Padri anapaswa kuhubiri kama mwokozi wa roho, akifanya kazi
mfululizo kwa wokovu wa wengi. Hatakiwi kuwa amepokea upadri bure. Ni vilevile
kuhusu huduma ya kitubio na uongozi wa Kiroho. Padri anapaswa kuwa mtu
mwangavu na motomoto, la sivyo huduma hiyo inaweza kuwa hatari kwake na
kumpotosha mwenyewe, badala ya kuokoa watu. Maisha yasipopanda juu,
yanateremka chini; ili yasiteremke ni lazima yapande juu kama mwali wa moto.
Hasa hapa inafaa kusema: asiyesonga mbele, anarudi nyuma. Hatimaye, wanaweza
wakamuelekea padri watu ambao Mungu anawadai zaidi; ni lazima wakute kwake
msaada wa hakika kwa kufuata njia nyofu ya utakatifu; haifai waende mbali naye
pasipo kupata chochote toka kwake.
Mh.
Antoni Chevrier alikuwa akiwafundisha mapadri aliowalea wawe daima na pango,
Kalivari na tabenakulo machoni mwao. Pango
liwakumbushe ufukara; padri
anapaswa kuwa fukara katika nyumba yake, mavazi yake na chakula chake.
Anapaswa kuwa mnyenyekevu kwa Mungu na kwa watu. Kadiri alivyo hivyo
anamtukuza Mungu na kumfaa jirani. Padri
ni mtu asiye na kitu. Kalivari imkumbushe haja ya kujitoa
sadaka, kujifisha kuhusu mwili wake, roho yake, matakwa yake, heshima
yake, familia yake na ulimwengu. Anapaswa kujitoa sadaka kwa kimya, kazi,
malipizi, mateso na kifo. Kadiri padri alivyokwishakufa hivyo anao uzima ndani
mwake na kuwashirikisha wengine. “Padri
ni msulubiwa. Kwa mfano wa Mwalimu anapaswa kwa upendo kujitoa mwili,
roho, muda, mali, afya, uhai; anapaswa kutoa uhai kwa imani yake, mafundisho
yake, maneno yake, sala zake, athari yake, mifano yake. Anapaswa kuwa mkate
mtamu. Padri ni mtu wa kuliwa”. Tabenakulo imkumbushe upendo anaopaswa kuwa nao.
Ndicho
kipeo cha upadri ambacho kila mmoja awe nacho: “Nimewapa kielelezo; ili kama
mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh. 13:15).
Kisha
kusema juu ya ukamilifu wa Kikristo, tunapaswa kuzungumzia tofauti iliyopo
kati ya hatua tatu za maisha ya Kiroho; hilo ni mojawapo katika maswala makuu
ya fani hiyo. Hatua hizo zinaitwa za wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika;
au za utakaso, mwanga na muungano. Tofauti na wanateolojia kadhaa wa karne za
mwishomwisho, walimu wakuu wa maisha ya Kiroho waliamini watu
wowote wanaweza kutamani na kujiombea kwa unyenyekevu neema ya kuzama katika
mafumbo ya imani, ambayo yote yanadhihirisha wema wa Mungu usio na mipaka.
Waliona huko kuzama katika sala ni kwa lazima kwa muungano wa ndani na Mungu
ulio ukamilifu wa Kikristo. Kwa msingi huo walifafanua kila hatua ya maisha ya
Kiroho.
Tutataja
madondoo machache tu yaliyo muhimu zaidi, baada ya yale mengi tuliyokwishatoa.
Katika Injili, hasa kadiri ya heri nane, tumeona ukuu wa ukamilifu wa Kikristo
tusioweza kuupata tusipofisha yale yote yasiyofaa ndani mwetu, tusipobeba
msalaba kwa uvumilivu, tusipomuomba Baba aliyefichika moyoni mwetu,
tusipomsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu kila anapotuangaza, ili kwa msaada
wake wa pekee tuzame kwa upendo katika mafumbo ya wokovu.
Mt.
Paulo aliandika yanayofaa kwa kawaida kwa hatua ya waliokamilika: “Iko
hekima tusemayo kati ya wakamilifu…twanena hekima ya Mungu katika siri,
ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu
wetu... Mambo ambayo jicho halikuyaona, wala sikio halikuyasikia, wala
hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia
wampendao… ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata
mafumbo ya Mungu” (1Kor. 2:6-10). Ndiyo yanayotazamwa na waliokamilika
wanaposali. “Kwa hiyo nampigia Baba magoti… awajalieni,
kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa
imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae
mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina
na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote
jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate
kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef. 3:14-19). Ndiyo sifa maalumu ya
hatua ya waliokamilika: kujaliwa kuzama katika fumbo la Kristo na kuungana na
Mungu kutokana nako.
Katika maisha ya mitume, waliolelewa
na Bwana moja kwa moja, kuna hatua tatu
tofauti zinazolingana na zile za maisha ya Kiroho. Hatua ya kwanza ya
maisha yao ya Kiroho, ambayo ni ile ya wanaoanza, ilichukua tangu
waongoke hadi kwenye mateso ya Bwana, ambapo walipitia shida kubwa hata
mt. Petro akamkana Mwalimu wake. Halafu akajuta, na ndio wongofu wake wa pili,
katika ule utakaso wa Kimungu uliokuwa kama usiku wa giza na mateso. Kitu cha
namna hiyo kiliwatokea mitume wengine pia walipojaliwa kughairi baada ya
kukimbia. Hatua ya pili ya maisha yao ya Kiroho, ambayo ni ile ya
wanaoendelea, ilichukua kuanzia Mateso
hadi Pentekoste. Kipindi hicho walikuwa bado waoga, imani yao ilihitaji
kuangazwa, tumaini lao lilihitaji kuimarishwa, nao upendo wao haukuwa bado na
ari ile uliyopaswa kuwa nayo. Hatua hiyo ilitimia kwa kuondolewa uwepo wa
kimwili wa Bwana alipopaa mbinguni. Hapo walipaswa kuendelea kwa imani tupu,
wakikabili dhuluma walizotabiriwa. Hatua ya tatu iliwaanzia Pentekoste,
ambayo ikawa kwao kama wongofu wa tatu, utakaso
halisi wa Kimungu na mageuzo yaliyowaingiza katika maisha makamilifu.
Iliangaza akili yao na kuimarisha utashi wao ili wamhubiri popote Yesu
msulubiwa. Sifa maalumu ya hatua hiyo ni kuzidi kuungana kwa ndani na Mungu,
kujitoa sadaka kikamilifu hadi kufia dini. Hapo mbele tutazirudia hatua zao
hizo ambazo kila moja inaanza
na wongofu au mageuzo ya roho. Tukizitafakari zinaangaza kweli hatua tatu za
maisha ya Kiroho. Maelekezo hayo ya Maandiko yanathibitishwa na Mababu wa
Kanisa.
Tuone
kwanza ushuhuda wa Mababu wa Mashariki.
