HISTORIA YA UTAWA |
![]() |
UTANGULIZI
Mwezi
Oktoba 1994 huko Roma ilifanyika Sinodi ya tisa ya kawaida kuhusu “Maisha
yaliyowekwa wakfu na utume wake katika Kanisa na katika ulimwengu”. Maaskofu
na watawa waliokutanika kutoka dunia nzima walitambua upya tofauti za mitindo ya
kitawa, zinazotokana na wakati na mahali mbalimbali ambapo Roho Mtakatifu
aliwakirimia watu wake wajitoe kabisa kwa ufalme wa Mungu. Hatuwezi kuelewa
utawa tukidhani ni kitu kimoja, bali jina hilo linajumlisha maisha ya aina
nyingi yanayomshuhudia Kristo katika sifa na kazi zake mbalimbali.
Tunataka kufuata historia ya
maisha hayo kama kitabu bora kilichoandikwa na Mungu siku kwa siku kadiri ya
mpango wake wa hekima kwa ujenzi wa taifa lake takatifu. Kuna hatua kuu nne
ambazo zilizaa mitindo mipya zaidi, hasa upande wa Magharibi, lakini bila ya
kufuta ile iliyotangulia:
1.
Hadi karne ya XII ulitawala mtindo wa kimonaki ukifuatwa na ule wa
kikanoniki (Bazili, Benedikto na Norberti ndio watakatifu maarufu zaidi).
2.
Kati ya karne ya XIII hadi ya XV yalitokea mashirika ya waombaomba (Fransisko
na Dominiko ndio watakatifu wakuu).
3.
Kati ya karne ya XVI hadi ya XIX yalitokea mashirika mengi ya wakleri
wafuatakanuni, ya maisha ya kitume na ya watoahuduma (Ignasi wa Loyola ndiye
mtakatifu muhimu zaidi).
4.
Hatimaye karne ya XX imeona uanzishaji wa mashirika ya kilimwengu na wa
jumuia za aina mpya.
MWANZO: UBIKIRA NA JUHUDI NYUMBANI
Kufuatana na
mifano ya Bikira Maria na hasa ya Yesu Kristo, tunasoma katika Agano Jipya
habari za wanaume na wanawake waliojinyima ndoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu,
kama vile mabinti wanne wa shemasi Filipo waliokuwa mabikira na manabii (Mdo.
21:9). Hasa mtume Paulo aliwahimiza Wakristo wowote wanaoweza wafanye hivyo kama
alivyofanya mwenyewe kufuatana na shauri la Bwana (taz. 1Kor. 7:25-34).
Hata katika
maandishi ya mababu wa Kanisa kuanzia karne ya I tunasoma sifa za watu wa toba
wanaozungukazunguka ili kuhubiri na za mabikira ambao utakatifu wao unaonyeshwa
kama alama ya ubora wa Ukristo juu ya ulimwengu wa anasa unaoliudhi Kanisa.
Polepole mabikira hao walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na Askofu na
kukusanywa katika jumuia (utawa wa mabikira). Ilitokea vilevile kwa wanaume wa
toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika
ufukara fulani wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku,
kuimba Zaburi na kusali kwa moyo.
UMONAKI NA KUKIMBIA ULIMWENGU
Tofauti na watu waliotangulia ambao waliishi
katika mazingira ya kawaida, mwishoni mwa karne ya III huko Misri ulianza mtindo
wa kukimbia ulimwengu hata kimakao (umonaki, kutoka neno la Kigiriki monos =
mmoja). Mmonaki alitafuta upweke kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu,
bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida ili moyo uweze
kutulia kabisa na kumpenda Mungu bila ya kugawanyika. Miundo mipya ya umonaki
ilitegemea matatu: mwanzilishi, kanuni, upweke. Mtindo huo wa maisha, ambao ndio
mchango mkuu wa Afrika kwa Kanisa lote, ulistawi hasa baada ya dola la Kirumi
kuruhusu Ukristo mwaka 313.
Anayeheshimiwa
kama baba wa wamonaki ni mt. Anthony abati (251-356) ambaye akizingatia maneno
mbalimbali ya Injili aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa amfuate Mwokozi.
Maisha yake yote akazidi kujitafutia mahali pa upweke kamili zaidi ili kumtafuta
Mungu tu. Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi sehemu mbalimbali, naye
Anthony aliwaongoza bila ya kuacha upweke wake. Maisha magumu ya makundi hayo
yaliamsha Kanisa lifuate Injili kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ambapo
ulihitajika ujasiri mbele ya hatari ya kuuawa. Hivyo umonaki ulionekana aina
mpya ya kifodini kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote.