Mt. Inyasi wa Antiokia aliandika
mara nyingi juu ya uwepo wa Kiroho wa Mwokozi ndani ya waamini, akiwaita
waleta-Kristo au waleta-Mungu na kuwahimiza hivi: “Tufanye tendo letu lolote
kwa kuzingatia kwamba Mungu anaishi ndani mwetu; hivyo tutakuwa mahekalu yake,
naye atakuwa Mungu wetu mwenye kukaa ndani mwetu”. Mwenyewe alitamani kuishi
kwa kuungana na Kristo zaidi na zaidi, na kufa ili kuungana naye milele. Barua
zake zimejaa ujuzi wa juu wa Kristo, imani hai yenye kupenya ambayo si tofauti
na sala ya kumiminiwa na ambayo inafurika katika utendaji wa kitume wenye
matunda mengi kutokana na upendo mkubwa. Lakini ili kufikia muungano huo wa
dhati ni lazima kujidharau pamoja na yale yote ambayo hayafai ndani mwetu na
ambayo yanafisha uzima wa Kimungu. Upande wake alitamani kusagwa na meno ya
simba awe unga wa ngano wa Kristo, kama vile Yesu alivyosagwa awe mkate wetu
wa ekaristi.
Mt.
Irenei alisisitiza binadamu akubali kufinyangwa na Mungu kama udongo mikononi
mwa mfinyanzi. Badala ya kupinga au kukwepa kazi hiyo, azidi kujionyesha
mtulivu kwa Roho Mtakatifu katika sala na hivyo atafikia upimaji wa Kiroho wa
mambo yote na kuishi kwa upendo wa Mungu tu.
Klementi
wa Aleksandria alieleza roho inavyopanda juu kupitia hali zifuatazo: kwanza uchaji wa
Mungu, halafu imani na tumaini, hatimaye upendo na hekima. Waliokamilika wana
amani na kutawaliwa na upendo; wamejaliwa hekima ya siri ya Mungu, ujuzi wa
dini ambao unatokana na mwanga wa Roho Mtakatifu kwa roho sikivu na kugeuza
maisha yao ya ndani kwa kuwafanya marafiki wa Mungu.
Sawa
naye, mwanafunzi wake Origenes alisema
kuwa aliyekamilika anaishi hasa kwa upendo na kwa kawaida anapokea kwa Roho
Mtakatifu hekima ya kujaliwa, ujuzi wa ndani wa fumbo la Utatu mtakatifu.
Kuhusu Injili ya Yohane aliandika, “Hakuna anayeweza kuelewa maana ya Injili
kama hajaegama kifuani pa Yesu wala hajapokea kutoka kwake mama Maria awe mama
yake pia”. Neno ndiye anayejifunua kwa waliokamilika na kuwaunda kama
alivyowaunda mitume. Mwenyewe alitofautisha wazi hatua tatu: ile ya wanaoanza,
ambao ndani mwao maono yasiyofaa yanapungukiwa nguvu; ile ya wanaoendelea,
ambao ndani mwao maono hayo yanaanza kuzimika kwa wingi wa neema; hatimaye ile
ya waliokamilika. Alihimiza usikivu kwa Roho Mtakatifu, ambaye kwa njia yake
tunaweza kumuendea Kristo na kwa njia yake tena tunapanda juu kwa Baba, katika
sala ya kumiminiwa inayosaidiwa na upweke.
Didimo
Kipofu alimualika kila Mkristo kuungana kikamilifu na Kristo, Bwanaarusi wa
roho iliyotakata.
Mt.
Bazili katika Kanuni zake alipanga maisha ya Kiroho imara yanayoandaa kwa sala
ya kumiminiwa na muungano na Mungu. Kutakata zaidi na zaidi ni sharti la
kuungana naye katika sala ya kumiminiwa: “Jicho la roho, kisha kuwa safi
pasipo kivuli, linatazama mambo ya Mungu kwa mwanga ambao unatoka juu na
kuijaza kwa wingi usiishibishe… Kisha kustahimili mapigano masumbufu sana na
kufaulu kuiokoa roho – iliyoambatana sana na mwili – katika mchanganyiko
wa maono, inakuwa ya kufaa kwa kuongea na Mungu… Aliyefikia hali hiyo
hatakiwi tena kukubali mvuke wa maono ya kidunia uchafue na kufunika kwa
ushungi macho ya roho yake na hivyo kuifanya ikose sala ya kumiminiwa ya
Kiroho na ya Kimungu”.
Mt.
Gregori wa Nazienzi alisema kuwa Mungu ni mwanga halisi tusioweza kuupata
tusipokuwa wenyewe mwanga na kutakata ili kupanda kutoka uchaji wa Mungu
kwenda hekima. Katika waandishi hao wote tunakuta majina haya matatu: utakaso,
mwanga na muungano.
Mt.
Gregori wa Nisa alionyesha tunavyopaswa kujitenga na viumbe na kuishi kwa Kristo ili
tukaribishwe kutazama umungu na kuungana nao. Ushindi huo juu ya adui
unapatikana kwa njia ya msalaba tu, na kwa kujitakasa zaidi na zaidi katika
mambo yote ya hisi. Ukamilifu unaifanya roho iwe bibiarusi wa Kristo.
Hata
mt. Efrem aliona kwamba sala ya kumiminiwa, tunayojaliwa kwa kuwa
wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ndiyo fadhili ya maisha makamilifu.
“Tutakapokuwa tumeshinda maono yetu, na kuangamiza ndani mwetu mapenzi
yoyote ya kimaumbile, na kuondoa kabisa rohoni mwetu hangaiko lolote
lisilosaidia wokovu, hapo Roho Mtakatifu, kwa kuikuta roho yetu katika
utulivu, na kuishirikisha akili yetu uwezo mpya, atatia mwanga mioyoni mwetu,
kama inavyowashwa taa iliyo tayari kwa utambi na mafuta… Basi, kabla ya
yote, tuandae roho zetu kupokea mwanga wa Kimungu, ili tustahili zawadi za
Mungu”.
Kwa
Dyonisi utakaso unaandaa kumjua Mungu kwa dhati; mwanga
unashirikisha ujuzi huo; hatimaye utakatifu unafanya uchanue kikamilifu. Hatua
ya muungano inahusu mafumbo na ni utangulizi wa uzima wa milele.
Mt.
Masimo alifafanua mafundisho hayo akitofautisha hatua tatu za sala,
zinazohusiana na hatua tatu za upendo. “Sala ya kawaida ni kama mkate:
inawatia nguvu wanaoanza; ikiongezewa neema ya kuzama kidogo katika mafumbo,
inakuwa kama mafuta tunayojipaka; hatimaye, tukizama kabisa ni kama divai tamu
mno inayolevya wanaoinywa hata wakajisahau… Kuzama katika sala kunatokana na
mwanga wa Roho Mtakatifu… Aliyetakata anaangazwa na kustahili kuingia ndani
kabisa mwa hekalu na kufurahia muungano na Neno”. Mwenyewe alionyesha
majaribu makali ambayo wanasala wanapaswa kuyapitia ili kutakaswa moja kwa
moja na kuthibitishwa katika upendo wa Mungu.
Hatimaye
mt. Yohane wa Damasko aliandika,
“Aliyefikia kiwango cha juu kabisa cha upendo, kama kwa kutoka nje ya nafsi
yake, anamvumbua Yule asiyeonekana; akiruka juu ya wingu lile la hisi
linalozuia macho ya roho yasione. Akidumu katika amani, anamkazia macho Jua la
Haki na kufurahia tamasha hilo asiloweza kulikinai… Kufikia kumtazama Mungu,
kisha kutekeleza kwa bidii maadili, ni hazina isiyonyang’anyika kamwe”.
Basi,
kadiri ya Mababu wa Mashariki, huko kuzama katika mafumbo ya Kimungu,
kunakotokana na kipaji cha hekima, ni kwenye njia ya kawaida ya utakatifu.
Mwanzo wake ni hatua ya wanaoendelea, halafu kunaendana kwa kawaida na upendo
wa waliokamilika.
Mababu
wa Kilatini wametuachia mafundisho hayohayo.
Mt.
Augustino alitofautisha ngazi mbalimbali, akisisitiza vita dhidi ya dhambi
(vilivyo kazi ngumu ya utakaso), vinavyofuatwa na mwanga kwa waliotakata, na
hatimaye na muungano na Mungu. Halafu akaelekeza safari ya roho kupanda kwa
Mungu kufuatana na vipaji vya Roho Mtakatifu: uchaji wa Mungu ndio kidato cha
kwanza, na hekima ndiyo kilele. Kati ya hivyo viwili alibainisha vipindi
viwili vya maandalizi yenye kutakasa. Alikiita kile cha mbali “maisha ya
utendaji”, yaani utekelezaji wa maadili ya kibinadamu yanayohusiana na
vipaji vya ibada, nguvu, elimu, shauri; halafu kile cha karibu “maisha ya
sala ya kumiminiwa”, yaani utekelezaji bora wa maadili ya Kimungu na wa
vipaji vya akili na hekima katika roho zilizo tulivu na sikivu kwa neema. Hapo
imani ni chanzo cha kuzama katika mafumbo, na upendo motomoto unaunganisha kwa
dhati roho na Mungu: ndiyo sala ya kumiminiwa.
Mt.
Yohane Kasiano alionyesha kuwa hapa duniani mwisho wa maisha ya Kiroho ni kumtazama
Mungu, ambako upendo kwake unatekelezwa kikamilifu. Tunapaswa kujiandaa
kufikia huko kwa njia ya kusali ili tusamehewe dhambi, kutekeleza maadili na
kutamani upendo wa kuwaka zaidi. Hapo sala inakuwa “yote ya moto” kutokana
na “kumtazama Mungu tu na kuwaka kwa upendo motomoto… Hivyo roho katika
chungu ya udongo inaanza kuonja malimbuko ya utukufu inaotumainia mbinguni”.
Mt.
Gregori Mkuu alikubali kugawa maisha ya Kiroho katika ngazi tatu: mapambano na
dhambi, maisha ya utendaji au utekelezaji wa maadili, na maisha ya sala ya
kumiminiwa ambayo yanahitajiwa na wahubiri wa Neno la Mungu na wale wanaotaka
kuufikia ukamilifu. Kwake matendo yote yanakosa ukamilifu mpaka roho ziwe
zimeangazwa na sala ya kumiminiwa kutoka juu. Ndio kikomo cha juhudi, tunda la
neema maalumu na utekelezaji wa kipaji cha hekima. Ni hali ya kujaliwa kuzama
katika mafumbo ambayo mtu ajiandae kuipokea kwa unyenyekevu, usafi wa moyo na
kukusanya mawazo karibu mfululizo. Mwenyewe alionyesha matakaso machungu
ambayo “yanakausha ndani mwetu kila aina ya mapenzi ya kihisi” na
kutuandaa tuzame katika sala na kuungana na Mungu, ambapo tunakuta nguvu kubwa
katika majaribu na upendo motomoto.
Mtakatifu
Thoma wa Akwino amefananisha hatua tatu za maisha ya Kiroho na zile za maisha
ya kimwili: utoto, ujana na utu uzima. Ni mfano unaostahili tuuzingatie kwa
kuangalia vipindi vya mpito kati ya hatua moja na nyingine.
Inakubalika
kuwa sehemu ya kwanza ya utoto inakwisha akili inapochangamka kwenye umri wa
miaka saba hivi, halafu inafuata sehemu ya pili inayodumu mpaka ubalehe,
kwenye miaka kumi na nne hivi. Ujana unaenea kati ya miaka hiyo na ishirini.
Halafu unafuata utu uzima, ambamo tunatofautisha kipindi kinachotangulia
ukomavu kamili na kile kinachoufuata kwenye miaka thelatini na tano hivi,
kabla ya kuanza mteremko wa uzee.
Namna
ya kuwaza inabadilika pamoja na mwili. Mtoto anafuata ubinifu na hisi; hajajua
kufanya utambuzi na kupanga, na hata akili inapoanza kuchangamka inaendelea
kutegemea mno hisi. Mtu anapobalehe anabadilika si kimwili tu, bali pia
kinafsi, kiakili na kiadili: haridhiki tena na ubunifu, bali anaanza
kutafakari maisha na haja ya kujiandaa kufanya kazi fulani. Kipindi hicho cha
mpito, kinachoitwa pengine umri usio na shukrani, hakikosi matatizo; ndipo
tabia adili inapoundika au inaharibika; pengine mtu anabaki nyuma, bila ya
msimamo, akiwa tofauti na kawaida. Mfano huo unaangaza maisha ya Kiroho ambamo
aliyeanza asipokuwa kwa wakati wake mtu anayeendelea, basi ama anaelekea maovu
ama anabaki nyuma na kuwa vuguvugu, aina ya mbilikimo upande wa roho.
“Kutotaka kusonga mbele ni kurudi nyuma” (mt. Bernardo), kumbe kulenga
ukamilifu moja kwa moja ni kuwa nao tayari kwa namna fulani.
Ikiwa
ubalehe ni kipindi kigumu upande wa mwili na wa maadili, ni kigumu vilevile
kile cha uhuru wa kwanza kinachomuingiza kijana kwenye utu uzima. Akimaliza
kukomaa kimwili anapaswa kuanza kushika nafasi yake katika jamii. Sawa na
mwana mpotevu, wengi wanapita vibaya kipindi hicho, wakichanganya uhuru
wanaoachiwa na idhini ya kutenda lolote. Kinyume chake, anayekomaa
inavyotakiwa na kushika njia nzuri, anajihusisha na mambo yake binafsi, ya
familia na ya jamii kwa namna bora kuliko kijana, akiyazingatia kwa upana
zaidi. Inatokea karibu hivyo katika maisha ya Kiroho kwa mtu anayeendelea:
namna yake ya kuwaza inainuka na kuwa ya Kiroho zaidi na zaidi; anazidi kuona
vizuri mambo ya ufalme wa Mungu au maisha ya Kanisa kuhusiana na uzima wa
milele.
Katika
hatua tatu za maisha ya Kiroho “kuna viwango mbalimbali vya upendo kulingana
na majukumu mbalimbali ambayo ustawi wa upendo unamdai mtu ayachukue. La
kwanza ni kukwepa dhambi na kushinda
mivuto ya tabia mbovu inayopingana na mivuto ya upendo: ndilo jukumu la wanaoanza,
ambao ndani mwao upendo unatakiwa kulishwa na kutunzwa usije ukapotea.
Hapo linakuja jukumu la pili: mtu anapaswa hasa kukesha
na kukua katika uadilifu, jambo linalowafaa wanaoendelea
ambao kazi yao hasa inalenga upendo uimarike kwa kustawi ndani mwao.