MAISHA YA PAMOJA MASHARIKI
Muda
mfupi baadaye, na sehemu ileile, yalianzishwa maisha ya pamoja ambamo mali na
vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata mna mwanzo wa kushughulikia
watu wa ulimwenguni.
Mt.
Pakomi (288-346) aliongokea imani kwa kuzingatia Wakristo walivyowatumikia
wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo na
kama kawaida yaliathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika
umonaki akajisikia wito wa kuishi kwa upendo na wengine akaanzisha maisha ya
pamoja upwekeni huko Misri Kusini. Ndiye wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa, na
ndani yake jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”. Kanuni hiyo ikaja
kupenya maisha ya wamonaki na kanuni Mashariki na Magharibi vilevile. Mbali ya
mafungo na sala ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani
kuwa na utiifu, huruma na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo
iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili.
Karibu na monasteri za kiume kuliko na nyingine za kike.
Pia
mt. Bazili Mkuu (330-379) alianzisha maisha ya pamoja baada ya kutembelea
wamonaki sehemu mbalimbali. Aliita monasteri “jamaa” kwa kuwa lengo lake kuu
lilikuwa kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni.
Tofauti na monasteri ya Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya wamonaki, jamaa hiyo
haikuwa kubwa sana wala kuwa na ngome, wala kuishi jangwani, bali karibu na mji
wa Kaisarea wa Kapadokia. Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa:
wamonaki wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wafuate
utakatifu wa wito wao, tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama kuhubiri na
hasa kuhudumia wenye shida. Mtindo wake ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu
kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa. Mpaka leo kanuni zake zinaongoza
karibu wamonaki wote wa Mashariki, na kwa njia yao makanisa ya Orthodoksi kwa
kuwa maaskofu kwanza ni wamonaki nao wanaelekeza wakristo wote kufuata mifano
yao.
MAISHA YA PAMOJA MAGHARIBI
Tangu
karne ya IV umonaki ulienea Magharibi pia: zinajulikana monasteri za kike na za
kiume huko Italia, Ufaransa na Hispania.
Babu
bora wa Kanisa lote, mt. Augustino (350-430), baada ya kuongoka na kuzitembelea
baadhi, alirudi kwao aanzishe maisha ya pamoja Afrika Kaskazini pia. Kwanza
aliishi na walei wenzake, halafu alipochaguliwa kuwa askofu aliishi na mapadri
wake, akiwashirikisha utajiri wake wa akili na roho, wafanye vizuri utume.
Katika kanuni yake, iliyowalenga wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe
la utawa, si jambo mojawapo tu.
Mt.
Benedikto wa Nursia (480-547), ingawa si mwanzilishi wa umonaki wa Magharibi,
ndiye aliyeuunda kwa namna ya kudumu na kwa njia hiyo akaja kuunda upya Ulaya
Magharibi. Hasa kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake na
mafundisho ya Bazili na ya mababu wa jangwani, iliunganisha vizuri maelekeo
mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa
umoja. Sifa nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo
zilirekebisha na kufufua uchumi wa Ulaya na kuokoa elimu ya zamani. Yeye
alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya
pekee kama baba na mwalimu wa kudumu wa wamonaki wote, ambao wanafafanuliwa na
Kanuni kuwa ndio “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati
mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye
mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za
misusuko (baada ya mfululizo wa uvamizi wa makabila ya Kijerumani), Benedikto
alidai udumifu katika monasteri. Kutokana na kujitegemea kwa kila monasteri,
Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano
kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.
Kati
ya mitindo mingine ya umonaki wa Magharibi ambayo ikaja kukubali kanuni ya
Benedikto inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ireland n.k.) ambao
hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na
kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara
kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa
Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa mt.
Kolumbani (540-615).
Hata
Wabenedikto walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. mt. Augustino wa
Canterbury (+604), mtume wa Uingereza, na mt. Bonifas (672-754), shahidi mtume
wa Ujerumani.
MAREKEBISHO YA KARNE YA X-XII
Ni
kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kulegea, kuanza safari kwa
kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi tofauti za bidii na
za ulegevu. Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linapatwa na ulegevu na ukosefu
wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili
kulirekebisha. Utawa wenyewe ulianzishwa jangwani ili kupinga ulegevu wa Kanisa
na unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili
pia.
Hasa
katika karne ya X-XII Kanisa la Magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho
katika umonaki na katika maisha yake yote. Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto
yaliyotokana na juhudi hizo yanakumbukwa hasa lile la Cluny (lililokazia
liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha
magumu katika ufukara na kazi, likamtoa mt. Bernardo – 1091-1153 - aliyeathiri
nyakati zake na zile zilizofuata, hasa upande wa maisha ya Kiroho), lile la
Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na mengineyo.