Jukumu la tatu la mtu ni kujitahidi hasa
kuungana na Mungu na kumfurahia: ndilo linalowafaa waliokamilika, wanaotamani kwenda zao wakae na Kristo (taz. Fil.
1:23)” (mt. Thoma wa Akwino).
Ni
muhimu tuongeze kuhusu mpito kati ya hatua na hatua. Kama vile kati ya utoto
na ujana kuna kipindi kigumu cha ubalehe, vilevile kuna kipindi cha namna hiyo
katika kuvuka toka hatua ya utakaso ya wanaoanza kwenda hatua ya mwanga ya
wanaoendelea. Hapo mtu aliyeanza kwa bidii yuko hatarini kwa kukwama katika
kasoro kadhaa asizozitambua, hasa kwa kuishia kwenye faraja za kihisi katika
sala; basi anaachishwa hizo ili kuingizwa katika njia ya Kiroho isiyotegemea hisi, ambapo katika ukavu anajaliwa
mwanzo wa sala ya kumiminiwa ili asonge mbele.
Ndivyo
alivyoeleza mt. Yohane wa Msalaba, “Usiku au utakaso wa Kimungu wa hisi
unaipatia roho usafi wake ukiivua upande wa hisi na kuulinganisha na upande wa
roho… Ni jambo la kawaida,
linalowatokea wanaoanza walio wengi”. Hapo wanakuja kutambua kwamba, ili
wakue katika upendo, wanapaswa kuwa maskini rohoni, kujinyima aina zote za
upuuzi, majivuno, kiburi na ulafi wa roho. “Hayo makao ya hisi yanapopata
kutulia hivyo, kwa maono kuratibiwa, tamaa mbaya kuzimwa, hamu kutulizwa na
kulala usingizi katika usiku wa utakaso, ndipo roho inapoweza kutoroka
iwajibike katika njia ya Kiroho. Inaanza kuwa miongoni mwa wanaoendelea,
na kujikuta katika hatua inayoitwa ya
mwanga. Ndipo Mungu anapolisha na kuimarisha roho kadiri anavyopenda kwa sala
ya kumiminiwa, pasipo roho kuichangia kwa mafuatano ya maneno, kwa msaada
wa utendaji au kushiriki kwake katika kazi hiyo” (walau kwa kawaida).
Mbele
zaidi alieleza kasoro maalumu za wanaoendelea: ushamba wa kimaumbile, haja ya
kujitokeza, kujiamini kipumbavu na kiburi cha chinichini. Hizo zinaonyesha
wanavyohitaji utakaso wa Kimungu wa roho
ili kuingia hatua ya waliokamilika. Jaribu
hilo ni kipindi kigumu kama kile kinachotokea katika maisha ya kawaida, kijana
anapoanza kutumia uhuru wake pengine kwa hasara yake mwenyewe.
Mt.
Yohane wa Msalaba ametufafanulia sheria
za juu za uzima wa neema zinazotimia kwa wale wanaosonga mbele kwa bidii
wasigeuke nyuma. Tukisoma kwa makini maisha ya watumishi wa Mungu, tunaona
katika matatizo yao utakaso huo wa kina wa hisi na wa roho ambao hatimaye
ukaweka utu wao wote chini ya Mungu. Mtakatifu
huyo alieleza vizuri kuliko wote vipindi
hivyo viwili vigumu vya mpito kutoka hatua moja hadi nyingine, akiviita
kwa haki matakaso ya Kimungu ya hisi na
roho. Hayo yanalingana na maumbile ya binadamu (yenye sehemu mbili, yaani
mwili na roho), tena na mfumo wa neema ya utakaso, mbegu ya uzima wa milele,
inayotakiwa kuhuisha zaidi na zaidi vipawa vyote tulivyonavyo na kuangaza
tendo letu lolote mpaka undani wa roho
utakate umimi wowote (kujipendea kwa kujitambua au la) uwe kweli wa Mungu tu.
Kwa
muhtasari ni kwamba katika wale wanaoanza, pamoja na kiwango
cha kwanza cha upendo, yanaonekana
maadili chipukizi yaani viwango vya kwanza vya upole, subira, usafi wa
moyo na unyenyekevu. Kujishinda kwao
kwa ndani na kwa nje kunazidi kuwaepusha na dhambi nyepesi za makusudi, au
kunawaongoza kuinuka mara kutoka dhambi ya mauti ikiwa wameiangukia. Upande wa
sala, wana sala ya midomo, kutafakari
kwa mafuatano ya mawazo ambako kunaelekea kugeuka sala nyofu ya mapenzi.
Ndani mwao vipaji vya Roho Mtakatifu
vinaanza tu kujitokeza, bado vikifichikafichika: mara mojamoja wanapata
miangaza yake ya pekee, lakini hawajawa tayari kufaidika nayo. Usikivu kwa
Roho Mtakatifu unaendelea kuwa dhaifu; mtu anatambua zaidi utendaji wake
mwenyewe na kulazimika mara nyingi kukiri umaskini wake katika kipindi kigumu cha ukavu wa hisi, utakaso mchungu wa Kimungu ambao
unastahimiliwa vizuri au kiasi na unaashiria kuvukia hatua ya mwanga.
Katika
wale wanaoendelea, pamoja na kiwango cha
pili cha upendo, yanaonekana maadili
imara, hasa upole, subira, unyenyekevu halisi zaidi unaoelekeza kuwa wema
kwa jirani, na roho ya mashauri matatu ya Kiinjili. Pamoja na hayo, vipaji
vya Roho Mtakatifu vinaanza kuonekana, hasa vile vitatu vya chini, yaani
uchaji, elimu na ibada. Mtu ni msikivu zaidi, na kufaidika zaidi na mianga ya
ndani. Hapo akijitahidi kweli, kwa kawaida inaanza sala
ya kumiminiwa kwa tendo mojamoja la kuzama katika sala wakati wa kukusanya
mawazo kwa hiari; halafu, akiwa mwaminifu, zinafuata polepole sala ya kujaliwa
kukusanya mawazo, sala ya utulivu (mkavu au wenye faraja), ambapo ni wazi
mchango wa kipaji cha ibada kinachotufanya tulie, “Aba! Yaani, Baba!”
(Rom. 8:15; Gal. 4:6). Ndipo maongezi na nafsi yetu yanapogeuka kuwa kweli
maongezi na Mungu. Hapo mtu, akijitahidi, anaona
ndani mwake kasoro za kiburi kinachofichika,
utovu wa wema kwa jirani, pengine ukali, utovu wa ari kwa wokovu wa watu wengi
wanaopotea; kasoro hizo zote hakuziona mwanzoni, nazo zinahitaji
utakaso mwingine wa Kimungu, ule wa roho.
Katika
wale waliokamilika, pamoja na kiwango
cha tatu cha upendo, ingawa wana kasoro kadhaa zisizo za hiari kabisa,
tunashuhudia walivyo na maadili ya hali
ya juu na pengine ya kishujaa: upole mkubwa, subira inayoyumbishwa kwa
nadra tu, unyenyekevu mkuu usioogopa dharau bali unapenda kudhalilishwa, imani
kubwa inayofanya waone mambo yote kutoka juu, tumaini kubwa kwa Mungu, moyo
mkuu unaolenga mambo makuu ingawa yanaendana na vizuio na kushindwa, halafu
kujiachilia kikamilifu katika matakwa ya Mungu ambayo
hali yetu ya kesho na ya milele inayategemea. Roho ni kama inatawaliwa na Roho Mtakatifu anayeiongoza kutekeleza maadili
kikamilifu zaidi. Vipaji vya akili na
hekima vinaonekana kwa namna wazi na
mara nyingi zaidi. Kwa kawaida ndipo inapojitokeza sala ya kumiminiwa ya
muungano. Hatimaye undani wa roho umetakata, na vipawa vyote vya maumbile vipo
moja kwa moja chini ya Mungu aliomo katika hekalu la ndani kama utangulizi wa
heri isiyo na mwisho kamwe.
Tunaweza kuonyesha hayo maendeleo ya Kiroho kwa jedwali ifuatayo, ambayo isomwe kuanzia chini kwenda juu.
|
VIWANGO
VYA UPENDO |
MAADILI |
VIPAJI |
MATAKASO |
SALA |
MAKAO
YA MT. TERESA |
|
WALIOKAMILIKA Hatua
ya muungano Maisha
ya mafumbo |
Maadili
ya juu na ya kishujaa: kiwango cha 3° cha upendo, unyenyekevu kamili,
imani kubwa, kujiachilia kwa Mungu, subira inayoyumbishwa kwa nadra tu. |
Vipaji
vya juu kuonekana vizuri na mara nyingi zaidi. Roho ni kama inatawaliwa
na Roho Mtakatifu. Mtu anamuacha atende tu, lakini mwenyewe haachi
kutekeleza maadili. |
Utakaso
wa Kimungu wa roho hasa chini ya kipaji cha akili (ambapo majaribu
yanaongozana na vipaji vya nguvu na shauri vinajitokeza): kuingia hatua
ya muungano. |
Sala
za kujaliwa ya muungano wa kawaida, ya muungano kamili (pengine kwa
kutoka nje ya nafsi), ya muungano unaotugeuza, chini ya kipaji cha
hekima kinachostawi (fadhili zinaongozana). |
5°,
6° na 7° |
|
WANAOENDE LEA Hatua
ya mwanga Kizingiti
cha maisha ya sala hasa |
Maadili
imara: kiwango cha 2° cha upendo, utiifu, unyenyekevu mkubwa, roho ya
mashauri ya Kiinjili. |
Vipaji
vya Roho Mtakatifu kuanza kuonekana, hasa vile vitatu vya chini (uchaji,
elimu na ibada). Mtu anazidi kuwa msikivu na kufaidi mianga ya ndani. |
Utakaso
wa Kimungu wa hisi, hasa chini ya vipaji vya uchaji na elimu (majaribu
yanaongozana): kuingia hatua ya mwanga. |
Zinaanza
sala za kumiminiwa: kuzama mara mojamoja katika mafumbo wakati wa
kujikusanya kwa hiari; halafu sala ya kujaliwa kukusanya mawazo, na ya
utulivu mkavu au wenye faraja. Kipaji cha ibada. |
3°
na 4° |
|
WANAOANZA Hatua
ya utakaso Maisha
ya juhudi |
Maadili
chipukizi: kiwango cha 1° cha upendo, kiasi, usafi, subira, ngazi za
kwanza za unyenyekevu. |
Vipaji
vya Roho Mtakatifu kufichikafichika: mianga ya mara mojamoja, ambayo mtu
hajawa tayari kufaidika nayo. Anatambua hasa utendaji wake mwenyewe. |
Utakaso
wa hiari wa hisi na wa roho, yaani kujishinda kwa nje na kwa ndani. |
Sala
za kujipatia yaani za kujikusanya kwa hiari (sala ya midomo, tafakuri ya
mafuatano ya mawazo, halafu sala ya mapenzi inayozidi kuwa sahili). |
1°
na 2° |
Kati
ya njia kuu za utakatifu zilizotolewa kwa wote, tunapaswa kuhesabu somo la
Kiroho, hasa la Maandiko. Katika sura hii tutalizungumzia, tukionyesha
misimamo inayohitajika ili kufaidika nalo.
Mara
nyingi udanganyifu, uzushi na uhuni vinatokana na maambukizo ya vitabu vibaya,
kumbe “kusoma vitabu vitakatifu ni uzima wa roho” (mt. Ambrosi). Mt.
Jeromu alisimulia jinsi alivyovutiwa na neema ya pekee asome kwa juhudi
Maandiko matakatifu. Alipoanza kutawa, akipenda bado vitabu vya kipagani,
alijiona katika ndoto yuko mbele ya Mungu na kuulizwa kwa ukali yeye ni nani.
Alipojibu kuwa ni Mkristo, Hakimu mkuu akamjibu, “Mwongo wewe, u mfuasi wa
Kikero; kwa sababu hazina yako ilipo, ndipo pia moyo wako ulipo”. Mara
akaagiziwa apigwe mijeledi. “Nilipoamka nilitambua haikuwa ndoto tu, bali
kweli, kwa sababu mabegani nilikuwa na alama za mapigo niliyoyapata. Kuanzia
hapo nimesoma Maandiko matakatifu kwa bidii nyingi zaidi kuliko zile ambazo
kwanza nilikuwa nikisoma vitabu visivyo vya dini”. Kutokana na hayo
tunaelewa aliyomuandikia Eustoki: “Usingizi ukukute tu ukisoma, tena angalia
sana usipatwe na usingizi juu ya kitabu tofauti na Maandiko matakatifu”.
Katika
kitabu gani tutaweza kuchota uzima kuliko katika kile kilichoandikwa na Mungu?
Hasa Injili, maneno ya Mwokozi na matukio ya maisha yake yanatakiwa kuwa
fundisho hai ambalo tulizingatie daima. Yesu alijua namna ya kufanya mambo
makuu yaeleweke kwa wote kutokana na unyofu alioutumia. Tena neno lake
halibaki nadharia tu, bali linaongoza mara kwenye unyenyekevu halisi, upendo
wa Mungu na wa jirani. Katika kila neno tunahisi kuwa hatafuti chochote
isipokuwa utukufu wa Baba aliyemtuma na wokovu wa watu. Turudie daima hotuba
ya mlimani (Math. 5-7) na maneno yaliyofuata karamu ya mwisho (Yoh. 13-17).
Tukiyasoma
maneno hayo ya Kimungu kwa unyenyekevu, imani na upendo, tunakuta ndani yake
neema ya pekee inayotuongoza kuiga kila siku vizuri zaidi maadili ya Mwokozi:
upole wake, subira yake na upendo wake wa kishujaa kwa msalaba. Pamoja na
ekaristi, ndiyo lishe halisi ya watakatifu: Neno la Mungu tuliloletewa na
Mwanae pekee, Neno aliyefanyika mwili. Chini ya maneno yake limefichika wazo
hai la Mungu, ambalo vipaji vya akili na hekima vinatuwezesha kulichimba na
kulionja zaidi na zaidi tukiwa wasikivu.