Wakati
huohuo mt. Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na
juhudi hadi leo (Wakartusi).
UKANONI KWA UREKEBISHO WA MAKLERI
Ili
kurekebisha maisha ya mapadri, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati
yao, ambamo waishi na kusali na kufanya utume kwa pamoja. Hasa karne za XI-XII
wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makuu au makubwa na kueneza mtindo mpya wa
kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji. Walifuata kanuni ya
mt. Augustino na kuitwa Wakanoni. Hata wao walichangia ustawi wa Kiroho wa
Kanisa. Mkuu katika ya watakatifu wao ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa
Wapremontree.
WATAWA
ASKARI NA WA HOSPITALI
Katika
karne ya XII Wakristo walianzisha vita vya msalaba dhidi ya Waislamu hasa katika
nchi takatifu. Kwa ajili hiyo ilianzishwa aina mpya ya watawa ambao, pamoja na
maisha ya Kiroho washike upanga ili kusindikiza, kulinda na kukaribisha
waliohiji Yerusalemu. Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini
yamebadili sana malengo na mbinu.
MASHIRIKA
YA WAOMBAOMBA
Kama
kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei
hawakuridhika. Pia hija na vita vya Msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya
Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo
mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni, wakisisitiza
ufukara na unyofu dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, hata wengi walifikia
hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu
kadhaa waukinai. Juu ya misingi hiyo yalianzishwa mashirika mbalimbali
yaliyoitwa ya waombaomba kwa jinsi walivyokaza ufukara.
Mt.
mzee Dominiko (1170-1221) akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi
kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili
alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya
kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya
kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa ajili hiyo utawa
wake ulipunguza miundo ya monaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya
kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao
wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi
na maisha ya sala na kusoma.
Hata
kuliko rafiki yake Dominiko, mt. mzee wetu Fransisko (1181-1226) alishikwa na
hamu ya kulingana na Yesu kwa kufuata nyayo zake inavyofundishwa na Injili.
Alifanya vilevile kazi ya kuhubiri, lakini si kwa kuzingatia elimu wala kwa
lengo la kubishana na wazushi, bali kwa kuonyesha njia ya toba kwanza kwa
matendo halafu kwa maneno machache na manyofu. Kwa ajili ya Kristo alijinyima
hata upweke alioupendelea, akawakaribia watu hasa wadogo. Utawa wake hauhitaji
monasteri wala maktaba kubwa. Jamaa inategemea ndugu wenyewe na nyumba yao ni
ulimwengu wote, ni popote pale wanapokutana. Katika kuzungukazunguka au walau
kuhamahama, ndugu wadogo walilingana na watu wa zamani hizo: hawakujifunga
kuishi daima mahali fulani na watu walewale, bali walifungamana na jamaa ya
kimataifa ambayo mkuu wake aweze kuwatuma popote. Hivyo iliwabidi kuwa tayari
kukabili mazingira yoyote na kushirikiana na ndugu mbalimbali. Tena udugu
haukuishia shirikani bali ulitakiwa kuenea kwa watu na viumbe vyote. Kutokana na
upya wa mtindo wa maisha, hata miundo ya utawa ilipaswa kuwa mipya ili kudumisha
umoja wao. Ufransisko ulilingana kikamilifu na madai ya urekebisho ya walei, pia
uliwapendeza viongozi wa Kanisa walioona ulivyookoa utiifu wa watu kwao: hivyo
ulienea kasi ajabu, hata kati ya wanawake na watu wa ndoa. Watawa wa kike
hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia
ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa ndugu wadogo. Mt. Klara
(1193-1253), mche mdogo wa mt. Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga
kanuni ya kitawa.
MASHIRIKA
YA KUTOA HUDUMA
Hata
karne ya XVI ilidai sana urekebisho wa Kanisa lote. Katika jitihada hizo wengine
walifikia hatua ya kujitenga (Uprotestanti), wengine walianzisha matapo mapya ya
Kiroho na mashirika ya aina mpya, yanayolenga hasa utume, kwa kupunguza ukubwa
wa nyumba na liturujia ya pamoja: pengine jumuia ni kuishi mahali pamoja bila ya
ushirikiano isipokuwa kati ya kiongozi na mtawa mmojammoja. Mashirika hayo
hayana kanuni isipokuwa katiba tu.
Kati
ya yote lile la Yesu (Wajesuiti) ndio muhimu zaidi. Mwanzilishi wake ni mt.