Baada
ya Injili hakuna kinachotulisha vizuri kuliko Matendo
ya Mitume na Nyaraka zao. Ndiyo
mafundisho ya Mwokozi yaliyotekelezwa na wafuasi wake wa kwanza, walioagizwa
kutulea katika shule yake; ni mafundisho yaliyofafanuliwa kulingana na
mahitaji ya waamini. Maisha ya kishujaa ya Kanisa la mwanzoni, uenezi wake
kati ya matatizo makubwa, yale yote yanayoelezwa na Matendo
ya Mitume ni fundisho la kumtumainia Mungu na kujiaminisha kwake. Tutaona
wapi kurasa zenye undani na uhai kuliko zile za Nyaraka kuhusu nafsi na kazi za Kristo (taz. Kol. 1), uangavu wa
maisha ya Kanisa na ukuu wa upendo wa Mwokozi kwake (taz. Ef. 1-3), kujaliwa
uadilifu kwa njia ya kumuamini Kristo (taz. Rom. 1-11), ukuhani wa milele wa
Yesu (taz. Eb. 1-9)? Halafu tukizingatia sehemu za maadili za Nyaraka, tutaona
wapi mahimizo ya nguvu zaidi kwa ajili ya upendo, uwajibikaji, udumifu,
subira, utakatifu, pamoja na kanuni za mwenendo kuhusu wowote – wakubwa,
watu wa hali moja, wadogo – na kuhusu watu dhaifu, wakosefu, walimu wa
uongo? Tutaona wapi maelezo hai zaidi kuhusu wajibu wa Wakristo wote kwa
Kanisa?
Katika
Agano la Kale kila Mkristo anapaswa kujua hasa Zaburi,
ambazo zinadumu kuwa sala ya Kanisa.
Tukirudia
kusoma mfululizo, kwa heshima na upendo, Maandiko matakatifu, tutakuta ndani
yake mwanga na nguvu mpya daima. Mungu amelitia neno lake uweza usioisha, nasi
tukisha kusoma vitabu vingi na kuvikinai karibu vyote, hatimaye tutairudia
Injili kama utangulizi wa mwanga wa milele.
Baada
ya Biblia, vitabu vya Kiroho vya watakatifu ndivyo vinavyotuangaza na
kutuwasha zaidi. Ingawa havikuandikwa kwa uvuvio ule usioweza kukosea, hata
hivyo vimeandikwa kwa mwanga na mpako wa Roho Mtakatifu.
Haifai
kutojua vitabu bora vya watakatifu Augustino, Jeromu, Yohane Kasiano, Leo
Mkuu, Benedikto, Gregori Mkuu, Bazili na Yohane Krisostomo, halafu Dyonisi na
mt. Masimo Muungamadini.
Inafaa
kujua yanayohusu maisha ya Kiroho katika maandishi ya watakatifu Anselmi na
Bernardo, Richard wa mt. Viktori, watakatifu Alberto Mkuu, Thoma wa Akwino,
Bonaventura, mh. Anjela wa Foligno Yohane Thauler, mh. Henri Suso, mt.
Katerina wa Siena, Yohane Ruysbroeck, pamoja na Thomas wa Kempis anayedhaniwa
kuwa mwandishi wa Kumfuasa Yesu Kristo.
Kati
ya waandishi wa karne zilizofuata, inafaa kusoma vitabu vya Fransisko wa
Osuna, mt. Inyasi wa Loyola, Luis wa Blois, watakatifu Teresa wa Yesu na
Yohane wa Msalaba, Luis wa Granada, mt. Fransisko wa Sales, Luis Lallemant,
Yohane Olier, watakatifu Visenti wa Paulo na Yohane Eudes, Yakobo B. Bossuet,
mt. Luis Maria Grignion de Montfort, Petro Caussade, na mt. Alfonsi Maria wa
Liguori.
Hatuwataji
waandishi wa karne za mwishomwisho, ambao walio muhimu zaidi wanajulikana na
wote, hasa mt. Teresa wa Mtoto Yesu.
Tunapaswa
kuongeza juu ya usomaji wa maisha ya watakatifu, ambayo daima yanavutia na
mara nyingi yanawezekana kuigwa. Vitabu vya namna hiyo vinatueleza
walivyotenda, katika nafasi pengine ngumu, wanaume na wanawake wenye maumbile
sawa na ya kwetu, ambao mwanzoni walikuwa na kasoro na udhaifu sawa nasi,
lakini polepole neema na upendo vikaja kushinda maumbile kwa kuyaponya,
kuyainua na kuyatia uzima mpya. Hasa ndani mwao tunaweza kuona maana halisi na
uzito wote wa neno hili: “Neema haiangamizi maumbile (katika mema
yaliyonayo), bali inayakamilisha”. Katika watakatifu, hasa kwenye hatua ya
muungano, maumbile na neema vinalingana kweli.
Katika
maisha yao tunapaswa kuyazingatia hasa yanayoweza kuigwa. Katika yaliyo ya
pekee tuone tu ishara ya Kimungu tuliyopewa
ili tutoke usingizini na kuzingatia yaliyo
ya ndani na ya juu zaidi katika maisha ya Kikristo ya kawaida. Kwa mfano,
mateso ya wenye madonda ya Yesu yanatukumbusha Mateso ya Mwokozi yanapaswa
kuwa nini kwetu na jinsi tunavyotakiwa kusema vizuri zaidi kwenye Njia ya
Msalaba, “Mama mtakatifu, fanya hivi, choma kabisa moyoni mwangu madonda ya
Msulubiwa”. Neema ya pekee iliyowajalia watakatifu kadhaa kunywea katika
donda la Moyo wa Yesu inatukumbusha kila Komunyo inavyopaswa kuwa motomoto na
bora kuliko ile iliyotangulia. Mifano ya watakatifu kuhusu unyenyekevu,
subira, tumaini, upendo usiokoma, inatuvuta kuliko mafundisho ya kinadharia
tutekeleze maadili: “Mawazo hayasukumi”.
Inafaa
zaidi kusoma maisha ya watakatifu yaliyoandikwa na watakatifu, kama vile yale
ya mt. Fransisko wa Asizi yaliyoandikwa na mt. Bonaventura; yale ya mt.
Katerina wa Siena yaliyoandikwa na kiongozi wake, mh. Raimundi wa Capua; na
yale ya akina mt. Teresa yaliyoandikwa na wao wenyewe.
Sala
iliyofanywa vizuri mwanzoni inatupatia neema ya msaada ya kusoma kwa imani, tukikwepa udadisi wowote usio na faida, majivuno ya akili,
elekeo la kuhukumu tunayoyasoma badala ya kufaidika nayo. Imani inatuelekeza
kumtafuta Mungu mwenyewe katika maandishi ya Kiroho.
Badala
ya kuridhika na ujuzi peke yake, tunapaswa kuona namna ya kutekeleza wenyewe, tukiwa na hamu hai tena nyofu ya ukamilifu. Hapo, hata tukisoma yanayohusu
“maadili madogomadogo” (mt. Fransisko wa Sales) tunapata faida kubwa, kwa
kuwa yote yanahusiana na adili kuu la upendo. Waliosonga mbele katika njia ya
ukamilifu, pengine inawafaa warudie kusoma yale yanayowafaa wanaoanza; wataona
yote kwa mwanga wa juu zaidi na kushangaa yaliyofichika ndani yake; k.mf.
katika mistari ya kwanza ya katekisimu ndogo inayohusu malengo ya sisi kuwepo
duniani: “kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu ili kupata uzima wa
milele”.
Vilevile
inafaa wanaoanza wachungulie ukuu wa ukamilifu wa Kikristo, mradi wasidai
kuruka juu kabla hawajapewa neema. Kwa kuwa lengo
la kulifikia ni la mwisho katika hatua za utendaji, lakini ni la kwanza katika nia au hamu: toka mwanzo ni lazima tutake
kufikia utakatifu ule unaotuwezesha kuingia mbinguni mara baada ya kufa.
Hakika, toharani hakuna asiyetenda makosa aliyoweza kuyaepa.
Ikiwa
wanaoanza na wanaoendelea wana hamu kubwa ya utakatifu, watakuta katika
Maandiko matakatifu na katika vitabu vya watakatifu yale yanayowafaa na
watafundishwa na mlezi wa ndani. Lakini ni lazima kusoma
polepole, si kumeza vitabu, bali kupenyezwa na yale tunayoyasoma. Hapo
masomo ya Kiroho yanageuka kuwa sala. Kwa mt. Benedikto kusoma ni kidato cha
kwanza katika ngazi ifuatayo ya kupanda juu: “Lectio (kusoma), cogitatio
(kufikiri), studium (kuzingatia), meditatio (kutafakari), (oratio = kusali),
contemplatio (kutazama)”.
Inafaa
pia turudie kusoma baada ya miaka
vitabu bora vilivyokwishatusaidia. Maisha ni mafupi: turidhike kusoma na
kurudia kusoma yale ambayo kweli yana mhuri wa Mungu, bila ya kupoteza muda
katika masomo yasiyo na uhai wala thamani. Ni afadhali kuchimba kitabu bora
kimojawapo kuliko kusoma kijuujuu vile vyote vya waandishi wa Kiroho.
Halafu
tunatakiwa kusoma kwa roho ya ibada, “kwa
kutafuta sio ujuzi tu, bali ladha hasa” ya mambo ya Mungu (mt.
Bernardo). “Asomaye na afahamu” (Math. 24:15), akimuomba Mungu mwanga ili
aelewe vema. Wanafunzi wa Emau walikuwa hawajaelewa matabiri ya manabii mpaka
Bwana alipowafungua akili zao. Ndiyo sababu mt. Bernardo alisema, “Sala
ikatishe somo”: hapo tu litakuwa lishe ya roho na kuelekeza kusali.
Hatimaye
ni lazima tuanze mara kutekeleza
tunayoyasoma: “Kila asikiaye maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa
na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu
ya mwamba… Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa
na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu
ya mchanga” (Math. 7:24,26). “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria
walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa
haki” (Rom. 2:13). “Iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali
mkijidanganya nafsi zenu” (Yak. 1:22).
Hapo
somo linazaa matunda mema: “Nyingine zilianguka penye udongo mzuri; zikamea,
zikazaa moja kwa mia… ndio wale
ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha
huzaa matunda kwa kuvumilia” (Lk. 8:8,15). Ndivyo lilivyokuwa somo
alilolifanya mt. Augustino aliposikia maneno haya: “Chukua na kusoma”;
akafungua Nyaraka zilizokuwa mezani, akasoma: “Kama ilivyohusika na mchana
na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si
kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo” (Rom. 13:13-14). Kuanzia
hapo akaongoka, akajitenga faraghani kwa muda fulani, akajiandikisha kwa
ubatizo, matunda yakawa kweli mara mia, nayo yakawafaidisha wengi hadi leo.
1.17. UONGOZI WA KIROHO
Kati ya misaada ya nje kwa utakatifu unatakiwa kuhesabiwa uongozi wa Kiroho. Kwanza tutaongea juu ya haja yake kwa jumla na kwa hatua mbalimbali za maisha ya Kiroho; halafu juu ya sifa ambazo kiongozi awe nazo, na juu ya wajibu wa yule anayeongozwa.
HAJA YA UONGOZI KWA JUMLA
Ingawa
uongozi si wa lazima kwa utakatifu, ni njia ya kawaida ya maendeleo ya Kiroho.
Bwana alipounda Kanisa lake alitaka waamini wawe chini ya papa na maaskofu
upande wa nje, na chini ya waungamishi upande wa ndani, hao wakiwaelekeza njia
za kutoanguka tena dhambini na za kusonga mbele katika maadili. Mt. Paulo
alipoongoka, Yesu hakumfunulia mwenyewe mipango yake, bali alimtuma Damasko
kwa Anania, ajue kwa njia yake yatakayompasa kuyafanya (taz. Mdo. 9:6).
“Fanya
bidii sana na uangalifu mkubwa kabisa ili kumpata mtu ambaye aweze kukuongoza
kwa hakika katika kazi uliyokusudia ya kuishi kitakatifu; umchague mtu
anayeweza kuwaelekeza wenye mapenzi mema njia nyofu ya kumuendea Mungu… Ni
kiburi kabisa kudhani huna haja na mashauri” (mt. Bazili).
“Usijifanye
mwalimu wako mwenyewe, la sivyo utapotea haraka sana” (mt. Jeromu)
“Kama
vile kipofu asivyoweza kushika njia nyofu asipoongozwa na mtu, hakuna
anayeweza kutembea bila ya kiongozi” (mt. Augustino)
Kasiani
alifundisha kwamba anayetegemea akili yake hatafikia kamwe ukamilifu wala
hataweza kukwepa hila za Ibilisi; njia bora ya kushinda vishawishi vya hatari
ni kuvifunua kwa kiongozi mwenye busara na neema ya kutuangazia. Kweli, mara
nyingi inatosha kuvifunua kwa anayehusika ili viishe.
“Anayejifanya
kiongozi wake mwenyewe anajifanya mwanafunzi wa mpumbavu… Upande wangu
natamka kuwa kwangu ni rahisi zaidi na ya hakika zaidi kuwaagiza wengi kuliko
kujiongoza mimi tu” (mt. Bernardo). Katika kuwaongoza wengine umimi wetu
unatudanganya kidogo kuliko katika kujiongoza; na kama tungejua namna ya
kutekeleza wenyewe yale tunayowaambia wengine, maendeleo yetu yangekuwa
makubwa.
“Bwana
wetu, ambaye pasipo yeye hatuwezi kitu, hatamjalia kamwe neema yake mtu
ambaye, ingawa anaye mtu mwenye uwezo wa kumfundisha na kumuongoza, anapuuzia
chombo hicho muhimu cha utakatifu, akidhani anajitosheleza na kuweza kwa nguvu
zake kutafuta na kuona yanayofaa kwa wokovu wa milele… Aliye na kiongozi
ambaye anamtii katika yote na kikamilifu, atalifikia lengo lake kwa urahisi na
haraka sana kuliko kama akifanya peke yake, hata kama ana akili sana na vitabu
vyenye hekima kuhusu mambo ya Kiroho… Kwa jumla, wale wote waliofikia
ukamilifu wamefuata njia ya utiifu, isipokuwa kama kwa fadhili au neema ya
pekee Mungu alimfundisha mwenyewe mtu mmojammoja asiyekuwa na wa kumuongoza”
(mt. Visenti Ferrer).
Mt.