Ignas wa Loyola (1491-1556) ambaye kabla hajaongoka alikuwa askari, halafu
akaleta utawani mtindo wa kijeshi, akisisitiza utiifu kwa viongozi wa shirika na
kwa papa (wakijifunga kwake kwa nadhiri ya nne, nguzo kuu ya shirika). Hivyo
Mjesuiti jumuia yake halisi ni shirika tu ambalo linaweza kumtuma popote duniani
na kumbadilishia kazi yoyote, naye atafanya yote kwa niaba ya shirika, tayari
kukabili mazingira na hali yoyote.
Zaidi
ya mashirika 2000 yaliyoanzishwa baada ya hapo, hasa katika karne ya XIX,
yalifuata kwa kiasi fulani mtindo huo, yakilenga hasa huduma fulani iliyoonekana
inahitajika lakini haina wa kuitoa, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana,
kufundisha fukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji
habari. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati tofauti
na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa jimbo. Polepole hata wanawake
walikubaliwa kufanya utume na kuanzisha mashirika ya namna hiyo.
MASHIRIKA
YASIYO YA WAKFU
Karne
hizohizo zilijitokeza pia aina nyingine ambazo pengine hazina nadhiri au si za
hadhara. Kati ya wanawake mt. Anjela Merici (1474-1540) alianzisha muundo kwa
wasichana kulelewa nyumbani ili kujitolea kutenda huruma. Vilevile walifanya
Mary Ward (1585-1645) na mt. Luisa wa Marillac (1591-1660), wakitaka wafuasi wao
waishi na kutumikia kati ya watu. Upande wa wanaume tunamkumbuka hasa mt. Filipo
Neri (1515-1595) kati ya walioanzisha jumuia za maisha ya kitume ambapo watu
wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya
kujiweka wakfu.
KARNE
YA XX
Karne
hiyo ngumu kwa Kanisa na kwa dunia yote ilipata mang’amuzi mapya hasa katika
maisha ya ulimwenguni. Kwa mara nyingine walei walichangia sana hali mpya ndani
ya Kanisa, ya kuthamini na kushughulikia mambo ya kidunia. Katika juhudi za
kuratibu nyanja zote za maisha ya binadamu, baadhi walijisikia haja ya kujiweka
wakfu bila ya kujitenga na maisha ya kawaida. Polepole Kanisa likawakubalia
(1950) wito mpya wa mashirika ya ulimwenguni ambayo waamini wanawekwa wakfu wawe
chumvi, mwanga na chachu kati ya watu. Hivyo wanajitahidi kuwa na moyo wa
kujikana na bidii ya kitume kama watawa, lakini pia utaalamu wa kisasa na
urahisi wa kupenya mazingira yoyote kama walei.
Mtaguso
Mkuu wa II wa Vatikano (1962-1965) uliagiza uanzishwe tena utawa wa mabikira
ambao waishi ulimwenguni na kuwekwa wakfu kwa ajili ya jimbo, si kwa shirika
lolote.
Upande
mwingine watu wa karne hiyo waliona haja ya kujumuika hata nje ya miundo ya
kitawa, wakifuata mitindo wa kimonaki au kutoa huduma kwa wasiojiweza ndani ya
jumuia, ingawa baadhi yao wana ndoa au pengine si Wakristo.
Nusu
ya pili ya karne hiyo ilililetea Kanisa neema za matapo mengi yaliyoanzishwa kwa
kawaida na walei na kuenea kati ya watu milioni na milioni. Mbali ya watawa
wengi kuyafuata, na miito mingi kupatikana ndani yake, pia baadhi ya wafuasi wa
matapo hayo hawaingii katika shirika fulani bali wanakusanyika kuishi kijumuia
au kuwekwa wakfu katika matapo yenyewe na hivyo kuyaongoza Kiroho kwa kuchimba
karama yake.
Muundo
wa pekee ulikubaliwa kwa Opus Dei ambayo ina askofu wa pekee pamoja na mapadri
wake, seminari mbalimbali na walei popote duniani: ni kama jimbo lisilo na eneo
maalumu.
Mbele
ya upya huo wote sheria za Kanisa siku hizi zinamhimiza askofu yeyote atambue
aina mpya za maisha yaliyowekwa wakfu zikijitokeza jimboni.
Kazi
nyingine ya Roho Mtakatifu ni kuanzishwa upya kwa mashirika ya kitawa katika
Uprotestanti baada ya huo kuyafuta karne ya XVI kama kitu kinyume cha Injili.
Kuanzia mwaka 1836 katika nchi mbalimbali watu wa madhehebu hayo walianza tena
kuishi kijumuia kwa kufuata mapokeo ya Kibenedikto na ya Kifransisko.