Fransisko wa Sales alionyesha kuwa hatuwezi kuamua kwa haki katika kesi zetu
wenyewe, kutokana na aina ya kujipendea “ya siri na isiyotambulikana ambayo
tusipoona vizuri hatuwezi kuivumbua; na wale wenyewe waliopatwa nayo hawaijui
wasipoonyeshwa”. Aliyekaa muda mrefu katika chumba ambacho milango na
madirisha yake yamefungwa hatambui kuwa humo hewa imekuwa chafu kwa njia ya
kupumua, kumbe anayeingia anatambua mara. Sisi sote tunakubali kwamba kiongozi
anahitajika ili kupanda mlima mrefu; bila ya shaka anahitajika zaidi ili
kupanda hadi kilele cha ukamilifu, hasa kwa sababu tunapaswa kukwepa hila za
yule asiyetaka tupande.
Mt.
Alfonsi aliorodhesha uongozi unahusika na nini zaidi: malipizi, namna ya
kupokea sakramenti, sala, utekelezaji wa maadili na namna ya kutenda
kitakatifu kazi za kila siku.
Shuhuda
hizo zote na nyinginezo zinaonyesha wazi haja ya uongozi kwa jumla. Tutaelewa
zaidi kwa kuzingatia hatua tatu za maisha ya Kiroho, yaani mahitaji ya
wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika.
Uongozi
wenye busara, imara na moyo wa kibaba unahitajiwa hasa na wanaoanza, kama
unavyofanywa na walezi utawani. Baadaye haja hiyo haisikiki tena vile,
isipokuwa katika vipindi vigumu yanapotokea mabadiliko na unapotakiwa uamuzi
muhimu.
Wanaoanza
wanahitaji kukingwa dhidi ya marudio ya makosa na dhidi ya kasoro mbili
zinazopingana. Baadhi wakipokea faraja za kihisi katika sala wanazichanganya
na neema za juu, na kwa kiburi wangetaka kuruka
mara moja hadi kufikia muungano bila ya kupitia hatua za lazima. Hao
wanahitaji kukumbushwa haja ya unyenyekevu na kusadikishwa kuwa safari ya
ukamilifu ni kazi ya maisha yote: haiwezekani kuruka bila ya mabawa, na katika
kujenga tunaanza na misingi. Lengo tuliloliona ni la kwanza kutamaniwa na
kukusudiwa, lakini ni la mwisho kufikiwa; tena haifai kupuuzia njia duni
ambazo ni za lazima ili kulifikia. Baadhi wana kiburi
cha siri katika kushika maisha magumu na kujitosa mno
katika malipizi hadi kuharibu afya. Baadaye, wakitaka kujitibu wanalegea
na kwenda kinyume cha mara ya kwanza. Hao wanahitaji kujifunza kiasi cha
Kikristo na kwamba haitoshi kuwa na maadili ya Kimungu pasipo maadili ya
kibinadamu ili kutawala polepole hisi.
Uongozi
unakuwa wa lazima hasa katika kipindi
kirefu cha ukavu ambapo kutafakari ni kwa shida tena kuna vishawishi
vikali pamoja na upinzani wa watu. Tutakavyoeleza, jaribu hilo linavusha
kutoka hatua ya utakaso kwenda hatua ya mwanga mradi ziwepo dalili tatu ambazo
kiongozi anatakiwa kuzitambua: 1) kutofurahia mambo ya Mungu wala ya dunia; 2)
hata hivyo, kuendelea kwa kawaida kumkumbuka Mungu, kutamani ukamilifu na
kuogopa kutomtumikia; 3) kushindwa kutafakari kwa mpangilio na badala yake
kuvutiwa na tendo la kumtazama tu Mungu.
Katika
kipindi hicho kigumu, kinachotakiwa kuwa kama wongofu wa pili, ni lazima
kumsikiliza kiongozi wa kufaa ili kusonga mbele kwa bidii badala ya kubaki
nyuma kama mchelewaji.
Kwa
kawaida uongozi wa wanaoendelea unaweza kufanyika haraka zaidi, kwa sababu
anayeongozwa ameshajua zaidi maisha ya Kiroho na mara nyingi anaweza kueleza
kwa neno moja anahitaji shauri kuhusu nini. Hapo kiongozi anakuwa kama shahidi
wa maendeleo yake; anatakiwa kutambua kazi ya mlezi wa ndani ili awe chombo
chake na kuhakikisha usikivu wa mtu kwa mianga ya Roho Mtakatifu, akipambanua
ndani yake pumba na mchele, yaani kilema kikuu ambacho apambane nacho, na
mvutio maalumu wa neema ambao aufuate.
Inafaa
tumkimbilie kiongozi hasa wakati wa mazoezi ya Kiroho ya kila mwaka ili
kumueleza kwa unyofu wote undani wa roho tusije tukajidanganya tu kwa
kuangukia kiburi kilichofichika na kujiamini kipumbavu.
Kwa
wanaoendelea pia kuna vipindi vigumu vinavyohitaji uongozi bora, kwa namna ya
pekee wanapotakiwa kuvukia hatua
ya muungano. Namna za majaribu hayo zinaweza kuwa mbalimbali, lakini kwa
kawaida ni kunyimwa kwa muda mrefu faraja si za kihisi tu, bali za roho pia.
Hapo vinatokea mara nyingi vishawishi dhidi ya imani, tumaini na upendo na
unahitajika kwa namna ya pekee msaada wa kiongozi mwenye mwanga na
mang’amuzi. Hata mtu anayeweza kuongoza wengine katika hatua hiyo hawezi
kujiongoza kwa sababu “hakuna tena mapito tayari” (mt. Yohane wa Msalaba),
hivyo anapaswa tu kufuata mwanga wa Roho Mtakatifu asiuchanganye na msukumo
mwingine unaoweza kufanana nao.
Waliokamilika
pia wanajisikia haja ya msaada huo ili kuona namna
ya kulinganisha msimamo wa kujiachilia
mikononi mwa Mungu na utendaji ambao
Bwana anawadai, ili kutekeleza vizuri msemo huu: “kushika uaminifu na
kujiachilia”. Wanajisikia haja ya kuongozwa ili kudumisha hai moyoni mwao
upendo kwa msalaba pamoja na unyenyekevu mkubwa. Basi, ikiwa hao wanahitaji
uongozi, zaidi tena wanauhitaji wanaoanza.
Kiongozi
“anatakiwa kuwa amejaa upendo, elimu
na busara: likikosekana mojawapo kati ya hayo matatu, kuna hatari” (mt.
Fransisko wa Sales). “Ni muhimu sana kwamba kiongozi awe na mwanga: yaani
awe na busara na mang’amuzi sana. Ikiwa
zaidi ya hayo ni mwanateolojia pia,
basi ni kamili. Lakini isipowezekana kumuona mtu mwenye sifa hizo tatu pamoja,
ni afadhali awe na zile mbili za kwanza, kwa sababu katika shida kuna
uwezekano wa kupata shauri la wasomi. Nionavyo mimi, hao wa mwisho,
wasipojitahidi katika sala, hawafai sana kwa wanaoanza; lakini sitaki kushauri
wasiwe na uhusiano nao… Elimu ni jambo kubwa… Mungu atuepushe na ibada za
kijuujuu na zilizojaa upuuzi” (mt. Teresa wa Yesu).
Upendo
wa kiongozi unapaswa kumfanya asijitafutie faida na aongoze mioyo kwa Mungu,
si kwake mwenyewe. Y. Thauler alisema viongozi wanaojivutia watu ni kama mbwa
ambao katika uwindaji wanamla mnyama badala ya kumleta kwa bwana wao; hapo
huyo anawapiga kweli.